< Yoshua 24 >
1 Ndipo Yoshua akaita pamoja makabila yote ya Israeli huko Shekemu. Akawaita wazee, viongozi, waamuzi na maafisa wa Israeli, nao wakaja mbele za Mungu.
Kisha Yoshua aliyakusanya pamoja makabila yote ya Israeli huko Shekemu na aliwaita wazee wa Israeli, viongozi, waamuzi na maafisa wao, nao wakajihudhurisha mbele za Mungu.
2 Yoshua akawaambia watu wote, “Hili ndilo Bwana, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Hapo zamani baba zenu, pamoja na Tera baba yake Abrahamu na Nahori, waliishi ngʼambo ya Mto nao waliiabudu miungu mingine.
Yoshua akawaambia watu wote, “Hiki ndicho Yahweh, Mungu wa Israeli anachokisema, 'Mababu zenu kwa miaka mingi iliyopita waliishi ng'ambo ya mto Frati - Tera, baba wa Ibrahimu na baba wa Nahori - nao waliabudu miungu mingine.
3 Lakini nilimwondoa baba yenu Abrahamu kutoka nchi hiyo ngʼambo ya Mto, nami nikamwongoza katika nchi yote ya Kanaani, nikampa wazao wengi. Nikampa Isaki,
Lakini nilimchukua baba yenu kutoka ng'ambo ya Frati na nikamwongoza mpaka katika nchi ya Kanaani, na nilimpa watoto wengi kupitia kwa Isaka mwanaye.
4 naye Isaki nikampa Yakobo na Esau. Esau nikampa nchi ya vilima ya Seiri, lakini Yakobo pamoja na wanawe wakashuka Misri.
Na Isaka nikampa Yakobo na Esau. Nilimpa Esau nchi ya milima ya Seiri ili aimiliki, lakini Yakobo na watoto wake walishuka kwenda Misri.
5 “‘Kisha nikawatuma Mose na Aroni, nami nikawapiga Wamisri kwa kile nilichokitenda huko, tena nikawatoa ninyi huko.
Nilimtuma Musa na Haruni, na niliwapiga Wamisri kwa mapigo. Baada ya hapo, niliwatoa ninyi.
6 Nilipowatoa baba zenu Misri, mlifika kwenye bahari, nao Wamisri wakawafuatia baba zenu kwa magari na wapanda farasi mpaka kwenye Bahari ya Shamu.
Niliwatoa baba zenu nje ya nchi ya Misri, nanyi mkafika hata katika bahari. Wamisri waliwafuata kwa magari na wapanda farasi hata katika bahari ya matete.
7 Lakini wakamlilia Bwana wakitaka msaada, naye akaweka giza kati yenu na Wamisri, akaileta bahari juu yao ikawafunika. Ninyi mliona kwa macho yenu wenyewe kile nilichowatendea Wamisri. Kisha mliishi jangwani kwa muda mrefu.
Na baba zenu walipomwita Yahweh, aliweka giza kati yenu na Wamisri. Aliileta bahari ije juu yao na kuwafunika. Mliona yale niliyoyakifanya huko Misri. Kisha mliishi jangwaani kwa muda mrefu.
8 “‘Nikawaleta katika nchi ya Waamori ambao waliishi mashariki mwa Yordani. Wakapigana nanyi, lakini nikawatia mikononi mwenu. Nikawaangamiza mbele yenu nanyi mkaimiliki nchi yao.
Niliwaleta katika nchi wa Waamori, ambao waliishi katika upande mwingine mwa Yordani. Walipigana nanyi, nami niliwatia katika mkono wenu. Mliimiliki nchi yao, nami niliwaangamiza mbele yenu.
9 Wakati Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, alipojiandaa kupigana dhidi ya Israeli, alimwita Balaamu mwana wa Beori apate kuwalaani.
Kisha Balaki mwana wa Zipori, mfalme wa Moabu, aliinuka na kuishambulia Israeli. Alimwita na kumtuma Baalamu mwana wa Beori, ili kuwalaani ninyi.
10 Lakini sikumkubali Balaamu, kwa hiyo aliwabariki tena na tena, nami niliwaokoa toka mkononi mwake.
Lakini sikumsikiliza Balaamu. Kwa hakika, aliwabarikia ninyi. Basi, niliwaokoa na mkono wake.
11 “‘Ndipo mlipovuka Yordani mkafika Yeriko. Raiya wa Yeriko wakapigana nanyi, kama walivyofanya Waamori, Waperizi, Wakanaani, Wahiti, Wagirgashi, Wahivi na Wayebusi, lakini niliwatia mikononi mwenu.
