< Ayubu 39 >

1 “Je, wajua ni wakati gani mbuzi wa mlimani wanapozaa? Je, watambua ni wakati gani kulungu jike azaapo mtoto wake?
Je unajua ni wakati gani mbuzi mwitu huzaa watoto wao katika miamba? Je waweza kuwangalia paa wakati wanapozaa watoto wao?
2 Je, waweza kuhesabu miezi hadi wazaapo? Je, unajua majira yao ya kuzaa?
Waweza kuhesabu miezi ya kuchukua mimba? Je unaujua muda ambao huzaa watoto wao?
3 Wao hujiinamisha na kuzaa watoto wao; utungu wa kuzaa unakoma.
Wanainama chini na kuzaa watoto wao, na kisha maumivu yao ya uzazi yanaishi.
4 Watoto wao hustawi na kuongezeka nguvu nyikani; huenda zao wala hawarudi tena.
Watoto wao huwa na nguvu na kukua katika uwanda wa wazi; hutoka nje na hawarudi tena.
5 “Ni nani aliyemwachia punda-mwitu awe huru? Ni nani aliyezifungua kamba zake?
Ni nani huwaacha punda mwitu waende huru? Je nani amevilegeza vifungo vya punda wepesi,
6 Nimempa nchi isiyokaliwa na watu kuwa masikani yake, nchi ya chumvi kuwa makao yake.
ni nyumba ya nani nimeifanya katika Araba, au nyumba yake katika nchi ya chumvi?
7 Huzicheka ghasia za mji, wala hasikii kelele za mwendesha gari.
Hucheka kwa dharau katika kelele katika mji; hasikilizi kelele za mwongozaji.
8 Huzunguka vilimani kwa ajili ya malisho na kutafuta kila kitu kibichi.
Hutembeatembea juu ya milima kama malisho yake; huko hutafuta kila mmea ulio wa kijani kwa ajili ya kula.
9 “Je, nyati atakubali kukutumikia? Atakaa karibu na hori lako usiku?
Je nyati atakuwa na furaha kukutumikia? Je atakubali kukaa katika zizi lako?
10 Je, waweza kumfungia kwenye matuta kwa kamba? Je, atalima mabonde nyuma yako?
Waweza kumwongoza nyati kulima mtaro kwa kamba? Je atachimba bonde kwa ajili yako?
11 Je, utamtumainia kwa ajili ya nguvu zake nyingi? Utamwachia yeye kazi zako nzito?
Je waweza kumtumaini kwasababu ya nguvu zake nyingi? Je waweza kumwachia kazi yako ili aifanye?
12 Utaweza kumwamini akuletee nafaka yako nyumbani kutoka shambani na kuikusanya kwenye sakafu yako ya kupuria?
Je waweza kumtegemea akuletee nyumbani nafaka, au kukusanya nafaka katika uwanda wako wa kupuria?
13 “Mbuni hupigapiga mabawa yake kwa furaha, lakini hayawezi kulinganishwa na mabawa na manyoya ya korongo.
Mabawa ya mbuni hupunga kwa majivuno, bali je mabawa na manyoya yana upendo?
14 Huyataga mayai yake juu ya ardhi, na kuyaacha yapate joto mchangani,
Kwa maana huuacha mayai yake katika nchi, na huyaacha yapate joto katika mavumbi;
15 bila kujali kuwa mguu waweza kuyaponda, kwamba baadhi ya wanyama wa porini wanaweza kuyakanyaga.
husahau kuwa mguu waweza kuyaharibu au kwamba mnyama mwitu aweza kuyakanyaga.
16 Yeye huyafanyia makinda yake ukatili kama vile si yake; hajali kwamba taabu yake inaweza ikawa bure,
Huyatendea vibaya makinda yake kana kwamba si yake; haogopi kwamba kazi yake yaweza kupotea bure,
17 kwa kuwa Mungu hakumjalia hekima, wala hakumpa fungu la akili njema.
kwasababu Mungu amemnyima hekima na hajampa ufahamu wowote.
18 Lakini akunjuapo mabawa yake kukimbia, humcheka farasi pamoja na yeye aliyempanda.
Na wakati anapokimbia kwa haraka, huwacheka kwa dharau farasi na mpanda farasi wake.
19 “Je, wewe humpa farasi nguvu au kuivika shingo yake manyoya marefu?
Je umempa farasi nguvu zake? Je umeivika shingo yake kwa manyoya?
20 Je, wewe humfanya farasi aruke kama nzige, akistaajabisha kwa tishio la mlio wake wa majivuno?
Je umemfanya aruke kama panzi? Enzi ya mlio wake ni wa kutisha.
21 Huparapara bila woga, akizifurahia nguvu zake, husonga mbele kukabiliana na silaha.
Hurarua kwa nguvu na kufurahia katika nguvu zake; hukimbia upesi kukutana na silaha.
22 Huicheka hofu, haogopi chochote, wala haukimbii upanga.
Huidharau hofu na hashangazwi; huwa harudi nyuma kutoka katika upanga.
23 Podo hutoa sauti kando yake, pamoja na mkuki unaongʼaa na fumo.
Podo hugongagonga ubavuni mwake, pamoja na mkuki unaong'aa na fumo.
24 Bila woga na kwa ghadhabu huimeza nchi, wala tarumbeta iliapo yeye hawezi kusimama.
Huimeza nchi kwa hasira na ghadhabu; katika sauti ya tarumbeta, hawezi kusimama sehemu moja.
25 Asikiapo sauti ya baragumu yeye hulia, ‘Aha!’ Hunusa harufu ya vita toka mbali, sauti ya mtoa amri na ukelele wa vita.
Wakati wowote tarumbeta inapolia, husema, 'Ooh! Huisikia harufu ya vita kutoka mbali - vishindo vya radi za makamanda na makelele.
26 “Je, mwewe huruka kwa hekima yako na kuyakunjua mabawa yake kuelekea kusini?
Je ni kwa hekima yako kwamba mwewe hupaa juu, na ya kuwa huyanyosha mabawa yake kwa upande wa kusini?
27 Je, tai hupaa juu kwa amri yako na kujenga kiota chake mahali pa juu?
Je ni kwa agizo lako kwamba tai huruka juu na kufanya kiota chake katika sehemu za juu?
28 Huishi juu ya miamba mirefu na kukaa huko usiku; majabali yenye ncha kali ndiyo ngome yake.
Huishi katika majabali na hufanya makao yake katika vilele vya majabali, na ngomeni.
29 Kutoka huko hutafuta chakula chake; macho yake hukiona kutoka mbali.
Kutoka huko hutafuta mawindo; macho yake huyaona mawindo kutoka mbali.
30 Makinda yake hujilisha damu, na pale palipo na machinjo, ndipo yeye alipo.”
Makinda yake hunywa damu pia; na pale walipo watu wafu, ndipo na yeye alipo.

< Ayubu 39 >