< Yohana 11 >
1 Basi mtu mmoja jina lake Lazaro alikuwa mgonjwa. Yeye alikuwa akiishi Bethania kijiji cha Maria na Martha dada zake.
Mtu mmoja aitwaye Lazaro, mwenyeji wa Bethania, alikuwa mgonjwa. (Kijiji cha Bethania kilikuwa mahali walipokaa Maria na Martha, dada yake.
2 Huyu Maria, ambaye Lazaro kaka yake alikuwa mgonjwa, ndiye yule ambaye alimpaka Bwana mafuta na kuifuta miguu yake kwa nywele zake.
Maria ndiye yule aliyempaka Bwana marashi na kumpangusa kwa nywele zake. Lazaro, kaka yake, ndiye aliyekuwa mgonjwa.)
3 Hivyo hawa dada wawili walituma ujumbe kwa Yesu kumwambia, “Bwana, yule umpendaye ni mgonjwa.”
Basi, hao dada wakatuma ujumbe huu kwa Yesu: “Bwana, rafiki yako ni mgonjwa!”
4 Lakini Yesu aliposikia hayo, akasema, “Ugonjwa huu hautaleta mauti bali umetokea ili kudhihirisha utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu apate kutukuzwa kutokana na ugonjwa huu.”
Yesu aliposikia hivyo akasema, “Ugonjwa huo hautaleta kifo, ila ni kwa ajili ya kumtukuza Mungu; ameugua ili kwa njia hiyo Mwana wa Mungu atukuzwe.”
5 Pamoja na hivyo, ingawa Yesu aliwapenda Martha, Maria na Lazaro ndugu yao,
Yesu aliwapenda Martha, dada yake na Lazaro.
6 baada ya kusikia kwamba Lazaro ni mgonjwa, aliendelea kukawia huko alikokuwa kwa siku mbili zaidi.
Alipopata habari kwamba Lazaro ni mgonjwa, Yesu aliendelea kukaa mahali hapo alipokuwa kwa siku mbili zaidi.
7 Ndipo akawaambia wanafunzi wake, “Haya, turudi Uyahudi.”
Kisha akawaambia wanafunzi wake, “Twendeni tena Yudea!”
8 Wanafunzi wake wakamwambia, “Rabi, Wayahudi walikuwa wanataka kukupiga mawe, nawe unataka kurudi huko?”
Wanafunzi wakamwambia, “Mwalimu! Muda mfupi tu umepita tangu Wayahudi walipotaka kukuua kwa mawe, nawe unataka kwenda huko tena?”
9 Yesu akawajibu, “Si kuna saa kumi na mbili za mchana katika siku moja? Wala watembeao mchana hawawezi kujikwaa kwa maana wanaona nuru ya ulimwengu huu.
Yesu akajibu, “Je, saa za mchana si kumi na mbili? Basi, mtu akitembea mchana hawezi kujikwaa kwa kuwa anauona mwanga wa ulimwengu huu.
10 Lakini wale watembeao usiku hujikwaa kwa sababu hakuna nuru ndani yao.”
Lakini mtu akitembea usiku atajikwaa kwa maana mwanga haumo ndani yake.”
11 Baada ya kusema haya, Yesu akawaambia, “Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini naenda kumwamsha.”
Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, akawaambia, “Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini mimi nitakwenda kumwamsha.”
12 Wanafunzi wakamwambia, “Bwana, kama amelala usingizi ataamka.”
Wanafunzi wake wakamwambia, “Bwana, ikiwa amelala, basi atapona.”
13 Hata hivyo, Yesu alikuwa anazungumzia kuwa Lazaro amekufa, lakini wanafunzi wake hawakuelewa, walidhani kwamba anasema Lazaro amelala usingizi tu.
Wao walidhani kwamba alikuwa amesema juu ya kulala usingizi, kumbe alikuwa amesema juu ya kifo cha Lazaro.
