< Yoshua 10 >

1 Baada ya haya Adoni-Sedeki mfalme wa Yerusalemu alisikia kuwa Yoshua alikuwa ameteka mji wa Ai na kuuangamiza kabisa, tena alikuwa ameua mfalme wake, kama alivyofanya huko Yeriko na mfalme wake, tena ya kuwa watu wa Gibeoni walikuwa wamefanya mapatano ya amani na Waisraeli, na walikuwa wakiishi karibu yao.
Ikawa Adonizedeki, mfalme wa Yerusalemu, alisikia kuwa Yoshua ameiteka Ai na ameiteketeza kabisa, kama alivyokwisha kufaya huko Yeriko na mfalme wake. Na alisikia jinsi ambavyo watu wa Gibeoni walivyofanya amani na watu wa Israeli na walikuwa wanaishi miongoni mwao.
2 Yeye na watu wake wakataharuki mno kwa kuwa Gibeoni ulikuwa mji mkubwa kama mmojawapo ya miji ya kifalme; ulikuwa mkubwa kuliko Ai, nao watu wake wote walikuwa mashujaa wa vita.
Watu wa Yerusalemu waliogopa sana kwasababu Gibeoni ulikuwa mji mkubwa, kama mmoja wa miji ya kifalme. Ilikuwa kubwa kuliko Ai, na watu wake wote walikuwa ni mashujaa wenye nguvu.
3 Hivyo Adoni-Sedeki mfalme wa Yerusalemu akaomba msaada kwa Hohamu mfalme wa Hebroni, Piramu mfalme wa Yarmuthi, Yafia mfalme wa Lakishi, na Debiri mfalme wa Egloni.
Hivyo Adonizedeki, mfalme wa Yerusalemu, alituma ujumbe kwa Hohamu, mfalme wa Hebroni, na kwa Piramu, mfalme wa Yarimuthi, na kwaYafia, mfalme wa Lakishi, na kwa Debiri, mfalme wa Eguloni:
4 Akawaambia, “Njooni mnisaidie kuipiga Gibeoni, kwa sababu imefanya mapatano ya amani na Yoshua na Waisraeli.”
“Njooni kwangu na mnisaidie. Tuishambulie Gibeoni kwasababu wamefanya amani na Yoshua pamoja na watu wa Israeli.
5 Ndipo hao wafalme watano wa Waamori, ambao ni wafalme wa Yerusalemu, Hebroni, Yarmuthi, Lakishi na Egloni, wakaunganisha majeshi yao. Wakapanda na vikosi vyao vyote, nao wakajipanga dhidi ya Gibeoni na kuishambulia.
Wafalme watano wa Waamori; mfalme wa Yerusalemu, mfalme wa Hebroni, mfalme wa Yarimuthi, mfalme wa Lakishi, na mfalme wa Eguloni walikwea, wao pamoja na majeshi yao yote. Walipanga sehemu yao kinyume na Wagibeoni na waliwashambulia.
6 Nao Wagibeoni wakatuma ujumbe kwa Yoshua kwenye kambi ya Gilgali na kumwambia, “Usiwatelekeze watumishi wako. Panda haraka uje kwetu kutuokoa! Tusaidie, kwa sababu wafalme wote wa Waamori wakaao kwenye nchi ya vilima wameunganisha majeshi yao pamoja dhidi yetu.”
Watu wa Gibeoni walituma ujumbe kwa Yoshua na kwa jeshi huko Giligali. Walisema, “Upesi! Msiuondoa mkono wenu kutoka kwa watumishi wenu. Kwaeni mje haraka na mtuokoe. Mtusaide, maana wafalme wote wa Waamori wanaoishi katika nchi ya milima wamekusanyika kwa pamoja ili watushambulie.
7 Basi Yoshua akaondoka Gilgali pamoja na jeshi lake lote, wakiwepo watu wote mashujaa wa vita.
“Yoshua alipanda kutoka Giligali, yeye na watu wote wa vita pamoja naye, na watu wote wapiganaji.
