< Yohana 17 >

1 Baada ya Yesu kusema haya, alitazama kuelekea mbinguni akawaombea na kusema: “Baba, saa imewadia. Umtukuze Mwanao, ili Mwanao apate kukutukuza wewe.
Yesu aliyasema mambo haya; kisha akainua macho yake kuelelea mbinguni na akasema, “Baba, saa imewadia; mtukuze mwanao ili na mwana naye akutukuze wewe -
2 Kwa kuwa umempa mamlaka juu ya wote wenye mwili ili awape uzima wa milele wale uliompa. (aiōnios g166)
kama vile ulivyompatia mamlaka juu ya vyote vyenye mwili ili awape uzima wa milele wale wote uliompatia. (aiōnios g166)
3 Nao uzima wa milele ndio huu, wakujue wewe uliye Mungu wa pekee, wa kweli na Yesu Kristo uliyemtuma. (aiōnios g166)
Huu ndio uzima wa milele: kwamba wakujue wewe, Mungu wa kweli na wa pekee, na yeye uliyemtuma, Yesu Kristo. (aiōnios g166)
4 Nimekutukuza wewe duniani kwa kuitimiza ile kazi uliyonipa niifanye.
Nilikutukuza hapa duniani, na kuikamilisha kazi uliyonipa niifanye.
5 Hivyo sasa, Baba, unitukuze mbele zako kwa ule utukufu niliokuwa nao pamoja na wewe kabla ulimwengu haujakuwepo.
Sasa, Baba, unitukuze mimi pamoja na wewe mwenyewe kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja na wewe kabla ya ulimwengu kuumbwa.
6 “Nimelidhihirisha jina lako kwa wale ulionipa kutoka ulimwengu. Walikuwa wako, nawe ukanipa mimi, nao wamelitii neno lako.
Nililifunua jina lako kwa watu ulionipa hapa duniani. Walikuwa watu wako; lakini ulinikabidhi mimi. nao wamelishika neno lako.
7 Sasa wamejua ya kuwa vyote ulivyonipa vimetoka kwako,
Sasa wanajua kuwa kila kitu ulichonipa mimi kinatoka kwako,
8 kwa kuwa maneno yale ulionipa nimewapa wao, nao wameyapokea na kujua kwamba kweli nimetoka kwako, nao wameamini kuwa wewe ulinituma.
kwa maneno yale uliyonipatia mimi— Nimekwisha wapatia wao maneno hayo. Waliyapokea na kweli wakajua ya kuwa mimi nimetoka kwako, na wakaamini kuwa wewe ndiye uliyenituma.
9 Ninawaombea wao. Mimi siuombei ulimwengu, bali nawaombea wale ulionipa kwa sababu wao ni wako.
Ninawaombea wao. Siuombei ulimwaengu bali wale ulionipa kwa kuwa wao ni wako.
10 Wote walio wangu ni wako na walio wako ni wangu, nami nimetukuzwa ndani yao.
Vitu vyote ambavyo ni vyangu ni vyako, na vile ulivyonavyo wewe ni vyangu; nami ninatukuzwa katika hivyo.
11 Mimi sasa simo tena ulimwenguni, lakini wao bado wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba Mtakatifu, uwalinde kwa uweza wa jina lako ulilonipa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja.
Mimi simo tena ulimwenguni, bali wao wamo ulimwenguni, nami sasa naja kwako. Baba Mtakatifu, watunze kwa jina lako lile ulilonipa sisi ili wao nao wawe na umoja, kama vile mimi na wewe tulivyo na umoja.
12 Nilipokuwa pamoja nao, niliwalinda, wakawa salama kwa lile jina ulilonipa. Hakuna hata mmoja aliyepotea, isipokuwa yule aliyekusudiwa upotevu, ili Maandiko yapate kutimia.
Nilipokuwa nao, niliwalinda kwa jina ulilonipa; Niliwalinda, na hakuna hata mmoja wao aliyepotea isipokuwa mwana wa upotevu, ili kwamba maandiko yatimie.