14 Kwa hiyo Yesu akawaambia waziwazi, “Lazaro amekufa.
Basi, Yesu akawaambia waziwazi, “Lazaro amekufa;
15 Hata hivyo nafurahi kwa kuwa sikuwepo huko kabla ya Lazaro kufa, ili mpate kuamini. Lakini sasa twendeni kwake.”
Lakini nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwako huko, ili mpate kuamini. Haya, twendeni kwake.”
16 Tomaso aliyeitwa Pacha akawaambia wanafunzi wenzake, “Sisi nasi twendeni tukafe pamoja naye.”
Thoma (aitwaye Pacha) akawaambia wanafunzi wenzake, “Twendeni nasi tukafe pamoja naye!”
17 Yesu alipowasili huko alikuta Lazaro amekuwa kaburini siku nne.
Yesu alipofika huko alikuta Lazaro amekwisha kaa kaburini kwa siku nne.
18 Basi Bethania ulikuwa karibu na Yerusalemu umbali wa karibu maili mbili,
Kijiji cha Bethania kilikuwa karibu na Yerusalemu umbali upatao kilomita tatu.
19 na Wayahudi wengi walikuwa wamekuja kuwafariji Martha na Maria kwa ajili ya kufiwa na ndugu yao.
Wayahudi wengi walikuwa wamefika kwa Martha na Maria kuwafariji kwa kifo cha kaka yao.
20 Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alitoka kwenda kumlaki, ila Maria alibaki nyumbani.
Basi, Martha aliposikia kwamba Yesu alikuwa anakuja, akaenda kumlaki; lakini Maria alibaki nyumbani.
21 Martha akamwambia Yesu, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, ndugu yangu hangalikufa.
Martha akamwambia Yesu, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa!
22 Lakini sasa ninajua kuwa chochote utakachomwomba Mungu, atakupa.”
Lakini najua kwamba hata sasa chochote utakachomwomba Mungu, atakupa.”
23 Yesu akamwambia, “Ndugu yako atafufuka.”
Yesu akamwambia, “Kaka yako atafufuka.”
24 Martha akamjibu, “Ninajua ya kuwa atafufuka wakati wa ufufuo wa wafu siku ya mwisho.”
Martha akamjibu, “Najua kwamba atafufuka wakati wa ufufuo, siku ya mwisho.”
25 Yesu akamwambia, “Mimi ndiye huo ufufuo na uzima. Yeye aniaminiye mimi, hata akifa atakuwa anaishi
Yesu akamwambia, “Mimi ndimi ufufuo na uzima. Anayeniamini mimi hata kama anakufa, ataishi:
26 na yeyote aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je, unasadiki haya?” (aiōn )
na kila anayeishi na kuniamini, hatakufa kamwe. Je, waamini hayo?” (aiōn )
27 Martha akamwambia, “Ndiyo Bwana, ninaamini ya kuwa wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yeye ajaye ulimwenguni.”
Martha akamwambia, “Ndiyo Bwana! Naamini kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni.”
28 Baada ya kusema haya Martha alikwenda, akamwita Maria dada yake faraghani na kumwambia, “Mwalimu yuko hapa anakuita.”
Baada ya kusema hayo, Martha alikwenda kumwita Maria, dada yake, akamwabia faraghani, “Mwalimu yuko hapa, anakuita.”
29 Maria aliposikia hivyo, akaondoka upesi akaenda mpaka alipokuwa Yesu.
Naye aliposikia hivyo, akainuka mara, akamwendea Yesu.
30 Yesu alikuwa hajaingia kijijini, bali alikuwa bado yuko mahali pale alipokutana na Martha.
Yesu alikuwa hajaingia kijijini, ila alikuwa bado mahali palepale Martha alipomlaki.
31 Wale Wayahudi waliokuwa pamoja na Maria nyumbani wakimfariji walipoona ameondoka haraka na kutoka nje, walimfuata wakidhani ya kwamba alikuwa anakwenda kule kaburini kulilia huko.
Basi, Wayahudi waliokuwa nyumbani pamoja na Maria wakimfariji walipomwona ameinuka na kutoka nje ghafla, walimfuata. Walidhani alikuwa anakwenda kaburini kuomboleza.