8 Bwana akamwambia Yoshua, “Usiwaogope watu hao, nimewatia mkononi mwako. Hakuna yeyote atakayeweza kushindana nawe.”
Yahweh akamwambia Yoshua, “Usiwaogope. Nimewatiwa wote katika mkono wako. Hakuna hata mmoja wao atakayeweza kuzuia mashambulizi yako.”
9 Baada ya Yoshua kutembea usiku kucha kutoka Gilgali, akawashambulia ghafula.
Baada ya kutembea usiku kucha kutoka Giligali, ghafla Yoshua aliwafikilia.
10 Bwana akawafadhaisha mbele ya Waisraeli, nao wakawashinda kwa ushindi mkuu huko Gibeoni. Israeli wakawafukuza kuelekea njia iendayo Beth-Horoni wakiwaua mpaka kufikia njia iendayo Azeka na Makeda.
Na Yahweh alichanganya maadui mbele za Israeli - ambao waliwaua mauaji makubwa mno huko Gibeoni, na wale waliowafuata njiani iendayo Bethi Horoni, nao waliuwaua katika njia iendayo Azeka na Makeda.
11 Walipokuwa wakikimbia mbele ya Israeli kwenye barabara iteremkayo kutoka Beth-Horoni hadi Azeka, Bwana akawavumishia mawe makubwa ya mvua kutoka mbinguni, na wengi wao wakauawa na hayo mawe kuliko wale waliouawa kwa upanga wa Waisraeli.
Na walipokuwa wakikimbia mbio kutoka kwa Waisraeli, chini ya mlima kutoka Bethi Horoni, Yahweh alitupa mawe makubwa kutoka mbinguni juu yao wote katika njia iendayo Azeka, nao wakafa. Watu waliouawa kwa mawe walikuwa ni wengi zaidi kuliko wale waliouawa kwa upanga wa watu wa Israeli.
12 Katika siku ile ambayo Bwana aliwapeana Waamori kwa Israeli, Yoshua akanena na Bwana akiwa mbele ya Waisraeli akasema: “Wewe jua, simama juu ya Gibeoni, wewe mwezi, tulia juu ya Bonde la Aiyaloni.”
Kisha Yoshua akamwambia Yahweh katika siku ambayo Yahweh aliwapa watu wa Israeli ushindi dhidi ya Waamori. Hiki ndicho Yoshua alichosema kwa Yahweh mbele ya Israeli. “Jua lisimame katika Gibeoni, na mwezi, usimame katika bonde la Aijaloni.”
13 Hivyo jua likasimama, nao mwezi ukatulia, hadi taifa hilo lilipokwisha kujilipizia kisasi kwa adui wake, kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Yashari. Jua likasimama kimya katikati ya mbingu, likachelewa kuzama muda wa siku moja nzima.
Jua lilisimama, na mwezi ukaacha kwenda mpaka taifa lilipolipiza kisasi dhidi ya maadui zao. Je hili halikuandikwa katika Kitabu cha Yashari? Jua lilikaa katikati ya anga; halilkuzama kwa siku nzima hivi.
14 Haijakuwepo siku nyingine kama hiyo kabla au baada, siku ambayo Bwana alimsikiliza mwanadamu. Hakika Bwana alikuwa akiwapigania Israeli.
Haijawahi kutokea siku nyingine kama hiyo kabla au baada yake, wakati Yahweh alipotii sauti ya mtu. Kwa kuwa Yahweh alikuwa akifanya vita badala ya Israeli.
15 Ndipo Yoshua akarudi kambini huko Gilgali pamoja na Israeli yote.
Yoshua na Israeli yote pamoja naye walirudi kambini huko Giligali.
16 Basi wale wafalme watano wakawa wamekimbia kujificha kwenye pango huko Makeda.
Basi wale wafalme watano walikuwa wametoroka na kujificha wao wenyewe katika pango huko Makeda.
