< Yeremia 51 >
1 Hili ndilo asemalo Bwana: “Tazama nitaamsha roho ya mwangamizi dhidi ya Babeli na watu wakaao Leb-Kamai.
Yahwe asema hivi: Tazama, ninakwenda kuleta upepo wa maangamizi dhidi ya Babeli na dhidi yao waishio ndani ya Leb Kamei.
2 Nitawatuma wageni Babeli kumpepeta na kuiharibu nchi yake; watampinga kila upande katika siku ya maafa yake.
Nitawatuma Babeli wageni. Watamtawanya na wataifanya ukiwa nchi yake, maana watakuja kinyume chake kutoka pote siku ya madhara.
3 Usimwache mpiga upinde afunge kamba upinde wake, wala usimwache avae silaha zake. Usiwaonee huruma vijana wake; angamiza jeshi lake kabisa.
Msiwaache wapiga mishale wakapinda pinde zao; msiwache wakavaa silaha zao. Msiwahifadhi vijana wake wa kiume; litengeni jeshi lake lote kwa maangamizi.
4 Wataanguka waliouawa katika Babeli, wakiwa na majeraha ya kutisha barabarani zake.
Maana watu waliojeruhiwa wataanguka katika nchi ya Wakaldayo; waliouawa wataanguka katika mitaa yake.
5 Kwa maana Israeli na Yuda hawajaachwa na Mungu wao, Bwana Mwenye Nguvu Zote, ingawa nchi yao imejaa uovu mbele zake yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.
Maana Israeli na Yuda hawajaachwa na Mungu wao, na Yahwe wa majeshi, japokuwa nchi yao imejaa na maasi yaliyotendwa kinyume cha Mmoja aliye Mtakatifu wa Israeli.
6 “Kimbieni kutoka Babeli! Okoeni maisha yenu! Msiangamizwe kwa sababu ya dhambi zake. Ni wakati wa kisasi cha Bwana, atamlipa kile anachostahili.
Kimbieni kutoka Babeli; kila mtu na ajiokoe mwenyewe. Msiangamie katika maasi yake. Maana ni wakati wa kisasi cha Yahwe. Atamlipa kwa yote.
7 Babeli alikuwa kikombe cha dhahabu katika mkono wa Bwana; aliufanya ulimwengu wote ulewe. Mataifa walikunywa mvinyo wake; kwa hiyo sasa wameingiwa na wazimu.
Babeli alikuwa kikombe cha dhahabu mkononi mwa Yahwe kilichoinywesha nchi yote; mataifa walikunywa mvinyo wake wakawa wendawazimu.
8 Babeli ataanguka ghafula na kuvunjika. Mwombolezeni! Tafuteni zeri ya kutuliza maumivu yake, labda anaweza kupona.
Babeli utaanguka ghafla na kuangamizwa. Mwombolezeeni! mpeni dawa kwa maumivu yake; pengine aweza kupona.
9 “‘Tungemponya Babeli, lakini hawezi kuponyeka; tumwacheni, na kila mmoja wetu aende nchi yake mwenyewe, kwa kuwa hukumu yake inafika angani, inapanda juu hadi mawinguni.’
Tulinuia kumponya Babeli, lakini hajaponywa, haya na tumwache twende, katika nchi yetu. Maana hatia yake imefika juu mbinguni; imerundikwa kufika mawinguni.
10 “‘Bwana amethibitisha haki yetu; njooni, tutangaze katika Sayuni kitu ambacho Bwana Mungu wetu amefanya.’
Yahwe ametamka kwamba sisi hatuna hatia. Njooni, teseme katika Sayuni matendo ya Yahwe Mungu wetu.'
11 “Noeni mishale, chukueni ngao! Bwana amewaamsha wafalme wa Wamedi, kwa sababu nia yake ni kuangamiza Babeli. Bwana atalipiza kisasi, kisasi kwa ajili ya Hekalu lake.
Noweni mishale na kuchukua ngao. Yahwe anaiimiza roho ya mfalme wa Umedi katika mpango wa kuiangamiza Babeli. Hii ni kwa kisasi cha Yahwe, kisasi kwa maangamizi ya hekalu lake.
12 Twekeni bendera juu ya kuta za Babeli! Imarisheni ulinzi, wekeni walinzi, andaeni waviziao! Bwana atatimiza kusudi lake, amri yake juu ya watu wa Babeli.
Inueni bendela juu ya kuta za Babeli; wekeni walinzi. Wekeni waangalizi; wekeni askari waviziao ili kumkamata kila akimbiliaye mjini, maana Yahwe atafanya kile alichokipanga. Atafanya alichokisema juu ya wakaao Babeli.
