< Ayubu 9 >
1 Kisha Ayubu akajibu:
2 “Naam, najua hili ni kweli. Lakini mwanadamu awezaje kuwa mwadilifu mbele za Mungu?
3 Ingawa mtu angetaka kushindana naye, asingaliweza kumjibu Mungu hata mara moja miongoni mwa elfu moja.
4 Hekima yake ni kubwa sana na ana uwezo mwingi mno. Ni nani aliyempinga naye akawa salama?
5 Aiondoa milima bila yenyewe kujua na kuipindua kwa hasira yake.
6 Aitikisa dunia kutoka mahali pake na kuzifanya nguzo zake zitetemeke.
7 Husema na jua, nalo likaacha kuangaza; naye huizima mianga ya nyota.
8 Yeye peke yake huzitandaza mbingu na kuyakanyaga mawimbi ya bahari.
9 Yeye ndiye Muumba wa nyota za Dubu, na Orioni, Kilimia, na makundi ya nyota za kusini.
10 Hutenda maajabu yasiyopimika, miujiza isiyoweza kuhesabiwa.
11 Anapopita karibu nami, siwezi kumwona; apitapo mbele yangu, simtambui.
12 Anapochukua kwa ghafula, ni nani awezaye kumzuia? Ni nani awezaye kumwambia, ‘Unafanya nini?’
13 Mungu hataizuia hasira yake; hata jeshi kubwa la Rahabu lenye nguvu linajikunyata miguuni pake.
14 “Ni vipi basi mimi nitaweza kubishana naye? Nawezaje kupata maneno ya kuhojiana naye?
15 Ingawa sikuwa na hatia, sikuweza kumjibu; ningeweza tu kumsihi Mhukumu wangu anihurumie.
16 Hata kama ningemwita kwenye shauri, naye akakubali, siamini kama angenisikiliza.
17 Yeye angeniangamiza kwa dhoruba na kuongeza majeraha yangu pasipo na sababu.
18 Asingeniacha nipumue bali angenifunika kabisa na huzuni kuu.
19 Kama ni suala la nguvu, yeye ni mwenye nguvu! Kama ni suala la haki, ni nani awezaye kumwita mahakamani?
20 Hata kama sikuwa na hatia, kinywa changu kingenihukumu; kama sikuwa na kosa, kingenitangaza kuwa mwenye hatia.
21 “Ingawa mimi sina kosa, haileti tofauti katika nafsi yangu; nauchukia uhai wangu.
22 Hayo yote ni sawa; ndiyo sababu nasema, ‘Yeye huwaangamiza wasio na makosa pamoja na waovu.’
23 Wakati pigo liletapo kifo cha ghafula, yeye hudhihaki kule kukata tamaa kwa yule asiye na kosa.
24 Wakati nchi inapoangukia mikononi mwa waovu, yeye huwafunga macho mahakimu wake. Kama si yeye, basi ni nani?
25 “Siku zangu zapita mbio kuliko mkimbiaji; zinapita upesi bila kuona furaha hata kidogo.
26 Zinapita upesi kama mashua ya mafunjo, mfano wa tai ayashukiaye mawindo kwa ghafula.
27 Kama nikisema, ‘Nitayasahau malalamiko yangu, nitabadili sura ya uso wangu na kutabasamu,’
28 bado ninahofia mateso yangu yote, kwa kuwa ninajua hutanihesabu kuwa sina hatia.
29 Kwa kuwa nimeonekana mwenye hatia, kwa nini basi nitaabishwe bure?
30 Hata kama ningejiosha kwa sabuni na kutakasa mikono yangu kwa magadi,
31 wewe ungenitupa kwenye shimo la utelezi kiasi kwamba hata nguo zangu zingenichukia sana.
32 “Yeye si mwanadamu kama mimi ili niweze kumjibu, ili kwamba tuweze kushindana naye mahakamani.
33 Laiti angelikuwepo mtu wa kutupatanisha kati yetu, aweke mkono wake juu yetu sote wawili,
34 mtu angeliiondoa fimbo ya Mungu juu yangu, ili utisho wake usiendelee kunitia hofu.
35 Ndipo ningenena naye, bila kumwogopa, lakini kama ilivyo kwangu sasa, sitaweza.