< Ayubu 22 >
1 Ndipo Elifazi Mtemani akajibu:
2 “Je, mwanadamu aweza kuwa wa faida kwa Mungu? Je, hata mtu mwenye hekima aweza kumfaidi?
3 Je, Mwenyezi angefurahia nini kama ungekuwa mwadilifu? Au je, yeye angepata faida gani kama njia zako zingekuwa kamilifu?
4 “Je, ni kwa ajili ya utaua wako ndiyo maana anakukemea na kuleta mashtaka dhidi yako?
5 Je, uovu wako si mkuu? Dhambi zako si hazina mwisho?
6 Umedai dhamana kwa ndugu zako bila sababu; umewavua watu nguo zao, ukawaacha uchi.
7 Hukumpa maji aliyechoka, nawe ulimnyima chakula mwenye njaa,
8 ingawa ulikuwa mtu mwenye uwezo ukimiliki nchi: mtu uliyeheshimiwa, ukiishi ndani yake.
9 Umewafukuza wajane mikono mitupu na kuzivunja nguvu za yatima.
10 Ndiyo sababu mitego imekuzunguka pande zote, hatari ya ghafula inakutia hofu,
11 ndiyo sababu ni giza sana huwezi kuona, tena ndiyo sababu mafuriko ya maji yamekufunika.
12 “Je, Mungu hayuko katika mbingu za juu? Juu kuliko nyota zilizo juu sana!
13 Hivyo wewe wasema, ‘Mungu anajua nini?’ Je, yeye huhukumu katika giza kama hilo?
14 Mawingu mazito ni pazia lake, hivyo hatuoni sisi atembeapo juu ya anga la dunia.
15 Je, utaifuata njia ya zamani, ambayo watu waovu waliikanyaga?
16 Waliondolewa kabla ya wakati wao, misingi yao ikachukuliwa na mafuriko.
17 Walimwambia Mungu, ‘Tuache sisi! Huyo Mwenyezi aweza kutufanyia nini?’
18 Lakini ndiye alizijaza nyumba zao na vitu vizuri, hivyo ninajitenga mbali na mashauri ya waovu.
19 “Wenye haki wanaona maangamizi yao na kufurahi, nao wasio na hatia huwadhihaki, wakisema,
20 ‘Hakika adui zetu wameangamizwa, nao moto umeteketeza mali zao.’
21 “Mjue sana Mungu ili uwe na amani, ndipo mema yatakapokujia.
22 Uyapokee mafundisho toka kinywani mwake, na maneno yake uyaweke moyoni mwako.
23 Kama ukimrudia Mwenyezi, utarudishwa upya: Kama ukiuondoa uovu uwe mbali na hema lako,
24 kama dhahabu yako ukiihesabu kama mavumbi, dhahabu yako ya Ofiri kama miamba ya mabondeni,
25 ndipo Mwenyezi atakuwa dhahabu yako, naye atakuwa fedha yako iliyo bora.
26 Hakika ndipo utakapojifurahisha kwa Mwenyezi, nawe utamwinulia Mungu uso wako.
27 Utamwomba yeye, naye atakusikia, nawe utazitimiza nadhiri zako.
28 Utakusudia jambo nalo litatendeka, nao mwanga utaangazia njia zako.
29 Watu watakaposhushwa, nawe ukasema, ‘Wainue!’ ndipo atamwokoa aliyevunjika moyo.
30 Atamwokoa hata yule ambaye ana hatia, ataokolewa kwa sababu ya usafi wa mikono yako.”