< Ayubu 28 >

1 “Kuna machimbo ya fedha, na mahali dhahabu isafishwapo.
Hakika kuna machimbo ya fedha, wanaposafisha dhahabu.
2 Chuma hupatikana ardhini, nayo shaba huyeyushwa kutoka mawe ya madini.
Chuma uchimbwa; shaba uyeyushwa kutoka katika jiwe.
3 Mwanadamu hukomesha giza; huyatafuta hadi sehemu iliyo mbali, kwa ajili ya kuchimbua mawe yenye madini katika giza jeusi sana.
Mtu anaondoa giza na kutafuta, katika mpaka wa mbali, mawe hayaonekani na giza totoro.
4 Huchimba shimo jembamba mbali na makao ya watu, mahali paliposahaulika na nyayo za wanadamu; mbali na wanadamu huningʼinia na kupembea kwa kamba.
Huchimba shimo mbali na makazi ya watu, mahali pasipopitwa na mtu. Huning'inia mbali na watu; uharakisha kwenda na kurudi.
5 Ardhi, ambako chakula hutoka, chini hugeuzwa kwa moto;
Kwa nchi, kizalishwapo chakula, inapinduliwa kama kwa moto.
6 yakuti samawi hutoka katika miamba yake, nalo vumbi lake lina vipande vya dhahabu.
Mawe yake yana johari, na vumbi lake lina dhahabu.
7 Hakuna ndege awindaye aijuaye njia ile iliyofichika, wala hakuna jicho la mwewe lililoiona.
Hata ndege mwindaji hapajui, wala jicho la kipanga halijapaona.
8 Wanyama wa porini wanaotamba hawajawahi kupakanyaga, wala simba azungukaye huko.
Ndege mwenye majivuna hajawai kuiona njia hiyo, wala simba mkali kupita pale.
9 Mikono ya mwanadamu hushambulia miamba migumu sana, na kuiacha wazi mizizi ya milima.
Mtu huchimba mwamba mgumu; hupindua milima katika vyanzo vyake.
10 Hutoboa shimo refu la kupenya chini kwa chini kwenye miamba; macho yake huona hazina zake zote.
Huweka njia katika miamba; macho yake pale kila kilicho cha thamani.
11 Hutafuta vyanzo vya mito na kuvileta vitu vilivyofichika katika nuru.
Hufunga vyanzo hata wasiondoke; kilichofichika pale hukifunua.
12 “Lakini hekima inaweza kupatikana wapi? Ufahamu unakaa wapi?
Hekima itakuwa wapi? Mahali pa ufahamu ni wapi?
13 Mwanadamu hatambui thamani yake; haiwezi kupatikana katika nchi ya walio hai.
Mtu hafahamu thamani yake; wala haipatikani katika nchi ya walio hai.
14 Kilindi husema, ‘Haiko ndani yangu’; bahari nayo husema, ‘Haiko pamoja nami.’
Vilindi vya maji chini ya nchi husema, 'Haiko kwangu'; bahari husema, 'Haipo pamoja nami.'
15 Haiwezi kununuliwa kwa dhahabu safi kuliko zote, wala thamani yake haiwezi kupimwa kwa fedha.
Hainunuliwi kwa dhahabu; wala hailinganishwi na fedha.
16 Haiwezi kununuliwa kwa dhahabu ya Ofiri, kwa shohamu ya thamani kubwa au yakuti samawi ya thamani kubwa.
Haiwezi kuthamanishwa na dhahabu ya Ofiri, kwa jiwe jeusi la thamani au johari.
17 Dhahabu wala mawe maangavu haviwezi kulinganishwa nayo, wala haiwezi hubadilishwa na vito vya dhahabu.
Dhahabu na fuwele hailingani nayo kwa thamani; wala haiwezi kubadilishwa kwa vito vya dhahabu safi.
18 Marijani na yaspi hazistahili kutajwa; thamani ya hekima ni zaidi ya akiki nyekundu.
Hailinganishwi na marijani wala yaspi; hakika, thamani ya hekima inapita madini ya rubi.
19 Yakuti manjano ipatikanayo Kushi haiwezi kulinganishwa nayo, wala haiwezi kununuliwa kwa dhahabu safi.
Topazi ya Ethiopia hailinganishwi nayo; wala kuthamanishwa kwa dhahabu safi.
20 “Ni wapi basi hekima itokako? Ufahamu hukaa wapi?
Je hekima inatoka wapi? Mahali pa ufahamu ni wapi?
21 Imefichika machoni pa kila kitu kilicho hai, imesitiriwa hata kwa ndege wa angani.
Hekima imejificha mbali na macho ya viumbe wote na ndege wa angani.
22 Uharibifu na Mauti husema, ‘Ni uvumi wake tu uliotufikia masikioni mwetu.’
Mauti na uharibifu husema, 'Tumesikia tu tetesi kwa masikio yetu.'
23 Mungu anaifahamu njia ya kuiendea hekima na ndiye peke yake anayefahamu inakokaa,
Mungu hufahamu njia ya kuipata; anapafahamu ilipo.
24 kwa maana yeye huitazama miisho ya dunia na huona kila kitu chini ya mbingu.
Kwani uona miisho yote ya dunia na huona chini ya mbingu zote.
25 Alipofanyiza nguvu za upepo na kuyapima maji,
Hapo kale, alifanya nguvu za upepo na kuyagawanya maji kwa kipimo.
26 alipofanya maagizo kwa ajili ya mvua na njia kwa ajili ya umeme wa radi,
Aliiwekea mvua tamko na njia ya radi na munguromo.
27 ndipo alipoitazama hekima na kuikadiria thamani yake, akaithibitisha na kuihakikisha.
Kisha akaiona hekima na kuitangaza; aliianzisha, bila shaka, na kuipima.
28 Naye Mungu akamwambia mwanadamu, ‘Kumcha Bwana: hiyo ndiyo hekima, nako kujitenga na uovu ndio ufahamu.’”
Aliwambia watu, 'Tazameni, kumcha Bwana - ni hekima; kuacha uovu ni ufahamu.”

< Ayubu 28 >