< Yoshua 3 >

1 Yoshua na Waisraeli wote wakaondoka asubuhi na mapema kutoka Shitimu, wakaenda mpaka Mto Yordani, ambako walipiga kambi kabla ya kuvuka.
Yoshua aliamka asubuhi na mapema, nao walisafiri kutoka Shitimu. Walifika Yordani, yeye na watu wote wa Israeli, na wakapiga kambi hapo kabla hawajavuka ng'ambo.
2 Baada ya siku tatu maafisa wakapita katika kambi yote,
Baada ya siku tatu, maafisa walienda katika kambi, wakawaagiza watu,
3 wakitoa maagizo kwa watu, wakiwaambia: “Mtakapoona Sanduku la Agano la Bwana Mungu wenu, likichukuliwa na Walawi ambao ndio makuhani, mtaondoka hapo mlipo na kulifuata.
“Mtakapoona sanduku la agano la Yahweh Mungu wenu, na makuhani kutoka miongoni mwa Walawi wamelibeba, ni lazima muondoke sehemu hii na kulifuata.
4 Ndipo mtakapotambua njia mtakayoiendea, kwa kuwa hamjawahi kuipita kabla. Lakini msisogee karibu, bali kuwe na umbali wa dhiraa 2,000 kati yenu na Sanduku.”
Lazima kuwe na umbali wa dhiraa elfu moja kati yenu na sanduku. Msilisogelee karibu, ili muweze kuiona njia ya kupitia, kwakuwa hamjawahi kupita njia hii kabla.
5 Ndipo Yoshua akawaambia hao watu, “Jitakaseni, kwa kuwa kesho Bwana atatenda mambo ya kushangaza katikati yenu.”
Yoshua akawaambia watu, “Jitakaseni ninyi wenyewe keso, kwa kuwa Yahweh atafanya maajabu miongoni mwenu.”
6 Yoshua akawaambia makuhani, “Liinueni Sanduku la Agano mkatangulie mbele ya watu.” Hivyo wakaliinua na kutangulia mbele yao.
Kisha Yoshua akawaambia makuhani, “Chukueni sanduku la agano, na kulipitisha mbele za watu.” Hivyo, wakalichukua sanduku la agano na wakaenda mbele za watu.
7 Ndipo Bwana akamwambia Yoshua, “Leo nitaanza kukutukuza machoni pa Israeli yote, ili wapate kujua kuwa niko pamoja nawe kama nilivyokuwa pamoja na Mose.
Yahweh akamwambia Yoshua, “Siku hii nitakufanya kuwa mtu mkubwa katika macho ya Waisraeli wote. Watajua kuwa kama nilivyokuwa na Musa ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe.
8 Uwaambie makuhani wanaochukua Sanduku la Agano, ‘Mnapofika kwenye ukingo wa maji ya Yordani, nendeni mkasimame ndani ya mto.’”
Utawaamuru makuhani ambao hulibeba sanduku la agano, 'Mtakapofika katika ukingo wa maji ya Yordani, ni lazima msimame katika Mto Yordani.'”
9 Yoshua akawaambia Waisraeli, “Njooni hapa msikilize maneno ya Bwana Mungu wenu.
Kisha Yoshu akawaambia watu wa Israeli, “Njooni hapa na msikilize maneno ya Yahweh Mungu wenu.
10 Hivi ndivyo mtakavyojua ya kuwa Mungu aliye hai yupo katikati yenu, na kwamba kwa hakika atawafukuza mbele yenu hao Wakanaani, Wahiti, Wahivi, Waperizi, Wagirgashi, Waamori na Wayebusi.
Kwa hili mtajua kwamba Mungu aliye hai yuko miongoni mwenu na kwamba atawaondosha mbele yenu Wakanaani, Wahiti, Wahivi, Waperizi, Wagrigashi, Waamori na Wayebusi.
11 Tazameni, Sanduku la Agano la Bwana wa dunia yote litaingia ndani ya Mto Yordani likiwa limewatangulia.
Tazama! Sanduku la agano la Bwana wa nchi yote litavuka mbele yenu katika Yordani.
12 Sasa basi, chagueni watu kumi na wawili kutoka makabila ya Israeli, mtu mmoja kutoka kila kabila.
Sasa chagueni wanaume kumi na wawili kutoka katika makabila ya Israeli, mmoja katika kila kabila.
13 Mara tu nyayo za makuhani walichukualo Sanduku la Bwana, Bwana wa dunia yote, zitakapokanyaga ndani ya Mto Yordani, maji hayo yatiririkayo kutoka juu yatatindika na kusimama kama chuguu.”
Wakati nyayo za miguu ya makuhani walichukualo sanduku la Yahweh, Bwana wa nchi yote, zitakapogusa maji ya Yordani, maji ya Yordani yatatindika, na hata maji yatiririkayo kutoka juu yatakoma kutiririka nayo yatasimama kama chuguu.
14 Basi, watu walipovunja kambi ili kuvuka Yordani, makuhani wakiwa wamebeba Sanduku la Agano waliwatangulia.
Hivyo wakati watu walipotoka ili kuvuka Yordani, makuhani waliobeba sanduku la agano waende mbele ya watu.
15 Wakati huu ulikuwa wakati wa mavuno, nao Mto Yordani ulikuwa umefurika hadi kwenye kingo zake. Ilikuwa kawaida ya Yordani kufurika nyakati zote za mavuno. Mara tu makuhani wale waliokuwa wamebeba Sanduku la Agano walipofika mtoni na nyayo zao kuzama ndani ya yale maji,
Mara tu wale walichukuao sanduku wakiisha kufika Yordani, na miguu ya watu wale waliobeba sanduku itakapotiwa katika ukingo wa maji (maana sasa Yordani hujaa hadi katika kingo zake zote katika kipindi chote cha mavuno),
16 maji hayo yaliyotiririka kutoka upande wa juu yaliacha kutiririka yakasimama kama chuguu mbali kabisa nao, kwenye mji ulioitwa Adamu kwenye eneo la Sarethani, wakati yale maji yaliyokuwa yanatiririka kuingia kwenye Bahari ya Araba (yaani Bahari ya Chumvi), yalitindika kabisa. Hivyo watu wakavuka kukabili Yeriko.
maji yote yaliyotiririka kutoka juu yalisimama katika chuguu kimoja. Maji yakakoma kutiririka kutoka katika umbali mrefu. Maji yaliacha kutiririka kutoka Adam, mji ulio karibu na Zarethani, hadi bahari ya Negevu, Bahari ya Chumvi. Na watu walivuka ng'ambo karibu na Yeriko.
17 Wale makuhani waliobeba Sanduku la Agano la Bwana, wakasimama imara mahali pakavu katikati ya Mto Yordani, wakati Waisraeli wote wakiwa wanapita hadi taifa lote likaisha kuvuka mahali pakavu.
Makuhani waliolibeba sanduku la agano la Yahweh walisimama katika nchi kavu katikati ya Yordani mpaka watu wote wa Israeli walipokwisha kuvuka katika nchi kavu.

< Yoshua 3 >