< Ayubu 11 >
1 Ndipo Sofari Mnaamathi akajibu:
Ndipo Sofari Mnaamathi alijibu na kusema,
2 “Je, maneno haya yote yapite bila kujibiwa? Je, huyu mnenaji athibitishwe kuwa na haki?
“Huo wingi wa maneno haupaswi kujibiwa? Mtu huyu, aliyejaa maneno mengi awe wa kuaminiwa?
3 Je, maneno yako ya upuzi yawafanye watu wanyamaze kimya? Je, mtu asikukemee unapofanya dhihaka?
Kujivuna kwako kunapaswa kuwafanya wengine wabaki wamenyamaza? Wakati unapoyadhihaki mafundisho yetu, hakuna awaye yote atakayekufanya wewe ujisikie mwenye aibu?
4 Unamwambia Mungu, ‘Imani yangu ni kamili nami ni safi mbele zako.’
Kwa kuwa wewe unasema kwa Mungu, 'Imani yangu ni safi, Mimi sina waa lolote machoni pako.'
5 Aha! Laiti kwamba Mungu angesema, kwamba angefungua midomo yake dhidi yako,
Lakini, laiti, Mungu huyo angesema na kufungua midomo yake dhidi yako;
6 naye akufunulie siri za hekima, kwa kuwa hekima ya kweli ina pande mbili. Ujue hili: Mungu amesahau hata baadhi ya dhambi zako.
hivyo angekuonyesha wewe siri za hekima! Kwa kuwa yeye ni mkuu katika ufahamu. Tena tambua huyo Mungu anataka kutoka kwako kidogo kuliko uovu wako unavyostahili.
7 “Je, waweza kujua siri za Mungu? Je, waweza kuyachunguza mambo yote kumhusu Mwenyezi?
Je, wewe unaweza kumfahamu Mungu kwa kumtafuta yeye? Unaweza kumtambua aliye mkuu kwa ukamilifu?
8 Ni juu mno kuliko mbingu: waweza kufanya nini? Kina chake ni kirefu kuliko kuzimu: wewe waweza kujua nini? (Sheol )
Upeo uko juu kama mbingu; unaweza kufanya nini wewe? Ni wenye kina kirefu kuliko kuzimu; waweza kufahamu nini wewe? (Sheol )
9 Kipimo chake ni kirefu kuliko dunia, nacho ni kipana kuliko bahari.
Vipimo vyake ni virefu kuliko nchi, na vipana kuliko bahari.
10 “Kama akija na kukufunga gerezani, na kuitisha mahakama, ni nani awezaye kumpinga?
kama yeye akipita kati na kumyamazisha mtu yeyote, kama yeye akimwita mtu yeyote hukumuni, tena ni nani anayeweza kumzuia yeye?
11 Hakika anawatambua watu wadanganyifu; naye aonapo uovu, je, haangalii?
Kwa maana anawajua watu waongo; wakati anapoona uovu, hawezi yeye kuukumbuka?
12 Mpumbavu aweza kuwa mwenye hekima, endapo mtoto wa punda-mwitu atazaliwa mwanadamu.
Lakini watu wapumbavu hawana ufahamu; wataupata wakati punda mwitu atakapozaa mtu.
13 “Hata sasa ukiutoa moyo wako kwake na kumwinulia mikono yako,
Lakini ikiwa umeuelekeza moyo wako kwa haki na umeunyosha mkono wako karibu na Mungu;
14 ukiiondolea mbali ile dhambi iliyo mkononi mwako wala usiuruhusu uovu ukae hemani mwako,
ikiwa huo uovu ulikuwa katika mikono yako, lakini hivyo tena unauweka mbali nawe, na haukuruhusu kutokuwa mwenye haki kukaa hemani mwako.
15 ndipo utainua uso wako bila aibu; utasimama imara bila hofu.
Ndipo kwa hakika ungeinua juu uso wako bila ishara ya aibu; Ni dhahiri, ungethibitika na usingeogopa.
16 Hakika utaisahau taabu yako, utaikumbuka tu kama maji yaliyokwisha kupita.
Wewe ungesahau mateso yako; ungeyakumbuka hayo tu kama maji ambayo yametiririka mbali.
17 Maisha yako yatangʼaa kuliko adhuhuri, nalo giza litakuwa kama alfajiri.
Maisha yako yangekuwa angavu kuliko adhuhuri; japokuwa kulikuwa na giza, litakuwa kama asubuhi.
18 Utakuwa salama, kwa kuwa lipo tumaini; utatazama pande zote na kupumzika kwa salama.
Ungekuwa salama kwa sababu kuna tumaini; ni dhahiri, wewe utapata usalama juu yako na utachukua pumziko lako katika usalama.
19 Utalala, wala hakuna atakayekuogofya, naam, wengi watajipendekeza kwako.
Pia ungelala chini katika pumziko, na hakuna ambaye angekufanya wewe uogope; hakika wengi wangetafuta upendeleo wako.
20 Bali macho ya waovu hayataona, wokovu utawaepuka; tarajio lao litakuwa ni hangaiko la mtu anayekata roho.”
Lakini macho ya watu waovu yatashindwa; hawatakuwa na njia ya kukimbia; tumaini lao la pekee litakuwa pumzi yao ya mwisho ya uhai.