< Ayubu 2 >
1 Siku nyingine wana wa Mungu walikuja kujionyesha mbele za Bwana. Shetani naye akaja pamoja nao kujionyesha mbele zake.
Kisha kulikuwa na siku wana wa Mungu walipokwenda kujihudhurisha mbele za BWANA. Shetani pia alikwenda kati yao kujihudhulisha mbele za BWANA.
2 Bwana akamuuliza Shetani, “Umetoka wapi?” Shetani akamjibu Bwana “Natoka kuzunguka pote duniani, nikitembea huku na huko humo.”
BWANA akamuuliza Shetani, “umetoka wapi wewe?” Kisha Shetani akamjibu BWANA na kusema, “Natoka kuzunguka zunguka duniani, kutembea huku na huko humo.”
3 Bwana akamwambia Shetani, “Je, umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Hakuna mtu mwingine duniani aliye kama yeye, mtu asiye na hatia, ni mnyofu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Naye bado anadumisha uadilifu wake, ingawa ulinichochea dhidi yake, ili nimwangamize pasipo sababu.”
BWANA akamuuliza Shetani, “Je umemwangalia mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mwenye haki na mkamilifu, mmoja aliye mcha Mungu na kuepukana na uovu. Hata sasa anashikamana na utimilifu wake, japokuwa ulinichochea juu yake, nimwangamize pasipo sababu.”
4 Shetani akamjibu Bwana, “Ngozi kwa ngozi! Mwanadamu atatoa vyote alivyo navyo kwa ajili ya uhai wake.
Shetani akamjibu BWANA na kusema, “Ngozi kwa ngozi, kweli; mtu atatoa vyote alivyo navyo kwaajili ya uhai wake.
5 Lakini nyoosha mkono wako na kuipiga nyama yake na mifupa yake, naye kwa hakika atakulaani mbele za uso wako.”
Lakini nyosha mkono wako sasa na uguse mifupa yake na nyama yake, na uone kama hatakufuru mbele ya uso wako.”
6 Bwana akamwambia Shetani, “Vema sana, kwa hiyo, yeye yumo mikononi mwako, lakini lazima umwachie uhai wake.”
BWANA akamwambia Shetani, “Tazama, yumo mkononi mwako; ni uhai wake tu ambao lazima uutunze.”
7 Basi Shetani akatoka mbele za Bwana naye akampiga Ayubu kwa majipu mabaya tangu nyayo za miguu yake hadi utosi wa kichwa.
Kisha Shetani akatoka mbele ya uso wa BWANA. Akampiga Ayubu na majipu mabaya toka wayo wa mguu hadi kichwani.
8 Ndipo Ayubu akachukua kigae na kujikuna nacho huku akiketi kwenye majivu.
Ayubu akachukua kipande cha kigae kujikunia, na akaketi chini majivuni.
9 Mke wake akamwambia, “Je, bado unashikamana na uadilifu wako? Mlaani Mungu nawe ukafe!”
Kisha mkewe akamuuliza, “Je hata sasa wewe unashikamana na utimilifu wako? Umkufuru Mungu na ufe.
10 Akamjibu, “Unazungumza kama vile ambavyo mwanamke mpumbavu yeyote angenena. Je, tupokee mema mikononi mwa Mungu, nasi tusipokee na udhia?” Katika mambo haya yote, Ayubu hakutenda dhambi katika kusema kwake.
Lakini yeye akamwambia, “Wewe unaongea kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu waongeavyo. Je sisi tupate mema toka kwa Mungu na tusipate mabaya?” Katika mambo hayo yote, Ayubu hakutenda dhambi kwa midomo yake.
11 Basi marafiki watatu wa Ayubu, ndio Elifazi Mtemani, na Bildadi Mshuhi na Sofari Mnaamathi, waliposikia juu ya taabu yote iliyompata Ayubu, wakajipanga toka manyumbani mwao, nao wakakutana pamoja kwa makubaliano kwenda kumtuliza katika taabu hiyo na kumfariji.
Sasa wakati rafiki zake watatu wa Ayubu walipopata habari ya mabaya yaliyompata, kila mmoja wao akaja kutoka mahali pake: Elifazi Mtemani, Bildadi Mshuhi, na Sofari Mnaamathi. Wakatenga muda ili waende kuomboleza naye na kumfariji.
12 Walipomwona kwa mbali, ilikuwa vigumu kumtambua. Wakaanza kulia kwa sauti kubwa, wakayararua majoho yao na kujirushia mavumbi juu ya vichwa vyao.
Walipoinua macho yao wakiwa mbali, hawakuweza kumtambua. Wakapaza sauti zao na kulia; kila mmoja wao akararua joho lake na kurusha majivu hewani na juu ya kichwa chake.
13 Kisha wakaketi chini kwenye udongo pamoja na Ayubu kwa siku saba usiku na mchana. Hakuna yeyote aliyesema naye neno, kwa sababu waliona jinsi mateso yake yalivyokuwa makubwa.
Kisha wakaketi chini pamoja naye kwa muda wa siku saba-mchana na usiku. Hakuna hata mmoja aliyesema naye neno, kwa kuwa waliona kuwa huzuni yake ilikuwa kuu mno.