32 Maria alipofika mahali pale Yesu alipokuwa, alipiga magoti miguuni Pake na kusema, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, ndugu yangu hangalikufa.”
Basi, Maria alipofika mahali pale Yesu alipokuwa na kumwona, alipiga magoti, akamwabia, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa!”
33 Yesu alipomwona Maria akilia na wale Wayahudi waliokuja pamoja naye pia wakilia, Yesu alisikia uchungu moyoni, akafadhaika sana.
Yesu alipomwona analia, na wale Wayahudi waliokuja pamoja naye wanalia pia, alijawa na huzuni na kufadhaika moyoni.
34 Akauliza, “Mmemweka wapi?” Wakamwambia, “Bwana, njoo upaone.”
Kisha akawauliza, “Mlimweka wapi?” Wakamwambia, “Bwana, njoo uone.”
36 Ndipo Wayahudi wakasema, “Tazama jinsi alivyompenda Lazaro!”
Basi, Wayahudi wakasema, “Tazameni jinsi alivyompenda!”
37 Lakini wengine wakasema, “Je, yule aliyefungua macho ya kipofu, hakuweza kumfanya na huyu asife?”
Lakini baadhi yao wakasema, “Je, huyu aliyemfumbua macho yule kipofu, hakuweza kumfanya Lazaro asife?”
38 Yesu kwa mara nyingine akiwa amefadhaika sana, akafika penye kaburi. Hilo kaburi lilikuwa pango ambalo jiwe lilikuwa limewekwa kwenye ingilio lake.
Basi, Yesu akiwa amehuzunika tena moyoni, akafika kaburini. Kaburi lenyewe lilikuwa pango, na lilikuwa limefunikwa kwa jiwe.
39 Yesu akasema, “Liondoeni hilo jiwe.” Martha ndugu yake yule aliyekuwa amekufa akasema, “Lakini Bwana, wakati huu atakuwa ananuka kwani amekwisha kuwa kaburini siku nne.”
Yesu akasema, “Ondoeni hilo jiwe!” Martha, dada yake huyo aliyekufa, akamwambia, “Bwana, amekwishaanza kunuka; amekaa kaburini siku nne!”
40 Yesu akamwambia, “Sikukuambia kwamba kama ukiamini utauona utukufu wa Mungu?”
Yesu akamwambia, “Je, sikukwambia kwamba ukiamini utaona utukufu wa Mungu?”
41 Kwa hiyo wakaliondoa lile jiwe kutoka kaburini. Yesu akainua macho yake juu akasema, “Baba, ninakushukuru kwa kuwa wanisikia.
Basi, wakaliondoa lile jiwe. Yesu akatazama juu mbinguni, akasema, “Nakushukuru Baba kwa kuwa wewe wanisikiliza.
42 Ninajua ya kuwa wewe hunisikia siku zote, lakini nimesema haya kwa ajili ya umati huu uliosimama hapa, ili wapate kuamini ya kuwa wewe umenituma.”
Najua kwamba unanisikiliza daima. Lakini nimesema hayo kwa ajili ya watu hawa waliopo hapa ili wapate kuamini kwamba wewe ndiwe uliyenituma.”
43 Baada ya kusema haya, Yesu akapaza sauti yake akaita, “Lazaro, njoo huku!”
Alipokwisha sema hayo, akaita kwa sauti kubwa: “Lazaro! Toka nje!”
44 Yule aliyekuwa amekufa akatoka nje, mikono yake na miguu yake ikiwa imeviringishiwa vitambaa vya kitani na leso usoni pake. Yesu akawaambia, “Mfungueni, mwacheni aende zake.”
Huyo aliyekuwa amekufa akatoka nje, huku amefungwa sanda miguu na mikono, na uso wake umefunikwa. Yesu akawaambia, “Mfungueni, mkamwache aende zake.”
45 Hivyo Wayahudi wengi waliokuwa wamekuja kumfariji Maria, walipoona yale Yesu aliyoyatenda wakamwamini.
Basi, Wayahudi wengi waliokuwa wamefika kwa Maria walipoona kitendo hicho alichokifanya Yesu wakamwamini.
