< Yuda 1 >
1 Yuda, mtumwa wa Yesu Kristo na nduguye Yakobo: Kwa wale walioitwa, wapendwa katika Mungu Baba na kuhifadhiwa salama ndani ya Yesu Kristo:
Mimi Yuda, mtumishi wa Yesu Kristo, ndugu yake Yakobo, nawaandikia ninyi mlioitwa na Mungu na ambao mnaishi katika upendo wa Mungu Baba, na katika ulinzi wa Yesu Kristo.
2 Rehema, amani na upendo viwe kwenu kwa wingi.
Nawatakieni huruma, amani na upendo kwa wingi.
3 Wapendwa, ingawa nilikuwa ninatamani sana kuwaandikia kuhusu wokovu ambao tunaushiriki sisi sote, niliona imenipasa kuwaandikia na kuwasihi kwamba mwitetee imani iliyokabidhiwa watakatifu kwa nafasi moja itoshayo.
Ndugu wapenzi, wakati nimo katika jitihada ya kuwaandikieni juu ya ule wokovu tunaoshiriki sote, nimeona lazima ya kuwaandikieni na kuwahimizeni mwendelee kupigana kwa ajili ya imani ambayo Mungu amewajalia watu wake mara moja tu kwa wakati wote.
4 Kwa kuwa kuna watu waliojipenyeza kwa siri katikati yenu, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, waovu, wapotoshao neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi wakimkana yeye aliye Bwana wetu wa pekee, Bwana Yesu Kristo.
Maana watu wasiomcha Mungu wamepata kujiingiza kwa siri miongoni mwetu, watu ambao, kwa faida ya maisha yao mabaya, wanaupotosha ujumbe wa neema ya Mungu wetu na kumkana Yesu Kristo aliye peke yake kiongozi na Bwana wetu. Maandiko Matakatifu yalikwisha bashiri tangu awali hukumu inayowangojea watu hao.
5 Ingawa mmekwisha kujua haya yote, nataka niwakumbushe kuwa Bwana akiisha kuwaokoa watu wake kutoka nchi ya Misri, baadaye aliwaangamiza wale ambao hawakuamini.
Nataka kuwakumbusheni mambo fulani ambayo mmekwisha yajua: kumbukeni jinsi Bwana alivyowaokoa watu wa Israeli na kuwatoa katika nchi ya Misri, lakini baadaye aliwaangamiza wale ambao hawakuamini.
6 Nao malaika ambao hawakulinda nafasi zao, lakini wakayaacha makao yao, hawa amewaweka katika giza, wakiwa wamefungwa kwa minyororo ya milele kwa ajili ya hukumu Siku ile kuu. (aïdios )
Na, malaika ambao hawakuridhika na cheo chao, wakayaacha makao yao ya asili, Mungu amewafunga gizani kwa minyororo ya milele wahukumiwe Siku ile kuu. (aïdios )
7 Vivyo hivyo, Sodoma na Gomora na pia ile miji iliyokuwa kandokando, ambayo kwa jinsi moja na hao, walijifurahisha kwa uasherati na kufuata tamaa za mwili zisizo za asili, waliwekwa wawe mfano kwa kuadhibiwa katika moto wa milele. (aiōnios )
Kumbukeni pia Sodoma na Gomora, na miji ya kandokando yake; wenyeji wake walifanya kama wale malaika; walifanya uzinzi na mambo yaliyo kinyume cha maumbile, wakapewa hukumu ya moto wa milele, iwe onyo kwa watu wote. (aiōnios )
8 Vivyo hivyo, hawa waotao ndoto huutia mwili unajisi, hukataa kuwa chini ya mamlaka na kunena mabaya juu ya wenye mamlaka.
Hivyo ndivyo pia walivyo watu hawa. ndoto zao huwaongoza katika kuichafua miili yao wenyewe, kuyadharau mamlaka ya Mungu na kuvitukana viumbe vitukufu vya huko juu.
9 Lakini hata malaika mkuu Mikaeli alipokuwa anashindana na ibilisi juu ya mwili wa Mose, hakuthubutu kumlaumu, bali alimwambia, “Bwana na akukemee!”
Hata Mikaeli, malaika mkuu, hakufanya hivyo. Katika ule ubishi kati yake na Ibilisi waliobishana juu ya mwili wa Mose, Mikaeli hakuthubutu kumhukumu Ibilisi kwa matusi; ila alisema: “Bwana mwenyewe na akukaripie.”
10 Lakini watu hawa hunena mabaya dhidi ya mambo wasiyoyafahamu. Na katika mambo yale wanayoyafahamu kwa hisia kama wanyama wasio na akili, hayo ndiyo hasa yanayowaharibu.
Lakini watu hawa hutukana chochote wasichokielewa; mambo yaleyale wanayoyajua kwa silika kama vile wanyama wanayoyajua ndiyo yanayowaangamiza.
11 Ole wao! Kwa kuwa wanaifuata njia ya Kaini, wamekimbilia faida katika kosa la Balaamu na kuangamia katika uasi wa Kora.
Ole wao! Watu hao wamefuata mwenendo uleule wa Kaini. Kwa ajili ya fedha, wamejiingiza katika mkosi uleule wa Baalamu. Wameasi kama Kora alivyoasi na wameangamizwa kama yeye alivyoangamizwa.
