< Yohana 5 >

1 Baada ya haya, kulikuwa na Sikukuu ya Wayahudi, naye Yesu akapanda kwenda Yerusalemu.
Baada ya hayo kulikuwa na sikukuu ya Wayahudi, naye Yesu akaenda Yerusalemu.
2 Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao Mlango wa Kondoo, palikuwa na bwawa moja lililoitwa kwa Kiebrania Bethzatha, ambalo lilikuwa limezungukwa na kumbi tano.
Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao Mlango wa Kondoo, kulikuwa na bwawa la maji liitwalo kwa Kiebrania Bethzatha, ambalo lilikuwa na baraza tano zenye matao.
3 Hapa palikuwa na idadi kubwa ya wasiojiweza, yaani, vipofu, viwete, na waliopooza [wakingojea maji yatibuliwe.
Humo barazani mlikuwa na wagonjwa wengi wamekaa: vipofu, viwete na waliopooza. Walikuwa wakingojea maji yatibuliwe,
4 Kwa maana malaika alikuwa akishuka wakati fulani, akayatibua maji. Yule aliyekuwa wa kwanza kuingia ndani baada ya maji kutibuliwa alipona ugonjwa wowote aliokuwa nao].
maana mara kwa mara malaika alishuka majini nyakati fulani na kuyatibua. Mtu yeyote aliyekuwa wa kwanza kuingia majini baada ya maji kutibuliwa, alipona ugonjwa wowote aliokuwa nao.
5 Mtu mmoja alikuwako huko ambaye alikuwa ameugua kwa miaka thelathini na minane.
Basi, hapo palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa mgonjwa kwa muda wa miaka thelathini na minane.
6 Yesu alipomwona akiwa amelala hapo, naye akijua kuwa amekuwa hapo kwa muda mrefu, akamwambia, “Je, wataka kuponywa?”
Naye alipomwona huyo mtu amelala hapo, akatambua kwamba alikuwa amekaa hapo kwa muda mrefu, akamwuliza, “Je, wataka kupona?”
7 Yule mgonjwa akamjibu, “Bwana, mimi sina mtu wa kuniingiza bwawani maji yanapotibuliwa. Nami ninapotaka kutumbukia bwawani, mtu mwingine huingia kabla yangu.”
Naye akajibu, “Mheshimiwa, mimi sina mtu wa kunipeleka majini wakati yanapotibuliwa. Kila nikijaribu kuingia, mtu mwingine hunitangulia.”
8 Yesu akamwambia, “Inuka! Chukua mkeka wako na uende.”
Yesu akamwambia, “Inuka, chukua mkeka wako utembee.”
9 Mara yule mtu akapona, akachukua mkeka wake, akaanza kutembea. Basi siku hiyo ilikuwa siku ya Sabato.
Mara huyo mtu akapona, akachukua mkeka wake, akatembea. Jambo hili lilifanyika siku ya Sabato.
10 Kwa hiyo Wayahudi wakamwambia yule mtu aliyeponywa, “Leo ni Sabato, si halali wewe kubeba mkeka wako.”
Kwa hiyo baadhi ya Wayahudi wakamwambia huyo mtu aliyeponywa, “Leo ni Sabato, si halali kubeba mkeka wako.”
11 Yeye akawajibu, “Yule mtu aliyeniponya aliniambia, ‘Chukua mkeka wako na uende.’”
Lakini yeye akawaambia, “Yule mtu aliyeniponya ndiye aliyeniambia: Chukua mkeka wako, tembea.”
12 Wakamuuliza, “Ni mtu gani huyo aliyekuambia uchukue mkeka wako uende?”
Nao wakamwuliza, “Huyo mtu aliyekwambia: Chukua mkeka wako, tembea, ni nani?”
13 Basi yule mtu aliyeponywa hakufahamu ni nani aliyemponya, kwa sababu Yesu alikuwa amejiondoa katika ule umati wa watu uliokuwa hapo.
Lakini yeye hakumjua huyo mtu aliyemponya, maana Yesu alikuwa amekwisha ondoka mahali hapo, kwani palikuwa na umati mkubwa wa watu.
14 Baadaye Yesu akamkuta yule mtu aliyemponya ndani ya Hekalu na kumwambia, “Tazama umeponywa, usitende dhambi tena. La sivyo, lisije likakupata jambo baya zaidi.”
Basi, baadaye Yesu alimkuta huyo aliyeponywa Hekaluni, akamwambia, “Sasa umepona; usitende dhambi tena, usije ukapatwa na jambo baya zaidi.”
15 Yule mtu akaenda, akawaambia wale Wayahudi kuwa ni Yesu aliyemponya.
Huyo mtu akaenda, akawaambia viongozi wa Wayahudi kwamba Yesu ndiye aliyemponya.
