< Yohana 19 >

1 Ndipo Pilato akamtoa Yesu akaamuru apigwe mijeledi.
Basi, Pilato akaamuru Yesu achukuliwe, apigwe viboko.
2 Askari wakasokota taji ya miiba, wakamvika Yesu kichwani. Wakamvalisha joho la zambarau.
Nao askari wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani, wakamvika na joho la rangi ya zambarau.
3 Wakawa wanapanda pale alipo tena na tena, wakisema, “Salamu! Mfalme wa Wayahudi!” Huku wakimpiga makofi usoni.
Wakawa wanakuja mbele yake na kusema: “Shikamoo, Mfalme wa Wayahudi!” Wakampiga makofi.
4 Pilato akatoka tena nje akawaambia wale waliokusanyika, “Tazameni, namkabidhi Yesu kwenu kuwajulisha kwamba mimi sikumwona ana hatia.”
Pilato akatoka tena nje, akawaambia, “Tazameni, namleta nje kwenu, mpate kujua kwamba mimi sikuona hatia yoyote kwake.”
5 Kwa hiyo Yesu akatoka nje akiwa amevaa ile taji ya miiba na lile vazi la zambarau. Pilato akawaambia, “Tazameni, huyu hapa huyo mtu!”
Basi, Yesu akatoka nje amevaa taji ya miiba na joho la rangi ya zambarau. Pilato akawaambia, “Tazameni! Mtu mwenyewe ni huyo.”
6 Wale viongozi wa makuhani na maafisa walipomwona, wakapiga kelele wakisema, “Msulubishe! Msulubishe!” Pilato akawaambia, “Mchukueni ninyi mkamsulubishe, mimi sioni hatia juu yake.”
Makuhani wakuu na walinzi walipomwona wakapaaza sauti: “Msulubishe! Msulubishe!” Pilato akawaambia, “Mchukueni basi, ninyi wenyewe mkamsulubishe, kwa maana mimi sikuona hatia yoyote kwake.”
7 Wayahudi wakamjibu, “Sisi tunayo sheria na kutokana na sheria hiyo, hana budi kufa kwa sababu yeye alijiita Mwana wa Mungu.”
Wayahudi wakamjibu, “Sisi tunayo Sheria, na kufuatana na Sheria hiyo, ni lazima afe, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu.”
8 Pilato aliposikia haya, akaogopa zaidi.
Pilato aliposikia maneno hayo akazidi kuogopa.
9 Akaingia tena ndani ya jumba la kifalme, akamuuliza Yesu, “Wewe umetoka wapi?” Lakini Yesu hakumjibu.
Basi, akaingia tena ndani ya ikulu, akamwuliza Yesu, “Umetoka wapi wewe?” Lakini Yesu hakumjibu neno.
10 Pilato akamwambia, “Wewe unakataa kuongea na mimi? Hujui ya kuwa nina mamlaka ya kukuachia huru au kukusulubisha?”
Hivyo Pilato akamwambia, “Husemi nami? Je, hujui kwamba ninayo mamlaka ya kukufungua na mamlaka ya kukusulubisha?”
11 Ndipo Yesu akamwambia, “Wewe hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu kama hungepewa kutoka juu. Kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako ana hatia ya dhambi iliyo kubwa zaidi.”
Yesu akamjibu, “Hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu kama hungepewa na Mungu. Kwa sababu hiyo, yule aliyenikabidhi kwako ana dhambi kubwa zaidi.”
12 Tangu wakati huo, Pilato akajitahidi kutafuta njia ya kumfungua Yesu, lakini Wayahudi wakazidi kupiga kelele wakisema, “Ukimwachia huyu mtu, wewe si rafiki wa Kaisari. Mtu yeyote anayedai kuwa mfalme anampinga Kaisari.”
Tangu hapo, Pilato akawa anatafuta njia ya kumwachilia, lakini Wayahudi wakapiga kelele: “Ukimwachilia huyu mtu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu anayejifanya kuwa Mfalme humpinga Kaisari!”
13 Pilato aliposikia maneno haya akamtoa Yesu nje tena akaketi katika kiti chake cha hukumu, mahali palipoitwa Sakafu ya Jiwe, kwa Kiebrania paliitwa Gabatha
Basi, Pilato aliposikia maneno hayo akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha hukumu, mahali paitwapo: “Sakafu ya Mawe” (kwa Kiebrania, Gabatha).
14 Basi ilikuwa siku ya Maandalio ya Pasaka, yapata kama saa sita hivi. Pilato akawaambia Wayahudi, “Huyu hapa mfalme wenu!”
Ilikuwa yapata saa sita mchana, siku ya maandalio ya Pasaka. Pilato akawaambia Wayahudi, “Tazameni, Mfalme wenu!”
15 Wao wakapiga kelele, “Mwondoe! Mwondoe! Msulubishe!” Pilato akawauliza, “Je, nimsulubishe mfalme wenu?” Wale viongozi wa makuhani wakamjibu, “Sisi hatuna mfalme mwingine ila Kaisari.”
Wao wakapaaza sauti: “Mwondoe! Mwondoe! Msulubishe!” Makuhani wakuu wakajibu, “Sisi hatuna Mfalme isipokuwa Kaisari!”