12 Watu hawa ni dosari katika karamu zenu za upendo, wakila pamoja nanyi bila hofu, wakijilisha pasipo hofu. Wao ni mawingu yasiyokuwa na maji, yakichukuliwa na upepo, miti isiyo na matunda wakati wa mapukutiko, ambayo hunyauka, iliyokufa mara mbili na kungʼolewa kabisa.
Kwa makelele yao yasiyo na adabu, watu hao ni kama madoa machafu katika mikutano yenu ya karamu ya Bwana. Hujipendelea wao wenyewe tu, na wako kama mawingu yanayopeperushwa huko na huko na upepo bila ya kuleta mvua. Wao ni kama miti isiyozaa matunda hata wakati wa majira yake, wamekufa kabisa.
13 Wao ni mawimbi makali ya bahari, yakitoa povu la aibu yao wenyewe, ni nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba waliowekewa milele. (aiōn )
Watu hao ni kama mawimbi makali ya bahari, na matendo yao ya aibu yanaonekana dhahiri kama vile mapovu ya mawimbi. Wao ni kama nyota zinazotangatanga, ambao Mungu amewawekea mahali pao milele katika giza kuu. (aiōn )
14 Enoki, mtu wa saba kuanzia Adamu alitoa unabii kuhusu watu hawa, akisema: “Tazama, Bwana anakuja pamoja na maelfu kwa maelfu ya watakatifu wake,
Henoki, ambaye ni babu wa saba tangu Adamu, alibashiri hivi juu ya watu hawa: “Sikilizeni! Bwana atakuja pamoja na maelfu ya malaika wake watakatifu
15 ili kumhukumu kila mmoja na kuwapatiliza wote wasiomcha Mungu kwa matendo yao yote ya uasi waliyoyatenda, pamoja na maneno yote ya kuchukiza ambayo wenye dhambi wamesema dhidi yake.”
kutoa hukumu juu ya binadamu wote, kuwahukumu wote kwa ajili ya matendo yao yote maovu waliyotenda na kwa ajili ya maneno yote mabaya ambayo watu waovu walimkashifu nayo.”
16 Watu hawa ni wenye kunungʼunika na wenye kutafuta makosa; wao hufuata tamaa zao mbaya, hujisifu kwa maneno makuu kuhusu wao wenyewe na kuwasifu mno watu wenye vyeo kwa ajili ya kujipatia faida.
Watu hawa wananung'unika daima na kuwalaumu watu wengine. Hufuata tamaa zao mbaya, hujigamba na kuwasifu watu wengine mno kusudi wafaulu katika mipango yao.
17 Lakini ninyi wapenzi, kumbukeni yale mitume wa Bwana Yesu Kristo waliyonena zamani.
Lakini ninyi wapenzi wangu, kumbukeni yale mliyoambiwa hapo awali ni mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo.
18 Kwa kuwa waliwaambia, “Siku za mwisho kutakuwa na watu wenye kudhihaki, watakaofuata tamaa zao wenyewe za upotovu.”
Waliwaambieni: “Siku za mwisho zitakapofika, watatokea watu watakaowadhihaki ninyi, watu wafuatao tamaa zao mbaya.”
19 Hawa ndio watu wanaowagawa ninyi, wafuatao tamaa zao za asili, wala hawana Roho.
Hao ndio watu wanaosababisha mafarakano, watu wanaotawaliwa na tamaa zao za kidunia, watu wasio na Roho wa Mungu.
20 Lakini ninyi wapendwa, jijengeni katika imani yenu iliyo takatifu sana tena ombeni katika Roho Mtakatifu.
Lakini ninyi, wapenzi wangu, endeleeni kujijenga kikamilifu katika imani yenu takatifu. Salini kwa nguvu ya Roho Mtakatifu,
21 Jilindeni katika upendo wa Mungu mkitazamia kwa furaha rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo ili awalete katika uzima wa milele. (aiōnios )
na kubaki katika upendo wa Mungu, mkiwa mnamngojea Bwana wetu Yesu Kristo awapeni uzima wa milele kwa huruma yake. (aiōnios )
22 Wahurumieni walio na mashaka;
Muwe na huruma kwa watu walio na mashaka;
23 wengine waokoeni kwa kuwanyakua kutoka kwenye moto; nao wengine wahurumieni mkiwa na hofu, mkichukia hata vazi lenye mawaa na kutiwa unajisi na mwili.
waokoeni kwa kuwanyakua kutoka motoni; na kwa wengine muwe na huruma pamoja na hofu, lakini chukieni hata mavazi yao ambayo yamechafuliwa na tamaa zao mbaya.
24 Kwake yeye awezaye kuwalinda ninyi msianguke na kuwaleta mbele za utukufu wake mkuu bila dosari na kwa furaha ipitayo kiasi:
Kwake yeye awezaye kuwalinda msije mkaanguka, na kuwaleta ninyi bila hatia mpaka mbele ya utukufu wake,
25 kwake yeye Mungu pekee Mwokozi wetu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu, utukufu, ukuu, uweza na mamlaka ni vyake tangu milele, sasa na hata milele! Amen. (aiōn )
kwake yeye aliye peke yake Mungu, Mkombozi wetu, uwe utukufu, ukuu, nguvu na mamlaka kwa njia ya Kristo Bwana wetu, tangu zama zote, sasa na hata milele! Amina. (aiōn )