< Ayubu 5 >

1 “Ita kama unataka, lakini ni nani atakayekujibu? Ni yupi kati ya hao watakatifu utakayemgeukia?
Ita sasa; je kuna yeyote ambaye atakujibu? Utamrudia yupi katika watakatifu hao?
2 Kuweka uchungu moyoni humuua mpumbavu, nao wivu humchinja mjinga.
Kwa kuwa hasira huua mtu mpumbavu; wivu huua mjinga.
3 Mimi mwenyewe nimemwona mpumbavu akistawi, lakini ghafula nyumba yake ikawa imelaaniwa.
Nimemuona mtu mpumbavu akishika mzizi, lakini ghafla niliyalaani makazi yake.
4 Watoto wake wako mbali na usalama, hushindwa mahakamani bila mtetezi.
Watoto wake wako mbali na uzima; wameangamia langoni mwa mji. Hakuna yeyote atakaye waponya.
5 Wenye njaa huyala mavuno yake, wakiyatoa hata katikati ya miiba, nao wenye kiu huitamani sana mali yake.
Mwenye njaa hula mavuno yao; hata huyachukua katikati ya miiba. Wenye kiu huzihemea mali zao.
6 Kwa maana taabu haioti kutoka kwenye udongo, wala udhia hauchipui kutoka ardhini.
Kwa kuwa magumu hayatoki udongoni; wala taabu haichipuki katika nchi.
7 Lakini mwanadamu huzaliwa ili kutaabika, kwa hakika kama cheche za moto zirukavyo kuelekea juu.
Badala yake, wanadamu huzaliwa kwaajili ya taabu, kama tu cheche za moto zirukavyo juu.
8 “Lakini ingekuwa ni mimi, ningemlalamikia Mungu, ningeliweka shauri langu mbele zake.
Lakini kwa mimi, ningemrudia Mungu mwenyewe; kwake ningeaminisha kusudi langu -
9 Yeye hutenda maajabu yasiyoweza kutambuliwa, miujiza isiyoweza kuhesabika.
yeye afanyae makuu na mambo yasiyochunguzika, mambo ya ajabu yasiyo na hesabu.
10 Yeye huipa nchi mvua, huyapeleka maji kunyesha mashamba.
Hutoa mvua juu ya nchi, na huyapeleka maji mashambani.
11 Huwainua juu wanyonge, nao wale waombolezao huinuliwa wakawa salama.
Hufanya haya kwaajili ya kuwainua juu hao walio chini; huwapandisha sehemu salama hao waombolezao.
12 Huipinga mipango ya wenye hila, ili mikono yao isifikie ufanisi.
Yeye huharibu mipango ya watu wenye hila, ili mikono yao isipate mafanikio.
13 Yeye huwanasa wenye hekima katika hila yao, nayo mipango ya wadanganyifu huifagilia mbali.
Yeye huwanasa watu wenye hekima katika matendo ya hila zao wenyewe; mipango ya watu waliogeuzwa huharibika haraka.
14 Giza huwapata wakati wa mchana; wakati wa adhuhuri hupapasa kama vile usiku.
Wao hupatwa na giza wakati wa mchana, na hupapasa mchana kama vile ni usiku.
15 Humwokoa mhitaji kutokana na upanga ulioko kinywani mwao; huwaokoa kutokana na makucha ya wenye nguvu.
Lakini yeye huokoa maskini kwa upanga wa vinywa vyao na mhitaji kwa mkono wa mtu mwenye nguvu.
16 Kwa hiyo maskini analo tarajio, nao udhalimu hufumba kinywa chake.
Hivyo mtu maskini ana matumaini, na udhalimu hufumba kinywa chake mwenyewe.
17 “Heri mtu yule ambaye Mungu humrudi; kwa hiyo usidharau adhabu yake Mwenyezi.
Tazama, amebarikiwa mtu ambaye hutiwa adabu na Mungu; kwa sababu hiyo, usidharau uongozi wa Mwenyezi.
18 Kwa kuwa hutia jeraha, lakini pia huyafunga; huumiza, lakini mikono yake pia huponya.
Kwa kuwa yeye hujeruhi na kisha huuguza; yeye hutia jeraha na kisha mikono yake huponya.
19 Kutoka majanga sita atakuokoa; naam, hata katika saba hakuna dhara litakalokupata wewe.
Yeye atakuokoa na mateso sita; kweli, katika mateso saba, hakuna uovu utakao kugusa.
20 Wakati wa njaa atakukomboa wewe na kifo, naye katika vita atakukomboa na pigo la upanga.
Wakati wa njaa atakukomboa na kifo, na kwa uwezo wa upanga wakati wa vita.
21 Utalindwa kutokana na kichapo cha ulimi, wala hutakuwa na sababu ya kuogopa maangamizi yatakapokujia.
Wewe utafichwa na mateso ya ulimi; na usitishike na uharibifu utakapokuja.
22 Utayacheka maangamizo na njaa, wala hutakuwa na sababu ya kuwaogopa wanyama wakali wa mwituni.
Wewe utaufurahia uharibifu na njaa, na hutatishika na wanyama wakali wa nchi.
23 Kwa kuwa utakuwa na agano na mawe ya mashamba, nao wanyama wa mwitu watakuwa na amani nawe.
Kwa kuwa wewe utakuwa na mapatano na mawe ya shambani mwako, na wanyama wa mwituni watakuwa na amani na wewe.
24 Utajua ya kwamba hema lako li salama; utahesabu mali zako wala hutakuta chochote kilichopungua.
Wewe utajua kwamba hema lako lina usalama; utatembelea zizi la kondoo wako na hutakosa kitu chochote.
25 Utajua ya kuwa watoto wako watakuwa wengi, nao wazao wako wengi kama majani ya nchi.
Pia utafahamu kwamba uzao wako utakuwa mwingi, na vizazi vyako vitakuwa kama nyasi ardhini.
26 Utaingia kaburini ukiwa na umri wa uzee mtimilifu, kama masuke ya ngano yakusanywapo kwa wakati wake.
Wewe utafika kaburini kwako mwenye umri kamili, kama vile rundo la mashuke ya nafaka liendavyo juu wakati wake.
27 “Tumelichunguza hili, nalo ni kweli. Hivyo lisikie na ulitendee kazi.”
Tazama, tumelipeleleza jambo hili; ndivyo lilivyo; lisikie, na ulifahamu kwa ajili yako mwenyewe.”

< Ayubu 5 >