< Ayubu 3 >

1 Baada ya jambo hili, Ayubu akafumbua kinywa chake na kuilaani siku ya kuzaliwa kwake.
Baada ya hayo, Ayubu akafunua kinywa chake na kuilani siku aliyozaliwa.
2 Kisha akasema:
Akasema,
3 “Siku ya kuzaliwa kwangu na ipotelee mbali, nao usiku ule iliposemekana, ‘Mtoto wa kiume amezaliwa!’
“Na ipotelee mbali siku niliyozaliwa mimi, usiku uliosema, 'Mimba ya mtoto wa kiume imetungwa.'
4 Siku ile na iwe giza; Mungu juu na asiiangalie; nayo nuru isiiangazie.
Siku hiyo na iwe giza; Mungu toka juu asiifikilie, wala mwanga usiiangazie.
5 Giza na kivuli kikuu kiikalie tena; wingu na likae juu yake; weusi na uifunike nuru yake.
Ishikwe na giza na giza la mauti liwe lake. Wingu na likae juu yake; kila kitu kiifanyacho siku kuwa giza kweli na kiitishe.
6 Usiku ule na ushikwe na giza kuu; usihesabiwe katika siku za mwaka, wala usihesabiwe katika siku za mwezi wowote.
Usiku huo, na ukamatwe na giza tororo. Usihesabiwe miongoni mwa siku za mwaka; na usiwekwe katika hesabu ya miezi.
7 Usiku ule na uwe tasa; sauti ya furaha na isisikike ndani yake.
Tazama, usiku huo na uwe tasa; na sauti ya shangwe isiwe ndani yake.
8 Wale wazilaanio siku wailaani hiyo siku, wale walio tayari kumwamsha Lewiathani.
Na wailani siku hiyo, hao wafahamuo namna ya kumuamsha lewiathani.
9 Nyota zake za alfajiri na ziwe giza; nao ungojee mwanga bila mafanikio, wala usiuone mwonzi wa kwanza wa mapambazuko,
Nyota za mapambazuko yake zitiwe giza. Siku hiyo iutafute mwanga, lakini isiupate; wala makope ya mapambazuko isiyaone,
10 kwa sababu huo usiku haukunifungia mlango wa tumbo la mama yangu, ili kuyaficha macho yangu kutokana na taabu.
kwasababu haikuifunga milango ya tumbo la mama yangu, na kwasababu haikunifichia taabu machoni pangu.
11 “Kwa nini sikuangamia wakati wa kuzaliwa? Kwa nini sikufa nilipokuwa ninatoka tumboni?
Kwanini si-kufa wakati lipotokeza katika tumbo la uzazi? Kwanini sikuitoa roho yangu hapo mama aliponizaa?
12 Kwa nini pakawa na magoti ya kunipokea na matiti ili nipate kunyonyeshwa?
kwanini magoti yake yalinipokea? Kwanini maziwa yake yanipokee hata ninyonye?
13 Kwa maana sasa ningekuwa nimepumzika kwa amani. Ningekuwa nimelala na kupumzika
Kwa sasa ningelikuwa nimelala chini kimya kimya. Ningelala usingizi na kupata pumziko
14 pamoja na wafalme na washauri wa dunia, waliojijengea mahali ambapo sasa ni magofu,
pamoja na wafalme na washauri wa dunia, ambao walijijengea makaburi ambayo sasa ni magofu.
15 pamoja na watawala waliokuwa na dhahabu, waliozijaza nyumba zao kwa fedha.
Au Ningelikuwa nimelala pamoja na wakuu wenye dhahabu, waliozijaza nyumba zao fedha.
16 Au kwa nini sikufichwa ardhini kama mtoto aliyezaliwa mfu, kama mtoto mchanga ambaye kamwe hakuuona mwanga?
Au pengine ningekuwa sijazaliwa, kama watoto wachanga wasio uona mwanga kabisa.
17 Huko waovu huacha kusumbua na huko waliochoka hupumzika.
Huko waovu huacha kusumbua; huko waliochoka hupumzika.
18 Wafungwa nao hufurahia utulivu wao, hawasikii tena sauti ya kukemea ya kiongozi wa watumwa.
Huko wafungwa kwa pamoja hupata amani; hawaisikii sauti ya msimamizi wa watumwa.
19 Wadogo na wakubwa wamo humo, na mtumwa ameachiwa huru kutoka kwa bwana wake.
Wote wadogo na watu maarufu wako huko; mtumishi yuko huru kwa bwana wake huko.
20 “Mbona nuru inawaangazia wale walio taabuni, na hao wenye uchungu kupewa uhai,
Kwa nini yeye aliye mashakani kupewa mwanga? Kwa nini hao wenye uchungu moyoni kupewa uhai,
21 wale wanaotamani kifo ambacho hakiji, wale watafutao kufa zaidi ya kutafuta hazina iliyofichwa,
ambao hutamani mauti lakini hawapati; ambao huyachimbulia mauti zaidi ya kutafuta hazina iliyofichika?
22 ambao hujawa na furaha, na hushangilia wafikapo kaburini?
Kwa nini kupewa mwanga ambao hushangilia mno na kufurahi walionapo kaburi?
23 Kwa nini uhai hupewa mtu ambaye njia yake imefichika, ambaye Mungu amemzungushia boma?
Kwanini kupewa mwanga mtu ambaye njia zake zimefichika, mtu ambaye Mungu amemzungushia uwa?
24 Kwa maana kulia kwangu kwa uchungu kwanijia badala ya chakula; kusononeka kwangu kunamwagika kama maji.
Kwa kuwa kushusha kwangu pumzi kwatokea badala ya kula; kuugua kwangu kumemiminika kama maji.
25 Lile nililokuwa naliogopa limenijia; lile nililokuwa ninalihofia limenipata.
Maana jambo lile niliogopalo limenipata; nalo linitialo hofu limenijilia.
26 Sina amani, wala utulivu; sina pumziko, bali taabu tu.”
Mimi sioni raha, sipati utulivu, na sipati pumziko; badala yake huja taabu.”

< Ayubu 3 >