46 Lakini baadhi yao wakaenda kwa Mafarisayo na kuwaambia mambo Yesu aliyoyafanya.
Lakini baadhi yao walikwenda kwa Mafarisayo wakatoa taarifa ya jambo hilo alilofanya Yesu.
47 Kwa hiyo viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakaita mkutano wa baraza. Wakaulizana, “Tufanyeje? Huyu mtu anafanya ishara nyingi.
kwa hiyo makuhani wakuu na Mafarisayo wakafanya kikao cha Baraza kuu, wakasema, “Tufanye nini? Mtu huyu anafanya ishara nyingi mno.
48 Kama tukimwacha aendelee hivi, kila mtu atamwamini, nao Warumi watakuja na kupaharibu mahali petu patakatifu na taifa letu.”
Tukimwacha tu watu wote watamwamini, nao Waroma watakuja kuliharibu Hekalu letu na taifa letu!”
49 Mmoja wao aliyeitwa Kayafa, ambaye alikuwa kuhani mkuu mwaka huo, akasema, “Ninyi hamjui kitu chochote!
Hapo, mmoja wao aitwaye Kayafa, ambaye alikuwa Kuhani Mkuu mwaka huo, akawaambia, “Ninyi hamjui kitu!
50 Hamjui kwamba ni afadhali mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, kuliko taifa lote liangamie?”
Je, hamwoni kwamba ni afadhali kwenu mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, kuliko taifa zima liangamizwe?”
51 Hakusema haya kutokana na mawazo yake mwenyewe bali kama kuhani mkuu mwaka huo, alitabiri kuwa Yesu angelikufa kwa ajili ya taifa la Wayahudi,
Yeye hakusema hivyo kwa hiari yake mwenyewe, bali kwa vile alikuwa Kuhani Mkuu mwaka huo, alibashiri kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya taifa lao;
52 wala si kwa ajili ya taifa hilo pekee, bali pia kwa ajili ya watoto wa Mungu waliotawanyika, ili kuwaleta pamoja na kuwafanya wawe wamoja.
na wala si kwa ajili yao tu, bali pia apate kuwaleta pamoja watoto wa Mungu waliotawanyika.
53 Hivyo tangu siku hiyo wakawa wanafanya mipango ili wamuue Yesu.
Basi, tangu siku hiyo viongozi wa Wayahudi walifanya mipango ya kumwua Yesu.
54 Kwa hiyo Yesu akawa hatembei hadharani miongoni mwa Wayahudi, bali alijitenga akaenda sehemu iliyo karibu na jangwa kwenye kijiji kiitwacho Efraimu. Akakaa huko na wanafunzi wake.
Kwa hiyo, Yesu hakutembea tena hadharani kati ya Wayahudi, bali alitoka hapo, akaenda mahali karibu na jangwa, katika mji uitwao Efraimu. Akakaa huko pamoja na wanafunzi wake.
55 Basi Pasaka ya Wayahudi ilipokuwa imekaribia, watu wengi walitoka vijijini wakaenda Yerusalemu kabla ya Pasaka ili wakajitakase.
Sikukuu ya Wayahudi ya Pasaka ilikuwa karibu, na watu wengi walikwenda Yerusalemu ili wajitakase kabla ya sikukuu hiyo.
56 Watu wakawa wanamtafuta Yesu, nao waliposimama kwenye eneo la Hekalu waliulizana, Je, mtu huyu hatakuja kamwe kwenye Sikukuu?
Basi, wakawa wanamtafuta Yesu; nao walipokusanyika pamoja Hekaluni wakaulizana, “Mwaonaje? Yaonekana kwamba haji kabisa kwenye sikukuu, au sivyo?”
57 Viongozi wa makuhani na Mafarisayo walikuwa wametoa amri kuwa yeyote atakayejua mahali Yesu aliko, lazima atoe taarifa ili wapate kumkamata.
Makuhani wakuu na Mafarisayo walikuwa wametoa amri kwamba mtu akijua mahali aliko Yesu awaarifu kusudi wamtie nguvuni.