< Yoshua 5 >

1 Basi wafalme wote wa Waamori magharibi ya Yordani na wafalme wote wa Kanaani waliokuwa kwenye pwani waliposikia jinsi Bwana alivyoukausha Mto Yordani mbele ya Waisraeli hata tulipokwisha kuvuka, mioyo yao ikayeyuka kwa hofu, wala hawakuwa na ujasiri kuwakabili Waisraeli.
Mara tu waliposikia wafalme wa Waamori walio upande wa magharibi wa Yordani, na wafalme wote wa Wakanaani waliokuwa katika pwani ya Ziwa kuu, waliposikia ya kwamba Yahweh alikuwa ameyakausha maji ya Yordani mpaka pale waisraeli wote walipomaliza kuvuka, mioyo yao ikayeyuka, na hapakuwa na moyo wowote ndani yao kwa sababu ya watu wa Israeli.
2 Wakati huo Bwana akamwambia Yoshua, “Tengeneza visu vya mawe magumu sana na uwatahiri Waisraeli tena.”
Kwa wakati huo Yahweh alimwambia Yoshua, “Tengenezeni visu vya mawe na mara moja mwatahiri wanaume wote wa Israeli.”
3 Kwa hiyo Yoshua akatengeneza visu vya mawe magumu sana na kutahiri Waisraeli huko Gibeath-Haaralothi.
Kisha Yoshua alijifanyia visu vya mawe na akawatahiri wanaume wote wa Gibea Haaraloti.
4 Hii ndiyo sababu ya Yoshua kufanya hivyo: Wanaume wote waliotoka Misri, wote wenye umri wa kwenda vitani, walikufa jangwani wakiwa njiani baada ya kuondoka Misri.
Na hii ndo sababu ya Yoshua kuwatahiri; wanaume wote waliotoka Misri, pamoja na wanaume wa vita walikuwa wamekwisha kufa njiani katika nyikani, baada ya kukwea kutoka Misri.
5 Watu wote waliotoka Misri walikuwa wametahiriwa, lakini watu wote waliozaliwa jangwani wakiwa safarini toka Misri walikuwa hawajatahiriwa.
Ingawa wanaume wote waliotoka Misri walikuwa wametahiriwa, bado hapakuwa na kijana yeyote aliyekuwa ametahiriwa kati ya vijana wote waliozaliwa nyikani katika njia ya kutoka Misri.
6 Waisraeli walitembea jangwani miaka arobaini mpaka wanaume wote wale waliokuwa na umri wa kwenda vitani wakati waliondoka Misri walipokwisha kufa, kwa kuwa hawakumtii Bwana. Kwa maana Bwana alikuwa amewaapia kuwa wasingeweza kuona nchi ambayo alikuwa amewaahidi baba zao katika kuapa kutupatia, nchi inayotiririka maziwa na asali.
Kwasababu watu wa Israeli walitembea nyikani miaka arobaini, mpaka watu wa vita, yaani wanaume wote waliotoka Misri walikufa, kwasababu hawakuitii sauti ya Yahweh. Yahweh aliwaapia kwamba hawataruhusu kuiona nchi ambayo aliwaapia mababa zao kwamba angetupatia sisi, nchi inayotiririka maziwa na asali.
7 Kwa hiyo akawainua wana wao baada yao na hawa ndio hao ambao Yoshua aliwatahiri. Walikuwa hawajatahiriwa bado kwa sababu walikuwa safarini.
Na badala yao, Yahweh aliwainua watoto wao kuchukua nafasi zao ambao Yoshua aliwatahiri, kwasababu walikuwa bado hajatahiriwa njiani.
8 Baada ya taifa lote kutahiriwa, waliendelea kukaa kambini mpaka walipokuwa wamepona.
Walipokwisha kutahiriwa wote, walibaki mahali walipokuwa katika kambi mpaka walipopona.
9 Bwana akamwambia Yoshua, “Leo nimeiondoa aibu ya Wamisri kutoka kwenu.” Basi mahali pale pakaitwa Gilgali hadi leo.
Na Yahweh akasema na Yoshua, “Siku hii nimeiondoa kwenu aibu ya Misri.” Hivyo, mahali pale paliitwa Gilgali hadi leo.
10 Jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi, wakiwa kambini huko Gilgali katika tambarare za Yeriko, Waisraeli wakaadhimisha Pasaka.
Watu wa Israeli walipiga kambi hapo Gilgali. Waliitunza Pasaka katika siku ya kumi na nne ya mwezi, wakati wa jioni, katika uwanda wa Yeriko.
11 Siku iliyofuata Pasaka, katika siku ile ile, wakala mazao ya nchi, mikate isiyotiwa chachu na nafaka za kukaanga.
Na siku iliyofuata baada ya Pasaka, walikula sehemu ya mazao ya nchi, mikate isiyotiwa chachu na nafaka iliyokaangwa katika siku hiyo iyo.
12 Mana ilikoma siku iliyofuata baada ya Waisraeli kula chakula kilichotoka katika nchi; hapakuwa na mana tena kwa ajili ya Waisraeli, ila mwaka huo walikula mazao ya nchi ya Kanaani.
Mana zilikoma siku ile walipokula mazao ya nchi. Hapakuwa tena na mana kwa watu wa Israeli, bali walikula mazao ya nchi ya Kanaani mwaka huo.
13 Basi wakati Yoshua alipokuwa karibu na Yeriko, akainua macho, akaona mtu aliyesimama mbele yake, akiwa na upanga mkononi uliofutwa kwenye ala. Yoshua akamwendea na kumuuliza, “Je, wewe uko upande wetu au upande wa adui zetu?”
Wakati Yoshua alipokaribia Yeriko, aliinua macho na kuangalia, na tazama, mtu alikuwa amesimama mbele yake, alikuwa amechomoa upanga wake na ulikuwa mkononi mwake. Yoshua alimwendea na kumwambia, “Je uko kwa ajili yetu au kwa ajli ya maadui zetu?”
14 Akajibu, “La, siko upande wowote, lakini mimi nimekuja nikiwa jemadari wa jeshi la Bwana.” Yoshua akaanguka kifudifudi hadi chini, akasujudu, akamuuliza, “Je, Bwana, una ujumbe gani kwa mtumishi wako?”
Akajibu, la hasha. Maana mimi ni amiri wa jeshi la Yahweh. Sasa nimekuja. Kisha Yoshua akainamisha uso wake juu ya nchi akaabudu na akamwambia, “Bwana wangu anasema nini kwa mtumwa wake?”
15 Jemadari wa jeshi la Bwana akajibu, “Vua viatu vyako, kwa maana mahali hapa unaposimama ni patakatifu.” Naye Yoshua akafanya hivyo.
Amiri wa jeshi la Yahweh akamwambia Musa, “Vua viatu vyako miguuni mwako, kwasababu sehemu uliyosimama ni takatifu.” Na Yoshua akafanya hivyo.

< Yoshua 5 >