< Yeremia 8 >
1 “‘Wakati huo, asema Bwana, mifupa ya wafalme na maafisa wa Yuda, mifupa ya makuhani na manabii, na mifupa ya watu wa Yerusalemu itaondolewa kutoka makaburi yao.
2 Itawekwa wazi kwa jua, na mwezi, na nyota zote za mbingu, ambazo walizipenda na kuzitumikia, na ambazo wamezifuata kutafuta ushauri na kuziabudu. Hawatakusanywa pamoja au kuzikwa, lakini watakuwa kama mavi yaliyotapakaa juu ya ardhi.
3 Popote nitakapowafukuzia, mabaki wote wa kizazi hiki kiovu watatamani kufa kuliko kuishi, asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.’
4 “Waambie, ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana: “‘Je, watu wanapoanguka hawainuki? Je, mtu anapopotea harudi?
5 Kwa nini basi watu hawa walipotea? Kwa nini Yerusalemu inapotea kila mara? Wanangʼangʼania udanganyifu na wanakataa kurudi.
6 Nimewasikiliza kwa makini, lakini hawataki kusema lililo sawa. Hakuna anayetubia makosa yake akisema, “Nimefanya nini?” Kila mmoja hufuata njia yake mwenyewe kama farasi anayekwenda vitani.
7 Hata korongo aliyeko angani anayajua majira yake yaliyoamriwa, nao njiwa, mbayuwayu na koikoi hufuata majira yao ya kurudi. Lakini watu wangu hawajui Bwana anachotaka kwao.
8 “‘Mwawezaje kusema, “Sisi tuna busara kwa sababu tunayo sheria ya Bwana,” wakati ambapo kwa hakika kalamu ya uongo ya waandishi imeandika kwa udanganyifu?
9 Wenye hekima wataaibika, watafadhaika na kunaswa. Kwa kuwa wamelikataa neno la Bwana, hiyo hekima waliyo nayo ni ya namna gani?
10 Kwa hiyo nitawapa watu wengine wake zao, na mashamba yao kwa wamiliki wengine. Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkubwa kabisa, wote wana tamaa ya kupata zaidi; manabii na makuhani wanafanana, wote wanafanya udanganyifu.
11 Wanafunga majeraha ya watu wangu bila uangalifu. Wanasema, “Amani, amani,” wakati hakuna amani.
12 Je, wanaona aibu kwa ajili ya tabia yao inayochukiza mno? Hapana, hawana aibu hata kidogo, hawajui hata kuona haya. Kwa hiyo wataanguka miongoni mwa hao walioanguka, watashushwa chini watakapoadhibiwa, asema Bwana.
13 “‘Nitayaondoa mavuno yao, asema Bwana. Hapatakuwepo zabibu kwenye mzabibu. Hapatakuwepo na tini kwenye mtini, majani yake yatanyauka. Kile nilichowapa watanyangʼanywa.’”
14 “Kwa nini tunaketi hapa? Kusanyikeni pamoja! Tukimbilie kwenye miji yenye maboma, tukaangamie huko! Kwa kuwa Bwana, Mungu wetu ametuhukumu kuangamia, na kutupa maji yenye sumu tunywe, kwa sababu tumemtenda dhambi.
15 Tulitegemea amani, lakini hakuna jema lililokuja, tulitegemea wakati wa kupona, lakini kulikuwa hofu tu.
16 Mkoromo wa farasi za adui umesikika kuanzia Dani, kwa mlio wa madume yao ya farasi, nchi yote inatetemeka. Wamekuja kuangamiza nchi na vyote vilivyomo, mji na wote waishio ndani yake.”
17 “Tazama, nitatuma nyoka wenye sumu kali katikati yenu, fira ambao hawawezi kulogwa, nao watawauma,” asema Bwana.
18 Ee Mfariji wangu katika huzuni, moyo wangu umezimia ndani yangu.
19 Sikia kilio cha watu wangu kutoka nchi ya mbali: “Je, Bwana hayuko Sayuni? Je, Mfalme wake hayuko tena huko?” “Kwa nini wamenikasirisha kwa vinyago vyao, kwa sanamu zao za kigeni zisizofaa?”
20 “Mavuno yamepita, kiangazi kimekwisha, nasi hatujaokolewa.”
21 Kwa kuwa watu wangu wamepondwa, nami nimepondeka pia; ninaomboleza, nayo hofu kuu imenishika.
22 Je, hakuna zeri ya kuponya katika Gileadi? Je, hakuna tabibu huko? Kwa nini basi hakuna uponyaji wa majeraha ya watu wangu?