< Yohana 9 >

1 Yesu alipokuwa akipita, akamwona mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa.
Yesu alipokuwa akipita alimwona mtu mmoja, kipofu tangu kuzaliwa.
2 Wanafunzi wake wakamuuliza, “Rabi, ni nani aliyetenda dhambi, ni huyu mtu au wazazi wake hata azaliwe kipofu?”
Basi, wanafunzi wakamwuliza, “Mwalimu! Ni nani aliyetenda dhambi: mtu huyu, ama wazazi wake, hata akazaliwa kipofu?”
3 Yesu akawajibu, “Huyu mtu wala wazazi wake hawakutenda dhambi. Alizaliwa kipofu ili kazi za Mungu zidhihirishwe katika maisha yake.
Yesu akajibu, “Jambo hili halikutukia kwa sababu ya dhambi zake yeye, wala dhambi za wazazi wake; ila alizaliwa kipofu ili nguvu ya Mungu ionekane ikifanya kazi ndani yake.
4 Yanipasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenituma wakati bado ni mchana, kwa kuwa usiku waja ambapo hakuna mtu awezaye kufanya kazi.
Kukiwa bado mchana yatupasa kuendelea kufanya kazi za yule aliyenituma; maana usiku unakuja ambapo mtu hawezi kufanya kazi.
5 Wakati niko ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu.”
Wakati ningali ulimwenguni, mimi ni mwanga wa ulimwengu.”
6 Baada ya kusema haya, akatema mate ardhini, akatengeneza tope kwa mate na kumpaka yule mtu kipofu machoni.
Baada ya kusema hayo, akatema mate chini, akafanyiza tope, akampaka yule kipofu machoni,
7 Kisha akamwambia, “Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu.” (Siloamu maana yake ni aliyetumwa.) Ndipo yule kipofu akaenda, akanawa, naye akarudi akiwa anaona.
akamwambia, “Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu.” (maana ya jina hili ni “aliyetumwa”). Basi, huyo kipofu akaenda, akanawa, kisha akarudi akiwa anaona.
8 Majirani zake na wale wote waliokuwa wamemwona hapo awali akiombaomba wakaanza kuuliza, “Je, huyu si yule aliyekuwa akiketi akiombaomba?”
Basi, jirani zake na wale waliokuwa wanajua kwamba hapo awali alikuwa maskini mwombaji, wakasema, “Je, huyu siye yule maskini aliyekuwa akiketi na kuomba?”
9 Wengine wakasema, “Ndiye.” Wengine wakasema, “Siye, bali wamefanana.” Lakini yeye akawaambia, “Mimi ndiye.”
Baadhi yao wakasema, “Ndiye.” Wengine wakasema, “La! Ila anafanana naye.” Lakini huyo aliyekuwa kipofu akasema, “Ni mimi!”
10 Wakamuuliza, “Basi macho yako yalifumbuliwaje?”
Basi, wakamwuliza, “Sasa, macho yako yalipataje kufumbuliwa?”
11 Yeye akawajibu, “Yule mtu aitwaye Yesu alitengeneza tope, akanipaka machoni mwangu, naye akaniambia nenda ukanawe katika Bwawa la Siloamu, ndipo nikanawa nami nikapata kuona!”
Naye akawajibu, “Yule mtu aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka machoni na kuniambia: Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu. Basi, mimi nikaenda, nikanawa, nikapata kuona.”
12 Wale wakamuuliza, “Yeye huyo mtu yuko wapi?” Akawajibu, “Sijui.”
Wakamwuliza, “Yeye yuko wapi?” Naye akawajibu, “Mimi sijui!”
13 Wakamleta kwa Mafarisayo yule mtu aliyekuwa kipofu hapo awali.
Kisha wakampeleka huyo mtu aliyekuwa kipofu kwa Mafarisayo.
14 Basi siku hiyo Yesu alipotengeneza tope na kuyafungua macho ya huyo mtu ilikuwa Sabato.
Siku hiyo Yesu alipofanya tope na kumfumbua macho mtu huyo, ilikuwa siku ya Sabato.
15 Mafarisayo nao wakaanza kumuuliza alivyopata kuponywa. Naye akawaambia, “Alinipaka tope kwenye macho yangu, nikanawa na sasa ninaona.”