17 Yoshua alipoambiwa kuwa wafalme hao watano wamekutwa wakiwa wamejificha ndani ya pango huko Makeda,
Taarifa zilimfikia Yoshua kusema, “Wafalme watano wamepatikana wamejificha katika pango huko Makeda!”
18 akasema, “Vingirisheni mawe makubwa kwenye mdomo wa hilo pango, tena wekeni walinzi wa kulilinda.
Yoshua akasema, “Viringisheni mawe makubwa katika mlango wa pango na muweke wanajeshi hapo ili kuwalinda.
19 Lakini msiwaache! Wafuatieni adui zenu, washambulieni kutoka nyuma, wala msiwaache wafike kwenye miji yao, kwa kuwa Bwana Mungu wenu amewatia mkononi mwenu.”
Msibaki na kukaa nyie wenyewe. Bali wafuatilieni maadui zenu na kuwashumbulia kutokea kwa nyuma. Msiwaruhusu kuingia katika miji yao, kwa kuwa Yahweh Mungu wenu amewatia katika mkono wenu.”
20 Hivyo Yoshua pamoja na Waisraeli wakawaangamiza kabisa karibu wote, lakini wachache waliosalia walifika kwenye miji yao yenye maboma.
Yoshua na wana Waisraeli walikuwa wamemaliza kuwaua kwa mauaji makubwa sana, mpaka pale walipokuwa wameteketezwa kabisa; watu wachache tu walipona waliotoroka walifika miji ya ngome.
21 Basi jeshi lote likarudi salama kwa Yoshua huko kambini Makeda, na hakuna yeyote aliyetoa neno kinyume cha Waisraeli.
Kisha jeshi lote lilirudi kwa Yoshua likiwa na amani katika kambi huko Makeda. Na hakuna hata mmoja aliyethubutu kusema hata neno moja kinyume na watu wa Israeli.
22 Ndipo Yoshua akasema, “Haya fungueni mdomo wa pango, mniletee hao wafalme watano.”
Kisha Yoshua akasema, “Fungueni mlango wa pango, watoeni nje na waleteni kwangu hawa wafalme watano.”
23 Kwa hiyo wakawatoa hao wafalme watano nje ya pango: wafalme wa Yerusalemu, Hebroni, Yarmuthi, Lakishi na Egloni.
Walifanya kama Yoshua alivyosema. Waliwaleta wafalme watano kutoka katika pango - mfalme wa Yerusalemu, mfalme wa Hebroni, mfalme wa Yarmuthi, mfalme wa Lakishi na mfalme wa Egloni.
24 Walipokuwa wamewaleta hawa wafalme kwa Yoshua, akawaita watu wote wa Israeli, na kuwaambia majemadari wa vita waliokwenda pamoja naye, “Njooni hapa mweke nyayo zenu juu ya shingo za hawa wafalme.” Basi wakaja wakaweka nyayo zao shingoni.
Na walipowaleta wafalme kwa Yoshua, alimwita kila mtu wa Israeli, na aliwaambia maakida wa wanajeshi waliokuwa wameenda vitani pamoja naye “Kanyageni miguu yenu juu ya shingo zao.” Basi walikuja na kukanyaga miguu yao juu ya shingo zao.
25 Yoshua akawaambia, “Msiogope, wala msivunjike moyo. Kuweni hodari na wenye ushujaa. Hili ndilo Bwana atakalowatendea adui zenu wote mnaokwenda kupigana nao.”
Kisha akawaambia, 'Msiogope wala kufadhaika. uwe na moyo mkuu na jasiri. Na hiki ndicho Mungu atakachokifanya kwa maadui wenu wote ambao mtapigana nao'.
26 Ndipo Yoshua akawapiga na kuwaua wale wafalme na kuwatundika juu ya miti mitano, nao wakaachwa wakiningʼinia juu ya ile miti hadi jioni.
Kisha Yoshua akawashambulia na kuwaua wafalme. Aliwatundika wote watano juu ya miti. Waliwatundika juu ya miti hata jioni.
