< Waamuzi 16 >

1 Siku moja Samsoni alienda Gaza, akamwona mwanamke kahaba, naye akaingia kwake.
Samsoni alikwenda Gaza na akamwona kahaba huko, naye akalala pamoja naye.
2 Watu wa Gaza wakaambiwa, “Samsoni amekuja huku!” Hivyo wakapazingira mahali pale nao wakamvizia usiku kucha, penye lango la mji. Wakanyamaza kimya usiku kucha, wakisema, “Tumvizie hadi mapambazuko, ndipo tutamuua.”
Watu wa Gaza wakaambiwa, “Samsoni amekuja hapa.” Watu wa Gaza wakazunguka mahali hapo kwa siri, wakamngoja usiku wote katika lango la jiji. Walikaa kimya usiku wote. Wakisema, “Hebu tusubiri mpaka mchana, na kisha tumwuue.”
3 Samsoni akalala mpaka usiku wa manane. Akaondoka katikati ya usiku, akashika milango ya lango la mji pamoja na miimo yake miwili, akaingʼoa, makomeo yake na vyote. Akaviweka mabegani mwake na kuvipeleka mpaka kwenye kilele cha mlima ule unaokabili Hebroni.
Samsoni akalala kitandani mpaka usiku wa manane. Usiku wa manane akaamka na akashika mlango wa jiji na miimo yake miwili. Akavivuta kutoka nje, komeo na vyote, akaviweka kwenye mabega yake, akavichukua hadi juu ya kilima, mbele ya Hebroni.
4 Baada ya hayo akampenda mwanamke mmoja katika Bonde la Soreki aliyeitwa Delila.
Baada ya hayo, Samsoni alimpenda mwanamke aliyeishi katika bonde la Soreki. Jina lake alikuwa Delila.
5 Viongozi wa Wafilisti wakamwendea yule mwanamke na kumwambia, “Umbembeleze ili upate kujua siri za nguvu zake zilizo nyingi na jinsi tutakavyoweza kumshinda ili tuweze kumfunga na kumtiisha. Nasi kila mmoja wetu tutakupa shekeli 1,100 za fedha.”
Wale wakuu wa Wafilisti wakamwendea, wakamwambia, “mdanganye Samsoni ili uone mahali zilipo nguvu zake kuu, na kwa namna gani tunaweza kumshinda, ili tumfunge na kumtesa. Fanya hili, na kila mmoja wetu atakupa vipande 1, 100 vya fedha.”
6 Hivyo Delila akamwambia Samsoni, “Naomba niambie siri ya hizi nguvu zako nyingi na jinsi utakavyoweza kufungwa ili kukutiisha.”
Ndipo Delila akamwambia Samsoni, “Tafadhali, niambie ni kwa jinsi gani wewe ni mwenye nguvu sana, na kwa namna gani mtu anaweza kukufunga, ili aweze kukudhibiti?”
7 Samsoni akamjibu, “Kama wakinifunga kwa kamba saba za upinde ambazo hazijakauka bado, hapo ndipo nitakapokuwa dhaifu kama mtu mwingine yeyote.”
Samsoni akamwambia, “Ikiwa watanifunga na kamba saba safi ambazo hazijakauka, nitakuwa dhaifu na kuwa kama mtu mwingine yeyote.”
8 Viongozi wa Wafilisti wakamletea yule mwanamke kamba saba za upinde ambazo hazijakauka bado, akamfunga nazo Samsoni.
Basi wakuu wa Wafilisti wakamletea Delila kamba saba ambazo hazijakauka, naye akamfunga Samsoni.
9 Wakati watu wakiwa wanamvizia katika chumba cha ndani, yule mwanamke akamwambia, “Samsoni, Wafilisti wanakujia!” Lakini yeye akazikata zile kamba za upinde, kama vile uzi wa pamba unapoguswa na moto. Hivyo siri ya nguvu zake haikujulikana.
Sasa alikuwa na watu waliojificha kwa siri, walikaa katika chumba chake cha ndani. Akamwambia, “Wafilisti wako juu yako, Samsoni!” Lakini akazikata kamba kama uzi wakati unapogusa moto. Na hawakujifunza siri ya nguvu zake.
10 Ndipo Delila akamwambia Samsoni, “Umenifanyia mzaha na kuniambia uongo. Tafadhali niambie waweza kufungwa kwa kitu gani?”
Ndipo Delila akamwambia Samsoni, “Ndivyo ulivyonidanganya mimi na kuniambia uongo. Tafadhali, niambie kwa namna gani unaweza kufungwa.”
11 Akamwambia, “Wakinifunga kwa uthabiti kwa kamba mpya ambazo hazijatumika, basi nitakuwa dhaifu kama mtu mwingine yeyote.”
Akamwambia, “Ikiwa watanifunga na kamba mpya ambayo haijawahi kutumika kwa kazi, nitakuwa dhaifu na kama mtu mwingine yeyote.”
12 Hivyo Delila akachukua kamba mpya na kumfunga nazo. Kisha akamwambia, “Samsoni, Wafilisti wanakujia!” Wale watu waliokuwa wanamvizia walikuwa katika chumba cha ndani. Lakini akazikata zile kamba zilizokuwa zimefunga mikono yake kama akatavyo uzi.
