< Yohana 2 >
1 Siku ya tatu kulikuwa na arusi katika mji wa Kana ya Galilaya, naye mama yake Yesu alikuwepo pale.
Baada ya siku tatu, kulikuwa na arusi huko Kana ya Galilaya na mama yake Yesu alikuwa huko.
2 Yesu pamoja na wanafunzi wake walikuwa wamealikwa arusini pia.
Yesu na wanafunzi wake walikuwa wamealikwa katika arusi.
3 Divai ilipokwisha, mama yake Yesu akamwambia, “Wameishiwa na divai.”
Wakati walipoishiwa na divai, mama yake Yesu akamwambia, “Hawana divai.”
4 Yesu akamwambia, “Mwanamke, nina nini nawe? Saa yangu haijawadia.”
Yesu akajibu, “Mwanamke hiyo inanihusu nini mimi? Muda wangu mimi bado haujatimia.”
5 Mama yake akawaambia wale watumishi, “Lolote atakalowaambia, fanyeni.”
Mama yake akawambia watumishi, “Chochote atakachowambia fanyeni.”
6 Basi ilikuwepo mitungi sita ya kuhifadhia maji iliyotengenezwa kwa mawe kwa ajili ya kujitakasa kwa desturi ya Kiyahudi; kila mtungi ungeweza kuchukua vipipa viwili au vitatu.
Basi kulikuwa na mitungi sita ya mawe pale iliyowekwa kwa ajili ya kunawa katika sikukuu za Wayahudi, kila moja lilikuwa na ujazo wa nzio mbili tatu.
7 Yesu akawaambia wale watumishi, “Ijazeni hiyo mitungi maji.” Nao wakaijaza ile mitungi mpaka juu.
Yesu akawambia, “Ijazeni maji mitungi ya mawe.” Wakajaza hadi juu.
8 Kisha akawaambia, “Sasa choteni hayo maji kidogo, mpelekeeni mkuu wa meza.” Hivyo wakachota, wakampelekea.
Kisha akawambia wale watumishi, “Chukueni kiasi sasa na mpeleke kwa muhudumu mkuu wa meza.” Wakafanya kama walivyoagizwa.
9 Yule mkuu wa meza akayaonja yale maji ambayo yalikuwa yamebadilika kuwa divai. Hakujua divai hiyo ilikotoka ingawa wale watumishi waliochota yale maji wao walifahamu. Basi akamwita bwana arusi kando
Mhudumu mkuu aliyaonja yale maji yaliyokuwa yamebadilika na kuwa divai, ila hakujua yalikotoka (lakini watumishi waliochota maji walijua yalikotoka). Kisha akamwita bwana harusi na
10 akamwambia, “Watu wote hutoa kwanza divai nzuri, kisha huleta ile divai hafifu wageni wakisha kunywa vya kutosha, lakini wewe umeiweka ile nzuri kupita zote mpaka sasa.”
kumwambia, “Kila mmoja huanza kuwahudumia watu divai nzuri na wakiishalewa huwapa divai isiyo nzuri. Lakini wewe umeitunza divai nzuri hadi sasa”
11 Huu, ndio uliokuwa muujiza wa kwanza Yesu aliofanya Kana ya Galilaya. Hivyo Yesu alidhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini.
Muujiza huu wa Kana ya Galilaya, ulikuwa ndio mwanzo wa ishara za miujiza aliyoifanya Yesu, akifunua utukufu wake, hivyo wanafunzi wake wakamwamini.
12 Baada ya hayo, Yesu pamoja na mama yake, ndugu zake na wanafunzi wake, walishuka mpaka Kapernaumu, wakakaa huko siku chache.
Baada ya hii, Yesu, mama yake, ndugu zake na wanafunzi wake walienda katika mji wa Kapernaum na wakaa huko kwa siku chache.
