< Yoshua 7 >
1 Lakini Waisraeli hawakuwa waaminifu kuhusu vile vitu vilivyowekwa wakfu; Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, alivichukua baadhi ya hivyo vitu. Hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya Israeli.
Lakini watu wa Israeli hawakutenda katika uaminifu kuhusiana na vitu vilivyotengwa kwa ajili ya uharibifu. Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, kutoka katika kabila la Yuda, alivitwaa baadhi ya vitu hivyo vilivyokuwa vimetengwa kwa ajili ya uharibifu, na hasira ya Yahweh iliwaka juu yawatu wa Israeli.
2 Basi Yoshua akatuma watu kutoka Yeriko waende Ai, karibu na Beth-Aveni mashariki ya Betheli, akawaambia, “Pandeni mkaipeleleze nchi.” Basi wale watu wakapanda wakaipeleleza Ai.
Yoshua alituma watu kutoka Yeriko kwenda Ai, mji uliokuwa karibu na Bethi Aveni, mashariki mwa Betheli. Aliwaambia, “Nendeni na mkaipeleleza nchi.” Wale watu walikwea na kuipeleleza Ai.
3 Waliporudi kwa Yoshua, wakasema, “Si lazima watu wote waende kupigana na Ai. Watume watu elfu mbili au tatu wakauteke huo mji. Usiwachoshe watu wote, kwa sababu huko kuna watu wachache tu.”
Waliporudi kwa Yoshua, walimwambia, “Usitume watu wote kwenda Ai. Tuma tu watu elfu mbili au elfu tatu waende kuiteka Ai. Usiwafanye watu wateseke katika vita, kwani ni watu wachache.”
4 Basi wakapanda kama watu elfu tatu tu, lakini wakashambuliwa na watu wa Ai,
Hivyo ni watu wapatao elfu tatu tu kutoka katika jeshi ndio walioenda, lakini watu hawa waliwakimbia watu wa Ai.
5 ambao waliwaua watu kama thelathini na sita miongoni mwao. Wakawafukuza Waisraeli kutoka lango la mji hadi Shebarimu, nao wakawauwa huko kwenye materemko. Kutokana na hili mioyo ya watu ikayeyuka ikawa kama maji.
Watu wa Ai waliwaua watu wapatao thelathini na sita, waliwafuata katika lango la mji hadi katika machimbo ya mawe, na waliwauwa walipokuwa wakishuka katika kilima. Na mioyo ya watu ilijawa hofu na ujasiri wao ukawatoka.
6 Ndipo Yoshua akayararua mavazi yake, akaanguka kifudifudi mbele ya Sanduku la Bwana, na akabakia hapo mpaka jioni. Wazee wa Israeli nao wakafanya vivyo hivyo wakatia mavumbi vichwani mwao.
Basi Yoshua alizirarua nguo zake. Yeye pamoja na wazewe wa Israeli waliweka mavumbi juu ya vichwa vyao na wakainamisha vichwa vyao hadi katika nchi mbele ya sanduku la Yahweh, na walibaki pale mpaka jioni.
7 Yoshua akasema, “Ee Bwana Mwenyezi, kwa nini umewavusha watu hawa ngʼambo ya Yordani ili kututia mikononi mwa Waamori watuangamize? Laiti tungeliridhika kukaa ngʼambo ile nyingine ya Yordani!
Kisha Yoshua akasema, “Oo, Yahweh Bwana, kwanini umewavusha watu hawa ng'ambo ya Yordani? Kutuweka katika mikono ya Waamori ili kutuangamiza? ikiwa kama tulifanya maamuzi tofauti na tungekaa katika upande mwingine wa Yordani!
8 Ee Bwana, niseme nini sasa, ikiwa sasa Israeli ameshafukuzwa na adui zake?
Bwana, niseme nini, baada ya Israeli kuwatega migongo maadui zao?
9 Wakanaani na watu wengine wa nchi watasikia habari hii, nao watatuzunguka na kutufutilia jina letu duniani. Utafanya nini basi kwa ajili ya jina lako mwenyewe lililo kuu?”
Kwa kuwa Wakaanani na wenyeji wote wa nchi watakaposikia, watatuzunguka na kuwafanya watu wa nchi kulisahau jina letu. Na utafanya nini kwa ajili ya jina lako kuu?
