< Ayubu 4 >
1 Ndipo Elifazi Mtemani akajibu:
2 “Kama mtu akithubutu kuzungumza nawe, kutakukasirisha? Lakini ni nani awezaye kujizuia asiseme?
3 Fikiri jinsi ambavyo umewafundisha watu wengi, jinsi ambavyo umeitia nguvu mikono iliyokuwa dhaifu.
4 Maneno yako yamewategemeza wale waliojikwaa; umeyatia nguvu magoti yaliyokuwa dhaifu.
5 Lakini sasa hii taabu imekujia wewe, nawe unashuka moyo; imekupiga wewe, nawe unafadhaika.
6 Je, kumcha Mungu kwako hakupaswi kuwa ndiyo matumaini yako na njia zako kutokuwa na lawama ndilo taraja lako?
7 “Fikiri sasa: Ni mtu yupi asiye na hatia ambaye aliwahi kuangamia? Ni wapi wanyofu waliwahi kuangamizwa?
8 Kwa jinsi ambavyo mimi nimechunguza, wale walimao ubaya na wale hupanda uovu, huvuna hayo hayo hayo.
9 Kwa pumzi ya Mungu huangamizwa; kwa mshindo wa hasira zake huangamia.
10 Simba anaweza kunguruma na kukoroma, lakini bado meno ya simba mkubwa huvunjika.
11 Simba anaweza kuangamia kwa kukosa mawindo, nao wana wa simba jike hutawanyika.
12 “Neno lililetwa kwangu kwa siri, masikio yangu yakasikia mnongʼono wake.
13 Katikati ya ndoto za kutia wasiwasi wakati wa usiku, hapo usingizi mzito uwapatapo wanadamu,
14 hofu na kutetemeka kulinishika na kufanya mifupa yangu yote itetemeke.
15 Kuna roho aliyepita mbele ya uso wangu, nazo nywele za mwili wangu zikasimama.
16 Yule roho akasimama, lakini sikuweza kutambua kilikuwa kitu gani. Umbo fulani lilisimama mbele ya macho yangu, kukawa na ukimya kisha nikasikia sauti:
17 ‘Je, binadamu aweza kuwa mwadilifu kuliko Mungu? Je, mtu aweza kuwa safi kuliko Muumba wake?
18 Kama Mungu hawaamini watumishi wake, kama yeye huwalaumu malaika zake kwa kukosea,
19 ni mara ngapi zaidi wale waishio katika nyumba za udongo wa mfinyanzi, ambazo misingi yake ipo mavumbini, ambao wamepondwa kama nondo!
20 Kati ya mawio na machweo huvunjwa vipande vipande; bila yeyote kutambua, huangamia milele.
21 Je, kamba za hema yao hazikungʼolewa, hivyo hufa bila hekima?’