13 Wewe uishiye kando ya maji mengi na uliye na wingi wa hazina, mwisho wako umekuja, wakati wako wa kukatiliwa mbali.
Enyi mwishio kati ya chemchemi nyingi za maji, ninyi mlio na wingi wa hazina, mwisho wenu umefika. upindo wa maisha yenu umepunguzwa.
14 Bwana Mwenye Nguvu Zote ameapa kwa nafsi yake mwenyewe: ‘Hakika nitakujaza na watu, kama kundi la nzige, nao watapiga kelele za ushindi juu yako.’
Yahwe wa majeshi ameapa kwa maisha yake, 'nitakujaza na adui zako, kama pigo la nzige; watainua kelele za vita juu yako.'
15 “Aliiumba dunia kwa uweza wake; akaweka misingi ya ulimwengu kwa hekima yake na akazitandaza mbingu kwa ufahamu wake.
Ameifanya dunia kwa nguvu zake; akaiweka dunia mahali kwa hekima yake. Kwa ufahamu wake alizitanda mbingu.
16 Atoapo sauti yake, maji yaliyo katika mbingu hunguruma, huyafanya mawingu yainuke kutoka miisho ya dunia. Hupeleka umeme wa radi pamoja na mvua, naye huuleta upepo kutoka ghala zake.
Anapovuma, kunakuwa na mvumo wa maji mbinguni, maana huleta umande kutoka miisho ya dunia. Hufanya radi kwa ajili ya mvua na kuituma na kuutuma upepo kutoka katika maghala ya nyumba zake.
17 “Kila mtu ni mjinga na hana maarifa; kila sonara ameaibishwa na sanamu zake. Vinyago vyake ni vya udanganyifu, havina pumzi ndani yavyo.
Kila mtu anakuwa kama mnyama asiye na akili; kila mfua chuma ameaibishwa na sanamu zake. Maana mwonekano wake unadanganya; maana hakuna uzima ndani yake.
18 Havifai kitu, ni vitu vya kufanyia mzaha, hukumu yavyo itakapowadia, vitaangamia.
Hazifai, kazi ya wafanya mzaa; wataangamizwa wakati wa kuadhibiwa kwao.
19 Yeye Aliye Fungu la Yakobo sivyo alivyo, kwani ndiye Muumba wa vitu vyote, pamoja na kabila la urithi wake: Bwana Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake.
Lakini Mungu, urithi wa Yakobo, siyo kama hawa, maana yeye ndiye afanyaye vitu vyote. Israeli ni kabila ya urithi wake; Yahwe wa majeshi ni jina lake.
20 “Wewe ndiwe rungu langu la vita, silaha yangu ya vita: kwa wewe navunjavunja mataifa, kwa wewe naangamiza falme,
Wewe ni nyundo ya vita yao, silaha ya vita yangu. Kwa wewe nitawaponda mataifa na kuharibu falme.
21 kwa wewe navunjavunja farasi na mpanda farasi, kwa wewe navunjavunja gari la vita na mwendeshaji wake,
Kwa wewe nitaponda farasi na wawapandao; kwa wewe nitaponda vibandawazi na madereva wake.
22 kwa wewe napondaponda mwanaume na mwanamke, kwa wewe napondaponda mzee na kijana, kwa wewe napondaponda kijana wa kiume na mwanamwali,
Kwa wewe nitawafutilia mbali mme na mke; kwa wewe nitafutilia mbali mzee na kijana. Kwa wewe nitafutilia mbali kijana wa kiume na wasichana bikra.
23 kwa wewe nampondaponda mchungaji na kundi, kwa wewe nampondaponda mkulima na maksai, kwa wewe nawapondaponda watawala na maafisa.
Kwa wewe nitafutilia mbali wachungaji na makundi yao; kwa wewe nitawafutilia mbali wakulima na jozi zao za kulimia. kwa wewe nitawafutilia mbali watawala na maafsa.
24 “Mbele ya macho yako nitamlipiza Babeli na wote waishio Ukaldayo kwa ajili ya makosa yote waliyofanya katika Sayuni,” asema Bwana.
Maana mbele yako nitamlipa Babeli na wote wakaao Ukaldayo kwa maovu yote waliyoyafanya huko Sayuni - hili ni tamko la Yahwe.
