< Ayubu 40 >
1 Bwana akamwambia Ayubu:
Yahweh aliendelea kuongea na Ayubu na kusema,
2 “Je, mwenye kushindana na Mwenyezi aweza kumsahihisha? Mwenye kumlaumu Mungu na ajibu.”
“Je mtu yeyote anayetaka kukosoa na ajaribu kumsahihisha Mwenye enzi? Na yeye anayehojiana na Mungu, na ajibu yeye.”
3 Ndipo Ayubu akamjibu Bwana:
Ndipo Ayubu akamjibu Yahweh na kusema, “
4 “Mimi sistahili kabisa: ninawezaje kukujibu wewe? Nauweka mkono wangu juu ya kinywa changu.
Tazama, mimi si mtu muhimu; je nawezaje kukujibu? Ninauweka mkono wangu juu ya mdomo wangu.
5 Nimesema mara moja, lakini sina jibu; naam, nimesema mara mbili, lakini sitasema tena.”
Ninazungumza mara moja, na sitakujibu; hakika, mara mbili, lakini sitaendelea zaidi.”
6 Ndipo Bwana akasema na Ayubu kutoka upepo wa kisulisuli:
Kisha Yahweh akamjibu Ayubu kutoka katika dhoruba kali na kusema,
7 “Jikaze kama mwanaume; nitakuuliza maswali, nawe yakupasa unijibu.
“Jifunge sasa mkanda kiunoni mwako kama mwanaume, kwa kuwa nitakuuliza maswali, nawe lazima unijibu.
8 “Je, utabatilisha hukumu yangu? Utanilaumu mimi ili kujihesabia haki mwenyewe?
Je waweza kusema kwa hakika kwamba mimi si mwenye haki? Je utanihukumu mimi ili useme wewe ni mwenye haki?
9 Je, una mkono kama wa Mungu, nawe waweza kutoa sauti ya ngurumo kama yake?
Je una mkono kama wa Mungu? Je waweza kutoa kishindo kwa sauti kama yeye?
10 Basi jivike mwenyewe utukufu na fahari, nawe uvae heshima na enzi.
Jivike sasa katika utukufu na katika utu; jivalie mwenyewe heshima na enzi.
11 Fungulia ukali wa ghadhabu yako, mtafute kila mwenye kiburi umshushe,
Sambaza ziada ya hasira yako; mtazame kila mmoja mwenye kiburi na umshushe chini.
12 mwangalie kila mtu mwenye kiburi na umnyenyekeze, waponde waovu mahali wasimamapo.
Mwangalie kila mmoja mwenye kiburi na umweke chini; wakanyage chini watu waovu mahali wanaposimama.
13 Wazike wote mavumbini pamoja; wafunge nyuso zao kaburini.
Wazike ardhini pamoja; zifunge nyuso zao katika sehemu zilizositirika.
14 Ndipo mimi mwenyewe nitakukubalia kuwa mkono wako mwenyewe wa kuume unaweza kukuokoa.
Ndipo pia nitakapokubali ya kwamba mkono wako wa kulia waweza kukuokoa.
15 “Mwangalie mnyama aitwaye Behemothi, niliyemuumba kama nilivyokuumba wewe, anayekula majani kama ngʼombe.
Mwangalie sasa kiboko, ambaye niliwafanya kama nilivyokufanya wewe; anakula nyasi kama ng'ombe.
16 Tazama basi nguvu alizo nazo kwenye viuno vyake, uwezo alio nao kwenye misuli ya tumbo lake!
Ona sasa, nguvu zake ziko katika viuno vyake; nguvu zake zi katika mishipa ya tumbo lake.
17 Mkia wake hutikisika kama mwerezi; mishipa ya mapaja yake imesukwa pamoja.
Yeye huuondoa mkia wake kama mti wa mwerezi; mishipa ya paja lake imeunganishwa pamoja.
18 Mifupa yake ni bomba za shaba, maungo yake ni kama fito za chuma.
Mifupa yake ni kama ya mirija ya shaba; na miguu yake ni kama kipande cha chuma.
19 Yeye ni wa kwanza miongoni mwa kazi za Mungu, lakini Muumba wake anaweza kumsogelea kwa upanga wake.
Yeye ni mkuu wa viumbe vya Mungu. Ni Mungu pekee, ambaye alimwumba, anaweza kumshinda.
20 Vilima humletea yeye mazao yake, nao wanyama wote wa porini hucheza karibu naye.
Kwa kuwa milima humpatia chakula; hayawani wa mashambani hucheza karibu.
21 Hulala chini ya mimea ya yungiyungi, katika maficho ya matete kwenye matope.
Hujilaza chini ya mimiea ya kivuli katika makao ya mianzi, na katika bwawa la matope.
22 Hiyo mimea ya yungiyungi humficha kwenye vivuli vyake; miti mirefu karibu na kijito humzunguka.
Miti yenye vivuli humfunika katika vivuli vyake; mierebi ya kijito inamzunguka pande zote.
23 Wakati mto ufurikapo, yeye hapati mshtuko wa hofu; yeye yu salama, hata kama Yordani ingefurika hadi kwenye kinywa chake.
Tazama, kama mto utazigharikisha kingo zake, hatikisiki; yeye anajiamini, hata kama Mto wa Yordani unajaa hadi katika pua yake.
24 Je, mtu yeyote anaweza kumkamata yeye akiwa macho, au kumnasa kwa mtego na kutoboa pua yake?
Je mtu yeyote aweza kumnasa kwa ndoano, au kuichoma pua yake kwa mtego?