13 Ilipokaribia wakati wa Pasaka ya Wayahudi, Yesu alipanda kwenda Yerusalemu.
Basi Pasaka ya Wayahudi ilikuwa imekaribia, hivyo Yesu akaenda Yerusalemu.
14 Huko Hekaluni aliwakuta watu wakiuza ngʼombe, kondoo na njiwa, nao wengine walikuwa wameketi mezani wakibadili fedha.
Akawakuta wauzaji wa ng'ombe, kondoo, na njiwa ndani ya Hekalu. Pia na wabadilisha fedha walikuwa wameketi ndani ya Hekalu.
15 Akatengeneza mjeledi kutokana na kamba, akawafukuza wote kutoka kwenye eneo la Hekalu, pamoja na kondoo na ngʼombe. Akazipindua meza za wale wabadili fedha na kuzimwaga fedha zao.
Yesu akatengeneza mjeledi wenye vifundo, akawatoa wote walikuwemo katika hekalu, ikijumuisha ng'ombe na kondoo. Akamwaga fedha za wabadili fedha na kuzipindua meza zao.
16 Akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, “Waondoeni hapa! Mnathubutuje kuifanya nyumba ya Baba yangu kuwa mahali pa biashara?”
Kwa wauzaji wa njiwa akawambia, “Toeni vitu hivi mbali na mahali hapa, acheni kuifanya nyumba ya Baba yangu kuwa mahali pa soko.”
17 Wanafunzi wake wakakumbuka kuwa imeandikwa: “Wivu wa nyumba yako utanila.”
Wanafunzi wake wakakumbuka kuwa ilikuwa imeandikwa, “Wivu wa nyumba yako utanila.”
18 Ndipo Wayahudi wakamuuliza, “Unaweza kutuonyesha ishara gani ili kuthibitisha mamlaka uliyo nayo ya kufanya mambo haya?”
Wakuu wa Kiyahudi wakajibu, wakamwambia, Ni ishara ipi utakayoionyesha kwa sababu unayafanya mambo haya?”
19 Yesu akawajibu, “Libomoeni hili Hekalu, nami nitalijenga tena kwa siku tatu!”
Yesu akawajibu, libomoeni Hekalu hili nami nitalijenga baada ya siku tatu.”
20 Wale Wayahudi wakamjibu, “Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arobaini na sita, nawe wasema utalijenga kwa siku tatu?”
Kisha wakuu wa Wayahudi wakasema, “Iligharimu miaka arobaini na sita kujenga hekalu hili nawe unasema utalijenga kwa siku tatu?”
21 Lakini yeye Hekalu alilozungumzia ni mwili wake.
Ingawa, yeye aliongea hekalu akimaanisha mwili wake.
22 Baada ya kufufuliwa kutoka kwa wafu, wanafunzi wake wakakumbuka yale aliyokuwa amesema. Ndipo wakayaamini Maandiko na yale maneno Yesu aliyokuwa amesema.
Hivyo baadaye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu, wanafunzi wake wakakumbuka kuwa alisema hivyo, wakaamini maandiko na kauli hii ambayo Yesu alikuwa amekwisha kuisema.
23 Ikawa Yesu alipokuwa Yerusalemu kwenye Sikukuu ya Pasaka, watu wengi waliona ishara na miujiza aliyokuwa akifanya, wakaamini katika jina lake.
Basi alipokuwa Yerusalemu wakati wa Pasaka, wakati wa sikukuu watu wengi waliamini jina lake, walipoona ishara ya miujiza aliyoifanya.
24 Lakini Yesu hakujiaminisha kwao kwa sababu aliwajua wanadamu wote.
Lakini Yesu hakuwa na imani nao kwa sababu aliwajua wanadamu wote.
25 Hakuhitaji ushuhuda wa mtu yeyote kuhusu mtu, kwa kuwa alijua yote yaliyokuwa moyoni mwa mtu.
Hakuhitaji mtu yeyote kumwambia kuhusu walivyo wanadamu kwa sababu alijua kilichokuwamo ndani yao.