Basi Delila alichukua kamba mpya akamfunga pamoja naye, akamwambia, “Wafilisti wako juu yako Samsoni!” Watu waliokuwa wakisubiri walikuwa ndani ya chumba cha ndani. Lakini Samsoni akaondoa kamba kutoka mikono yake kama kilikuwa kipande cha uzi.
13 Ndipo Delila akamwambia Samsoni, “Mpaka sasa, umenifanyia mzaha na kuniambia uongo. Nieleze ni jinsi gani utakavyoweza kufungwa.” Samsoni akamwambia, “Kama ukivisuka hivi vishungi saba vya nywele za kichwa changu katika mtande wa nguo na kukaza kwa msumari, ndipo nitakuwa dhaifu kama mtu mwingine yeyote.” Hivyo Samsoni alipokuwa amelala, Delila akachukua vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake na kuvifunga kwenye mtande wa nguo,
Delila akamwambia Samsoni, “Mpaka sasa umenidanganya na kuniambia uongo. Niambie kwa namna gani unaweza kufungwa.” Samsoni akamwambia, 'Ikiwa utavifuma vifungo saba vya nywele zangu na kuvifunga kwenye kitambaa, kisha kufunga kwenye msumari, nitakuwa kama mtu mwingine yeyote.”
14 na kuvikaza kwa msumari. Kisha akamwambia, “Samsoni, Wafilisti wanakujia!” Lakini akaamka kutoka usingizini na kuungʼoa ule msumari na ule mtande.
Alipokuwa amelala, Dalila akavifuma vifungo saba vya nywele zake akavifunga ndani ya kitambaa na kuzifunga kwenye msumari, akamwambia, “Wafilisti wako juu yako, Samsoni!” Aliamka kutoka usingizini akang'oa kitambaa na pini zilizokuwa zimefungwa.
15 Ndipo Delila akamwambia, “Wawezaje kusema, ‘Nakupenda,’ wakati moyo wako haupo pamoja nami? Umenifanyia mzaha mara hizi tatu na hujaniambia siri ya hizi nguvu zako nyingi.”
Akamwambia, “Wawezaje kusema,” Unanipenda, wakati hushiriki siri zako na mimi? Umenidhihaki mara tatu hizi na hukukuambia ni kwa jinsi gani unazo nguvu nyingi.”
16 Hatimaye, baada ya kuwa anamsumbua kwa maneno siku kwa siku na kumuudhi, roho yake ikataabika hata kufa.
Kila siku alisisitiza kwa bidii na maneno yake, naye akamkemea sana kiasi kwamba alitamani kufa.
17 Hivyo akamwambia yule mwanamke siri yake yote, akamwambia, “Wembe haujapita kamwe kichwani mwangu, kwa kuwa mimi ni Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni mwa mama yangu. Kama nywele za kichwa changu zikinyolewa, nguvu zangu zitanitoka, na nitakuwa dhaifu kama mtu mwingine yeyote!”
Basi Samsoni alimwambia kila kitu, akamwambia, “Wembe haujawahi kukata nywele juu ya kichwa changu, kwa maana nimekuwa Mnaziri kwa Mungu kutoka tumboni mwa mama yangu. Ikiwa kichwa changu kitanyolewa, basi nguvu zangu zitaniacha, nami nitakuwa dhaifu na kuwa kama kila mtu mwingine. '
18 Delila alipoona kuwa amemweleza siri yake yote, akatuma ujumbe kwa viongozi wa Wafilisti na kusema, “Njooni tena mara nyingine, maana amenieleza siri yake yote.” Basi viongozi wa Wafilisti wakaja kwa Delila, wakiwa na fedha mikononi mwao.
Delila alipoona kwamba amemwambia ukweli juu ya kila kitu, akawatuma na kuwaita watawala wa Wafilisti, akisema, “Njooni tena, kwa maana ameniambia kila kitu.” Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamwendea, wakaleta fedha mkononi mwao.
19 Delila akamfanya alale usingizi magotini pake, akamwita mtu akamnyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake. Akaanza kumsumbua ili aamke nazo nguvu zake zikamtoka.
Alimfanya alale katika magoti yake. Alimwita mtu avinyoe vifungo saba vya kichwa chake, naye akaanza kumshinda, kwa maana nguvu zake zilikuwa zimemwacha.
20 Yule mwanamke akamwita, “Samsoni, hao Wafilisti wanakujia!” Akaamka toka usingizini akasema, “Nitatoka nje kama hapo awali, nitawakungʼutia mbali na kuwa huru.” Lakini hakujua kuwa Bwana amemwacha.
Alisema, “Wafilisti wako juu yako, Samsoni!” Aliamka nje ya usingizi wake akasema, “Nitatoka nje kama nyakati nyingine na kujiweka huru.” Lakini hakujua kwamba Bwana amemwacha.