Mlivuka Yordani na mkafika Yeriko. Viongozi wa Yeriko waliinuka wapigane nanyi, pamoja na Waamori, Waperizi, Wakanaani, Wahiti, Wagirgashi, Wahivi na Wayebusi. Niliwapa ninyi ushindi dhidi yao na niliwaweka chini ya mamlaka yenu.
12 Nikatuma manyigu mbele yenu, ambao pia waliwafukuza mbele yenu, hao wafalme wawili wa Waamori. Siyo upanga au upinde wenu wenyewe vilivyowapatia ushindi.
Nilituma manyingu mbele yenu, ambayo yaliwafukuzia mbali na wafalme wawili wa Waamori watoke mbele yenu. Haikutokea kwa sababu ya upanga wenu wala kwa upinde wenu.
13 Hivyo nikawapa ninyi nchi ambayo hamkuitaabikia na miji ambayo hamkuijenga na mnaishi ndani yake na kula toka kwa mashamba ya mizabibu na mizeituni msiyoipanda.’
Niliwapeni ninyi nchi ambayo hamkuifanyia kazi na miji ambayo hamkuijenga, na sasa mnaishi ndani yake. Mnakula matunda ya mizabibu na na mashamba ya mizeituni ambayo hamkuyapanda'.
14 “Sasa basi mcheni Bwana na kumtumikia kwa uaminifu wote. Itupeni mbali miungu ambayo baba zenu waliiabudu huko ngʼambo ya Mto Frati na huko Misri, nanyi mtumikieni Bwana.
Basi sasa mcheni Yahweh na kumwabudu yeye kwa uadilifu na uaminifu wote; jitengeni na miungu ambayo baba zenu waliiabudu ng'ambo ya Frati na katika Misri, na mkamwabudu Yahweh.
15 Lakini msipoona vyema kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia, kama ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ngʼambo Frati, au miungu ya Waamori, ambao mnakaa katika nchi yao. Lakini mimi na nyumba yangu, tutamtumikia Bwana.”
Na kama inaonekana kuwa ni vibaya machoni penu kumwabudu Yahweh, chagueni ninyi katika siku hii ya leo ni nani mtakayemtumikia, kama ni miungu ambayo baba zenu waliiabudu ng'ambo ya Frati, au miungu ya Waamori, ambao ninyi mnakaa ndani ya nchi yao. Lakini kwangu mimi na nyumba yangu, tutumwabudu Yahweh.”
16 Ndipo hao watu wakajibu, “Hili jambo liwe mbali nasi la kumsahau Bwana na kuitumikia miungu mingine!
Watu walijibu na kusema, “Hatutaweza kumwacha Yahweh na kuitumikia miungu mingine,
17 Bwana Mungu wetu mwenyewe ndiye alitutoa sisi na baba zetu akatupandisha kutoka Misri, kutoka nchi ile ya utumwa, na kutenda zile ishara kubwa mbele ya macho yetu. Ndiye aliyetulinda katika safari yetu yote na kutokana na mataifa yote ambayo tulipita katikati yao.
kwa kuwa ni Yahweh Mungu wetu ambaye alitutoa sisi na baba zetu kutoka katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa, na ambaye alifanya hizo ishara kubwa mbele yetu, na ambaye alituhifadhi sisi katika njia zote ambazo sisi tuliziendea, na miongoni mwa mataifa yote ambayo tulipita kati kati yake,
18 Bwana akayafukuza mbele yetu mataifa yote pamoja na Waamori, walioishi katika nchi hii. Hivyo sisi nasi tutamtumikia Bwana kwa kuwa yeye ndiye Mungu wetu.”
Na Yahweh aliwaondoa mbele yetu watu wote, na Waamori walioishi katika nchi hii. Hivyo, tutamwabudu Yahweh pia, kwa kuwa ni Mungu wetu”
19 Yoshua akawaambia watu, “Hamwezi kumtumikia Bwana. Yeye ni Mungu Mtakatifu, ni Mungu mwenye wivu. Hatasamehe uasi wenu na dhambi zenu.
Lakini Yoshua akawaambia watu, “Hamwezi kumtumikia Yahweh, kwa kuwa ni Mungu mtakatifu; ni Mungu mwenye wivu; hatawasamehe makosa na dhambi zenu.
20 Ikiwa mkimwacha Bwana na kuitumikia miungu migeni, atageuka na kuwaleteeni maafa na kuwaangamiza, baada ya kuwa mwema kwenu.”
Kama mtamwacha Yahweh na kuabudu miungu ya kigeni, basi atageuka na kuwaharibu. Atawaangamizeni baada ya kuwa amewatendea mema.”
21 Lakini watu wakamwambia Yoshua, “Sivyo! Sisi tutamtumikia Bwana.”
Lakini watu walimwambia Yoshua, “Hapana, tutamwabudu Yahweh.”