25 “Mimi niko kinyume nawe, ee mlima unaoharibu, wewe uangamizaye dunia yote,” asema Bwana. “Nitanyoosha mkono wangu dhidi yako, nikuvingirishe kutoka kwenye kilele cha mwamba, na kukufanya mlima ulioteketezwa kwa moto.
Tazama, mimi ni kinyume chako, ewe mlima, wewe unayewaharibu watu wengine - hili ni tamko la Yahwe - kuiharibu dunia yote. Nitakupiga na mikono yangu na kuvingirisha chini kutoka ukingo wa kilima. Kisha nitakufanya mlima ulioteketezwa kabisa kwa moto.
26 Hakuna jiwe litakalochukuliwa kutoka kwako kwa ajili ya kufanywa jiwe la pembeni, wala jiwe lolote kwa ajili ya msingi, kwa maana utakuwa ukiwa milele,” asema Bwana.
Hivyo hawatachukua kwako jiwe lolote ili kujengea pembe ya nyumba au msingi; kwani utakuwa ukiwa wa milele - hili ni tamko la Yahwe.
27 “Twekeni bendera katika nchi! Pigeni tarumbeta katikati ya mataifa! Andaeni mataifa kwa ajili ya vita dhidi yake, iteni falme hizi dhidi yake: Ararati, Mini na Ashkenazi. Wekeni jemadari dhidi yake, pelekeni farasi wengi kama kundi la nzige.
Inua bendela ya vita juu ya nchi. Piga tarumbeta katika mataifa. Yaite mataifa yamshambuliye: Ararati, Mini na Ashkenazi. Teua majemedari wa kumshambulia; leta farasi kama nzige warukao.
28 Andaeni mataifa kwa ajili ya vita dhidi yake, wafalme wa Wamedi, watawala wao na maafisa wao wote, pamoja na nchi zote wanazotawala.
Waandae mataifa kumshambulia: wafalme wa Umedi na magavana wao, maafsa wake wote na nchi yake yete.
29 Nchi inatetemeka na kugaagaa, kwa kuwa makusudi ya Bwana dhidi ya Babeli yanasimama: yaani, kuangamiza nchi ya Babeli ili pasiwe na yeyote atakayeishi humo.
Maana nchi itatikisika na kudhoofika, kwa kuwa mipango ya Yahwe inaendelea juu ya Babeli, kuifanya nchi ya Babeli kuwa nchi isiyofaa mahali pasipo na mtu.
30 Mashujaa wa Babeli wameacha kupigana, wamebaki katika ngome zao. Nguvu zao zimekwisha, wamekuwa kama wanawake. Makazi yake yameteketezwa kwa moto, makomeo ya malango yake yamevunjika.
Maaskari wameacha kupigana huko Babeli; wamekaa katika ngome zao. Nguvu zao zimeshindwa; wamekuwa wanawake - nyumba zake zipo motoni, makomeo ya malango yake yamevunjika.
31 Tarishi mmoja humfuata mwingine, na mjumbe humfuata mjumbe, kumtangazia mfalme wa Babeli kwamba mji wake wote umetekwa,
Mjumbe hukimbia ili amwambie mjumbe mwingine, na mtoa habari humwambia mtoa habari mwingine ili amwambie mfalme wa Babeli kwamba mji wake umetwaliwa kutoka mwisho hata mwisho.
32 Vivuko vya mito vimekamatwa, mabwawa yenye mafunjo yametiwa moto, nao askari wameingiwa na hofu kuu.”
Hivyo vivuko katika mito vimekamatwa; adui anaunguza mafunjo ya bwawa, na wapiganaji wa Babeli wamechanganyikiwa.
33 Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: “Binti Babeli ni kama sakafu ya kupuria wakati inapokanyagwa; wakati wa kumvuna utakuja upesi.”
Maana Yahwe wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Binti Babeli ni kama sakafu ya kupuria. Ni muda wa kumkanyaga. Ni kitambo kidogo wakati wa mavuno utakuja juu yake.
34 “Nebukadneza mfalme wa Babeli ametula, ametufanya tuchangayikiwe, ametufanya tuwe gudulia tupu. Kama nyoka ametumeza na kujaza tumbo lake kwa vyakula vyetu vizuri, kisha akatutapika.
Yerusalemu husema, 'Nebukadneza mfalme wa Babeli amenirarua. Amenikausha na amenifanya kuwa mtungi mtupu. Amenimeza kama joka. Alijishibisha kwa chakula changu chema. Amenitupa mbali.'
35 Jeuri iliyofanyiwa miili yetu na iwe juu ya Babeli,” ndivyo wasemavyo wakaao Sayuni. “Damu yetu na iwe juu ya wale waishio Babeli,” asema Yerusalemu.
