< Ayubu 38 >
1 Kisha Bwana akamjibu Ayubu kutoka upepo wa kisulisuli. Akasema:
Ndipo Yahweh alimwita Ayubu kutoka katika dhoruba kali na kumwambia,
2 “Nani huyu atiaye mashauri yangu giza kwa maneno yasiyo na maarifa?
“Huyu ni nani aletaye giza katika mipango kwa njia ya maneno bila maarifa?
3 Jikaze kama mwanaume; nitakuuliza swali, nawe unijibu.
Basi sasa jifunge kiunoni mwako kama mwanaume kwa kuwa nitakuuliza maswali, nawe lazima unijibu.
4 “Ulikuwa wapi nilipoweka misingi ya dunia? Niambie, kama unafahamu.
Wewe ulikuwa wapi wakati nilipoitandaza misingi ya dunia? Niambie, kama unao ufahamu zaidi.
5 Ni nani aliyeweka alama vipimo vyake? Hakika wewe unajua! Ni nani aliyenyoosha kamba ya kupimia juu yake?
Je ni nani aliyeamuru vipimo vyake? Niambie, kama unajua, ni nani alivinyosha vipimo juu yake?
6 Je, misingi yake iliwekwa juu ya nini, au ni nani aliyeweka jiwe la pembeni,
Misingi yake ilitandazwa juu ya nini? Ni nani aliyeliweka jiwe lake la pembeni
7 wakati nyota za asubuhi zilipoimba pamoja, na malaika wote walipokuwa wakipiga kelele kwa furaha?
wakati nyota za asubuhi zilipoimba pamoja na wana wote wa Mungu walipopiga kelele kwa furaha?
8 “Ni nani aliyeifungia bahari milango ilipopasuka kutoka tumbo,
Ni nani huifunga bahari kwa milango wakati inapofurika, kana kwamba inatoka katika tumbo,
9 nilipoyafanya mawingu kuwa vazi lake, na kuyafungia katika giza nene,
wakati nilipoyafanya mawingu kuwa ni mavazi yake, na giza nene kuwa mkanda wake wa kujifungia?
10 nilipoamuru mipaka yake, na kuiweka milango yake na makomeo mahali pake,
Hapo ilikuwa wakati nilipoweka bahari mpaka wangu, na nilipoweka makomeo yake na milango,
11 niliposema, ‘Unaweza kufika mpaka hapa wala si zaidi; hapa ndipo mawimbi yako yenye kiburi yatakapokomea’?
na wakati nilipoiambia, 'Unaweza kuja hapa kutoka mbali, lakini si zaidi; na hapa ndipo nitauweka mpaka kwa fahari ya mawimbi yako.'
12 “Umepata kuiamrisha asubuhi ipambazuke, au kuyaonyesha mapambazuko mahali pake,
Je tangu mwanzo wa siku zako, ulishawahi kuigiza asubuhi ianze, na kuyafanya mapambazuko yajue sehemu yake katika mpangilio wa vitu,
13 yapate kushika miisho ya dunia, na kuwakungʼuta waovu waliomo?
ili kwamba ishikilie sehemu za dunia ili watu waovu watikiswe mbali nayo.
14 Dunia hubadilika kama udongo wa mfinyanzi chini ya lakiri; sura yake hukaa kama ile ya vazi.
Dunia imebadilishwa katika mwonekano kama udongo unavyobadilika chini ya muhuri; vitu vyote husimama juu yake dhahiri kama cha kibindo cha nguo.
15 Waovu huzuiliwa nuru yao, nao mkono wao ulioinuliwa huvunjwa.
'Mwanga' wao umeondolewa kutoka kwa watu waovu; na mkono wao ulioinuliwa umevunjwa.
16 “Je, umepata kufika kwenye chemchemi za bahari? Au kutembea mahali pa ndani pa vilindi?
Je umeshaenda kwenye vyanzo vya maji ya bahari? Je umeshatembea sehemu za chini kabisa za kilindi?
17 Umewahi kuonyeshwa malango ya mauti? Umewahi kuiona milango ya uvuli wa mauti?
Je malango ya mauti yamefunuliwa kwako? Je umeshaona malango ya uvuli wa mauti?
18 Je, wewe unafahamu ukubwa wa dunia? Niambie kama unajua haya yote.
Je umeifahamu dunia katika upana wake? Niambie kama unayajua yote hayo.
19 “Njia ya kufika kwenye makao ya nuru ni ipi? Nako maskani mwa giza ni wapi?
Je iko wapi njia ya sehemu ya kupumzikia kwa mwanga, na kama ilivyo kwa giza, iko wapi sehemu yake?
20 Je, unaweza kuvirudisha kwenye makao yake? Unajua njia za kufika maskani mwake?
Je unaweza kuuongoza mwanga na giza katika sehemu zake za kazi? Waweza kuitambua njia ya kurudi katika nyumba zao?
