< Ayubu 37 >

1 “Kwa hili moyo wangu unatetemeka, nao unaruka kutoka mahali pake.
Hakika, moyo wangu hutetemeka kwa hili; umeondolewa kutoka katika sehemu yake.
2 Sikiliza! Sikiliza ngurumo ya sauti yake, sauti ya ngurumo itokayo kinywani mwake.
Sikia, Ee, Sikia kelele za sauti yake, sauti inayotoka katika mdomo wake.
3 Huuachilia umeme wake wa radi chini ya mbingu yote na kuupeleka hata miisho ya dunia.
Huiagiza sauti chini ya mbingu yote, na huutuma mwanga wake katika mipaka ya dunia.
4 Baada ya hayo huja sauti ya ngurumo yake; Mungu hunguruma kwa sauti yake ya fahari. Wakati sauti yake ingurumapo tena, huuachilia umeme wake wa radi.
Sauti huunguruma baada yake; yeye huunguruma kwa sauti ya ukuu wake; hauzuii mshindo wa mwanga wakati sauti yake inaposikika.
5 Sauti ya Mungu hunguruma kwa namna za ajabu; yeye hutenda mambo makuu kupita ufahamu wetu.
Mungu huunguruma kwa sauti yake kwa namna ya ajabu; yeye hufanya mambo makubwa ambayo sisi hatuwezi kuyafahamu.
6 Huiambia theluji, ‘Anguka juu ya dunia,’ nayo manyunyu ya mvua, ‘Uwe mvua ya nguvu.’
Kwa kuwa huiambia theluji, 'Angukeni juu ya dunia'; hali kadhalika kwa manyunyu ya mvua, 'Iweni manyunyu makubwa ya mvua.'
7 Ili wanadamu wote aliowaumba wapate kujua kazi zake, yeye humzuilia kila mtu shughuli zake.
Huuzuia mkono wa kila mtu usifanye kazi, ili kwamba watu wote aliowaumba wataona matendo yake.
8 Wanyama hujificha; hubakia kwenye mapango yao.
Kisha hayawani huenda na kujificha na kukaa katika mapango yake.
9 Dhoruba hutoka katika chumba chake, baridi hutoka katika upepo uendao kasi.
Dhoruba hutoka katika chumba chake upande wa kusini na baridi kutoka katika pepo zilizotawanyika katika upande wa Kaskazini.
10 Pumzi ya Mungu hutoa barafu, eneo kubwa la maji huganda.
Barafu imetolewa kwa pumzi ya Mungu; upana wa maji umeganda kama chuma.
11 Huyasheheneza mawingu kwa maji, naye husambaza umeme wake wa radi kupitia hayo.
Hakika, huyapima mawingu manene yenye unyevu; yeye huusambaza mwanga wake katika mawingu.
12 Nayo mawingu huzungukazunguka pande zote kwa amri yake, juu ya uso wa dunia yote, kufanya lolote ayaamuruyo.
Yeye huyazungusha mawingu kwa uongozi wake, ili yafanye chochote anayoyaagiza juu ya uso wote wa ulimwengu.
13 Huleta mawingu ili kuadhibu wanadamu, au kuinyeshea dunia yake na kuonyesha upendo wake.
Huyafanya haya yote yatokee; wakati mwingine hutokea kwa ajili ya kusahihisha, wakati mwingine kwa ajili ya nchi yake, na wakati mwingine ni kwa matendo ya agano la uaminifu.
14 “Ayubu, sikiliza hili; nyamaza na uyafikiri maajabu ya Mungu.
Yasikilize haya, Ayubu; acha na ufikiri juu matendo ya ajabu ya Mungu.
15 Je, unajua jinsi Mungu anavyoyaongoza mawingu, na kufanya umeme wake wa radi utoe mwanga?
Je unajua ni kwa namna gani Mungu hushurutisha mawingu na kuufanya mwanga wa radi ung'ae ndani yake?
16 Je, wajua jinsi mawingu yanavyokaa yakiwa yametulia, hayo maajabu yake yeye aliye mkamilifu katika maarifa?
Je unafahamu kuelea kwa mawingu, matendo ya ajabu ya Mungu, Je ni nani aliyemkamilifu katika maarifa?
17 Wewe unayeshindwa na joto katika nguo zako wakati nchi imenyamazishwa kimya bila upepo wa kusini,
Je unafahamu ni kwa jinsi gani mavazi yako huwa ya moto wakati nchi ikiwa imetulia kwasababu ya upepo unaotoka upande wa kusini?
18 je, waweza kuungana naye katika kuzitandaza anga, zilizo ngumu kama kioo cha shaba ya kuyeyushwa?
Je unaweza kulitandaza anga kama anavyofanya - anga ambalo lina nguvu kama kioo cha chuma kigumu?
19 “Tuambieni yatupasayo kumwambia; hatuwezi kutayarisha shauri letu kwa sababu ya ujinga wetu.
Tufundishe sisi kile tunachopaswa kumwambia yeye, kwa kuwa hatuwezi kutoa hoja zetu katika mpangilio kwasababu ya kiza katika akili zetu.
20 Je, aambiwe kwamba nataka kuongea? Je, yuko mtu ambaye angeomba kumezwa?
Je anapaswa kuambiwa kwamba ninapenda kuongea naye? Je mtu angependa kumezwa?
21 Basi hakuna awezaye kulitazama jua, jinsi linavyongʼaa angani, upepo ukishafagia mawingu.
Sasa, watu hawawezi kulitazama jua wakati linang'aa katika anga baada ya upepo kupita katikati yake na umelisafisha kwa mawingu yake.
22 Kutoka kaskazini yeye huja na fahari kuu; Mungu huja katika utukufu wa kutisha.
Kutoka upande wa kaskazini hutokea fahari ya dhahabu - juu ya Mungu kuna ukuu wa kutisha.
23 Yeye Mwenyezi hatuwezi kumfikia, naye ametukuzwa katika uweza; katika hukumu zake na haki yake kuu, hataonea.
Na kuhusu Mwenye nguvu, hatuwezi kumpata; yeye ni mkuu katika nguvu na haki. Yeye hatesi watu.
24 Kwa hiyo, wanadamu mheshimuni, kwa kuwa yeye hamstahi yeyote anayejidhania kuwa ana hekima.”
Hivyo basi, watu humwogopa. Yeye huwa hawajali wale ambao ni wenye hekima katika akili zao wenyewe.”

< Ayubu 37 >