< Yeremia 8 >
1 “‘Wakati huo, asema Bwana, mifupa ya wafalme na maafisa wa Yuda, mifupa ya makuhani na manabii, na mifupa ya watu wa Yerusalemu itaondolewa kutoka makaburi yao.
Wakati huo - BWANA asema - wataleta kutoka makaburini mifupa ya wafalme wa Yuda na wakuu wake, mifupa ya makuhani na ya manabii na mifupa ya wakazi wa Yerusalemu.
2 Itawekwa wazi kwa jua, na mwezi, na nyota zote za mbingu, ambazo walizipenda na kuzitumikia, na ambazo wamezifuata kutafuta ushauri na kuziabudu. Hawatakusanywa pamoja au kuzikwa, lakini watakuwa kama mavi yaliyotapakaa juu ya ardhi.
Kisha wataitandaza nje mchana kweupe na mbalamwezi na nyota zote za angani; hivi vitu katika anga vimenifuata na kunitumikia, na kwamba vimetembea na kutafuta, na kwamba vimeniabudu. Mifupa haitakusanywa na kuzikwa tena. Itakuwa kama mavi juu ya uso wa dunia.
3 Popote nitakapowafukuzia, mabaki wote wa kizazi hiki kiovu watatamani kufa kuliko kuishi, asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.’
Na katika kila eneo lililobaki ambalo nimewafukuza, Watachagua mauti badala ya uzima kwa ajili yao, wote ambao watasalia kutokana na taifa hili ovu - asema BWANA wa majeshi.
4 “Waambie, ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana: “‘Je, watu wanapoanguka hawainuki? Je, mtu anapopotea harudi?
Kwa hiyo uwaambie, 'BWANA asema hivi: Je, kuna mtu anyeanguka na hasimami? Je, kuna mtu anayepotea na hawezi kujaribu kurudi?
5 Kwa nini basi watu hawa walipotea? Kwa nini Yerusalemu inapotea kila mara? Wanangʼangʼania udanganyifu na wanakataa kurudi.
Kwa nini hawa watu, Yerusalemu, wamegeukia uasi daima? Wanashikilia uongo na wanakataa kutubu.
6 Nimewasikiliza kwa makini, lakini hawataki kusema lililo sawa. Hakuna anayetubia makosa yake akisema, “Nimefanya nini?” Kila mmoja hufuata njia yake mwenyewe kama farasi anayekwenda vitani.
Nilikaa kwa uangalifu na nikasikiliza, lakini hawakuongea kilicho sahihi; hakuna aliyetubia uovu wake, hakuna asemaye, “Nimefanya nini?” Kila mmoja wao huenda kule anakotaka, kama farasi aendaye kasi vitani.
7 Hata korongo aliyeko angani anayajua majira yake yaliyoamriwa, nao njiwa, mbayuwayu na koikoi hufuata majira yao ya kurudi. Lakini watu wangu hawajui Bwana anachotaka kwao.
Hata koikoi angani hujua wakati sahihi; na njiwa, na mbayuayu, n a korongo. Huhama kwa wakati sahihi, lakini watu wangu hawayajui maagizo ya BWANA.
8 “‘Mwawezaje kusema, “Sisi tuna busara kwa sababu tunayo sheria ya Bwana,” wakati ambapo kwa hakika kalamu ya uongo ya waandishi imeandika kwa udanganyifu?
Kwa nini mnasema, “Sisi tuna hekima! na sheria ya BWANA tunayoi?” Hakika, Tazama! Kalamu yenye uongo ya mwandishi imefanya uongo.
9 Wenye hekima wataaibika, watafadhaika na kunaswa. Kwa kuwa wamelikataa neno la Bwana, hiyo hekima waliyo nayo ni ya namna gani?
Wenye hekima wataaibishwa. Wameyeyuka na na kunaswa. Tazama! wanakataa neno la BWANA, kwa hiyo hekima yao ni kwa ajili ya matumizi gani?
10 Kwa hiyo nitawapa watu wengine wake zao, na mashamba yao kwa wamiliki wengine. Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkubwa kabisa, wote wana tamaa ya kupata zaidi; manabii na makuhani wanafanana, wote wanafanya udanganyifu.
Kwa wake zao nitawapa wengine, na mashamba yao kwa wale watakaowamiliki, kwa kuwa kuanzia kijana hadi mkuu, kwa pamoja ni wachoyo! Kuanzia nabii hadi kuhani, wote wanasema uongo.
