< Ayubu 12 >

1 Ndipo Ayubu akajibu:
Ndipo Ayubu akajibu na kusema,
2 “Bila shaka ninyi ndio watu, nayo hekima itakoma mtakapokufa!
“Hakuna shaka ninyi wanadamu; Hekima mtakufa nayo.
3 Lakini mimi ninao ufahamu kama ninyi; mimi si duni kwenu. Ni nani asiyejua mambo haya yote?
Lakini nina ufahamu kama vile ninyi; Mimi siyo duni kwenu. Ni dhhiri, ni nani asiyefahamu vitu hivyo kama hivi?
4 “Nimekuwa mtu wa kuchekwa na rafiki zangu, ingawa nilimwita Mungu naye akanijibu: mimi ni mtu wa kuchekwa tu, ingawa ni mwadilifu na nisiye na hatia!
Mimi ni kitu cha kuchekwa na jirani-Mimi, ni mmoja aliyemwita Mungu na ambaye alijibiwa na yeye! Mimi, ni mwenye haki na mtu asiyekuwa na hatia-Mimi sasa nimekuwa kitu cha kuchekwa.
5 Wanadamu wakiwa katika utulivu huwa na dharau kwa wale wenye msiba kana kwamba ndiyo haki ya wale ambao miguu yao inateleza.
Katika mawazo yake mtu fulani aliye katika kufurahi, kuna kudharau kwa mashaka; hufikiri katika njia ambayo huleta mambo mabaya zaidi kwa wale ambao miguu yao inateleza.
6 Hema za wanyangʼanyi hazisumbuliwi, wale wanaomghadhibisha Mungu wako salama: wale wamchukuao mungu wao mikononi mwao.
Hema za wezi hufanikiwa, na wale ambao humkasirisha Mungu huhisi salama; mikono yao wenyewe ni miungu wao.
7 “Lakini ulizeni wanyama, nao watawafundisha, au ndege wa angani, nao watawaambia;
Lakini sasa waulize hao wanyama wa mwituni, na watakufundisha wewe; waulize ndege wa angani, na watakuambia wewe.
8 au zungumzeni na dunia, nayo itawafundisha, au acheni samaki wa baharini wawape taarifa.
Au iambie ardhi, na itakufundisha wewe; samaki wa baharini watakutangazia wewe.
9 Ni nani miongoni mwa hawa wote asiyejua kwamba mkono wa Bwana ndio uliofanya hili?
Ni myama yupi miongoni mwa hawa asiyefahamu kuwa mkono wa Yahwe umetenda haya?
10 Mkononi mwake kuna uhai wa kila kiumbe, na pumzi ya wanadamu wote.
Katika mkono wake mna uzima wa kila kiumbe hai na pumzi ya wanadamu wote.
11 Je, sikio haliyajaribu maneno kama vile ulimi uonjavyo chakula?
Je, sikio haliyajaribu maneno kama vile kaakaa lionjavyo chakula chake?
12 Je, hekima haipatikani katikati ya wazee? Je, maisha marefu hayaleti ufahamu?
Kwa wazee mna hekima; katika wingi wa siku mna ufahamu.
13 “Hekima na nguvu ni vya Mungu; shauri na ufahamu ni vyake yeye.
Pamoja na Mungu mna hekima na ukuu; yeye anayo mashauri na ufahamu.
14 Kile anachokibomoa hakiwezi kujengeka tena; mtu aliyefungiwa naye hawezi kufunguliwa.
Tazama, yeye huangusha chini, na haiwezekani kujengwa tena; kama yeye akimtia gerezani mtu yeyote, hakutakuwa tena kufunguliwa.
15 Akizuia maji, huwa pana ukame; akiyaachia maji, huharibu nchi.
Tazama, kama yeye akiyazuia maji, yanakauka; na kama akiyaachilia nje yanaitaabisha ardhi.
16 Kwake kuna nguvu na ushindi; adanganywaye na adanganyaye, wote wawili ni wake.
Pamoja na yeye mna nguvu na hekima; watu ambao wamedanganywa na mdanganyi wote pamoja wako katika nguvu zake.
17 Yeye huwaondoa washauri wakiwa wametekwa nyara, naye huwapumbaza wanaotoa maamuzi.
Yeye huwaongoza washauri mbali bila kuvaa viatu katika huzuni; huwarudisha hakimu katika upumbavu.
18 Huondoa pingu zilizofungwa na wafalme, na kuwafunga mishipi ya kiunoni.
Yeye Huondoa minyororo ya mamlaka kutoka kwa wafalme; yeye hufunika viuno vyao kwa nguo.
19 Huwaondoa makuhani wakiwa wametekwa nyara, na kuwaangusha waliojiimarisha muda mrefu.
Yeye huwaongoza makuhani mbali bila kuvaa viatu na kuwapindua watu wakuu.
20 Hunyamazisha midomo ya washauri wanaoaminika, na kuondoa busara ya wazee.
Yeye huondoa hotuba ya wale waliokuwa wameaminiwa na huondoa mbali ufahamu wa wazee.
21 Huwamwagia dharau wanaoheshimika, na kuwavua silaha wenye nguvu.
Yeye humwaga aibu juu ya binti za wafalme na hufungua mishipi ya watu wenye nguvu.
22 Hufunua mambo ya ndani ya gizani, na kuyaleta nuruni yale yaliyositirika sana.
Yeye huweka wazi vitu vya kina kutoka katika giza na kuvileta nje kumuika vivuli mahali ambapa watu waliokufa wapo.
23 Huyafanya mataifa yatukuke na kuyaangamiza; hufanya mataifa kuwa makubwa, naye huyatawanya.
Yeye huyafanya mataifa kuwa na nguvu, na pia huyaharibu; Yeye pia huyakuza mataifa, na pia yeye huyaongoza mbali kama wafungwa.
24 Huwaondolea viongozi wa nchi akili zao; huwapeleka watangetange nyikani pasipo na njia.
Yeye huondoa mbali ufahamu kutoka kwa viongozi wa watu wa nchi; huwafanya wao kutangatanga msituni mahali pasipo na njia.
25 Hupapasa gizani pasipokuwa na mwanga; huwafanya wapepesuke kama walevi.
Wao wanapapasa katika giza bila kuwa na mwanga; yeye huwafanya wao kuweweseka kama mtu mlevi.

< Ayubu 12 >