21 Basi Wafilisti wakamkamata, wakamngʼoa macho yake, wakamchukua wakamteremsha mpaka Gaza. Wakiwa wamemfunga kwa pingu za shaba, wakamweka ili asage ngano huko gerezani.
Wafilisti walimkamata na kumng'oa macho. Wakampeleka Gaza na kumfunga kwa shaba. Alikuwa akisaga ngano katika gerezani.
22 Wakati huo nywele za kichwa chake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa.
Lakini nywele juu ya kichwa chake zilianza kukua tena baada ya kunyolewa.
23 Basi viongozi wa Wafilisti wakakusanyika pamoja ili kutoa kafara kwa mungu wao Dagoni na kufanya karamu, wakisema, “Mungu wetu amemtia adui yetu Samsoni mikononi mwetu.”
Watawala wa Wafilisti walikusanyika ili kutoa dhabihu kubwa kwa Dagoni mungu wao, na kufurahi. Walisema, “mungu wetu amemshinda Samsoni, adui yetu, na kumtia katika ufahamu wetu.”
24 Watu walipomwona Samsoni wakamsifu mungu wao, wakisema: “Sasa mungu wetu amemtia adui yetu mikononi mwetu, yule aliyeharibu nchi yetu na kuwaua watu wengi miongoni mwetu.”
Watu walipomwona, walimsifu mungu wao, kwa sababu walisema, “mungu wetu ameshinda adui yetu na kutupa sisi - mharibifu wa nchi yetu, ambaye aliwaua wengi wetu.”
25 Mioyo yao ilipokuwa imefurahishwa wakasema, “Mleteni Samsoni aje acheze ili tufurahi.” Basi wakamleta Samsoni kutoka mle gerezani naye akacheza mbele yao. Wakamweka kati ya nguzo mbili.
Walipokuwa wakisherehekea, wakasema, 'Mwite Samsoni, aje kutufurahisha.' Walimwita Samsoni nje ya jela na akawafanya wacheke. Walimsimamisha katikati ya nguzo.
26 Samsoni akamwambia mtumishi aliyeshika mkono wake, “Niweke mahali ambapo ninaweza kuzigusa nguzo ambazo zinategemeza jengo ili nipate kuziegemea.”
Samsoni akamwambia yule kijana ambaye alikuwa ameshika mkono wake, 'Niruhusu nishike nguzo zilizoshikilia nyumba hii, ili nipate kuegemea.”
27 Basi lile jengo lilikuwa na wingi wa watu waume kwa wake; viongozi wote wa Wafilisti walikuwamo humo, na kwenye sakafu ya juu walikuwepo watu 3,000 waume kwa wake, waliokuwa wakimtazama Samsoni wakati anacheza.
Sasa nyumba ilikuwa imejaa wanaume na wanawake. Watawala wote wa Wafilisti walikuwa huko. Juu ya paa kulikuwa na wanaume na wanawake elfu tatu, ambao walikuwa wakiangalia wakati Samsoni alipokuwa akiwafurahisha.
28 Ndipo Samsoni akamwomba Bwana, akasema, “Ee Bwana Mwenyezi, unikumbuke. Ee Mungu, nakusihi ukanitie nguvu mara hii moja tena, ili kwa tendo hili nipate kulipiza kisasi juu ya Wafilisti kwa ajili ya macho yangu mawili.”
Samsoni akamwita Bwana, akasema, “Bwana MUNGU, nipe nia! Tafadhali niimarishe mara moja tu, Mungu, ili nipate kulipiza kisasi kwa Wafilisti kwa kuchukua macho yangu mawili.
29 Ndipo Samsoni akazikaribia zile nguzo mbili za katikati ambazo lile jengo lilikuwa linazitegemea. Akazishika moja kwa mkono wa kuume na nyingine mkono wa kushoto.
Samsoni aliweka nguzo mbili katikati ambzo zinashikilia nyumba hiyo, naye akaegemea juu yake, nguzo moja kwa mkono wake wa kuume, na mwingine kwa kushoto kwake.
30 Samsoni akasema, “Nife pamoja na Wafilisti!” Ndipo akazisukuma zile nguzo kwa nguvu zake zote, lile jengo likaanguka juu ya viongozi na watu wote waliokuwamo mle ndani yake. Hivyo akawaua watu wengi wakati wa kufa kwake kuliko siku za uhai wake.
Samsoni akasema, “Na nife pamoja na Wafilisti!” Alipanda kwa nguvu zake na jengo likaanguka juu ya watawala na juu ya watu wote waliokuwa ndani yake. Hivyo waliouawa wakati alikufa walikuwa zaidi ya wale waliouawa wakati wa maisha yake.
31 Basi ndugu zake na jamaa yote ya baba yake wakateremka kwenda kumchukua. Wakampandisha na kumzika kati ya Sora na Eshtaoli kwenye kaburi la Manoa baba yake. Naye Samsoni alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka ishirini.
Kisha ndugu zake na nyumba yote ya baba yake wakashuka. Wakamchukua, wakamrudisha na kumzika kati ya Sora na Eshtaoli katika mahali pa kuzikwa Manoa, baba yake. Samsoni alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka ishirini.

< Waamuzi 16 >