< Ayubu 33 >
1 “Lakini Ayubu, sasa, sikiliza maneno yangu; zingatia kila kitu nitakachosema.
2 Karibu nitafungua kinywa changu; maneno yangu yapo katika ncha ya ulimi wangu.
3 Maneno yangu yanatoka katika moyo mnyofu; midomo yangu hunena kwa uaminifu yale niyajuayo.
4 Roho wa Mungu ameniumba; pumzi ya Mwenyezi hunipa uhai.
5 Unijibu basi, kama unaweza; jiandae kunikabili mimi.
6 Mimi ni kama wewe mbele za Mungu; mimi pia nimetolewa kwenye udongo.
7 Huna sababu ya kuniogopa, wala mkono wangu haupaswi kukulemea.
8 “Lakini umesema nikiwa ninakusikia, nami nilisikia maneno yenyewe:
9 ‘Mimi ni safi na sina dhambi; mimi ni safi na sina hatia.
10 Lakini bado Mungu amepata dosari kwangu, naye ananiona kama adui yake.
11 Ananifunga miguu kwa pingu, tena anaziangalia njia zangu zote kwa karibu.’
12 “Lakini mimi ninakuambia, katika jambo hili wewe una makosa, kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mwanadamu.
13 Kwa nini unamlalamikia kwamba yeye hamjibu mwanadamu?
14 Kwa kuwa Mungu husema, wakati huu kwa njia moja, au wakati mwingine kwa njia nyingine, ingawa mwanadamu anaweza asielewe.
15 Mungu husema na mwanadamu katika ndoto, katika maono ya usiku, wakati usingizi mzito uwaangukiapo wanadamu wasinziapo vitandani mwao,
16 anaweza akasemea masikioni mwao, na kuwatia hofu kwa maonyo,
17 ili kumgeuza mtu kutoka kwenye kutenda mabaya na kumwepusha na kiburi,
18 kuiokoa nafsi yake na shimo, uhai wake usiangamizwe kwa upanga.
19 Mtu anaweza kutiwa adabu kwa maumivu kitandani mwake, kwa dhiki za mfululizo katika mifupa yake,
20 kiasi kwamba maisha yake yenyewe yanakataa chakula nayo nafsi yake ikakichukia kabisa hata chakula kizuri.
21 Nyama ya mwili wake huisha kwa kukonda, nayo mifupa yake ambayo mwanzoni ilikuwa imefichika, sasa inatokeza nje.
22 Nafsi yake inakaribia kaburi, nao uhai wake karibu na wajumbe wa kifo.
23 “Kama bado kuna malaika upande wake kama mtetezi, mmoja miongoni mwa elfu, wa kumwambia mwanadamu lililo jema kwake,
24 kumwonea huruma na kusema, ‘Mwokoe asije akatumbukia shimoni; nimepata ukombozi kwa ajili yake’:
25 ndipo nyama ya mwili wake hufanywa mpya kama ya mtoto; hurudishwa upya kama siku za ujana wake.
26 Humwomba Mungu, akapata kibali kwake, huuona uso wa Mungu na kushangilia kwa furaha; Mungu humrudisha katika hali yake ya uadilifu.
27 Ndipo huja mbele za watu na kusema, ‘Nilitenda dhambi na kupotosha kilichokuwa haki, lakini sikuadhibiwa kama nilivyostahili.
28 Alinikomboa nafsi yangu nisitumbukie shimoni, nami nitaishi ili kuufurahia mwanga.’
29 “Mungu hufanya haya yote kwa mwanadamu; mara mbili hata mara tatu,
30 ili aigeuze nafsi yake toka shimoni, ili nuru ya uzima imwangazie.
31 “Ayubu, zingatia, nisikilize mimi; nyamaza, nami nitanena.
32 Kama unalo lolote la kusema, unijibu; sema, kwa maana ninataka uonekane huna hatia.
33 Lakini kama huna la kusema, basi nisikilize mimi; nyamaza, nami nitakufundisha hekima.”