10 Bwana akamwambia Yoshua, “Simama! Unafanya nini hapo chini kifudifudi?
Yahweh akamwambia Yoshua, “Inuka! kwanini umelala kifudifudi?
11 Israeli ametenda dhambi. Wamekiuka agano langu nililowaamuru kulishika. Wamechukua baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu, wameiba, wamesema uongo, wameviweka pamoja na mali zao.
Israeli imetenda dhambi. Wamevunja agano langu nililowaagiza. Wameiba baadhi ya vitu vilivyokuwa vimetengwa. Wameiba na kisha pia wakaficha dhambi yao kwa kuweka vitu vile walivyochukua miongoni mwa mali zao wenyewe.
12 Ndiyo sababu Waisraeli hawawezi kusimama dhidi ya adui zao. Wanawapa visogo na kukimbia kwa kuwa wanastahili maangamizi. Sitakuwa pamoja nanyi tena mpaka mwangamize kila kitu miongoni mwenu kilichotengwa kwa maangamizi.
Na matokeo yake ni kwamba watu wa Israeli hawataweza kusimama mbele za maadui zao. Walitega migongo yao kwa maadui zao kwasababu wao wenyewe wametengwa kwa ajili ya uharibifu. Sitakuwa pamoja nanyi tena mpaka pale mtakapoteketeza vitu vile vilivyotakiwa kuharibiwa, lakini sasa bado viko miongoni mwenu.
13 “Nenda, ukawatakase watu. Waambie, ‘Jitakaseni mjiandae kwa kesho; kwa sababu hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: Kitu kilichowekwa wakfu kipo katikati yenu, ee Israeli. Hamwezi kusimama dhidi ya adui zenu mpaka mtakapokiondoa.
Inuka! Waweke watu wakfu kwangu, na uwaambie, 'Jiwekeeni wakfu ninyi wenyewe kesho. Kwa kuwa, Yahweh, Mungu wa Israeli asema hivi, “Kuna vitu vilitengwa ili kuteketezwa ambavyo bado viko miongoni mwenu, Israeli. Hamtaweza kusimama mbele ya maadui zenu mpaka pale mtakapoviondoa miongoni mwenu vitu vyote ambavyo vilitengwa kwa ajili ya kuteketezwa.”
14 “‘Asubuhi, mjihudhurishe kabila kwa kabila. Itakuwa kabila lile atakalolitwaa Bwana litakuja mbele ukoo kwa ukoo, ukoo ule atakaoutwaa Bwana utakuja mbele jamaa kwa jamaa, nayo jamaa ile atakayoitwaa Bwana itakuja mbele mtu kwa mtu.
Asubuhi, mtajisogeza wenyewe kwa makabila. Kabila lile ambalo Yahweh atalichagua litasogea karibu kwa koo zake. Ukoo ule ambao Yahweh atauchagua lazima usogee karibu kwa nyumba. Nyumba ambayo Yahweh ataichagua lazima isogee karibu kwa mtu mmoja mmoja.
15 Yule atakayekutwa na vitu vilivyowekwa wakfu, atateketezwa kwa moto, pamoja na vitu vyote alivyo navyo. Kwa kuwa amelivunja agano la Bwana na kufanya kitu cha aibu katika Israeli!’”
Itakuwa hivi mtu yule atakayechaguliwa na aliye navyo vitu hivyo vilivyotengwa kwa ajili ya kuharibiwa, atachomwa moto, yeye na kila kitu alichonacho, kwasababu amelivunja agano la Yahweh na kwasababu amefanya jambo la aibu katika Israeli.'”
16 Kesho yake asubuhi na mapema Yoshua akawaamuru Israeli kuja mbele kabila kwa kabila; na Yuda akatwaliwa.
Basi, Yoshua aliamka asubuhi na mapema na aliwaleta Israeli karibu, kabila kwa kabila, na kabila la Yuda lilichaguliwa.
17 Koo za Yuda zikaja mbele, naye akawatwaa Wazera. Akaamuru ukoo wa Wazera kuja mbele jamaa kwa jamaa, nayo jamaa ya Zabdi ikatwaliwa.
