< Ayubu 24 >
1 “Kwa nini Mwenyezi asiweke nyakati kwa ajili ya hukumu? Kwa nini wale wamjuao wazitafute siku kama hizo bila mafanikio?
Kwa nini nyakati za kuwahukumu waovu hazikuwekwa na Mwenyezi? Kwa nini siyo wale waliowaaminifu kwa Mungu huziona siku za hukumu zikija?
2 Watu husogeza mawe ya mpaka; huchunga makundi ya wanyama waliyonyangʼanya kwa nguvu.
Kuna waovu waondoao alama za mipaka; kuna waovu walichukua kundi kwa nguvu na kulifanya lao.
3 Huwanyangʼanya yatima punda wao, na kumchukua rehani fahali wa mjane.
Wanawadhurumu wanyonge punda wao; wanachukua ng'ombe wa mjane kuwa dhamana.
4 Humsukuma mhitaji kutoka njia, na kuwafanya maskini wote wa nchi kulazimika kujificha.
Wanawaondoa wahitaji katika njia zao kwa lazima; masikini wa dunia yote wanajificha kutoka kwao.
5 Kama punda-mwitu jangwani, maskini huzunguka katika kazi zao za kutafuta chakula; mahali palipo jangwa huwapa chakula cha watoto wao.
Tazama, masikini hawa huenda kufanya kazi kama punda-mwitu mwituni, akitafuta chakula kwa uangalifu; pengine Araba itawapatia chakula kwa ajili ya watoto wao.
6 Hukusanya chakula mashambani na kuokota masazo katika mashamba ya mizabibu ya waovu.
Masikini huvuna katika mashamba ya wengine usiku; wanakusanya zabibu kidogo kutokana na mapato ya waovu.
7 Kwa kukosa nguo, usiku kucha hukaa uchi; hawana chochote cha kujifunika baridi.
Wana lala bila kujifunika wakati wa usiku; hawana cha kujifunika wakati wa baridi.
8 Hutota kwa mvua za mlimani, nao huikumbatia miamba kwa ajili ya kukosa pa kujisitiri.
Wanalowanishwa na mvua ya milimani; wanalala pembeni mwa miamba mikubwa kwani hawana makao.
9 Mtoto yatima hupokonywa matitini; mtoto wachanga wa maskini hunyakuliwa kwa ajili ya deni.
Kuna waovu wanaowapokonya yatima katika kifua cha mama zao, na waovu wawachukuao watoto kama dhamana kutoka kwa masikini.
10 Kwa kukosa nguo, hutembea uchi; hubeba miganda ya ngano, lakini huwa na njaa.
Lakini masikini wanatembea uchi; wajapokaa na njaa, wanabebea wengine chakula.
11 Hukamua zeituni katika mawe ya kusagia; hukanyaga mashinikizo, lakini wanaona kiu.
Masikini wanazalisha vinono ndani ya nyumba za waovu; wanakanyaga mashinikizo ya waovu, lakini wanakiu.
12 Kilio cha huzuni cha wanaokufa kinapaa kutoka mjini, nazo nafsi za waliojeruhiwa zinalilia msaada. Lakini Mungu hamlaumu mtu yeyote kwa kutenda mabaya.
Watu wananung'unika mjini; waliojeruhiwa wanaomboleza, lakini Mungu hasikilizi maombi yao.
13 “Wako wale wanaoiasi nuru, wasiofahamu njia zake wala hawakai katika mapito yake.
Baadhi ya waovu hawa wanaiasi nuru; hawafahamu njia zake, wala kukaa katika njia zake.
14 Wakati mwanga wa mchana unapotoweka, muuaji huinuka naye huwaua maskini na mhitaji; wakati wa usiku hunyemelea kama mwizi.
Muaji huinuka na nuru; huuwa masikini na waitaji; ni kama mwizi wakati wa usiku.
15 Jicho la mzinzi hungojea wakati wa giza, naye hufikiri, ‘Hakuna jicho litakaloniona,’ naye huuficha uso wake.
Pia, mzinifu hungoja wakati wa usiku; husema, 'Hakuna anionaye.' Hujibadilisha.
16 Katika giza, huvunja majumba, lakini wakati wa mchana hujifungia ndani; hawataki kufanya lolote nuruni.
Waovu huingia katika nyumba gizani, lakini hujifungia wakati wa mchana; hawajari nuru.
17 Kwa wote hawa, giza nene ndiyo asubuhi yao; hujifanya rafiki na vitisho vya gizani.
Kwa kuwa asubuhi kwao wote ni kama giza totoro; wanaamani na vitisho vya giza totoro.
18 “Lakini wao ni povu juu ya maji; sehemu yao juu ya nchi imelaaniwa, hivyo hakuna hata mmoja aendaye kwenye shamba la mizabibu.
Wanapotea polepole, lakini, kama povu juu ya maji; shamba lao limelaaniwa; hakuna anayekwenda kufanya kazi katika mashamba yao ya mizabibu.
19 Kama vile joto na hari vinyakuavyo theluji iliyoyeyuka, ndivyo kuzimu kuwanyakuavyo waliotenda dhambi. (Sheol )
Kiangazi na joto huondoa barafu; ndivyo kuzimu pia kunavyowaaribu waliotenda dhambi. (Sheol )
20 Tumbo lililowazaa huwasahau, nao huwa karamu ya mabuu; watu waovu hawakumbukwi tena, lakini huvunjika kama mti.
Mama yake atamsahau; polepole funza watamuuma; hatakumbukwa tena; kwa hiyo, waovu watavunjika kama mti.
21 Huwafanya mawindo wanawake tasa na wasio na watoto, nao hawaonyeshi huruma kwa wajane.
Mwovu anamrarua mgumba; hawatendi jema lolote kwa mjane.
22 Lakini Mungu huwakokota wenye nguvu kwa uwezo wake; ingawa wamestawi, hawana hakika ya maisha.
Bado Mungu huwaondoa wenye nguvu kwa nguvu zake; huinuka na kuwadhoofisha.
23 Aweza akawaacha wakapumzika wakijihisi salama, lakini macho yake yanaona njia zao.
Mungu huwaacha wajione wako salama, na wanalifurahia hilo, lakini anayaangalia maisha yao.
24 Kwa kitambo kidogo hutukuka, hatimaye hutoweka; hushushwa na kukusanywa kama wengine wote, hukatwa kama masuke ya nafaka.
Watu hawa wanatukuzwa; bado, kitambo tu, watapotea; hakika, watashushwa; watakusanywa kama wengine wote; wataondolewa kama sehemu ya juu ya masikio ya nafaka.
25 “Kama hili sivyo, ni nani awezaye kunithibitisha kuwa mwongo, na kuyafanya maneno yangu kuwa si kitu?”
Ikiwa sivyo, nani atanithibitisha kuwa mwongo; atakaye fanya maneno yangu kuwa si kitu?”