16 Kwa hiyo Wayahudi wakaanza kumsumbua Yesu, kwa sababu alikuwa anafanya mambo kama hayo siku ya Sabato.
Kwa vile Yesu alifanya jambo hilo siku ya Sabato, Wayahudi walianza kumdhulumu.
17 Yesu akawajibu, “Baba yangu anafanya kazi yake daima hata siku hii ya leo, nami pia ninafanya kazi.”
Basi, Yesu akawaambia, “Baba yangu anafanya kazi daima, nami pia nafanya kazi.”
18 Maneno haya yaliwaudhi sana viongozi wa Wayahudi. Wakajaribu kila njia wapate jinsi ya kumuua, kwani si kwamba alivunja Sabato tu, bali alikuwa akimwita Mungu Baba yake, hivyo kujifanya sawa na Mungu.
Kwa sababu ya maneno haya, viongozi wa Wayahudi walizidi kutafuta njia ya kumwua Yesu: si kwa kuwa aliivunja Sheria ya Sabato tu, bali pia kwa kuwa alisema kwamba Mungu ni Baba yake, na hivyo akajifanya sawa na Mungu.
19 Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, Mwana hawezi kufanya jambo lolote peke yake, yeye aweza tu kufanya lile analomwona Baba yake akifanya, kwa maana lolote afanyalo Baba, Mwana pia hufanya vivyo hivyo.
Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, Mwana hawezi kufanya kitu peke yake; anaweza tu kufanya kile anachomwona Baba akikifanya. Maana kile anachofanya Baba, Mwana hukifanya vilevile.
20 Baba ampenda Mwana na kumwonyesha yale ambayo yeye Baba mwenyewe anayafanya, naye atamwonyesha kazi kuu kuliko hizi ili mpate kushangaa.
Baba ampenda Mwana, na humwonyesha kila kitu anachokifanya yeye mwenyewe, tena atamwonyesha mambo makuu kuliko haya, nanyi mtastaajabu.
21 Hakika kama vile Baba awafufuavyo wafu na kuwapa uzima, vivyo hivyo Mwana huwapa uzima wale anaopenda.
Kama vile Baba huwafufua wafu na kuwapa uzima, vivyo hivyo naye Mwana huwapa uzima wale anaopenda.
22 Wala Baba hamhukumu mtu yeyote, lakini hukumu yote amempa Mwana,
Baba hamhukumu mtu yeyote; shughuli yote ya hukumu amemkabidhi Mwana,
23 ili wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Yeyote asiyemheshimu Mwana, hamheshimu Baba aliyemtuma.
ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba ambaye amemtuma.
24 “Amin, amin nawaambia, yeyote anayesikia maneno yangu na kumwamini yeye aliyenituma, anao uzima wa milele, naye hatahukumiwa, bali amepita kutoka mautini, na kuingia uzimani. (aiōnios g166)
“Kweli nawaambieni, anayesikia neno langu, na kumwamini yule aliyenituma, anao uzima wa milele. Hatahukumiwa kamwe, bali amekwisha pita kutoka kifo na kuingia katika uzima. (aiōnios g166)
25 Amin, amin nawaambia, saa yaja, nayo saa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, nao watakaoisikia watakuwa hai.
Kweli nawaambieni, wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo wafu wataisikia sauti ya Mwana wa Mungu, nao watakaoisikia, wataishi.
26 Kama vile Baba alivyo na uzima ndani yake, vivyo hivyo amempa Mwana kuwa na uzima ndani yake.
Kama vile Baba alivyo asili ya uhai, ndivyo pia alivyomjalia Mwanawe kuwa asili ya uhai.
27 Naye amempa Mwanawe mamlaka ya kuhukumu kwa kuwa yeye ni Mwana wa Adamu.
Tena amempa mamlaka ya kuhukumu kwa sababu yeye ni Mwana wa Mtu.
28 “Msishangae kusikia haya, kwa maana saa inakuja ambapo wale walio makaburini wataisikia sauti yake.
Msistaajabie jambo hili; maana wakati unakuja ambapo wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake,
29 Nao watatoka nje, wale waliotenda mema watafufuka wapate uzima na wale waliotenda maovu, watafufuka wahukumiwe.
nao watafufuka: wale waliotenda mema watafufuka na kuishi, na wale waliotenda maovu watafufuka na kuhukumiwa.
30 “Mimi siwezi kufanya jambo lolote peke yangu. Ninavyosikia ndivyo ninavyohukumu, nayo hukumu yangu ni ya haki kwa kuwa sitafuti kufanya mapenzi yangu mwenyewe, bali mapenzi yake yeye aliyenituma.
“Mimi siwezi kufanya kitu kwa uwezo wangu mwenyewe. Mimi nina hukumu kama ninavyosikia kutoka kwa Baba, nayo hukumu yangu ni ya haki. Nia yangu si kufanya nipendavyo mwenyewe, bali apendavyo yule aliyenituma.
