< Ayubu 22 >

1 Ndipo Elifazi Mtemani akajibu:
Kisha Elifazi Mtemani akajibu na kusema,
2 “Je, mwanadamu aweza kuwa wa faida kwa Mungu? Je, hata mtu mwenye hekima aweza kumfaidi?
Je mtu anaweza kumfaa Mungu “Je mwenye hekima anaweza kufaa kwake.
3 Je, Mwenyezi angefurahia nini kama ungekuwa mwadilifu? Au je, yeye angepata faida gani kama njia zako zingekuwa kamilifu?
Je inafurahisha kwa Mwenyezi ikiwa u mwenye haki? Je ni faida yake ukiyafanya safi maisha yako?
4 “Je, ni kwa ajili ya utaua wako ndiyo maana anakukemea na kuleta mashtaka dhidi yako?
Je ni kwa sababu ya uchaji wako kwake hata akukemee na kukuadhibu?
5 Je, uovu wako si mkuu? Dhambi zako si hazina mwisho?
Je si kwa sababu ya wingi wa uovu wako? Je hakuna mwisho wa makosa yako?
6 Umedai dhamana kwa ndugu zako bila sababu; umewavua watu nguo zao, ukawaacha uchi.
Kwa maana umechukua dhamana kutoka kwa ndugu yako bila sababu; umechukua mavazi ya mtu na kumwacha uchi.
7 Hukumpa maji aliyechoka, nawe ulimnyima chakula mwenye njaa,
Haukuwapa wenye kiu maji ya kunywea; umewanyima chakula wenye njaa
8 ingawa ulikuwa mtu mwenye uwezo ukimiliki nchi: mtu uliyeheshimiwa, ukiishi ndani yake.
japokuwa wewe, mwenye uwezo, uliimiliki nchi, japokuwa wewe, mwenye kuheshimiwa, uliishi ndani yake.
9 Umewafukuza wajane mikono mitupu na kuzivunja nguvu za yatima.
Umewaacha wajane waondoke bila kitu; umewatesa yatima.
10 Ndiyo sababu mitego imekuzunguka pande zote, hatari ya ghafula inakutia hofu,
Kwa hiyo, mabaya yanakuzunguka, na hofu za ghafla zinakusumbua.
11 ndiyo sababu ni giza sana huwezi kuona, tena ndiyo sababu mafuriko ya maji yamekufunika.
Kuna giza, hata usione; gharika inakufunika.
12 “Je, Mungu hayuko katika mbingu za juu? Juu kuliko nyota zilizo juu sana!
Je Mungu hayupo juu mbinguni? Anaangalia juu ya nyota, jinsi zilivyo juu!
13 Hivyo wewe wasema, ‘Mungu anajua nini?’ Je, yeye huhukumu katika giza kama hilo?
Unasema, 'Mungu anajua nini? Je anaweza kuamua kupitia giza totoro?
14 Mawingu mazito ni pazia lake, hivyo hatuoni sisi atembeapo juu ya anga la dunia.
Mawingu ni kifuniko chake, hata asituone; anatembea anga la mbinguni.'
15 Je, utaifuata njia ya zamani, ambayo watu waovu waliikanyaga?
Je utayaishi maisha ya zamani walioishi waovu -
16 Waliondolewa kabla ya wakati wao, misingi yao ikachukuliwa na mafuriko.
walioondolewa kabla ya siku zao, ambao misingi yao imeondolewa kama mto,
17 Walimwambia Mungu, ‘Tuache sisi! Huyo Mwenyezi aweza kutufanyia nini?’
waliomwambia Mungu, 'Ondoka kwetu'; waliosema, 'Mwenyezi anaweza kututenda nini?
18 Lakini ndiye alizijaza nyumba zao na vitu vizuri, hivyo ninajitenga mbali na mashauri ya waovu.
Hata hivyo bado alizijaza nyumba zao kwa mema; mipango ya waovu iko mbali nami.
19 “Wenye haki wanaona maangamizi yao na kufurahi, nao wasio na hatia huwadhihaki, wakisema,
Wenye haki wanayaona yawapatayo waovu na kufurahi; wasio na hatia wanawacheka kwa dhihaka.
20 ‘Hakika adui zetu wameangamizwa, nao moto umeteketeza mali zao.’
Wanasema, 'Bila shaka walioinuka kinyume chetu wameondolewa; moto umeteketeza mali zao.'
21 “Mjue sana Mungu ili uwe na amani, ndipo mema yatakapokujia.
Basi patana na Mungu na uwe na amani naye; kwa njia hiyo, mema yatakujia.
22 Uyapokee mafundisho toka kinywani mwake, na maneno yake uyaweke moyoni mwako.
Nakusihi, pokea, maelekezo yake; uyatii maneno yake.
23 Kama ukimrudia Mwenyezi, utarudishwa upya: Kama ukiuondoa uovu uwe mbali na hema lako,
Ukimrudia Mwenyezi, utajengwa, ukiacha kutenda uovu makaoni mwako.
24 kama dhahabu yako ukiihesabu kama mavumbi, dhahabu yako ya Ofiri kama miamba ya mabondeni,
Weka hazina zako mavumbini, dhahabu ya Ofiri kati ya mawe ya vijito,
25 ndipo Mwenyezi atakuwa dhahabu yako, naye atakuwa fedha yako iliyo bora.
na Mwenyezi atakuwa hazina zako, fedha ya thamani kwako.
26 Hakika ndipo utakapojifurahisha kwa Mwenyezi, nawe utamwinulia Mungu uso wako.
Nawe utajifurahisha katika Mwenyezi; utamwangalia Mungu.
27 Utamwomba yeye, naye atakusikia, nawe utazitimiza nadhiri zako.
Utamwomba, naye atakusikiliza; utamtolea nadhiri.
28 Utakusudia jambo nalo litatendeka, nao mwanga utaangazia njia zako.
Lakini pia utatamka lolote, nawe utapewa; nuru itaangaza maishani mwako.
29 Watu watakaposhushwa, nawe ukasema, ‘Wainue!’ ndipo atamwokoa aliyevunjika moyo.
Mungu humshusha mwenye kiburi, naye humwinua mnyenyekevu.
30 Atamwokoa hata yule ambaye ana hatia, ataokolewa kwa sababu ya usafi wa mikono yako.”
Atamwokoa asiye na hatia; utaokolewa kupitia usafi wa mikono yako.”

< Ayubu 22 >