< Ayubu 36 >
1 Elihu akaendelea kusema:
Elihu aliendelea na kusema,
2 “Nivumilie kidogo zaidi nami nitakuonyesha kwamba yako mengi zaidi ya kusemwa kwa ajili ya Mungu.
“Niruhusu niseme kidogo zaidi, nami nitakuonesha baadhi ya mambo kwasababu nina maneno machache ya kusema kwa ajili ya Mungu.
3 Ninayapata maarifa yangu kutoka mbali, nami nitamhesabia haki Muumba wangu.
Nitapata maarifa yangu kutoka mbali; nitatambua kwamba haki ni ya Muumba wangu.
4 Uwe na hakika kwamba maneno yangu si ya uongo; mmoja aliye mkamilifu katika maarifa yuko pamoja na wewe.
Kwa kweli, maneno yangu hayatakuwa ya uongo; mtu fulani aliyekomaa katika maarifa yu pamoja nawe.
5 “Mungu ni mwenye nguvu, lakini hamdharau mwanadamu; ni mwenye nguvu, naye ni thabiti katika shauri lake.
Angalia, Mungu ni mwenye nguvu, na hamdharau mtu yeyote; yeye ni mwenye nguvu katika uweza wa ufahamu.
6 Hawaachi waovu waendelee kuishi, bali huwapa walioteswa haki yao.
Yeye huwa hayahifadhi maisha ya watu waovu bali badala yake hufanya yaliyo ya haki kwa wale wanaoteseka.
7 Yeye haondoi macho yake kwa wenye haki; huwaketisha penye viti vya enzi pamoja na wafalme na kuwatukuza milele.
Haondoi macho yake kwa wenye haki bali badala yake huwaweka juu ya viti vya enzi kama wafalme milele, nao wameinuliwa juu.
8 Lakini ikiwa watu wamefungwa kwenye minyororo, wakiwa wameshikiliwa na kamba za mateso,
Ikiwa wamefungwa minyororo na kunaswa katika kamba za mateso,
9 huwaonyesha yale waliyoyatenda, kwamba wametenda dhambi kwa majivuno.
kisha huwafunulia kile walichokifanya, na maovu yao na kiburi chao.
10 Huwafanya wao kusikia maonyo, na huwaagiza kutubu uovu wao.
Hufungua pia masikio yao kwa ajili ya agizo lake, na huwaamuru wageuke kutoka katika uovu.
11 Kama wakitii na kumtumikia, wataishi siku zao zilizobaki katika mafanikio, na miaka yao katika utoshelevu.
Ikiwa watamsikiliza na kumwabudu yeye, wataishi katika mafanikio katika siku zao, na miaka yao katika hali ya kuridhika.
12 Lakini wasiposikiliza, wataangamia kwa upanga, nao watakufa pasipo maarifa.
Hata hivyo, kama hawatasikiliza, wataangamia kwa upanga; watakufa kwasababu hawana maarifa.
13 “Wasiomcha Mungu moyoni mwao huficha chuki; hata anapowafunga, hawamwombi msaada.
Na wale wasiomjua Mungu hutunza hasiria zao katika mioyo; hawaombi msaada hata wakati ambapo Mungu huwafunga.
14 Wanakufa wangali vijana, miongoni mwa wanaume hanithi wa mahali pa kuabudia miungu.
Hawa hufa katika ujana wao; na maisha yao hukoma kati ya makahaba.
15 Bali wao wanaoteseka huwaokoa katika mateso yao, na kuzungumza nao katika dhiki zao.
Mungu huwainua watu walioonewa kwa njia ya mateso yao; hufungua masikio yao kwa njia ya uonevu wao.
16 “Yeye anakubembeleza utoke katika mataya ya dhiki, ili kukuweka mahali palipo na nafasi mbali na kizuizi, hadi kwenye meza yako ya faraja iliyojaa vyakula vizuri.
Kwa hakika, yeye angependa kuwatoa ninyi katika mateso na kuwaweka katika sehemu pana ambapo hakuna masumbufu na mahali ambapo meza yenu ingewekwa ikiwa na chakula kilichojaa mafuta.
