< Ayubu 8 >
1 Kisha Bildadi Mshuhi akajibu:
2 “Hata lini wewe utasema mambo kama haya? Maneno yako ni kama upepo mkuu.
3 Je, Mungu hupotosha hukumu? Je, Mwenyezi hupotosha kile kilicho haki?
4 Watoto wako walipomtenda dhambi, aliwapa adhabu ya dhambi yao.
5 Lakini ukimtafuta Mungu, nawe ukamsihi Mwenyezi,
6 ikiwa wewe ni safi na mnyofu, hata sasa atainuka mwenyewe kwa niaba yako, na kukurudisha katika mahali pako pa haki.
7 Ijapokuwa mwanzo wako ulikuwa mdogo, lakini mwisho wako utakuwa wa mafanikio.
8 “Ukaulize vizazi vilivyotangulia na uone baba zao walijifunza nini,
9 kwa kuwa sisi tumezaliwa jana tu na hatujui lolote, nazo siku zetu duniani ni kama kivuli tu.
10 Je, hawatakufundisha na kukueleza? Je, hawataleta maneno kutoka kwenye kufahamu kwao?
11 Je, mafunjo yaweza kumea mahali pasipo na matope? Matete yaweza kustawi bila maji?
12 Wakati bado yanaendelea kukua kabla ya kukatwa, hunyauka haraka kuliko majani mengine.
13 Huu ndio mwisho wa watu wote wanaomsahau Mungu; vivyo hivyo matumaini ya wasiomjali Mungu huangamia.
14 Lile analolitumainia huvunjika upesi; lile analolitegemea ni utando wa buibui.
15 Huutegemea utando wake, lakini hausimami; huungʼangʼania, lakini haudumu.
16 Yeye ni kama mti ulionyeshewa vizuri wakati wa jua, ukieneza machipukizi yake bustanini;
17 huifunganisha mizizi yake kwenye lundo la mawe, na kutafuta nafasi katikati ya mawe.
18 Unapongʼolewa kutoka mahali pake, ndipo mahali pale huukana na kusema, ‘Mimi kamwe sikukuona.’
19 Hakika uhai wake hunyauka, na kutoka udongoni mimea mingine huota.
20 “Hakika Mungu hamkatai mtu asiye na hatia, wala kuitia nguvu mikono ya mtenda mabaya.
21 Bado atakijaza kinywa chako na kicheko, na midomo yako na kelele za shangwe.
22 Adui zako watavikwa aibu, nazo hema za waovu hazitakuwepo tena.”