< Yohana 1 >

1 Hapo mwanzo alikuwako Neno, huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.
Hapo Mwanzo, Neno alikuwako; naye alikuwa na Mungu, naye alikuwa Mungu.
2 Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu.
Tangu mwanzo Neno alikuwa na Mungu.
3 Vitu vyote viliumbwa kwa yeye, wala pasipo yeye hakuna chochote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa.
Kwa njia yake vitu vyote viliumbwa; hakuna hata kiumbe kimoja kilichoumbwa pasipo yeye.
4 Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima na huo uzima ulikuwa nuru ya watu.
Yeye alikuwa chanzo cha uhai na uhai huo ulikuwa mwanga wa watu.
5 Nuru hungʼaa gizani nalo giza halikuishinda.
Na mwanga huo huangaza gizani, nalo giza halikuweza kuushinda.
6 Alikuja mtu mmoja aliyetumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana.
Mungu alimtuma mtu mmoja jina lake Yohane,
7 Alikuja kama shahidi apate kuishuhudia hiyo nuru, ili kwa kupitia kwake watu wote waweze kuamini.
ambaye alikuja kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Alikuja ili kwa ujumbe wake watu wote wapate kuamini.
8 Yeye mwenyewe hakuwa ile nuru, bali alikuja kuishuhudia hiyo nuru.
Yeye hakuwa huo mwanga, ila alikuja tu kuwaambia watu juu ya huo mwanga.
9 Kwamba nuru halisi, imwangaziayo kila mtu ilikuwa inakuja ulimwenguni.
Huu ndio mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu wote.
10 Huyo Neno alikuwako ulimwenguni na ingawa ulimwengu uliumbwa kupitia kwake, haukumtambua.
Basi, Neno alikuwako ulimwenguni; na kwa njia yake ulimwengu uliumbwa, lakini ulimwengu haukumtambua.
11 Alikuja kwa walio wake, lakini wao hawakumpokea.
Alikuja katika nchi yake mwenyewe, nao walio wake hawakumpokea.
12 Bali wote waliompokea, aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake.
Lakini wale wote waliompokea na kumwamini, hao aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu.
13 Hawa ndio wasiozaliwa kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili au kwa mapenzi ya mtu, bali kwa mapenzi ya Mungu.
Hawa wamekuwa watoto wa Mungu si kwa uwezo wa kibinadamu, wala kwa nguvu za kimwili, wala kwa mapenzi ya mtu, bali Mungu mwenyewe ndiye baba yao.
14 Neno alifanyika mwili, akakaa miongoni mwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli.
Naye Neno akawa mwanadamu, akakaa kwetu. Nasi tumeuona utukufu wake, utukufu wake yeye aliye Mwana wa pekee wa Baba; amejaa neema na ukweli.
15 Yohana alishuhudia habari zake, akapaza sauti, akisema, “Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Yeye ajaye baada yangu ni mkuu kuniliko mimi, kwa kuwa alikuwepo kabla yangu.’”
Yohane aliwaambia watu habari zake, akasema kwa sauti, “Huyu ndiye niliyemtaja wakati niliposema: Anakuja mtu mmoja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa.”
16 Kutokana na ukamilifu wake, sisi sote tumepokea neema juu ya neema.
Kutokana na ukamilifu wake sisi tumepokea neema mfululizo.
17 Kwa kuwa sheria ilitolewa kwa mkono wa Mose, lakini neema na kweli imekuja kupitia Yesu Kristo.
Maana Mungu alitoa Sheria kwa njia ya Mose, lakini neema na kweli vimekuja kwa njia ya Kristo.
18 Hakuna mtu yeyote aliyemwona Mungu wakati wowote, ila ni Mungu Mwana pekee, aliye kifuani mwa Baba ndiye ambaye amemdhihirisha.
Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote ule. Mwana wa pekee aliye sawa na Mungu ambaye ameungana na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za Mungu.
19 Huu ndio ushuhuda wa Yohana wakati Wayahudi walipowatuma makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu kumuuliza, “Wewe ni nani?”
Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa wakati viongozi wa Wayahudi kule Yerusalemu walipowatuma makuhani wa Walawi kwake wamwulize: “Wewe u nani?”
20 Yohana alikiri waziwazi pasipo kuficha akasema, “Mimi si Kristo.”
Yohane hakukataa kujibu swali hilo, bali alisema waziwazi, “Mimi siye Kristo.”
21 Wakamuuliza, “Wewe ni nani basi? Je, wewe ni Eliya?” Yeye akajibu, “Hapana, mimi siye.” “Je, wewe ni yule Nabii?” Akajibu, “Hapana.”
