< Yoshua 13 >
1 Yoshua alipokuwa mzee na umri wake ukiwa umesogea sana, Bwana akamwambia, “Wewe ni mzee sana, na bado kumesalia sehemu kubwa sana za nchi ambazo ni za kutwaliwa.
2 “Nchi iliyosalia ni hii: maeneo yote ya Wafilisti na Wageshuri:
3 kutoka Mto Shihori ulioko mashariki mwa Misri, kuelekea kaskazini kwenye eneo la Ekroni, ambayo yote ilihesabika kama ya Wakanaani (maeneo yale matano ya watawala wa Kifilisti, ambayo ni Gaza, Ashdodi, Ashkeloni, Gathi na Ekroni: ndiyo nchi ya Waavi);
4 kuanzia kusini, nchi yote ya Wakanaani, kuanzia Ara ambayo ni ya Wasidoni, ikienea hadi Afeki, na eneo la Waamori,
5 eneo la Wagebali; Lebanoni yote kuelekea mashariki, kuanzia Baal-Gadi chini ya Mlima Hermoni hadi Lebo-Hamathi.
6 “Na kuhusu wakaaji wote katika maeneo ya milima, kuanzia Lebanoni hadi Misrefoth-Maimu, pamoja na eneo lote la Wasidoni, mimi mwenyewe nitawafukuza watoke mbele ya Waisraeli. Hakikisha umegawa nchi hii kwa Israeli kuwa urithi, kama nilivyokuagiza,
7 sasa basi, ligawanye eneo hili kwa yale makabila tisa na ile nusu ya kabila la Manase kuwa urithi.”
8 Ile nusu nyingine ya Manase, Wareubeni na Wagadi, walishapokea urithi Mose aliokuwa amewapa mashariki mwa Yordani, sawasawa na mtumishi wa Bwana alivyowagawia.
9 Eneo lao lilienea toka Aroeri, iliyoko ukingoni mwa Bonde la Arnoni kuanzia mji ulio katikati ya bonde, likijumlisha nchi ya uwanda wa juu wote wa Medeba mpaka Diboni,
10 nayo miji yote ya Sihoni mfalme wa Waamori, aliyetawala Heshboni, hadi mpakani mwa Waamoni.
11 Vilevile ilijumlisha Gileadi, eneo la Wageshuri na Wamaaka, mlima wote wa Hermoni na Bashani yote ikienea hadi Saleka:
12 yaani ufalme wote wa Ogu katika Bashani, aliyekuwa ametawala katika Ashtarothi na Edrei, na ndiye pekee alisalia kwa Warefai. Mose alikuwa amewashinda na kuteka nchi yao.
13 Lakini Waisraeli hawakuwafukuza watu wa Geshuri na wa Maaka, kwa hiyo wanaendelea kuishi miongoni mwa Waisraeli mpaka leo hii.
14 Lakini kwa kabila la Lawi, Mose hakupeana urithi, kwa kuwa sadaka za kuteketezwa kwa moto zilizotolewa kwa Bwana, Mungu wa Israeli, ndizo zilizokuwa urithi wao, kama alivyowaahidi.
15 Haya ndiyo maeneo ambayo Mose alikuwa amewapa kabila la Reubeni ukoo kwa ukoo:
16 Eneo la Aroeri lililo ukingoni mwa Bonde la Arnoni, na kuanzia mji ulio katikati ya bonde, pia uwanda wote wa juu kupita Medeba
17 hadi Heshboni na miji yake yote kwenye uwanda wa juu, ikijumlishwa miji ya Diboni, Bamoth-Baali, Beth-Baal-Meoni,
18 Yahasa, Kedemothi, Mefaathi,
19 Kiriathaimu, Sibma, Sereth-Shahari juu ya kilima kilicho katika bonde,
20 Beth-Peori, materemko ya Pisga na Beth-Yeshimothi:
21 miji yote ya uwanda wa juu na eneo lote la utawala wa Sihoni mfalme wa Waamori, aliyetawala katika Heshboni. Mose alikuwa amemshinda Sihoni, pia watawala wakuu wa Wamidiani, ambao ni Evi, Rekemu, Suri, Huri na Reba, waliokuwa wameungana na Sihoni, ambao waliishi katika nchi ile.
22 Pamoja na wale waliouawa katika vita, Waisraeli walikuwa wamemuua kwa upanga Balaamu mwana wa Beori aliyekuwa mchawi.
23 Mpaka wa Wareubeni ulikuwa ni ukingo wa Mto Yordani. Miji hii na vijiji vyake ndiyo iliyokuwa urithi wa Wareubeni ukoo kwa ukoo.
24 Haya ndiyo maeneo ambayo Mose alikuwa amewapa kabila la Gadi, ukoo kwa ukoo:
25 Nchi ya Yazeri, miji yote ya Gileadi na nusu ya nchi ya Amoni iliyoenea hadi Aroeri, karibu na Raba;
26 na kuanzia Heshboni mpaka Ramath-Mispa na Betonimu, na kutoka Mahanaimu hadi eneo la Debiri;
27 na katika bonde, Beth-Haramu, Beth-Nimra, Sukothi na Safoni na sehemu iliyobaki ya eneo la utawala wa Sihoni mfalme wa Heshboni (upande wa mashariki mwa Mto Yordani, eneo inayoishia kwenye Bahari ya Kinerethi).
28 Miji hii na vijiji vyake ilikuwa urithi wa kabila la Gadi ukoo kwa ukoo.
29 Haya ndiyo maeneo ambayo Mose alikuwa amewapa hiyo nusu ya kabila la Manase, yaani kwa nusu ya jamaa ya uzao wa Manase, ukoo kwa ukoo:
30 Eneo lililoenea kuanzia Mahanaimu, na kujumlisha Bashani yote, ufalme wote wa Ogu mfalme wa Bashani, makazi yote ya Yairi huko Bashani, miji sitini,
31 nusu ya Gileadi, na Ashtarothi na Edrei (miji ya kifalme ya Ogu katika Bashani). Hii ilikuwa kwa ajili ya wazao wa Makiri mwana wa Manase, kwa ajili ya nusu ya wana wa Makiri, ukoo kwa ukoo.
32 Huu ndio urithi alioupeana Mose wakati alipokuwa katika tambarare za Moabu, ngʼambo ya Yordani mashariki mwa Yeriko.
33 Lakini kwa kabila la Walawi, Mose hakuwapa urithi; Bwana Mungu, Mungu wa Israeli ndiye urithi wao, kama alivyowaahidi.