27 Wakati wa kuzama jua Yoshua akaamuru, nao wakawashusha kutoka kwenye ile miti na kuwatupa kwenye lile pango ambalo walikuwa wamejificha. Kwenye mdomo wa lile pango wakaweka mawe makubwa, ambayo yapo hadi leo.
Ilipokuwa jioni, Yoshua alitoa maagizo, nao waliwashusha chini ya miti na kisha wakawatupa katika pango ambalo walikuwa wamejificha wao wenyewe. Waliweka mawe makubwa juu ya mlango wa pango. Mawe hayo yapo pale hadi leo hii.
28 Siku ile Yoshua akateka Makeda. Akamuua kila mmoja katika ule mji, pamoja na mfalme wake kwa upanga. Hakubakiza mtu yeyote. Akamfanyia mfalme wa Makeda kama vile alivyokuwa amemfanyia mfalme wa Yeriko.
Na kwa namna hii, katika siku hiyo Yoshua aliuteka mji wa Makeda na aliwaua watu wote huko kwa upanga, pamoja na mfalme wake. Aliwateketeza wote kabisa pamoja na kila kiumbe hai kilichokuwa huko. Hakuna hata mmoja aliyesalia. Alichomfanyia mfalme wa Makeda ni sawa sawa na kile alichokuwa amemfanyia mfalme wa Yeriko.
29 Ndipo Yoshua akaondoka Makeda akiwa pamoja na Israeli yote mpaka mji wa Libna na kuushambulia.
Yoshua na Israeli wote waliipita Makeda na kufika Libna. Na huko waliingia katika vita dhidi ya Libna.
30 Bwana pia akautia huo mji wa Libna pamoja na mfalme wake mikononi mwa Israeli. Yoshua akaangamiza ule mji na kila mtu aliyekuwa ndani yake kwa upanga. Hakubakiza huko mtu yeyote. Akamfanyia mfalme wa Libna kama alivyokuwa amemfanyia mfalme wa Yeriko.
Yahweh pia aliitia katika mkono wa Israeli pamoja na mfalme wake. Yoshua alishambulia kila kiumbe hai ndani yake kwa upanga. Hakuacha hai hata mtu mmoja. Alichomfanyia mfalme ni sawa sawa na kile alichokuwa amemfanyia mfalme wa Yeriko.
31 Kisha Yoshua akaondoka Libna kwenda Lakishi akiwa pamoja na Israeli yote; wakajipanga dhidi yake na kuushambulia.
Baadaye Yoshua na Israeli wote pamoja naye walipanda kutoka Libna na kwenda Lakishi. Alipiga kambi karibu yake na wakafanya vita dhidi yake.
32 Bwana akautia Lakishi mikononi mwa Israeli, Yoshua akauteka siku ya pili. Yoshua akauangamiza mji na kila kilichokuwa ndani yake kwa upanga, kama tu vile alivyokuwa ameufanyia mji wa Libna.
Yahweh aliitia Lakishi katika mkono wa Israeli. Yoshua aliiteka katika siku ya pili. Alishambulia kwa upanga kilia kiumbe hai kilichokuwa ndani yake, kama vile aliyokuwa amefanya huko Libna.
33 Wakati huo huo, Horamu mfalme wa Gezeri alikuwa amepanda ili kusaidia Lakishi, lakini Yoshua akamshinda pamoja na jeshi lake, hadi hapakubakia mtu yeyote.
Kisha Horamu, mfalme wa Gezeri alikwea ili kuisaida Lakishi. Yoshua alimshambulia yeye na jeshi lake mpaka pale ambapo hapakuwa na mtu hata mmoja aliyesalia.
34 Ndipo Yoshua akaondoka Lakishi kwenda Egloni akiwa pamoja na Israeli yote; wakajipanga dhidi yake na kuushambulia.
Baada ya hapo, Yoshua na Israeli wote walitoka Lakishi na kwenda Egloni. Walipiga kambi karibu yake na kisha wakafanya vita dhidi yake,
35 Wakauteka mji huo siku ile ile, wakaupiga kwa upanga na kumwangamiza kila mmoja aliyekuwa ndani yake, kama vile walivyokuwa wameufanyia Lakishi.
na siku hiyo hiyo wakaiteka. Waliupiga kwa upanga na waliteketeza kila mtu ndani yake kama vile Yoshua alivyofanya huko Lakishi.