Hapo wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Je, wewe ni Eliya?” Yohane akajibu, “La, mimi siye.” Wakamwuliza, “Je, wewe ni yule nabii?” Yohane akawajibu, “La!”
22 Ndipo wakasema, “Basi tuambie wewe ni nani ili tupate jibu la kuwapelekea wale waliotutuma. Wewe wasemaje juu yako mwenyewe?”
Nao wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Wasema nini juu yako mwenyewe? Tuambie, ili tuwapelekee jibu wale waliotutuma.”
23 Akawajibu kwa maneno ya nabii Isaya, akisema, “Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, ‘Yanyoosheni mapito ya Bwana.’”
Yohane akawajibu, “Mimi ndiye yule ambaye nabii Isaya alisema habari zake: Sauti ya mtu imesikika jangwani: Nyoosheni njia ya Bwana.”
24 Basi walikuwa wametumwa watu kutoka kwa Mafarisayo
Hao watu walikuwa wametumwa na Mafarisayo.
25 wakamuuliza, “Kama wewe si Kristo, wala si Eliya na wala si yule Nabii, kwa nini basi unabatiza?”
Basi, wakamwuliza Yohane, “Kama wewe si Kristo, wala Eliya, wala yule nabii, mbona wabatiza?”
26 Yohana akawajibu, “Mimi ninabatiza kwa maji, lakini katikati yenu yupo mtu msiyemjua.
Yohane akawajibu, “Mimi nabatiza kwa maji, lakini yuko mmoja kati yenu, msiyemjua bado.
27 Yeye ajaye baada yangu, sistahili hata kufungua kamba za viatu vyake.”
Huyo anakuja baada yangu, lakini mimi sistahili hata kumfungua kamba za viatu vyake.”
28 Mambo haya yote yalitukia huko Bethania, ngʼambo ya Mto Yordani, mahali Yohana alipokuwa akibatiza.
Mambo haya yalifanyika huko Bethania, ng'ambo ya mto Yordani ambako Yohane alikuwa anabatiza.
29 Siku iliyofuata, Yohana alimwona Yesu akimjia akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu!
Kesho yake, Yohane alimwona Yesu akimjia, akasema, “Huyu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu!
30 Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Mtu anakuja baada yangu ambaye ni mkuu kuniliko mimi, kwa kuwa alikuwepo kabla yangu.’
Huyu ndiye niliyesema juu yake: Baada yangu anakuja mtu mmoja aliye mkuu zaidi kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa!
31 Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini sababu ya kuja nikibatiza kwa maji ni ili yeye apate kufunuliwa kwa Israeli.”
Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini nimekuja kubatiza kwa maji ili watu wa Israeli wapate kumjua.”
32 Kisha Yohana akatoa ushuhuda huu: “Nilimwona Roho akishuka kutoka mbinguni kama hua, akakaa juu yake.
Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa: “Nilimwona Roho akishuka kama njiwa kutoka mbinguni na kutua juu yake.
33 Mimi nisingemtambua, lakini yeye aliyenituma nibatize kwa maji alikuwa ameniambia, ‘Yule mtu utakayemwona Roho akimshukia na kukaa juu yake, huyo ndiye atakayebatiza kwa Roho Mtakatifu.’
Mimi sikumjua, lakini yule aliyenituma nikabatize watu kwa maji alikuwa ameniambia: Mtu yule utakayemwona Roho akimshukia kutoka mbinguni na kukaa juu yake, huyo ndiye anayebatiza kwa Roho Mtakatifu.
34 Mimi mwenyewe nimeona jambo hili na ninashuhudia kuwa huyu ndiye Mwana wa Mungu.”
Mimi nimeona na ninawaambieni kwamba huyu ndiye Mwana wa Mungu.”
35 Siku iliyofuata, Yohana alikuwa huko tena pamoja na wanafunzi wake wawili.
Kesho yake, Yohane alikuwa tena mahali hapo pamoja na wanafunzi wake wawili.
36 Alipomwona Yesu akipita, akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu!”
Alipomwona Yesu akipita akasema, “Tazameni! Huyu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu.”
37 Wale wanafunzi wawili walipomsikia Yohana akisema haya, wakamfuata Yesu.
Hao wanafunzi walimsikia Yohane akisema maneno hayo, wakamfuata Yesu.
38 Yesu akageuka, akawaona wakimfuata akawauliza, “Mnataka nini?” Wakamwambia, “Rabi,” (maana yake Mwalimu), “Unaishi wapi?”
