< Yoshua 17 >
1 Huu ndio mgawo wa kabila la Manase kama mzaliwa wa kwanza wa Yosefu, yaani kwa ajili ya Makiri, mzaliwa wa kwanza wa Manase. Makiri alikuwa baba wa Wagileadi, ambao walipokea Gileadi na Bashani kwa sababu Wamakiri walikuwa askari wakuu.
2 Kwa hiyo mgawo huu ulikuwa kwa ajili ya watu wa Manase waliokuwa wamebaki, ambao ni koo za Abiezeri, Heleki, Asirieli, Shekemu, Heferi na Shemida. Hawa ndio wanaume wale wengine wa uzao wa Manase mwana wa Yosefu kwa koo zao.
3 Basi Selofehadi mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase hakuwa na wana waume ila mabinti tu, ambao majina yao yalikuwa Mahla, Noa, Hogla, Milka na Tirsa.
4 Wakamwendea kuhani Eleazari, Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi, wakasema: “Bwana alimwagiza Mose atupatie urithi miongoni mwa ndugu zetu.” Kwa hiyo Yoshua akawapa urithi pamoja na ndugu wa baba yao, kufuatana na agizo la Bwana.
5 Fungu la Manase lilikuwa na sehemu kumi za nchi, licha ya Gileadi na Bashani mashariki mwa Yordani,
6 kwa sababu wale binti za kabila la Manase walipokea urithi miongoni mwa wana wa kiume. Nchi ya Gileadi ilikuwa mali ya wazao wa Manase waliobaki.
7 Eneo la Manase lilienea kuanzia Asheri hadi Mikmeta mashariki mwa Shekemu. Mpaka ule ulielekea upande wa kusini kutoka pale kujumuisha watu walioishi En-Tapua.
8 (Nchi ya Tapua ilikuwa mali ya Manase, lakini Tapua yenyewe iliyo mpakani mwa nchi ya Manase ilikuwa ya Waefraimu.)
9 Kisha mpaka ule uliendelea kuelekea kusini hadi Bonde la Kana. Kulikuwepo miji ya Efraimu iliyokuwa miongoni mwa miji ya Manase, lakini mpaka wa Manase ulikuwa upande wa kaskazini wa lile bonde na kuishia kwenye bahari.
10 Nchi ya kusini ilikuwa ya Efraimu, na ile iliyokuwa upande wa kaskazini ilikuwa ya Manase. Eneo la Manase lilifika bahari na ikapakana na Asheri upande wa kaskazini, na Isakari upande wa mashariki.
11 Katika Isakari na Asheri Manase alikuwa na miji pia: Beth-Shani, Ibleamu na watu wa Dori, Endori, Taanaki na Megido, pamoja na vijiji vyote vinavyohusika na miji hiyo (ya tatu katika orodha ni Nafothi).
12 Lakini Wamanase hawakuweza kuimiliki miji hii, kwa kuwa Wakanaani walikazana kuishi katika maeneo hayo.
13 Hata hivyo, Waisraeli walivyoendelea kupata nguvu waliwatumikisha Wakanaani na kuwatia katika kazi za kulazimishwa, lakini hawakuwafukuza kabisa.
14 Watu wa Yosefu wakamwambia Yoshua, “Kwa nini umetupa sisi mgawo mmoja tu na sehemu moja tu kuwa urithi? Sisi tu watu wengi sana, na Bwana ametubariki kwa wingi.”
15 Yoshua akajibu, “Kama ninyi ni wengi sana, na kama nchi ya vilima ya Efraimu ni ndogo sana kwenu, pandeni msituni mkafyeke eneo kwa ajili yenu wenyewe huko kwenye nchi ya Waperizi na Warefai.”
16 Watu wa Yosefu wakajibu, “Hiyo nchi ya vilima haitutoshi, nao Wakanaani wote wanaoishi katika tambarare wanayo magari ya vita ya chuma, wote wa Beth-Shani na miji yake, na wale walio katika Bonde la Yezreeli.”
17 Lakini Yoshua akanena na nyumba ya Yosefu, yaani Efraimu na Manase: “Ninyi ni wengi sana na wenye nguvu sana. Hamtakuwa na mgawo mmoja tu,
18 bali pia nchi hii ya kilima yenye msitu. Ifyekeni, nayo mipaka yake itakuwa yenu umbali mtakaoweza kufika. Ingawa Wakanaani wana magari ya chuma, nao wana nguvu, mwaweza kuwafukuza humo.”