36 Kisha Yoshua akapanda kutoka Egloni kwenda Hebroni akiwa pamoja na Israeli yote na kuushambulia.
Kisha Joshua na Israeli wote wakatoka Egloni na kwenda Hebroni. Wakainua vita dhidi yake.
37 Wakauteka mji na kuupiga kwa upanga, pamoja na mfalme wake, vijiji vyake na kila mmoja aliyekuwa ndani yake. Hawakubakiza mtu yeyote. Kama vile huko Egloni, waliuangamiza kabisa pamoja na kila mmoja aliyekuwa ndani yake.
Waliuteka mji na kuwaua kwa upanga watu wote ndani yake pamoja na mfalme wake, kujumuisha na vijiji vyote vilivyoizunguka. Waliteketeza kabisa kila kiumbe hai ndani yake, hawakuacha hata mtu mmoja aliyesalia, ni sawa sawa na vile Yoshua alivyoitenda Egloni. Aliiteketeza kabisa, na kila kiumbe hai ndani yake.
38 Ndipo Yoshua na Israeli wote wakageuka na kuushambulia Debiri.
Baada ya hapo, Yoshua alirudi pamoja na jeshi lote la Israeli pamoja naye, wakasafiri kwenda Debiri na kufanya vita dhidi yake.
39 Wakauteka mji, mfalme wake na vijiji vyake, na kuupiga kwa upanga. Kila mmoja aliyekuwa ndani yake wakamwangamiza kabisa. Hawakubakiza mtu yeyote. Wakaufanyia Debiri na mfalme wake kama vile walivyokuwa wameifanyia miji ya Libna na Hebroni na wafalme wao.
Aliuteka mji na mfalme wake, pamoja na vijiji vyake vya jirani. Waliwaua wote kwa upanga na waliteketeza kila kiumbe hai ndani yake. Joshua hakuacha hata mmoja hai, kama alivyokuwa amefanya kwa Hebroni na mfalme wake, na kama alivyokuwa amefanya kwa Libna na mfalme wake.
40 Hivyo Yoshua akalishinda eneo hilo lote, ikiwa ni pamoja na nchi ya vilima, na Negebu, na sehemu ya magharibi chini ya vilima, materemko ya milima, pamoja na wafalme wake wote. Hakubakiza mtu yeyote. Akaangamiza kabisa kila kitu chenye pumzi, kama vile Bwana, Mungu wa Israeli, alivyokuwa ameamuru.
Yoshua aliishinda nchi yote, nchi ya milima, Negevu, nchi, nchi ya tambarare na nchi ya miteremko. Hakuna hata mfalme moja aliyebaki hai kati ya wafalme wake wote. Kwa kweli aliteketeza kila kiumbe hai, kama ambavyo Yahweh, Mungu wa Israeli alivyomwaagiza.
41 Yoshua akawashinda kuanzia Kadesh-Barnea hadi Gaza na kutoka eneo lote la Gosheni hadi Gibeoni.
Yoshua aliwaua kwa upanga kutoka Kadeshi Barnea hadi Gaza, na nchi yote ya Gosheni hata Gibeoni.
42 Wafalme hawa wote pamoja na nchi zao Yoshua aliwashinda kwa wakati mmoja, kwa sababu Bwana, Mungu wa Israeli, aliwapigania Israeli.
Yoshua aliwateka wafalme wote hawa na nchi zao kwa wakati mmoja, kwasababu Yahweh, Mungu wa Israeli, alipigana kwa ajili ya Israeli.
43 Ndipo Yoshua akarudi pamoja na Israeli yote kwenye kambi huko Gilgali.
Baada ya hayo Yoshua na Waisraeli wote pamoja naye, walirudi katika kambi huko Gilgali.

< Yoshua 10 >