Yoshua akazisogeza koo za Yuda karibu, na ukoo wa Zera ulichaguliwa. Akausogeza karibu ukoo wa Zera mtu kwa mtu, na Zabdi alichaguliwa.
18 Yoshua akaamuru watu wa jamaa ya Zabdi kuja mbele mtu kwa mtu, naye Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, akatwaliwa.
Akaisogeza karibu nyumba ya Zabdi mtu kwa mtu, na Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, kutoka kabila la Yuda, alichaguliwa.
19 Ndipo Yoshua akamwambia Akani, “Mwanangu, mtukuze Bwana, Mungu wa Israeli, nawe ukiri kwake. Niambie ni nini ulichotenda; usinifiche.”
Kisha Yoshua akamwambia Akani, “Mwanangu, niambie ukweli mbele za Yahweh, Mungu wa Israel, na ufanye ukiri wako kwake. Tafadhali niambie kile ulichofanya. Usinifiche.”
20 Akani akamjibu Yoshua, “Ni kweli! Nimetenda dhambi dhidi ya Bwana, Mungu wa Israeli. Hili ndilo nililofanya:
Akani akamjibu Yoshua, “Kwa kweli nimetenda dhambi mbele Yahweh, Mungu wa Israeli.
21 Nilipoona katika nyara joho zuri la kutoka Babeli, shekeli mia mbili za fedha, na kabari ya dhahabu ya uzito wa shekeli hamsini, nikavitamani na nikavichukua. Tazama, vimefichwa ardhini ndani ya hema langu, pamoja na hiyo fedha chini yake.”
Nilichofanya ni hiki: Nilipoona miongoni mwa nyara mkoti mzuri kutoka Babeli, shekeli mia mbili za fedha, na kipande cha dhahabu chenye uzito wa shekeli hamsini, nilivitamani na nikavichukua. Vimefichwa chini ardhini katikati ya hema langu, na fedha iko chini yake.”
22 Kwa hiyo Yoshua akatuma wajumbe, nao wakapiga mbio mpaka hemani, tazama, vile vitu vilikuwa vimefichwa hemani mwake, pamoja na ile fedha chini yake.
Yoshua akatuma wajumbe waliokimbia mpaka kwenye hema mahali palipokuwa na vile vitu. Walipoangalia, waliviona vimefichwa katika hema lake, na fedha chini yake.
23 Wakavichukua vile vitu toka mle hemani, wakamletea Yoshua pamoja na Waisraeli wote, na wakavitandaza mbele za Bwana.
Walivichukua vitu hivyo kutoka katikati ya hema na kuvileta kwa Yoshua na watu wote wa Israeli. Walivimwaga mbele za Yahweh.
24 Basi Yoshua, pamoja na Israeli yote, wakamchukua Akani mwana wa Zera, pamoja na ile fedha, lile joho, ile kabari ya dhahabu, wanawe na binti zake, ngʼombe, punda na kondoo wake, hema yake pamoja na vitu vyote alivyokuwa navyo, wakavileta katika Bonde la Akori.
Kisha Yoshua na Waisraeli wote pamoja naye, walimchukua Akani mwana wa Zera, na fedha, na koti, na kipande cha dhahabu, wana na binti zake, ng'ombe zake, punda zake, kondoo zake, hema lake, na kila kitu alichokuwa nacho, na wakavileta hata bonde la Akori.
25 Yoshua akasema, “Kwa nini umeleta taabu hii juu yetu? Bwana ataleta taabu juu yako leo hii.” Ndipo Israeli yote ikampiga Akani kwa mawe, na baada ya kuwapiga jamaa yake yote kwa mawe, wakawateketeza kwa moto.
Kisha Yoshua akasema, “Kwanini umetusumbua? Leo Yahweh atakutesa na wewe.” Waisraeli wote wakampiga kwa mawe. Na wakawachoma wote kwa moto, na wakawapiga mawe.
26 Wakakusanya lundo la mawe juu ya Akani, ambalo lipo mpaka leo. Naye Bwana akageuka kutoka hasira yake kali. Kwa hiyo mahali pale pakaitwa Bonde la Akori tangu siku hiyo.
Kisha wakaweka juu yake kichuguu kikubwa cha mawe ambayo yapo hata leo. Yahweh akaachilia mbali hasira yake. Hivyo basi, jina la mahali hapo likawa Akori hata leo.