Basi, Mafarisayo wakamwuliza mtu huyo, “Umepataje kuona?” Naye akawaambia, “Alinipaka tope machoni, nami nikanawa na sasa naona.”
16 Baadhi ya Mafarisayo wakasema, “Huyu mtu hatoki kwa Mungu, kwa sababu hashiki Sabato.” Lakini wengine wakasema, “Awezaje mtu mwenye dhambi kufanya miujiza kama hii?” Wakagawanyika.
Baadhi ya Mafarisayo wakasema, “Mtu huyu hakutoka kwa Mungu, maana hashiki sheria ya Sabato.” Lakini wengine wakasema, “Mtu mwenye dhambi awezaje kufanya ishara za namna hii?” Kukawa na mafarakano kati yao.
17 Hivyo wakamwambia tena yule mtu aliyekuwa kipofu, “Wewe ndiwe uliyefumbuliwa macho, wasemaje kuhusu mtu huyo?” Maana macho yako ndiyo yaliyofumbuliwa. Yeye akawajibu, “Yeye ni nabii.”
Wakamwuliza tena huyo mtu aliyekuwa kipofu, “Maadam yeye amekufungua macho, wasemaje juu yake?” Naye akawaambia, “Yeye ni nabii!”
18 Wale Wayahudi hawakuamini ya kuwa mtu huyo alikuwa kipofu, akapata kuona, mpaka walipowaita wazazi wake.
Viongozi wa Wayahudi hawakusadiki kwamba mtu huyo alikuwa kipofu hapo awali na sasa anaona mpaka walipowaita wazazi wake.
19 Wakawauliza, “Je, huyu ni mtoto wenu, ambaye mnasema alizaliwa kipofu? Imekuwaje basi sasa anaona?”
Basi, wakawauliza hao wazazi, “Je, huyu ndiye mtoto wenu ambaye ninyi mwasema alizaliwa kipofu? Sasa amepataje kuona?”
20 Wazazi wake wakajibu, “Tunajua ya kuwa huyu ni mtoto wetu na ya kuwa alizaliwa kipofu.
Wazazi wake wakajibu, “Tunajua kwamba huyu ni mtoto wetu, na kwamba alizaliwa kipofu.
21 Lakini sisi hatujui ni kwa jinsi gani kwamba sasa anaona, wala hatujui ni nani aliyemfungua macho yake. Muulizeni, yeye ni mtu mzima na anaweza kujieleza mwenyewe.”
Lakini amepataje kuona, hatujui; na wala hatumjui yule aliyemfumbua macho. Mwulizeni yeye mwenyewe; yeye ni mtu mzima, anaweza kujitetea mwenyewe.”
22 Wazazi wake walisema hivi kwa sababu waliwaogopa Wayahudi kwani walikuwa wamekubaliana kuwa mtu yeyote atakayemkiri Yesu kuwa ndiye Kristo atafukuzwa kutoka sinagogi.
Wazazi wake walisema hivyo kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi kwani viongozi hao walikuwa wamepatana ya kwamba mtu yeyote atakayekiri kwamba Yesu ni Kristo atafukuzwa nje ya sunagogi.
23 Kwa hiyo wazazi wake wakasema, “Yeye ni mtu mzima. Muulizeni.”
Ndiyo maana wazazi wake walisema: “Yeye ni mtu mzima, mwulizeni.”
24 Hivyo kwa mara ya pili wakamwita yule aliyekuwa kipofu, nao wakamwambia, “Mpe Mungu utukufu! Sisi tunafahamu kuwa mtu huyu aliyekuponya ni mwenye dhambi.”
Basi, wakamwita tena aliyekuwa kipofu, wakamwambia, “Sema ukweli mbele ya Mungu! Sisi tunajua kwamba mtu huyu ni mwenye dhambi.”
25 Akawajibu, “Mimi sijui kama yeye ni mwenye dhambi. Lakini jambo moja ninalojua, nilikuwa kipofu na sasa ninaona.”
Yeye akajibu, “Kama ni mwenye dhambi mimi sijui. Lakini kitu kimoja najua: Nilikuwa kipofu, na sasa naona.”
26 Wakamuuliza, “Alikufanyia nini? Aliyafumbuaje macho yako?”
Basi, wakamwuliza, “Alikufanyia nini? Alikufumbuaje macho yako?”
