< Ayubu 30 >
1 “Lakini sasa watu wadogo kwa umri kuniliko wananidhihaki, watu ambao baba zao ningekataa kwa dharau kuwaweka pamoja na mbwa wangu wa kulinda kondoo.
2 Nguvu za mikono yao zingekuwa na faida gani kwangu, kwa kuwa nguvu zao zilikuwa zimewaishia?
3 Wakiwa wamekonda kutokana na kupungukiwa na kwa njaa, walizurura usiku katika nchi kame iliyo ukiwa.
4 Katika vichaka walikusanya mimea ya chumvi, nacho chakula chao kilikuwa mizizi ya mti wa mfagio.
5 Walifukuzwa mbali na watu wao, wakipigiwa kelele kama wevi.
6 Walilazimika kuishi katika mikondo ya vijito vilivyokauka, kwenye majabali na mahandaki.
7 Kwenye vichaka walilia kama punda, na walijisongasonga pamoja kwenye vichaka.
8 Wao ni watoto wa wapumbavu wenye asili ya ubaya, waliofukuzwa watoke katika nchi.
9 “Nao sasa wana wao wananidhihaki katika nyimbo; nimekuwa kitu cha dhihaka kwao.
10 Wananichukia sana na kujitenga nami, wala hawasiti kunitemea mate usoni.
11 Sasa kwa kuwa Mungu ameilegeza kamba ya upinde wangu na kunitesa, wamekuwa huru kunitendea waonavyo.
12 Kuume kwangu kundi linashambulia; wao huitegea miguu yangu tanzi, na kunizingira.
13 Huizuia njia yangu, nao hufanikiwa katika kuniletea maafa, nami sina yeyote wa kunisaidia.
14 Wananijia kama watu wapitao katika ufa mpana; katikati ya magofu huja na kunishambulia.
15 Vitisho vimenifunika; heshima yangu imetoweshwa kama kwa upepo, salama yangu imetoweka kama wingu.
16 “Sasa maisha yangu yamefikia mwisho; siku za mateso zimenikamata.
17 Usiku mifupa yangu inachoma; maumivu yanayonitafuna hayatulii kamwe.
18 Kwa uwezo wake mkuu Mungu huwa kwangu kama nguo; hushikamana nami kama ukosi wa vazi langu.
19 Yeye amenitupa kwenye matope, nami nimekuwa kama mavumbi na majivu.
20 “Ee Bwana, ninakulilia wewe lakini hunijibu; ninasimama, nawe unanitazama tu.
21 Wewe unanigeukia bila huruma; unanishambulia kwa nguvu za mkono wako.
22 Unaninyakua na kunipeperusha kwa upepo; umenirusha huku na huko kwenye dhoruba kali.
23 Ninajua utanileta mpaka kifoni, mahali ambapo wenye uhai wote wamewekewa.
24 “Hakika hakuna yeyote amshambuliaye mhitaji, anapoomba msaada katika shida yake.
25 Je, sikulia kwa ajili ya wale waliokuwa katika taabu? Je, nafsi yangu haikusononeka kwa ajili ya maskini?
26 Lakini nilipotazamia mema, mabaya yalinijia; nilipotafuta nuru, ndipo giza lilipokuja.
27 Kusukwasukwa ndani yangu kamwe hakutulii; siku za mateso zinanikabili.
28 Ninazunguka nikiwa nimeungua, lakini si kwa jua; ninasimama katika kusanyiko nikiomba msaada.
29 Nimekuwa ndugu wa mbweha, rafiki wa mabundi.
30 Ngozi yangu imekuwa nyeusi nayo inachunika; mifupa yangu inaungua kwa homa.
31 Kinubi changu kimegeuka kuwa maombolezo, nayo filimbi yangu imekuwa sauti ya kilio.