16 Ndipo Pilato akamkabidhi Yesu kwao ili wamsulubishe. Kwa hiyo askari wakamchukua Yesu.
Basi, hapo Pilato akamtia Yesu mikononi mwao ili asulubiwe. Basi, wakamchukua Yesu.
17 Yesu, akiwa ameubeba msalaba wake, akatoka kuelekea mahali palipoitwa Fuvu la Kichwa (kwa Kiebrania ni Golgotha).
Naye akatoka akiwa amejichukulia msalaba wake kwenda mahali paitwapo “Fuvu la Kichwa”, (kwa Kiebrania Golgotha).
18 Hapo ndipo walipomsulubisha. Pamoja naye walisulubisha watu wengine wawili, mmoja kila upande wake, naye Yesu katikati.
Hapo ndipo walipomsulubisha, na pamoja naye waliwasulubisha watu wengine wawili; mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto, naye Yesu katikati.
19 Pilato akaamuru tangazo liandikwe na liwekwe juu kwenye msalaba wa Yesu, likasema: “Yesu wa Nazareti, Mfalme wa Wayahudi.”
Pilato aliandika ilani akaiweka juu ya msalaba. Nayo ilikuwa imeandikwa hivi: “Yesu wa Nazareti, Mfalme wa Wayahudi.”
20 Kwa kuwa mahali hapo Yesu aliposulubiwa palikuwa karibu na mjini, Wayahudi wengi walisoma maandishi haya yaliyokuwa yameandikwa kwa lugha za Kiebrania, Kiyunani na Kilatini.
Wayahudi wengi waliisoma ilani hiyo, maana mahali hapo aliposulubiwa Yesu palikuwa karibu na mji. Tena ilani hiyo ilikuwa imeandikwa kwa Kiebrania, Kilatini, na Kigiriki.
21 Viongozi wa makuhani wa Wayahudi wakapinga, wakamwambia Pilato, “Usiandike ‘Mfalme wa Wayahudi,’ bali andika kwamba mtu huyu alisema yeye ni mfalme wa Wayahudi.”
Basi, makuhani wakuu wakamwambia Pilato, “Usiandike: Mfalme wa Wayahudi, ila Yeye alisema, Mimi ni Mfalme wa Wayahudi.”
22 Pilato akawajibu, “Nilichokwisha kuandika, nimeandika!”
Pilato akajibu, “Niliyoandika, nimeandika!”
23 Askari walipokwisha kumsulubisha Yesu, walichukua nguo zake wakazigawa mafungu manne, kila askari fungu lake. Ila walikubaliana wasilichane lile vazi lake kwa maana lilikuwa halina mshono bali limefumwa tangu juu hadi chini.
Askari walipokwisha msulubisha Yesu, walizichukua nguo zake, wakazigawa mafungu manne, fungu moja kwa kila askari. Walichukua pia na kanzu yake; kanzu hiyo ilikuwa imefumwa kwa kipande kimoja tu, bila mshono.
24 Wakaambiana, “Tusilichane ila tulipigie kura ili kuamua ni nani atalichukua.” Hili lilitukia ili Maandiko yapate kutimizwa yale yaliyosema, “Wanagawana nguo zangu, na vazi langu wanalipigia kura.” Hayo ndiyo waliyoyafanya wale askari.
Basi, hao askari wakashauriana: “Tusiipasue, ila tuipigie kura itakuwa ya nani.” Jambo hilo lilifanyika ili yatimie Maandiko Matakatifu yasemayo: “Waligawana mavazi yangu, na nguo yangu wakaipigia kura.” Basi, ndivyo walivyofanya hao askari.
25 Wakati huo huo karibu na msalaba wa Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada wa mamaye, na Maria mke wa Klopa, na Maria Magdalene.
Karibu na msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada ya mama yake, Maria mke wa Kleopa, na Maria Magdalene.
26 Yesu alipomwona mama yake mahali pale pamoja na yule mwanafunzi aliyempenda wamesimama karibu, akamwambia mama yake, “Mwanamke, huyo hapo ndiye mwanao,”
Yesu alipomwona mama yake, na karibu naye amesimama yule mwanafunzi aliyempenda, akamwambia mama yake: “Mama! Tazama, huyo ndiye mwanao.”
27 kisha akamwambia yule mwanafunzi, “Nawe huyo hapo ndiye mama yako.” Tangu wakati huo yule mwanafunzi akamchukua mama yake Yesu nyumbani kwake.
Halafu akamwambia yule mwanafunzi: “Tazama, huyo ndiye mama yako.” Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake.
28 Baada ya haya, Yesu hali akijua kuwa mambo yote yamemalizika, alisema ili kutimiza Maandiko, “Naona kiu.”
Yesu alijua kwamba yote yalikuwa yametimia; na, ili Maandiko Matakatifu yapate kutimia, akasema, “Naona kiu.”
29 Hapo palikuwa na bakuli lililojaa siki. Kwa hiyo wakachovya sifongo kwenye hiyo siki, wakaiweka kwenye ufito wa mti wa hisopo, wakampelekea mdomoni.
