< Waamuzi 19 >
1 Katika siku hizo Israeli hawakuwa na mfalme. Basi Mlawi mmoja aliyeishi sehemu za mbali katika nchi ya vilima ya Efraimu, akamchukua suria mmoja kutoka Bethlehemu ya Yuda.
Katika siku hizo, wakati hakuna mfalme katika Israeli, kulikuwa na mtu, Mlawi, aliyekuwa akiishi kwa muda kidogo katika eneo la mbali zaidi ya nchi ya Efraimu. Alijichukulia mwanamke, masuria kutoka Bethlehemu huko Yuda.
2 Lakini suria wake akafanya ukahaba dhidi yake, naye akamwacha akarudi nyumbani kwa baba yake huko Bethlehemu ya Yuda. Baada ya kukaa huko kwa muda wa miezi minne,
Lakini mkewe hakuwa mwaminifu kwake; akaondoka na kurudi nyumbani kwa baba yake huko Bethlehemu ya Yuda. Alikaa huko kwa muda wa miezi minne.
3 mume wake akaenda kumsihi ili arudi. Alikwenda na mtumishi wake na punda wawili. Yule mwanamke akamkaribisha nyumbani mwa baba yake, baba yake alipomwona akamkaribisha kwa furaha.
Kisha mumewe akaondoka na kumfuata ili kumshawishi arudi. Mtumishi wake alikuwa pamoja naye, na punda wawili. Akamleta nyumbani kwa baba yake. Baba wa msichana alipomwona, alifurahi.
4 Baba mkwe wake, yaani, baba yake yule msichana, akamzuia ili akae, hivyo akakaa na huyo baba mkwe wake kwa siku tatu, wakila, wakinywa na kulala huko.
Baba mkwe wake, baba wa msichana, alimshawishi kukaa siku tatu. Walikula na kunywa, na walikaa usiku huko.
5 Siku ya nne wakaamka mapema naye akajiandaa kuondoka, lakini baba wa yule msichana akamwambia mkwewe, “Ujiburudishe kwa kula kitu chochote, ndipo uweze kwenda.”
Siku ya nne waliamka mapema na alijiandaa kuondoka, lakini baba wa msichana akamwambia mkwewe, “Jipe nguvu na mkate kidogo, kisha unaweza kwenda.”
6 Basi wakaketi wote wawili ili kula na kunywa pamoja. Baadaye baba wa msichana akamwambia, “Tafadhali ubakie usiku huu upate kujifurahisha nafsi yako.”
Basi hao wawili wakaketi kula na kunywa pamoja. Kisha baba ya msichana akasema, “Tafadhali uwe tayari kukaa usiku huu na kuwa na wakati mzuri.'
7 Basi yule mtu alipotaka kuondoka baba wa yule msichana akamsihi, basi akabaki usiku ule.
Mlawi alipoinuka ili aondoke, baba wa mwanamke huyo alimwomba akae, hivyo alibadili mpango wake na akalala usiku tena.
8 Asubuhi ya siku ya tano, alipoamka ili aondoke, baba wa yule msichana akamwambia, “Jiburudishe nafsi yako. Ngoja mpaka mchana!” Kwa hiyo wote wawili wakala chakula pamoja.
Siku ya tano aliamka mapema kuondoka, lakini baba wa msichana akasema, 'Jitie nguvu mwenyewe, na kusubiri mpaka alasiri.' Kwa hiyo hao wawili wakala chakula.
9 Basi wakati yule mtu alipoinuka aende zake, pamoja na suria wake na mtumishi wake, baba mkwe wake, yaani, baba wa yule msichana akamwambia, “Tazama sasa jioni inakaribia. Ulale hapa usiku unakaribia. Ukae, ukajifurahishe nafsi yako. Kesho unaweza kuamka mapema asubuhi na uende nyumbani kwako.”
Mlawi na suria wake na mtumishi wake wakainuka ili kuondoka, baba mkwe wake, baba wa msichana akamwambia, “Angalia, sasa mchana unaelekea jioni. Tafadhali kaa usiku mwingine, na uwe na wakati mzuri. Unaweza kuamka kesho mapema na kurudi nyumbani.”
10 Lakini akakataa kulala tena, akaondoka na kwenda mpaka Yebusi (ndio Yerusalemu), akiwa na punda wake wawili waliotandikiwa, pamoja na suria wake.