Wenyeji wa Sayuni watasema, 'Gasia nilizofanyiwa na mwili wangu na ziwe kwa Babeli.' Yerusalem atasema, Damu yangu na iwe juu ya wakaao Ukaldayo.'
36 Kwa hiyo, hili ndilo Bwana asemalo: “Tazama, nitatetea shauri lako na kulipiza kisasi kwa ajili yako; nitaikausha bahari yake na kuzikausha chemchemi zake.
Kwa hiyo Yahwe asema hivi: Tazama, nikotayari kulitetea shitaka lako na kuleta kisasi kwa ajili yako. Maana nitayakausha maji ya Babeli na kufanya vyanzo vyake kukauka.
37 Babeli utakuwa lundo la magofu na makao ya mbweha, kitu cha kutisha na kudharauliwa, mahali asipoishi mtu.
Babeli utakuwa rundo la magofu, pango la mbwea, sehemu itishayo, kitu cha kutoa sauti ya nyoka, pasipo na watu.
38 Watu wake wote wananguruma kama simba wadogo, wanakoroma kama wana simba.
Wababeli wataunguruma kwa pamoja kama wanasimba. Watanguruma kama watoto wa simba.
39 Lakini wakati wakiwa wameamshwa, nitawaandalia karamu na kuwafanya walewe, ili wapige kelele kwa kicheko, kisha walale milele na wasiamke,” asema Bwana.
wanapopashwa moto kwa hasira, nitawafanyia sherehe; nitawalewesha hata wafurahi, na kisha kulala usingizi usio na mwisho hata wasiamke - hili ni tamko la Yahwe -
40 “Nitawateremsha kama wana-kondoo waendao machinjoni, kama kondoo dume na mbuzi.
nitawapeleka chini kama wanakondoo kwa mchinjaji, kama kondoo dume pamoja na mbuzi majike.
41 “Tazama jinsi Sheshaki atakamatwa, majivuno ya dunia yote yatakavyonyakuliwa. Babeli atakuwa mwenye hofu kiasi gani kati ya mataifa!
Jinsi Babeli ulivyotekwa! Hivyo fahari ya dunia yote imekamatwa. Jinsi Babeli ulivyofanyika sehemu yenye magofu kati ya mataifa.
42 Bahari itainuka juu ya Babeli; mawimbi yake yenye kunguruma yatamfunika.
Bahari imekuja juu ya Babeli! Amefunikwa na mawimbi yavumayo.
43 Miji yake itakuwa ukiwa, kame na jangwa, nchi ambayo hakuna yeyote anayeishi ndani yake, ambayo hakuna mtu anayepita humo.
Miji yake imekuwa ukiwa, sehemu kame na nyika, nchi isiyo na watu, na hakuna mtu apitaye hapo.
44 Nitamwadhibu Beli katika Babeli, na kumfanya atapike kile alichokimeza. Mataifa hayatamiminika tena kwake. Nao ukuta wa Babeli utaanguka.
Hivyo nitamwadhibu Beli huko Babeli; nitakitoa kinywani mwake alichokimeza, na mataifa hawatamminikia tena pamoja na wazao wao. Kuta za Babeli zitaanguka.
45 “Tokeni ndani yake, enyi watu wangu! Okoeni maisha yenu! Ikimbieni hasira kali ya Bwana.
Tokeni kati yake, enyi watu wangu. Kila mmoja wenu aokowe maisha yake kutoka katika hasira ya gadhabu yangu.
46 Msikate tamaa wala msiogope tetesi zitakaposikika katika nchi; tetesi moja inasikika mwaka huu, nyingine mwaka unaofuata; tetesi juu ya jeuri katika nchi, na ya mtawala dhidi ya mtawala.
Msiache mioyo yenu ikaogopa au kuhofu habari iliyosikiwa nchini, maana habari itakuja siku moja. Baada yake mwaka unaofuata kutakuwa na habari, na ghasia zitakuwa nchini. Mtawala atakuwa kinyume cha mtawala.
47 Kwa kuwa hakika wakati utawadia nitakapoziadhibu sanamu za Babeli; nchi yake yote itatiwa aibu, na watu wake wote waliouawa wataangukia ndani yake.
Kwa hiyo, tazama, siku zinakuja nitakapoadhibu sanamu za Babeli. Nchi yake yote itaaibika, na wote waliochinjwa wataanguka ndani yake.
