< Ayubu 42 >

1 Ndipo Ayubu akamjibu Bwana:
Kisha Ayubu akamjibu Yahweh na kusema,
2 “Ninajua ya kuwa unaweza kufanya mambo yote, wala hakuna mpango wako unaoweza kuzuilika.
“Ninajua kwamba unaweza kufanya mambo yote, ya kuwa hakuna kusudi lako linaweza kuzuiliwa.
3 Uliuliza, ‘Ni nani huyu afichaye mashauri yangu bila maarifa?’ Hakika nilisema juu ya mambo niliyokuwa siyaelewi, mambo ya ajabu mno kwangu mimi kuyajua.
Ni nani huyo ambaye pasipo maarifa huificha mipango? Kwa kweli nilisema mambo ambayo sikuyaelewa, mambo magumu kwangu kuyafahamu, ambayo juu yake sikujua chochote.
4 “Ulisema, ‘Sikiliza sasa, nami nitanena; nitakuuliza swali, nawe yakupasa kunijibu.’
Uliniambia, 'Sikiliza sasa, nami nitasema; nitakuuliza mambo, nawe utaniambia.'
5 Masikio yangu yalikuwa yamesikia habari zako, lakini sasa macho yangu yamekuona.
Nimekuwa nikikusikia kwa usikivu wa sikio langu, lakini sasa jicho langu linakuona wewe.
6 Kwa hiyo najidharau mwenyewe, na kutubu katika mavumbi na majivu.”
Basi ninajidharau mwenyewe; ninatubu kwa mavumbi na majivu.”
7 Baada ya Bwana kusema mambo haya yote na Ayubu, akamwambia Elifazi Mtemani, “Nina hasira juu yako na juu ya rafiki zako wawili, kwa sababu hamkusema yaliyo sawa kwa habari yangu, kama alivyosema mtumishi wangu Ayubu.
Ilitokea baada ya kuwa amekwisha kusema maneno hata kwa Ayubu, Yahweh alimwambia Elifazi Mtemani, “Ghadhabu yangu imewaka dhidi yako na dhidi ya marafiki zako wawili kwa kuwa hamkusema maneno ya haki juu yangu kama alivyofanya mtumishi wangu Ayubu.
8 Basi sasa chukueni mafahali saba na kondoo dume saba mkamwendee mtumishi wangu Ayubu nanyi mkatoe sadaka za kuteketezwa kwa ajili yenu wenyewe. Mtumishi wangu Ayubu ataomba kwa ajili yenu, nami nitayakubali maombi yake ili nisiwatendee sawasawa na upumbavu wenu. Ninyi hamkusema yaliyo sawa kwa habari yangu, kama alivyosema mtumishi wangu Ayubu.”
Sasa basi, jitwalieni mafahari saba na mabeberu saba, kisha mmwendee mtumishi wangu Ayubu na mtoe sadaka ya kuteketezwa kwa ajili yenu. Ndipo Mtumishi wangu Ayubu atawaombea ninyi, nami nitayapokea maombi yake, ili kwamba nisiwashughulikie sawasawa na upumbavu wenu. Maana hamkusema mambo ya haki juu yangu, kama alivyofanya mtumishi wangu Ayubu.”
9 Kwa hiyo Elifazi Mtemani, Bildadi Mshuhi, na Sofari Mnaamathi wakafanya kama Bwana alivyowaambia; naye Bwana akayakubali maombi ya Ayubu.
Basi Elifazi Mtemani, Bildadi Mshuhi na Zofari Mnaamathi walienda na kufanya kama vile Yahweh alivyowaamuru, na Mungu alimtakabali Ayubu.
10 Baada ya Ayubu kuwaombea rafiki zake, Bwana akamwondoa kwenye uteka, akamfanikisha tena naye akampa mara mbili ya vile alivyokuwa navyo hapo mwanzoni.
Na wakati Ayubu alimpowaombea rafiki zake, Yahweh alirejeza bahati yake. Yahweh alimjalia mara mbili ya kile alichokimiliki hapo awali.
11 Ndipo ndugu zake wote waume kwa wake na kila mtu aliyemfahamu mwanzoni, wakaja wakala pamoja naye katika nyumba yake. Wakamfariji na kumtuliza moyo juu ya taabu yote Bwana aliyoileta juu yake, nao kila mmoja akampa kipande cha fedha na pete ya dhahabu.
Ndipo ndugu zake na Ayubu, na wale jamaa zake wote walikuwa wanajuana naye hapo mwanzo, walikuja hapo kwake na kula chakula pamoja naye katika nyumba yake. Waliomboleza pamoja naye na walimfariji kwa ajili majanga yote ambayo Yahweh alikuwa ameyaleta juu yake. Kila mtu alimpa Ayubu kipande cha fedha na pete ya dhahabu.
12 Bwana akaibariki sehemu ya mwisho ya maisha ya Ayubu kuliko ile ya kwanza. Alikuwa na kondoo elfu kumi na nne, ngamia elfu sita, jozi za mafahali elfu moja, na punda wa kike elfu moja.
Yahweh aliubarikiwa mwisho wa maisha ya Ayubu kuliko mwanzo wake; alikuwa na kondoo kumi na nne elfu, ngamia elfu sita, jozi elfu moja, na punda jike elfu moja.
13 Tena alikuwa na wana saba na binti watatu.
Pia alikuwa na wana saba na mabinti watatu.
14 Binti wa kwanza aliitwa Yemima, wa pili Kesia na wa tatu Keren-Hapuki.
Binti wa kwanza alimwita Yemima, na wa pili Kezia, na wa tatu Kerenihapuki.
15 Hapakuwepo mahali popote katika nchi ile yote palipopatikana wanawake wazuri kama binti za Ayubu; naye baba yao akawapa urithi pamoja na ndugu zao.
Katika nchi yote hawakupatikana wanawake wazuri kama mabinti wa Ayubu. Baba yao aliwapa urithi miongoni mwa kaka zao.
16 Baada ya hili Ayubu akaishi miaka 140; akawaona wanawe na wana wa wanawe hata kizazi cha nne.
Baada ya haya, Ayubu aliishi miaka 140; aliwaona wana wake na wana wa wanawe, hata kizazi cha nne.
17 Hivyo Ayubu akafa, akiwa mzee aliyekuwa ameshiba siku.
Basi Ayubu alifariki, akiwa mzee na akijawa na siku nyingi.

< Ayubu 42 >