Lakini Mlawi hakuwa tayari kukaa usiku. Aliamka na kuondoka. Akaenda kuelekea Yebusi (hiyo ni Yerusalemu). Alikuwa na pande mbili za punda-na masuria wake alikuwa pamoja naye.
11 Alipokaribia Yebusi na usiku ukiwa umekaribia, mtumishi akamwambia bwana wake, “Haya sasa natuingie katika mji huu wa Wayebusi tulale humo.”
Walipokuwa karibu na Yebusi, siku hiyo ilikuwa imeenda mno, na mtumishi akamwambia bwana wake, Haya, tupate kwenda kwa mji wa Wayebusi, tukakae ndani yake usiku huu.
12 Lakini bwana wake akamjibu, “Hapana. Hatutaingia kwenye mji wa kigeni, ambao watu wake si Waisraeli. Tutaendelea mpaka tufike Gibea.”
Bwana wake akamwambia, “Hatuwezi kwenda katika mji wa wageni ambao si wa wana wa Israeli.” Tutakwenda Gibea.
13 Akasema, “Haya, tujitahidi tufike Gibea au Rama, nasi tutalala katika mji mmojawapo.”
Mlawi akamwambia yule kijana, “Njoo, twende sehemu moja wapo, na tukae usiku huko Gibea au Rama.”
14 Hivyo wakaendelea na safari, jua likachwea walipokaribia Gibea ambao ni mji wa Benyamini.
Basi, wakaenda, na jua likachwea wakiwa karibu na Gibea, katika eneo la Benyamini.
15 Wakageuka ili kuingia na kulala Gibea. Wakaingia humo, wakaketi kwenye uwanja wa mji, wala hakuna mtu yeyote aliyewakaribisha kwake ili wapate kulala.
Wakageuka huko ili wawezenkukaa usiku huko Gibea. Naye akaingia na kukaa katika njia kuu ya jiji, maana hakuna mtu aliyewaingiza nyumbani kwake usiku.
16 Jioni ile mtu mmoja mzee toka nchi ya vilima ya Efraimu, aliyekuwa anaishi huko Gibea (watu wa sehemu ile walikuwa Wabenyamini), akarudi kutoka kwenye kazi za shamba.
Lakini mtu mzee alikuwa akija kutoka kazini kwake katika shamba jioni hiyo. Alikuwa kutoka mlima wa Efraimu, naye alikuwa akikaa kwa muda huko Gibea. Lakini watu wanaoishi mahali hapo walikuwa Wabenyamini.
17 Alipotazama na kuwaona hao wasafiri katika uwanja wa mji, yule mzee akawauliza, “Ninyi mnakwenda wapi? Nanyi mmetoka wapi?”
Aliinua macho na kumwona msafiri katika njia kuu ya jiji. Huyo mzee akasema, “Unakwenda wapi? Unatoka wapi?”
18 Akamwambia, “Tumepita kutoka Bethlehemu ya Yuda, tunaelekea katika nchi ya vilima ya Efraimu, ambako ndiko ninakoishi. Nilikwenda Bethlehemu ya Yuda na sasa ninakwenda katika nyumba ya Bwana. Hakuna mtu yeyote aliyenikaribisha katika nyumba yake.
Mlawi akamwambia, “Tunaenda kutoka Betelehemu ya Yuda mpaka sehemu ya mbali zaidi ya nchi ya kilima ya Efraimu, ambako mimi hutoka. Nilikwenda Bethlehemu huko Yuda, nami nenda nyumbani mwa Bwana; lakini hakuna mtu atakayenichukua nyumbani kwake.
19 Tunazo nyasi na chakula cha punda wetu na mkate na divai kwa ajili yetu sisi watumishi wako, yaani mimi, mtumishi wako mwanamke, pamoja na huyu kijana tuliyefuatana naye. Hatuhitaji kitu chochote.”
Tuna nyasi za kulisha punda zetu, na kuna mkate na divai kwa ajili yangu na mtumishi wako mwanamke hapa, na kwa kijana huyu pamoja na watumishi wako. Hatujapungukiwa chochote. '
20 Yule mzee akawaambia, “Amani iwe kwenu! Karibuni nyumbani mwangu. Nitawapa mahitaji yenu yote, msilale katika uwanja huu wa mji.”
Huyo mzee akawasalimu, “Amani iwe na wewe! Nitakupatia mahitaji yako yote. Usikae usiku tu katika njia kuu.”
21 Hivyo akamwingiza nyumbani mwake na kuwalisha punda wake. Baada ya kunawa miguu yao, wakala na kunywa.
Basi huyo mtu akamleta Mlawi nyumbani kwake, akawalisha punda. Wakaosha miguu yao na kula na kunywa.