21 Hakika unajua, kwa kuwa ulikuwa umeshazaliwa! Kwani umeishi miaka mingi!
Bila shaka unajua, kwa kuwa ulizaliwa wakati huo; hesabu ya siku zako ni kubwa sana!
22 “Je, umeshawahi kuingia katika ghala za theluji, au kuona ghala za mvua ya mawe,
Je ulishaingia katika ghala ya barafu, au umeshaiona ghala ya mawe ya mvua,
23 ambazo nimeziweka akiba kwa ajili ya wakati wa taabu, na kwa ajili ya wakati wa vita na mapigano?
vitu hivi nimeviweka kwa ajili ya siku za mateso, kwa siku za mapigano na vita?
24 Ni ipi njia iendayo mahali umeme wa radi unapotawanyiwa, au mahali upepo wa mashariki unaposambaziwa juu ya dunia?
Je iko wapi njia ya mshindo wa mwanga hutokea au je upepo husambazwa kutoka mashariki juu ya dunia?
25 Ni nani aliyepasua mifereji kwa ajili ya maji mengi ya mvua yaendayo kasi na njia ya umeme wa radi,
Ni nani aliyezitengeneza mifereji ya gharika ya mvua, au ni nani aliyezifanya njia za milipuko ya radi,
26 ili kusababisha mvua kunyeshea mahali pasipokaliwa na mtu, jangwa lisilo na yeyote ndani yake,
na kuifanya mvua inyeshe juu ya nchi ambazo hakuna mtu aishiye ndani yake, na juu ya jangwa, ambayo ndani yake hakuna mtu yeyote,
27 ili kuitosheleza nchi ya ukiwa na jangwa, na majani yaanze kumea ndani yake?
kwa kusudi la kutimiza mahitaji ya mikoa iliyo kame na yenye ukiwa, na kuyastawisha majani mororo?
28 Je, mvua ina baba? Ni nani baba azaaye matone ya umande?
Je kuna baba wa mvua? Ni nani aliyeyafanya matone ya umande?
29 Barafu inatoka tumbo la nani? Ni nani azaaye ukungu kutoka mbinguni,
Je barafu ilitoka katika tumbo la nani? Na ni nani aliyeizaa theluji nyeupe katika anga?
30 wakati maji yawapo magumu kama jiwe, wakati uso wa vilindi vya maji unapoganda?
Maji hujificha menyewe na kuwa kama jiwe; sehemu za juu za vilindi huwa kama barafu.
31 “Je, waweza kuufunga mnyororo wa Kilimia? Waweza kulegeza kamba za Orioni?
Je unaweza kuzifunga minyororo ya Kilimia, au kuvifungua vifundo vya Orioni?
32 Waweza kuyaongoza makundi ya nyota kwa majira yake, au kuongoza Dubu na watoto wake?
Je unaweza kuziongoza nyota kutokea katika nyakati zake? Je waweza kuongoza dubu pamoja na watoto wake?
33 Je, unajua sheria zinazotawala mbingu? Waweza kuweka utawala wa Mungu duniani?
Je unazijua sheria za anga? Wewe uliweza kuanzisha sheria za anga juu ya dunia?
34 “Waweza kuiinua sauti yako mpaka mawinguni, na kujifunika mwenyewe na gharika ya maji?
Je waweza kupaza sauti yako hadi mawinguni, ili kwamba maji mengi ya mvua yakufunike?
35 Je, wewe hutuma umeme wa radi kwenye njia zake? Je, hutoa taarifa kwako kukuambia, ‘Sisi tuko hapa’?
Je waweza kuagiza miali ya mwanga ili itokee, na kukwambia, 'Sisi tupo hapa'?
36 Ni nani aliyeujalia moyo hekima au kuzipa akili ufahamu?
Ni nani ameweka hekima katika mawingu au ni nani ameweka ufahamu kwa ukungu?
37 Nani mwenye hekima ya kuyahesabu mawingu? Ni nani awezaye kuinamisha magudulia ya mbinguni
Nani anaweza kuyahesabu mawingu kwa maarifa yake? Na ni nani awezaye kuvimwaga viriba vya anga
38 wakati mavumbi yawapo magumu, na mabonge ya udongo kushikamana pamoja?
wakati mavumbi yanapoungana kuwa kitu kigumu na mabonge ya dunia yanaposhikama kwa pamoja?
39 “Je, utamwindia simba jike mawindo, na kuwashibisha simba wenye njaa
Je waweza kuwinda mawindo kwa ajili ya simba jike au kutosheleza hamu ya watoto wadogo wa simba
40 wakati wao wamejikunyata mapangoni mwao, au wakivizia kichakani?
wakati wanapokwaruza kwaruza katika pango lao na kukaa katika kificho ili kulala katika hali ya kuvizia?
41 Ni nani ampaye kunguru chakula wakati makinda yake yanamlilia Mungu, yakizungukazunguka kwa ajili ya kukosa chakula?
Ni nani aletaye mawindo kwa ajili ya kunguru wakati ambapo watoto wao wanapomlilia Mungu na kutangatanga kwa kukosa chakula?