< Ayubu 30 >

1 “Lakini sasa watu wadogo kwa umri kuniliko wananidhihaki, watu ambao baba zao ningekataa kwa dharau kuwaweka pamoja na mbwa wangu wa kulinda kondoo.
Sasa vijana wananidhihaki - vijana ambao baba zao wasingeweza hata kuwahudumia mbwa wa kundi langu.
2 Nguvu za mikono yao zingekuwa na faida gani kwangu, kwa kuwa nguvu zao zilikuwa zimewaishia?
Kwa kweli, nguvu za mikono ya baba zao, zingenisaidia nini - watu ambao hawakuwa na nguvu wakati wa kukua kwao?
3 Wakiwa wamekonda kutokana na kupungukiwa na kwa njaa, walizurura usiku katika nchi kame iliyo ukiwa.
Walidhoofishwa na umasikini na njaa; walisaga nchi kavu mafichoni.
4 Katika vichaka walikusanya mimea ya chumvi, nacho chakula chao kilikuwa mizizi ya mti wa mfagio.
Walichuma mche chumvi na majani ya vichaka; mizizi ya mti wa ufagio ilikuwa ndiyo chakula chao.
5 Walifukuzwa mbali na watu wao, wakipigiwa kelele kama wevi.
Waliondolewa miongoni mwa watu waliopiga kelele nyuma yao kama ambavyo mtu angempigia kelele mwizi.
6 Walilazimika kuishi katika mikondo ya vijito vilivyokauka, kwenye majabali na mahandaki.
Hivyo walipaswa kuishi katika mabonde ya mto, katika mashimo ya ardhi na miamba.
7 Kwenye vichaka walilia kama punda, na walijisongasonga pamoja kwenye vichaka.
Walilia kwa uchungu porini kama punda; chini ya vichaka walikutana.
8 Wao ni watoto wa wapumbavu wenye asili ya ubaya, waliofukuzwa watoke katika nchi.
Walikuwa uzao wa wapumbavu, hakika, wa watu wasiofaa; waliondolewa duniani kama waarifu.
9 “Nao sasa wana wao wananidhihaki katika nyimbo; nimekuwa kitu cha dhihaka kwao.
Lakini sasa, nimekua sababu ya wimbo wa dhihaka kwa wana wao; hakika, nimekuwa mzaa kwao.
10 Wananichukia sana na kujitenga nami, wala hawasiti kunitemea mate usoni.
Wananichukia na kusimama mbali nami; hawaachi kunitemea usoni.
11 Sasa kwa kuwa Mungu ameilegeza kamba ya upinde wangu na kunitesa, wamekuwa huru kunitendea waonavyo.
Kwa maana Mungu ameondoa kamba katika upinde wangu na amenipiga, na hivyo watu hawa wanashindwa kujizuia mbele yangu.
12 Kuume kwangu kundi linashambulia; wao huitegea miguu yangu tanzi, na kunizingira.
Kundi la vijana wabaya wanashambulia nguvu zangu; wananiondolea mbali na kukusanya kinyume changu rundo la kuhusuru.
13 Huizuia njia yangu, nao hufanikiwa katika kuniletea maafa, nami sina yeyote wa kunisaidia.
Wanaharibu maisha yangu; wanapeleka mbele maangamizi yangu, watu wasio na wakuwazuia.
14 Wananijia kama watu wapitao katika ufa mpana; katikati ya magofu huja na kunishambulia.
Wanakuja kinyume changu kama jeshi katika tundu pana katika ukuta wa mji; katikati ya maangamizi wanajizungusha juu yangu.
15 Vitisho vimenifunika; heshima yangu imetoweshwa kama kwa upepo, salama yangu imetoweka kama wingu.
Hofu zimeniandama; heshima yangu imeondolewa mbali nami kama kwa upepo; mafanikio yangu yameondolewa kama wingu.
16 “Sasa maisha yangu yamefikia mwisho; siku za mateso zimenikamata.
Sasa uhai wangu umeondolewa ndani yangu; siku nyingi za maumivu zimenipita.
17 Usiku mifupa yangu inachoma; maumivu yanayonitafuna hayatulii kamwe.
Mifupa inauma ndani yangu wakati wa usiku; maumivu yanayonisaga hayaishi.
18 Kwa uwezo wake mkuu Mungu huwa kwangu kama nguo; hushikamana nami kama ukosi wa vazi langu.
Nguvu kuu ya Mungu imeshika mavazi yangu; yananizunguka kama kala ya vazi langu.
19 Yeye amenitupa kwenye matope, nami nimekuwa kama mavumbi na majivu.
Amenitupa matopeni; nimekuwa kama vumbi na majivu.
20 “Ee Bwana, ninakulilia wewe lakini hunijibu; ninasimama, nawe unanitazama tu.
Nakulilia wewe, Mungu, lakini haunijibu; ninasimama, nawe unaniangalia tu.
21 Wewe unanigeukia bila huruma; unanishambulia kwa nguvu za mkono wako.
Umegeuka na kuwa mkali kwangu; kwa nguvu za mkono wako umenitesa.
22 Unaninyakua na kunipeperusha kwa upepo; umenirusha huku na huko kwenye dhoruba kali.
Unaniinua katika upepo na kuufanya unikokote; unanirusha huku na kule katika dhoruba.
23 Ninajua utanileta mpaka kifoni, mahali ambapo wenye uhai wote wamewekewa.
Kwa maana najua ya kwamba utanipeleka mautini, nyumba ya hatima kwa viumbe vyote.
24 “Hakika hakuna yeyote amshambuliaye mhitaji, anapoomba msaada katika shida yake.
Lakini, je hakuna ainuaye mkono wake kuomba msaada aangukapo? Je hakuna aombaye msaada akiwa tabuni?
25 Je, sikulia kwa ajili ya wale waliokuwa katika taabu? Je, nafsi yangu haikusononeka kwa ajili ya maskini?
Je sikulia kwa ajili yake aliyekuwa tabuni? Je sijahuzunika kwa ajili ya mwitaji?
26 Lakini nilipotazamia mema, mabaya yalinijia; nilipotafuta nuru, ndipo giza lilipokuja.
Nilipotazamia mema, ndipo yalipokuja mabaya; niliposubiri nuru, giza lilikuja badala yake.
27 Kusukwasukwa ndani yangu kamwe hakutulii; siku za mateso zinanikabili.
Moyo wangu umetaabika na hautulii; siku za mateso zimenipata.
28 Ninazunguka nikiwa nimeungua, lakini si kwa jua; ninasimama katika kusanyiko nikiomba msaada.
Nimekuwa na ngozi nyeusi lakini si kwa sababu ya jua; nasimama katika kusanyiko na kulilia msaada.
29 Nimekuwa ndugu wa mbweha, rafiki wa mabundi.
Nimekuwa ndugu kwa mbwea, mshirika wa mbuni.
30 Ngozi yangu imekuwa nyeusi nayo inachunika; mifupa yangu inaungua kwa homa.
Ngozi yangu imekuwa nyeusi na inapukutika; mifupa yangu imeunguzwa na joto.
31 Kinubi changu kimegeuka kuwa maombolezo, nayo filimbi yangu imekuwa sauti ya kilio.
Kwa hiyo kinubi changu kimefunguliwa kwa nyimbo za maombolezo, zomari yangu kwa kuimba kwao waombolezao.

< Ayubu 30 >