22 Walipokuwa wakijiburudisha, watu waovu wa mji huo, wakaizingira ile nyumba. Wakagonga mlango na kusema na yule mzee mwenye nyumba, “Mtoe nje yule mtu aliyeingia kwako, tupate kumlawiti.”
Walipokuwa wakifurahisha mioyo yao, watu wengine wa jiji, watu wasiokuwa na maana, walizunguka nyumba, wakipiga mlango. Wakamwambia yule mzee, mwenye nyumba, wakisema, “Mtoe mtu aliyeingia nyumbani kwako, ili tuweze kufanya mapenzi naye.”
23 Yule mwenye nyumba akatoka nje na kuwaambia, “Hapana, ndugu zangu msiwe waovu namna hii, ninawasihi. Kwa kuwa huyu mtu ni mgeni wangu msifanye jambo hili la aibu.
Yule mtu, mwenye nyumba, akawajia, akawaambia, “Hapana, ndugu zangu, tafadhali msifanye jambo baya! Kwa kuwa mtu huyu ni mgeni nyumbani kwangu, musifanye jambo hili baya!”
24 Tazameni, hapa yupo binti yangu ambaye ni bikira na suria wa huyu mtu. Nitawatoleeni hawa sasa, mkawatwae kwa nguvu na kuwafanyia lolote mtakalo. Lakini kwa mtu huyu msimfanyie jambo ovu hivyo.”
Angalia, binti yangu bikira na masuria wake hawa hapa. Ngoja niwalete sasa. Wapuuze na kufanya nao chochote mnachopenda. Lakini msifanyie jambo hili mbaya kwa mtu huyu!”
25 Lakini wale watu hawakumsikia. Hivyo yule mtu akamtoa yule suria wake nje kwa wale watu, nao wakambaka na kumnajisi usiku ule kucha mpaka asubuhi. Kulipoanza kupambazuka wakamwachia aende.
Lakini watu hawakumsikiliza, kwa hiyo huyo mwanamume akamshika yule mwanamke, akamleta nje. Walimkamata, wakambaka, na kumtendea uovu usiku mzima, na asubuhi wakamruhusu aende.
26 Alfajiri yule mwanamke akarudi kwenye ile nyumba bwana wake alikokuwa, akaanguka chini mlangoni, akalala pale hata kulipopambazuka.
Asubuhi mwanamke alikuja akaanguka chini ya mlango wa nyumba ya mtu ambapo bwana wake alikuwa, na yeye akalala pale mpaka kulipokucha.
27 Bwana wake alipoamka asubuhi na kufungua mlango wa nyumba na kutoka nje ili kuendelea na safari yake, tazama, yule suria wake alikuwa ameanguka pale penye ingilio la nyumba na mikono yake ikiwa penye kizingiti cha chini.
Bwana wake akaondoka asubuhi na kufungua milango ya nyumba, akatoka kwenda njiani. Aliweza kumwona mwanamke wake amelala pale mlangoni, mikono yake ikiwa juu ya kizingiti.
28 Akamwambia yule suria, “Inuka, twende.” Lakini hakujibu. Yule bwana akamwinua akampandisha juu ya punda wake, wakaondoka kwenda nyumbani.
Mlawi akamwambia, “Simama twende.” Lakini hakujibiwa. Alimuweka juu ya punda, na huyo mtu akaondoka nyumbani.
29 Alipofika nyumbani, akachukua kisu na kumkatakata yule suria kiungo kwa kiungo, sehemu kumi na mbili, na kuvipeleka hivyo vipande katika sehemu zote za Israeli.
Mlawi alipofika nyumbani kwake, akachukua kisu, naye akamshika suria wake, akamkataa, mguu kwa mguu, akafanya vipande kumi na viwili, akapeleka vipande kila mahali katika Israeli.
30 Kila mtu aliyeona akasema, “Jambo la namna hii halijaonekana wala kutendeka, tangu Israeli walipopanda kutoka Misri. Fikirini juu ya jambo hili! Tafakarini juu ya jambo hili! Tuambieni tufanye nini!”
Wote waliona hili wakasema, “Kitu hicho hakijawahi kufanyika au kuonekana tangu siku ambayo watu wa Israeli walikuja kutoka nchi ya Misri mpaka leo. Fikiria juu ya hili! Tupe ushauri! Tuambie nini cha kufanya!”