13 “Lakini sasa naja kwako, nami ninasema mambo haya wakati bado nikiwa ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu kamili ndani yao.
Sasa ninakuja kwako; lakini ninasema haya ulimwenguni ili kwamba furaha yangu ikamilishwe ndani yao wenyewe.
14 Nimewapa neno lako, nao ulimwengu umewachukia kwa kuwa wao si wa ulimwengu kama mimi nisivyo wa ulimwengu huu.
Nimewapa neno lako; ulimwengu imewachukia kwa sababu wao si wa ulimwengu, kama vile mimi nisivyokuwa wa ulimwengu
15 Siombi kwamba uwaondoe ulimwenguni, bali uwalinde dhidi ya yule mwovu.
Siwaombei kwamba uwatoe ulimwenguni bali uwalinde na yule mwovu.
16 Wao si wa ulimwengu huu, kama vile mimi nisivyo wa ulimwengu.
Wao si wa dunia kama vile mimi nisivyokuwa wa ulimwenguni.
17 Uwatakase kwa ile kweli, neno lako ndilo kweli.
Uwaweke wakfu kwako mwenyewe katika Kweli; neno lako ndiyo kweli.
18 Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami nawatuma vivyo hivyo.
Ulinituma ulimwenguni, nami nimewatuma ulimwenguni.
19 Kwa ajili yao najiweka wakfu ili wao nao wapate kutakaswa katika ile kweli.
Kwa ajili yao mimi mwenyewe ninajitoa kwako ili kwamba na wao wajitoe kwako kwa ile kweli.
20 “Siwaombei hawa peke yao, bali nawaombea na wale wote watakaoniamini kupitia neno lao
Si hawa tu ninaowaombea, bali na wale watakaoamini kupitia neno lao
21 ili wawe na umoja kama vile wewe Baba ulivyo ndani yangu na mimi nilivyo ndani yako, wao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kuamini ya kuwa wewe ndiye uliyenituma mimi.
ili kwamba wao nao wawe na umoja, kama vila wewe Baba, ulivyo ndani yangu nami ndani yako. Nawaombea ili kwamba wao pia waweze kuwa ndani yetu ili ulimwengu uweze kuamini kuwa wewe ndiye uliyenituma.
22 Utukufu ule ulionipa nimewapa wao, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja.
Utukufu ule ulionipa mimi - nimewapa wao, ili kwamba waweze kuwa na umoja, kama vile sisi tulivyo umoja -
23 Mimi ndani yako na wewe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja na ulimwengu upate kujua ya kuwa umenituma, nami nimewapenda wao kama unavyonipenda mimi.
Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili waweze kukamilishwa katika umoja; ili ulimwengu ujue kuwa hakika wewe ndiye uliyenituma, na kuwapenda, kama vile wewe ulivyonipenda, mimi.
24 “Baba, shauku yangu ni kwamba, wale ulionipa wawe pamoja nami pale nilipo, ili waweze kuuona utukufu wangu, yaani, utukufu ule ulionipa kwa kuwa ulinipenda hata kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu.
Baba, kile ulichonipa mimi - Natamani kwamba wao pia waweze kuwa pamoja nami mahali nilipo ili waweze kuona utukufu wangu, ule ulionipa: kwa kuwa wewe ulinipenda mimi kabla ya kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu.
25 “Baba Mwenye Haki, ingawa ulimwengu haukujui, mimi ninakujua, nao wanajua ya kuwa umenituma.
Baba mwenye haki, ulimwengu haukukujua wewe, lakini mimi nakujua wewe; na wanajua kwamba ulinituma.
26 Nimefanya jina lako lijulikane kwao nami nitaendelea kufanya lijulikane, ili kwamba upendo ule unaonipenda mimi uwe ndani yao na mimi mwenyewe nipate kuwa ndani yao.”
Nililifanya jina lako lijulikane kwao, na nitalifanya lijulikane ili kwamba lile pendo ambalo kwalo ulinipenda mimi liweze kuwa ndani yao, na mimi niweze kuwa ndani yao.”

< Yohana 17 >