< Yoshua 1 >

1 Baada ya kifo cha Mose mtumishi wa Bwana, Bwana akamwambia Yoshua mwana wa Nuni, msaidizi wa Mose:
Sasa ilitokea baada ya kufa kwa Musa, mtumishi wa Yahweh, Yahweh alimwambia Yoshua, mwana wa Nuni, msaidizi mkuu wa Musa, kusema,
2 “Mtumishi wangu Mose amekufa. Sasa basi, wewe pamoja na watu wote hawa, jiandaeni kuvuka huu Mto Yordani kuingia nchi ambayo karibu nitawapa wana wa Israeli.
“Musa, mtumishi wangu amekufa. Sasa basi inuka, vuka mto huu wa Yordani, wewe na watu hawa wote, kuingia katika nchi ambayo ninawapa - watu waisraeli.
3 Kila mahali nyayo za miguu yenu zitakapokanyaga nimewapa, kama vile nilivyomwahidi Mose.
Nimewapa ninyi kila sehemu ambapo nyayo za miguu yenu itakanyaga. Nimewapa ninyi, kama nilivyomwahidi Musa.
4 Nchi yenu itaenea kuanzia jangwa hili hadi Lebanoni, tena kuanzia mto mkubwa wa Frati, yaani nchi yote ya Wahiti, hadi Bahari ile Kubwa iliyoko upande wa magharibi.
kuanzia jangwani na Lebanoni, hadi mto mkubwa wa Frati, nchi yote ya Wahiti, na hata Bahari kuu, ambako jua huzama, itakuwa nchi yenu.
5 Hakuna mtu yeyote atakayeweza kushindana na wewe siku zote za maisha yako. Kama vile nilivyokuwa pamoja na Mose, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe, sitakuacha wala sitakupungukia.
Hakuna mtu awaye yote atakayeweza kusimama kinyume chako siku zote za maisha yako. Nitakuwa pamoja nawe kama nilivyokuwa na Musa. Sitakupungukia wala kukuacha.
6 “Uwe hodari na shujaa, kwa sababu wewe ndiwe utakayewaongoza watu hawa kuirithi nchi niliyowaapia baba zao kuwapa.
Uwe hodari na jasiri. Wewe utawafanya watu hawa wairithi nchi ambayo niliwaahidi baba zao kuwa ningewapa.
7 Uwe hodari na uwe na ushujaa mwingi. Uwe na bidii kutii sheria yote aliyokupa Mose mtumishi wangu, usiiache kwa kugeuka kuelekea kuume au kushoto, ili upate kufanikiwa popote uendako.
Uwe hodari na jasiri sana. uwe makini kutii sheria zote ambazo Musa mtumishi wangu alikuagiza. Usikengeuke upande wa kulia au wa kushoto, ili uweze kufanikiwa kila mahali utakapoenda.
8 Usiache Kitabu hiki cha Sheria kiondoke kinywani mwako; yatafakari maneno yake usiku na mchana, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapofanikiwa na kisha utastawi.
Siku zote uuongee juu ya kitabu hiki cha sheria. Utakitafakari mchana na usiku ili kwamba uweze kutii yote yaliyoandikwa humo. Kisha utastawi na kufanikiwa.
9 Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakuwa pamoja nawe kokote uendako.”
Je si mimi niliyekuagiza? Uwe hadori na jasiri! Usiogope. Usivunjike moyo. Yahweh Mungu wako yuko pamoja nawe kila uendeko.
10 Ndipo Yoshua akawaagiza maafisa wa watu akisema,
Kisha Yoshua akawaagiza viongozi wa watu,
11 “Pitieni katika kambi yote mkawaambie watu, ‘Wekeni tayari mahitaji yenu. Siku tatu kuanzia sasa mtavuka hii Yordani ili kuingia na kuimiliki nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa iwe yenu wenyewe.’”
“Nendeni katika kambi na waagizeni watu, 'andaeni chakula kwa ajili yenu. Baada ya siku tatu mtavuka mto huu wa Yordani na kuingia ndani na kuimiliki nchi ambayo Yahweh Mungu wenu awapeni ninyi ili kuimiliki.””
12 Lakini kwa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase, Yoshua akasema,
Yoshua akawaambia Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase,
13 “Kumbukeni agizo lile Mose mtumishi wa Bwana alilowapa: ‘Bwana Mungu wenu anawapa ninyi raha, naye amewapa nchi hii.’
“Kumbukeni maneno ambayo Musa, mtumishi wa Yahweh, aliwaaagiza aliposema, 'Yahweh Mungu wenu awapeni ninyi pumziko, naye awapeni ninyi nchi hii.'
14 Wake zenu, watoto wenu na mifugo yenu watakaa katika nchi ile Mose aliyowapa mashariki ya Yordani, lakini mashujaa wenu wote, wakiwa wamevikwa silaha kikamilifu lazima wavuke mbele ya ndugu zenu. Imewapasa kuwasaidia ndugu zenu hadi
Wake zenu, na watoto wenu na mifugo yenu itakaa katika nchi ambayo Musa aliwapa ninyi ng'ambo ya Yordani. Lakini watu wenu wa vita wataenda pamoja na ndugu zao na kuwasaidia.
15 Bwana awape nao raha, kama alivyokwisha kufanya kwa ajili yenu hadi wao pia watakapokuwa wamemiliki nchi ile Bwana Mungu wenu anayowapa. Baada ya hilo, mwaweza kurudi na kukalia nchi yenu wenyewe, ambayo Mose mtumishi wa Bwana aliwapa mashariki mwa Yordani kuelekea linakochomoza jua.”
Mpaka hapo Yahweh atakapowapa ndugu zenu pumziko kama alivyowapa ninyi. Na wao pia watamiliki nchi ambayo Yahweh Mungu wenu awapeni ninyi. Kisha mtarudi katika nchi yenu na kuimiliki, nchi ambayo Musa mtumishi wa Yahweh aliwapa ninyi ng'ambo ya Yordani, mahali pa mapambazuko ya jua.”
16 Ndipo wakamjibu Yoshua, “Chochote ambacho umetuagiza tutafanya na popote utakapotutuma tutakwenda.
Nao wakamjibu Yoshua, na kusema, “Mambo yote uliyotuagiza tutayafanya, na kila mahali utakapotutuma tutaenda.
17 Kama vile tulivyomtii Mose kikamilifu, ndivyo tutakavyokutii wewe. Bwana Mungu wako na awe pamoja nawe tu kama vile alivyokuwa pamoja na Mose.
Tutakutii kama tulivyomtii Musa. Yahweh Mungu wako na awe pamoja nawe tu kama aliyokuwa pamoja na Musa.
18 Yeyote atakayeasi neno lako na kuacha kuyatii maneno yako, au chochote utakachowaamuru, atauawa. Uwe imara na hodari tu!”
Yeyote anayeasi maagizo yako na kutotii maneno yako atauawa. Uwe hodari na jasiri tu.

< Yoshua 1 >