22 Ndipo Yoshua akawaambia, “Ninyi mmekuwa mashahidi juu yenu wenyewe kuwa mmechagua kumtumikia Bwana.” Nao wakajibu, “Ndiyo, tu mashahidi.”
Kisha Yoshua akawaambia watu, “Ninyi ni mashahidi dhidi yenu wenyewe kuwa mmemchagua Yahweh ninyi wenyewe, ili mmwabudu yeye.” Watu walijibu, “Sisi ni mashahidi.”
23 Yoshua akawaambia, “Sasa basi, itupeni mbali hiyo miungu migeni iliyo katikati yenu, nanyi mtoleeni Bwana, Mungu wa Israeli, mioyo yenu.”
“Sasa wekeni mbali miungu ya kigeni iliyoko kwenu, na geuzeni moyo wenu umwelekee Yahweh, Mungu wa Israeli.”
24 Nao watu wakamwambia Yoshua, “Tutamtumikia Bwana Mungu wetu na kumtii yeye.”
Watu wakamwambia Yoshua, “Tutamwabudu Yahweh Mungu wetu. Tutaisikiliza sauti yake.
25 Siku ile Yoshua akafanya agano kwa ajili ya watu na hapo Shekemu ndipo alipowaandikia amri na sheria.
Yoshua alifanya agano na watu siku hiyo. Aliziweka maagizo na sheria huko Shekemu.
26 Naye Yoshua akayaandika mambo haya katika Kitabu cha Sheria ya Mungu. Ndipo akalitwaa jiwe kubwa, akalisimamisha huko chini ya mwaloni, karibu na mahali patakatifu pa Bwana.
Yoshua aliyaandika maneno haya katika kitabu cha sheria za Mungu. Alichukua jiwe kubwa na kulisimamisha hapo chini ya mti wa mwaloni uliokuwa karibu na mahali pa takatifu pa Yahweh.
27 Yoshua akawaambia watu wote, “Angalieni! Jiwe hili litakuwa shahidi juu yetu. Limesikia maneno yote Bwana aliyotuambia. Litakuwa shahidi juu yenu kama mtakuwa waongo kwa Mungu wenu.”
Yoshua akawaambia watu, “Tazama, jiwe hili litakuwa ushuhuda dhidi yenu. Limeyasikia maneno yote ambayo Yahweh alitwambia. Hivyo, litakuwa ni shahidi dhidi yenu, hamtakiwi kumkana Mungu wenu.”
28 Basi Yoshua akawatuma watu kila mmoja aende katika urithi wake mwenyewe.
Basi Yoshua aliwaacha watu waende zao, kila mmoja alienda kwenye urithi wake.
29 Baada ya mambo haya, Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Bwana akafa akiwa na umri wa miaka mia moja na kumi.
Baada ya mambo haya, Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Yahweh, alikufa akiwa na miaka 110.
30 Nao wakamzika katika nchi ya urithi wake, huko Timnath-Sera katika nchi ya vilima ya Efraimu, kaskazini ya Mlima wa Gaashi.
Walimzika katika mpaka wa urithi wake mwenyewe huko Timnathi Sera, ambayo iko kwenye nchi ya milima ya Efraimu, upande wa Mlima Gaashi.
31 Israeli wakamtumikia Bwana siku zote za maisha ya Yoshua, na za hao wazee walioishi baada ya Yoshua kufa, ambao waliona kila kitu Bwana alichowatendea Israeli.
Israeli ilimwabudu Yahweh siku zote za maisha ya Yoshua, na siku zote za wazee ambao walidumu pamoja na Yoshua, wale ambao waliona kila kitu ambacho Yahweh alikuwa ameifanyia Israeli.
32 Nayo ile mifupa ya Yosefu, ambayo Waisraeli waliipandisha kutoka huko Misri, wakaizika huko Shekemu kwenye eneo, ambalo Yakobo alilinunua kwa wana wa Hamori baba yake Shekemu, kwa vipande mia vya fedha. Eneo hili likawa ni urithi wa uzao wa Yosefu.
Mifupa ya Yusufu ambayo watu wa Israeli waliileta kutoka Misri, waliizika huko shekemu, katika sehemu ya nchi ambayo Yakobo alikuwa ameinunua kutoka kwa wana wa Hamori, baba wa Shekemu. Aliinunua kwa vipande mia moja vya fedha, na ulikuwa urithi kwa wazawa wa Yusufu.
33 Naye Eleazari mwana wa Aroni akafariki akazikwa huko Gibea, mlima aliokuwa amepewa mtoto wake Finehasi, kwenye nchi ya vilima ya Efraimu.
Eliazeri mwana wa Haruni alikufa pia. Walimzika huko Gibea, katika mji wa ambao alikuwa amepewa Finehasi mwanaye, na ulikuwa katika nchi ya milima ya Efraimu.