< Ayubu 36 >
1 Elihu akaendelea kusema:
2 “Nivumilie kidogo zaidi nami nitakuonyesha kwamba yako mengi zaidi ya kusemwa kwa ajili ya Mungu.
3 Ninayapata maarifa yangu kutoka mbali, nami nitamhesabia haki Muumba wangu.
4 Uwe na hakika kwamba maneno yangu si ya uongo; mmoja aliye mkamilifu katika maarifa yuko pamoja na wewe.
5 “Mungu ni mwenye nguvu, lakini hamdharau mwanadamu; ni mwenye nguvu, naye ni thabiti katika shauri lake.
6 Hawaachi waovu waendelee kuishi, bali huwapa walioteswa haki yao.
7 Yeye haondoi macho yake kwa wenye haki; huwaketisha penye viti vya enzi pamoja na wafalme na kuwatukuza milele.
8 Lakini ikiwa watu wamefungwa kwenye minyororo, wakiwa wameshikiliwa na kamba za mateso,
9 huwaonyesha yale waliyoyatenda, kwamba wametenda dhambi kwa majivuno.
10 Huwafanya wao kusikia maonyo, na huwaagiza kutubu uovu wao.
11 Kama wakitii na kumtumikia, wataishi siku zao zilizobaki katika mafanikio, na miaka yao katika utoshelevu.
12 Lakini wasiposikiliza, wataangamia kwa upanga, nao watakufa pasipo maarifa.
13 “Wasiomcha Mungu moyoni mwao huficha chuki; hata anapowafunga, hawamwombi msaada.
14 Wanakufa wangali vijana, miongoni mwa wanaume hanithi wa mahali pa kuabudia miungu.
15 Bali wao wanaoteseka huwaokoa katika mateso yao, na kuzungumza nao katika dhiki zao.
16 “Yeye anakubembeleza utoke katika mataya ya dhiki, ili kukuweka mahali palipo na nafasi mbali na kizuizi, hadi kwenye meza yako ya faraja iliyojaa vyakula vizuri.
17 Lakini sasa umelemewa na hukumu kwa ajili ya uovu; hukumu na haki vimekukamata.
18 Uwe mwangalifu ili yeyote asikushawishi kwa utajiri; usipotoshwe kwa fungu kubwa la rushwa.
19 Je, utajiri wako hata nguvu zako nyingi vinaweza kukusaidia usiingie kwenye dhiki?
20 Usiutamani usiku uje, ili uwaburute watu mbali na nyumba zao.
21 Jihadhari usigeukie uovu, ambao unaupenda zaidi kuliko mateso.
22 “Mungu ametukuzwa katika nguvu zake. Ni nani aliye mwalimu kama yeye?
23 Ni nani aliyemwelekeza katika njia zake, au kumwambia, ‘Wewe umetenda yasiyo sawa’?
24 Kumbuka kuzitukuza kazi zake, ambazo watu wamezisifu katika wimbo.
25 Wanadamu wote wameiona; watu wanaikazia macho kwa mbali.
26 Tazama jinsi Mungu alivyo mkuu, kupita ufahamu wetu! Hesabu ya miaka yake haitafutiki.
27 “Yeye huvuta juu matone ya maji, ayachujayo kama mvua kutoka kwenye vijito;
28 mawingu huangusha chini maji yake, nayo mvua nyingi huwanyeshea wanadamu.
29 Ni nani ajuaye jinsi ayatandazavyo mawingu, jinsi angurumavyo kutoka hemani mwake.
30 Tazama jinsi anavyotandaza umeme wa radi kumzunguka, naye huvifunika vilindi vya bahari.
31 Hivi ndivyo atawalavyo mataifa, na kuwapa chakula kwa wingi.
32 Huujaza mkono wake kwa umeme wa radi, na kuuagiza kulenga shabaha yake.
33 Ngurumo zake hutangaza dhoruba inayokuja; hata mifugo hujulisha kukaribia kwake.