31 “Kama ningejishuhudia mimi mwenyewe, ushuhuda wangu si kweli.
Nikijishuhudia mimi mwenyewe, ushahidi wangu hauwezi kukubaliwa kuwa wa kweli.
32 Lakini yuko mwingine anishuhudiaye na ninajua kwamba ushuhuda wake ni wa kweli.
Lakini yuko mwingine ambaye hutoa ushahidi juu yangu, nami najua kwamba yote anayosema juu yangu ni ya kweli.
33 “Mlituma wajumbe kwa Yohana, naye akashuhudia juu ya kweli.
Ninyi mlituma ujumbe kwa Yohane naye aliushuhudia ukweli.
34 Si kwamba naukubali ushuhuda wa mwanadamu, la, bali ninalitaja hili kusudi ninyi mpate kuokolewa.
Si kwamba mimi nautegemea ushahidi wa wanadamu, lakini nasema mambo haya ili mpate kuokolewa.
35 Yohana alikuwa taa iliyowaka na kutoa nuru, nanyi kwa muda mlichagua kuifurahia nuru yake.
Yohane alikuwa kama taa iliyokuwa ikiwaka na kuangaza, nanyi mlikuwa tayari kufurahia mwanga huo kwa kitambo.
36 “Lakini ninao ushuhuda mkuu zaidi kuliko wa Yohana. Kazi zile nizifanyazo, zinashuhudia juu yangu, zile ambazo Baba amenituma nizikamilishe, naam, ishara hizi ninazofanya, zinashuhudia kuwa Baba ndiye alinituma.
Lakini mimi nina ushahidi juu yangu ambao ni mkuu zaidi kuliko ule wa Yohane. Kwa maana kazi ninazofanya, kazi alizonipa Baba nizifanye, ndizo zinazonishuhudia kwamba Baba ndiye aliyenituma.
37 Naye Baba mwenyewe ameshuhudia juu yangu. Hamjapata kamwe kuisikia sauti yake wala kuona umbo lake,
Naye Baba aliyenituma hunishuhudia. Ninyi hamjapata kamwe kusikia sauti yake, wala kuuona uso wake,
38 wala hamna neno lake ndani yenu, kwa sababu hamkumwamini yeye aliyetumwa naye.
na ujumbe wake haukai ndani yenu maana hamkumwamini yule aliyemtuma.
39 Ninyi mnachunguza Maandiko mkidhani ya kuwa ndani yake mna uzima wa milele, maandiko haya ndiyo yanayonishuhudia Mimi. (aiōnios g166)
Ninyi huyachunguza Maandiko Matakatifu mkidhani kwamba ndani yake mtapata uzima wa milele; na kumbe maandiko hayohayo yananishuhudia! (aiōnios g166)
40 Lakini mnakataa kuja kwangu ili mpate uzima.
Hata hivyo, ninyi hamtaki kuja kwangu ili mpate uzima.
41 “Mimi sitafuti kutukuzwa na wanadamu.
“Shabaha yangu si kupata sifa kutoka kwa watu.
42 Lakini ninajua kwamba hamna upendo wa Mungu mioyoni mwenu.
Lakini nawajua ninyi, najua kwamba upendo kwa Mungu haumo mioyoni mwenu.
43 Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, nanyi hamnipokei, lakini mtu mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea.
Mimi nimekuja kwa mamlaka ya Baba yangu, lakini hamnipokei; bali mtu mwingine akija kwa mamlaka yake mwenyewe, mtampokea.
44 Ninyi mwawezaje kuamini ikiwa mnapeana utukufu ninyi kwa ninyi, lakini hamna bidii kupata utukufu utokao kwa Mungu?
Mwawezaje kuamini, hali ninyi mnapenda kupokea sifa kutoka kwenu ninyi wenyewe, wala hamtafuti sifa kutoka kwake yeye aliye peke yake Mungu?
45 “Lakini msidhani kuwa mimi nitawashtaki mbele za Baba, mshtaki wenu ni Mose, ambaye mmemwekea tumaini lenu.
Msifikiri kwamba mimi nitawashtaki kwa Baba. Mose ambaye ninyi mmemtumainia ndiye atakayewashtaki.
46 Kama mngelimwamini Mose, mngeliniamini na mimi kwa maana aliandika habari zangu.
Kama kweli mngemwamini Mose, mngeniamini na mimi pia; maana Mose aliandika juu yangu.
47 Lakini ikiwa hamwamini aliyoandika Mose, mtaaminije ninayoyasema?”
Lakini hamuyaamini yale aliyoandika, mtawezaje basi, kuamini maneno yangu?”

< Yohana 5 >