27 Akawajibu, “Tayari nimekwisha kuwaambia, nanyi hamtaki kunisikiliza. Mbona mnataka kusikia tena? Je, ninyi nanyi mnataka kuwa wanafunzi wake?”
Huyo mtu akawajibu, “Nimekwisha waambieni, nanyi hamkusikiliza; kwa nini mwataka kusikia tena? Je, ninyi pia mnataka kuwa wafuasi wake?”
28 Ndipo wakamtukana na kusema, “Wewe ndiwe mwanafunzi wake, Sisi ni wanafunzi wa Mose.
Lakini wao wakamtukana wakisema, “Wewe ni mfuasi wake; sisi ni wafuasi wa Mose.
29 Tunajua kwamba Mungu alisema na Mose, lakini kwa habari ya mtu huyu hatujui atokako.”
Sisi tunajua kwamba Mungu alisema na Mose, lakini mtu huyu hatujui ametoka wapi!”
30 Yule mtu akawajibu, “Hili ni jambo la ajabu! Hamjui anakotoka, naye amenifungua macho yangu!
Naye akawajibu, “Hili ni jambo la kushangaza! Ninyi hamjui ametoka wapi, lakini amenifumbua macho yangu!
31 Tunajua ya kuwa Mungu hawasikilizi wenye dhambi, lakini huwasikiliza wote wanaomcha na kumtii.
Tunajua kwamba Mungu hawasikilizi watu wenye dhambi, ila humsikiliza yeyote mwenye kumcha na kutimiza mapenzi yake.
32 Tangu zamani hatujasikia kwamba mtu amemponya yeyote aliyezaliwa kipofu. (aiōn g165)
Tangu mwanzo wa ulimwengu haijasikika kwamba mtu ameyafumbua macho ya mtu aliyezaliwa kipofu. (aiōn g165)
33 Kama huyu mtu hakutoka kwa Mungu, asingeweza kufanya lolote.”
Kama mtu huyu hakutoka kwa Mungu, hangeweza kufanya chochote!”
34 Wao wakamjibu, “Wewe ulizaliwa katika dhambi kabisa, nawe unajaribu kutufundisha?” Wakamfukuza atoke nje.
Wao wakamjibu, “Wewe ulizaliwa na kulelewa katika dhambi; unawezaje kutufundisha sisi?” Basi, wakamfukuzia mbali.
35 Yesu aliposikia kuwa wamemfukuzia nje yule mtu aliyemfumbua macho, alimkuta akamuuliza, “Je, unamwamini Mwana wa Adamu?”
Yesu alisikia kwamba walikuwa wamemfukuzia mbali, naye alipomkuta akamwuliza, “Je, wewe unamwamini Mwana wa Mtu?”
36 Yule mtu akamjibu, “Yeye ni nani, Bwana? Niambie ili nipate kumwamini.”
Huyo mtu akajibu, “Mheshimiwa, niambie yeye ni nani, ili nipate kumwamini.”
37 Yesu akamjibu, “Umekwisha kumwona, naye anayezungumza nawe, ndiye.”
Yesu akamwambia, “Umekwisha mwona, naye ndiye anayesema nawe sasa.”
38 Yule mtu akasema, “Bwana, naamini.” Naye akamwabudu.
Basi, huyo mtu akasema, “Ninaamini Bwana!” Akamsujudia.
39 Yesu akasema, “Nimekuja ulimwenguni humu kwa ajili ya kuhukumu, ili wale walio vipofu wapate kuona, nao wale wanaoona, wawe vipofu.”
Yesu akasema, “Mimi nimekuja ulimwenguni kutoa hukumu, kusudi wasioona wapate kuona, na wale wanaoona wawe vipofu.”
40 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa karibu naye wakamsikia na kumwambia, “Je, kweli sisi ni vipofu?”
Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa pamoja naye walisikia maneno hayo, wakamwuliza, “Je, sisi pia ni vipofu?”
41 Yesu akawajibu, “Kama mngekuwa vipofu kweli, msingekuwa na hatia ya dhambi, lakini kwa kuwa mnasema, ‘Tunaona,’ basi mna hatia.
Yesu akawajibu, “Kama mngekuwa vipofu, hamngekuwa na hatia; lakini sasa ninyi mwasema: Sisi tunaona, na hiyo yaonyesha kwamba mna hatia bado.

< Yohana 9 >