< Ayubu 18 >
1 Bildadi Mshuhi akajibu:
2 “Je, ni lini utafika mwisho wa maneno haya? Uwe mwenye busara, nasi ndipo tutakapoweza kuongea.
3 Kwa nini sisi tunafikiriwa kama wanyama, na kuonekana wajinga machoni pako?
4 Wewe unayejirarua mwenyewe vipande vipande katika hasira yako, je, dunia iachwe kwa ajili yako wewe? Au ni lazima miamba iondolewe mahali pake?
5 “Taa ya mwovu imezimwa, nao mwali wa moto wake umezimika.
6 Mwanga hemani mwake umekuwa giza; taa iliyo karibu naye imezimika.
7 Nguvu za hatua zake zimedhoofishwa; shauri lake baya litamwangusha.
8 Miguu yake imemsukumia kwenye wavu, naye anatangatanga kwenye matundu ya wavu.
9 Tanzi litamkamata kwenye kisigino; mtego utamshikilia kwa nguvu.
10 Kitanzi kimefichwa ardhini kwa ajili yake; mtego uko kwenye njia yake.
11 Vitisho vimemtia hofu kila upande, na adui zake humwandama kila hatua.
12 Janga linamwonea shauku; maafa yako tayari kwa ajili yake aangukapo.
13 Nayo yatakula sehemu ya ngozi yake; mzaliwa wa kwanza wa mauti atakula maungo yake.
14 Atangʼolewa kutoka usalama wa hema lake, na kupelekwa kwa mfalme wa vitisho.
15 Moto utakaa katika hema lake; moto wa kiberiti utamwagwa juu ya makao yake.
16 Mizizi yake chini itakauka na matawi yake juu yatanyauka.
17 Kumbukumbu lake litatoweka katika dunia, wala hatakuwa na jina katika nchi.
18 Ameondolewa nuruni na kusukumiwa gizani, naye amefukuzwa mbali atoke duniani.
19 Hana mtoto wala mzao miongoni mwa watu wake, wala aliyenusurika mahali alipoishi.
20 Watu wa magharibi watashangaa yaliyompata; watu wa mashariki watapatwa na hofu.
21 Hakika ndivyo yalivyo makao ya mtu mwovu; ndivyo palivyo mahali pake mtu asiyemjua Mungu.”