Basi, Yesu aligeuka, na alipowaona hao wanafunzi wanamfuata, akawauliza, “Mnatafuta nini?” Nao wakamjibu, “Rabi (yaani Mwalimu), unakaa wapi?”
39 Yesu akawajibu, “Njooni, nanyi mtapaona!” Hivyo wakaenda na kupaona mahali alipokuwa anaishi, wakakaa naye siku ile, kwa kuwa ilikuwa yapata saa kumi.
Yesu akawaambia, “Njoni, nanyi mtaona.” Hao wanafunzi wakamfuata, wakaona mahali alipokuwa anakaa, wakashinda naye siku hiyo. Ilikuwa yapata saa kumi jioni.
40 Andrea nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliosikia yale Yohana aliyokuwa amesema, naye ndiye alimfuata Yesu.
Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa hao wawili waliokuwa wamemsikia Yohane akisema hivyo, wakamfuata Yesu.
41 Kitu cha kwanza Andrea alichofanya ni kumtafuta Simoni nduguye na kumwambia, “Tumemwona Masiya” (yaani, Kristo).
Andrea alimkuta kwanza Simoni, ndugu yake, akamwambia, “Tumemwona Masiha” (maana yake Kristo).
42 Naye akamleta kwa Yesu. Yesu akamwangalia na kusema, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohana. Utaitwa Kefa” (ambalo limetafsiriwa Petro).
Kisha akampeleka Simoni kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama Simoni akasema, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohane. Sasa utaitwa Kefa.” (maana yake ni Petro, yaani, “Mwamba.”)
43 Siku iliyofuata Yesu aliamua kwenda Galilaya. Akamkuta Filipo, akamwambia, “Nifuate.”
Kesho yake Yesu aliamua kwenda Galilaya. Basi, akamkuta Filipo, akamwambia, “Nifuate.”
44 Basi Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji alikotoka Andrea na Petro.
Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji wa akina Andrea na Petro.
45 Filipo naye akamkuta Nathanaeli na kumwambia, “Tumemwona yeye ambaye Mose aliandika habari zake katika Sheria na ambaye pia manabii waliandika kumhusu, yaani, Yesu wa Nazareti, mwana wa Yosefu.”
Naye Filipo akamkuta Nathanieli, akamwambia, “Tumemwona yule ambaye Mose aliandika juu yake katika kitabu cha Sheria, na ambaye manabii waliandika habari zake, yaani Yesu Mwana wa Yosefu, kutoka Nazareti.”
46 Nathanaeli akauliza, “Nazareti! Je, kitu chochote chema chaweza kutoka Nazareti?” Filipo akamwambia, “Njoo uone.”
Naye Nathanieli akamwuliza Filipo, “Je, kitu chema chaweza kutoka Nazareti?” Filipo akamwambia, “Njoo uone.”
47 Yesu alipomwona Nathanaeli anakaribia, akanena habari zake akasema, “Tazama huyu ni Mwisraeli kweli kweli; hana hila ndani yake.”
Yesu alipomwona Nathanieli akimjia alisema juu yake, “Tazameni! Huyo ni Mwisraeli halisi: hamna hila ndani yake.”
48 Nathanaeli akamuuliza, “Umenifahamuje?” Yesu akamjibu, “Nilikuona ulipokuwa bado uko chini ya mtini, kabla hata Filipo hajakuita.”
Naye Nathanieli akamwuliza, “Umepataje kunijua?” Yesu akamwambia, “Ulipokuwa chini ya mtini hata kabla Filipo hajakuita, nilikuona.”
49 Nathanaeli akamwambia, “Rabi, wewe ni Mwana wa Mungu! Wewe ni Mfalme wa Israeli!”
Hapo Nathanieli akamwambia, “Mwalimu, wewe ni Mwana wa Mungu. Wewe ni Mfalme wa Israeli!”
50 Yesu akamwambia, “Unaamini kwa kuwa nilikuambia nilikuona ulipokuwa bado uko chini ya mtini? Basi utaona mambo makuu zaidi kuliko hilo.”
Yesu akamwambia, “Je, umeamini kwa kuwa nimekwambia kwamba nilikuona chini ya mtini? Utaona makubwa zaidi kuliko haya.”
51 Ndipo akawaambia, “Amin, amin nawaambia, ninyi mtaona mbingu ikifunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.”
Yesu akaendelea kusema, “Nawaambieni kweli, mtaona mbingu zinafunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Mtu.”

< Yohana 1 >