11 Wanafunga majeraha ya watu wangu bila uangalifu. Wanasema, “Amani, amani,” wakati hakuna amani.
Kwa kuwa wametibu jeraha ya binti za watu wangu kwa juu juu. Walijisemea, “Amani, Amani,” na kumbe hapakuwa na amani.
12 Je, wanaona aibu kwa ajili ya tabia yao inayochukiza mno? Hapana, hawana aibu hata kidogo, hawajui hata kuona haya. Kwa hiyo wataanguka miongoni mwa hao walioanguka, watashushwa chini watakapoadhibiwa, asema Bwana.
Je, waliona aibu walipofanya machukizo? Hawakuaibika. Hawakuwa na utu. Kwa hiyo wataanguka wakati wa adhabu, pamoja na wale walioanguka. Watatupwa chini, asema BWANA.
13 “‘Nitayaondoa mavuno yao, asema Bwana. Hapatakuwepo zabibu kwenye mzabibu. Hapatakuwepo na tini kwenye mtini, majani yake yatanyauka. Kile nilichowapa watanyangʼanywa.’”
Nitawaondoa kabisa - asema BWANA - hapatakuwa na zabibu kwenye mizabibu yao, wala tini katika mitini yao. kwa kuwa jani litanyauka, na kile nilichowapatia kitaisha.
14 “Kwa nini tunaketi hapa? Kusanyikeni pamoja! Tukimbilie kwenye miji yenye maboma, tukaangamie huko! Kwa kuwa Bwana, Mungu wetu ametuhukumu kuangamia, na kutupa maji yenye sumu tunywe, kwa sababu tumemtenda dhambi.
Kwa nini tunakaa hapa? Njoni pamoja; twendeni kwenye hiyo miji yenye maboma, na tutakaa kimya kule katika kifo. Kwa kuwa BWANA, Mungu wetu atatunyamazisha. Atatufanya tunywe sumu, kwa kuwa tumemtenda dhambi.
15 Tulitegemea amani, lakini hakuna jema lililokuja, tulitegemea wakati wa kupona, lakini kulikuwa hofu tu.
Tunatumainia amani, lakini hakutakuwa na jema. Tunatumainia wakati wa uponyaji, lakini tazama kutakuwa na hofu.
16 Mkoromo wa farasi za adui umesikika kuanzia Dani, kwa mlio wa madume yao ya farasi, nchi yote inatetemeka. Wamekuja kuangamiza nchi na vyote vilivyomo, mji na wote waishio ndani yake.”
Mkoromo wa farasi wake umesikika kutoka Dani. Dunia nzima inatikisika kwa sababu ya sauti ya kukaribia kwa farasi wake wenye nguvu. Kwa kuwa watakuja kuiangamiza nchi na utajiri wake, mji na wote wakaao nadani yake.
17 “Tazama, nitatuma nyoka wenye sumu kali katikati yenu, fira ambao hawawezi kulogwa, nao watawauma,” asema Bwana.
Hebu tazama, ninawatuma nyoka kati yenu, fira ambao hawawezi kuzuiliwa kwa uganga. Watawauma - asema BWANA,”
18 Ee Mfariji wangu katika huzuni, moyo wangu umezimia ndani yangu.
Huzuni yangu haina ukomo, na moyo wangu unaugua.
19 Sikia kilio cha watu wangu kutoka nchi ya mbali: “Je, Bwana hayuko Sayuni? Je, Mfalme wake hayuko tena huko?” “Kwa nini wamenikasirisha kwa vinyago vyao, kwa sanamu zao za kigeni zisizofaa?”
Tazama! sauti ya maumivu ya binti wa watu wangu kutoka mbali! Je, BWANA hayumo Sayuni? Je, mfalme wake hayumo ndani yake? Kwa nini sasa wananichukiza kwa vitu vya kuchongwa na sanamu za kigeni zilizo batili?
20 “Mavuno yamepita, kiangazi kimekwisha, nasi hatujaokolewa.”
Mavuno yamepita, wakati wa hari umekwisha. Lakini sisi hatujaokoka.
21 Kwa kuwa watu wangu wamepondwa, nami nimepondeka pia; ninaomboleza, nayo hofu kuu imenishika.
Nimeumia kwa sababu ya maumivu ya binti wa watu wangu. Ninaomboleza kwa sababu ya mambo ya kushangaza ambayo yametokea kwake; Nimeyeyuka.
22 Je, hakuna zeri ya kuponya katika Gileadi? Je, hakuna tabibu huko? Kwa nini basi hakuna uponyaji wa majeraha ya watu wangu?
Je, kule Gileadi hakuan dawa? Je, huko hayuko mponyaji? Kwa nini uponyaji wa binti wa watu wangu hautokei?