Hapo palikuwa na bakuli limejaa siki. Basi, wakachovya sifongo katika hiyo siki, wakaitia juu ya ufito wa husopo, wakamwekea mdomoni.
30 Baada ya kuionja hiyo siki, Yesu akasema, “Imekwisha.” Akainamisha kichwa chake, akaitoa roho yake.
Yesu alipokwisha pokea hiyo siki, akasema, “Yametimia!” Kisha akainama kichwa, akatoa roho.
31 Kwa kuwa ilikuwa siku ya Maandalio ya Pasaka, Wayahudi hawakutaka miili ibaki msalabani siku ya Sabato, hasa kwa kuwa hiyo Sabato ingekuwa Sikukuu. Wakamwomba Pilato aamuru miguu ya wale waliosulubiwa ivunjwe ili wafe haraka miili iondolewe kwenye misalaba.
Ilikuwa Ijumaa, siku ya Maandalio. Kwa hiyo, kusudi miili isikae msalabani siku ya Sabato, maana siku hiyo ya Sabato ilikuwa siku kubwa, Wayahudi walimwomba Pilato miguu ya hao waliosulubiwa ivunjwe na miili yao iondolewe.
32 Kwa hiyo askari wakaenda wakavunja miguu ya mtu wa kwanza aliyesulubiwa pamoja na Yesu na yule mwingine pia.
Basi, askari walikwenda, wakaivunja miguu ya yule mtu wa kwanza na yule wa pili ambao walikuwa wamesulubiwa pamoja na Yesu.
33 Lakini walipomkaribia Yesu, wakaona ya kuwa amekwisha kufa, hivyo hawakuvunja miguu yake.
Lakini walipomfikia Yesu waliona kwamba alikwisha kufa, na hivyo hawakumvunja miguu.
34 Badala yake mmoja wa wale askari akamchoma mkuki ubavuni na mara pakatoka damu na maji.
Lakini askari mmoja alimtoboa ubavuni kwa mkuki, na mara ikatoka damu na maji.
35 Mtu aliyeona mambo hayo ndiye alitoa ushuhuda, nao ushuhuda wake ni kweli. Anajua kuwa anasema kweli, naye anashuhudia ili pia nanyi mpate kuamini.
(Naye aliyeona tukio hilo ametoa habari zake ili nanyi mpate kuamini. Na hayo aliyosema ni ukweli, tena yeye anajua kwamba anasema ukweli.)
36 Kwa maana mambo haya yalitukia ili Maandiko yapate kutimia, yale yasemayo, “Hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.”
Jambo hilo lilitendwa ili Maandiko Matakatifu yatimie: “Hapana hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.”
37 Tena Andiko lingine lasema, “Watamtazama yeye waliyemchoma.”
Tena Maandiko mengine yanasema: “Watamtazama yule waliyemtoboa.”
38 Baada ya mambo haya, Yosefu wa Arimathaya, aliyekuwa mfuasi wa Yesu, ingawa kwa siri kwa sababu ya kuwaogopa Wayahudi, alimwomba Pilato ruhusa ili kuuchukua mwili wa Yesu. Pilato alimruhusu, hivyo akaja, akauchukua.
Baada ya hayo, Yosefu, mwenyeji wa Armathaya, alimwomba Pilato ruhusa ya kuuchukua mwili wa Yesu. (Yosefu alikuwa mfuasi wa Yesu, lakini kwa siri, maana aliwaogopa viongozi wa Wayahudi). Basi, Pilato akamruhusu. Hivyo Yosefu alikwenda, akauondoa mwili wa Yesu.
39 Naye Nikodemo, yule ambaye kwanza alimwendea Yesu usiku, akaja, akaleta mchanganyiko wa manemane na manukato, yenye uzito wa zaidi ya kilo thelathini
Naye Nikodemo ambaye hapo awali alikuwa amemwendea Yesu usiku, akaja akiwa amechukua mchanganyiko wa manemane na ubani kiasi cha kilo thelathini.
40 Wakauchukua mwili wa Yesu, wakaufunga katika sanda ya kitani safi pamoja na yale manukato, kama ilivyokuwa desturi ya Wayahudi.
Basi, waliutwaa mwili wa Yesu, wakaufunga sanda pamoja na manukato kufuatana na desturi ya Wayahudi katika kuzika.
41 Basi palikuwa na bustani karibu na mahali pale aliposulubiwa, na pale ndani ya ile bustani palikuwa na kaburi jipya, ambalo halikuwa limezikiwa mtu bado.
Mahali hapo aliposulubiwa Yesu palikuwa na bustani, na katika bustani hiyo kulikuwa na kaburi jipya ambalo hakutiwa bado mtu yeyote ndani yake.
42 Kwa hiyo, kwa kuwa ilikuwa siku ya Wayahudi ya Maandalio, nalo kaburi hilo lilikuwa karibu, wakamzika Yesu humo.
Basi, kwa sababu ya shughuli za Wayahudi za maandalio ya Sabato, na kwa vile kaburi hilo lilikuwa karibu, wakamweka Yesu humo.

< Yohana 19 >