17 Lakini sasa umelemewa na hukumu kwa ajili ya uovu; hukumu na haki vimekukamata.
Lakini wewe umejaa hukumu juu ya watu waovu; hukumu na haki umeziachilia.
18 Uwe mwangalifu ili yeyote asikushawishi kwa utajiri; usipotoshwe kwa fungu kubwa la rushwa.
Usiuache utajiri ukuvute katika udanganyifu; na sehemu kubwa ya rushwa isikugeuze upande kutoka katika haki.
19 Je, utajiri wako hata nguvu zako nyingi vinaweza kukusaidia usiingie kwenye dhiki?
Je utajiri wako waweza kukunufaisha, ili kwamba usiwe katika taabu, au nguvu zako zote za uwezo zaweza kukusaidia?
20 Usiutamani usiku uje, ili uwaburute watu mbali na nyumba zao.
Usiutamani usiku ili utende dhambi dhidi ya wengine wakati ambapo mataifa hukatiliwa mbali katika nafasi zao.
21 Jihadhari usigeukie uovu, ambao unaupenda zaidi kuliko mateso.
Uwe mwangalifu ili kwamba usigeukie dhambi kwasababu unajaribiwa kwa mateso ili kwamba ukae mbali na dhambi.
22 “Mungu ametukuzwa katika nguvu zake. Ni nani aliye mwalimu kama yeye?
Angalia, Mungu ameinuliwa katika nguvu zake; ni nani aliye mwalimu kama yeye?
23 Ni nani aliyemwelekeza katika njia zake, au kumwambia, ‘Wewe umetenda yasiyo sawa’?
Ni nani alishamwalekeza njia yake? Nani anayeweza kumwambia, 'Wewe umetenda mambo yasiyo ya haki?'
24 Kumbuka kuzitukuza kazi zake, ambazo watu wamezisifu katika wimbo.
Kumbuka kuyasifu matendo yake, ambayo watu wameyaimba.
25 Wanadamu wote wameiona; watu wanaikazia macho kwa mbali.
Watu wote wameshayatazama hayo matendo, lakini wanayaona tu matendo hayo kwa mbali sana.
26 Tazama jinsi Mungu alivyo mkuu, kupita ufahamu wetu! Hesabu ya miaka yake haitafutiki.
Tazama, Mungu ni mkuu, lakini sisi hatumfahamu yeye vizuri; hesabu ya miaka yake haihesabiki.
27 “Yeye huvuta juu matone ya maji, ayachujayo kama mvua kutoka kwenye vijito;
Kwa kuwa yeye huvuta matone ya maji ili kuyachuja kama mvua katka mvuke wake,
28 mawingu huangusha chini maji yake, nayo mvua nyingi huwanyeshea wanadamu.
ambayo mawingu yake huyamwaga chini na kuyandondosha kwa wingi kwa mwanadamu.
29 Ni nani ajuaye jinsi ayatandazavyo mawingu, jinsi angurumavyo kutoka hemani mwake.
Hakika, kuna hata mmoja awezaye kuelewa kwa undani kusambaa kwa mawingu na radi kutoka katika nyumba yake?
30 Tazama jinsi anavyotandaza umeme wa radi kumzunguka, naye huvifunika vilindi vya bahari.
Angalia, hueneza mwanga wake kumzunguka na kufunika mizizi ya bahari.
31 Hivi ndivyo atawalavyo mataifa, na kuwapa chakula kwa wingi.
Kwa namna hii huyahukumu mataifa na kuwapa chakula kwa wingi.
32 Huujaza mkono wake kwa umeme wa radi, na kuuagiza kulenga shabaha yake.
Yeye huuijaza mikono yake kwa mwanga mpaka pale anapouamuru kupiga shabaha yake.
33 Ngurumo zake hutangaza dhoruba inayokuja; hata mifugo hujulisha kukaribia kwake.
Na muungurumo wake huonya kwa dhoruba, wanyama wanaweza kusikia kuja kwake.