48 Ndipo mbingu na dunia na vyote vilivyomo ndani yake vitapiga kelele za shangwe juu ya Babeli, kwa kuwa kutoka kaskazini waharabu watamshambulia,” asema Bwana.
Kisha mbingu na nchi, na vyote vilivyomo ndani yake vitafurahi juu ya Babeli. Maana mwalibifu atamwijia kutoka kaskazini - hili ni tamko la Yahwe.
49 “Babeli ni lazima aanguke kwa sababu ya kuwaua Waisraeli, kama vile waliouawa duniani kote walivyoanguka kwa sababu ya Babeli.
“Kama Babeli alivyowafanya waliouawa wa Israeli kuanguka, hivyo waliouawa katika nchi yake wataanguka katika Babeli.
50 Wewe uliyepona upanga, ondoka wala usikawie! Mkumbuke Bwana ukiwa katika nchi ya mbali, na utafakari juu ya Yerusalemu.”
Ondokeni!, manusura wa vita, Msikawiye. Mkumbukeni Yahwe tokea mbali; Yerusalemu na ikumbukwe.
51 “Tumetahayari, kwa maana tumetukanwa na aibu imefunika nyuso zetu, kwa sababu wageni wameingia mahali patakatifu pa nyumba ya Bwana.”
Tumeaibika, maana tumesikia matusi; dhihaka imefunika nyuso zetu, maana wageni wameingia mahali patakatifu pa nyumba ya Yahwe.
52 “Lakini siku zinakuja,” asema Bwana, “nitakapoadhibu sanamu zake, na katika nchi yake yote waliojeruhiwa watalia kwa maumivu makali.
Kwa hiyo, tazama, siku zinakuja - hivi ndivyo asemavyo Yahwe - nitakapoziadhibu sanamu zake, na waliojeruhiwa watanung'unika kwa maumivu katika nchi yake yote.
53 Hata kama Babeli ikifika angani na kuziimarisha ngome zake ndefu, nitatuma waharabu dhidi yake,” asema Bwana.
Maana hata kama Babeli angepanda mbinguni au kujenga ngome zake ndefu, aharibuye kutoka kwangu angemwendea - hili ni tamko la Yahwe.
54 “Sauti ya kilio inasikika kutoka Babeli, sauti ya uharibifu mkuu kutoka nchi ya Wakaldayo.
Kelele ya maangamizi ilitoka Babeli, anguko kubwa kutoka nchi ya Wakaldayo.
55 Bwana ataiangamiza Babeli, atanyamazisha makelele ya kishindo chake. Mawimbi ya adui yatanguruma kama maji makuu, ngurumo ya sauti zao itavuma.
Maana Yahwe anaiharibu Babeli. Anaifanya kelele ya sauti yake kuisha. Adui zake wanaunguruma kama mawimbi ya maji mengi; kelele yao imekuwa na nguvu.
56 Mharabu atakuja dhidi ya Babeli, mashujaa wake watakamatwa, nazo pinde zao zitavunjwa. Kwa kuwa Bwana ni Mungu wa kisasi, yeye atalipiza kikamilifu.
Maana aharibuye amekuja kinyume chake - kinyume cha Babeli! - na shujaa wake wametekwa. Pinde zao zimevunjwa, maana Yahwe ni Mungu wa kisasi; atatekeleza kisasi hiki.
57 Nitawafanya maafisa wake na wenye busara walewe, watawala wao, maafisa, pamoja na wapiganaji wao; watalala milele na hawataamka,” asema Mfalme, ambaye jina lake ni Bwana Mwenye Nguvu Zote.
Maana nitawafanya wana wafalme wake, wenye hekima wake, maofsa wake, na maaskari wake kulewa, nao watalala usingizi kwa usingizi usioisha na bila kuamka - hili ni tamko la mfalme: Yahwe wa majeshi ndilo jina lake.
58 Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo: “Ukuta mnene wa Babeli utasawazishwa, na malango yaliyoinuka yatateketezwa kwa moto; mataifa yanajichosha bure, taabu ya mataifa ni nishati tu ya miali ya moto.”
Yahwe wa majeshi asema hivi: Ukuta mnene wa Babeli utaangushwa kabisa, na malango marefu yataunguzwa. Kisha watu wanaokuja kumsaidia watafanya kazi isiyofaa; kila mataifa wanachojaribu kikifanya kwa ajili yake kitateketezwa kwa moto.”
59 Huu ndio ujumbe Yeremia aliompa afisa Seraya mwana wa Neria mwana wa Maaseya, alipokwenda Babeli pamoja na Sedekia mfalme wa Yuda, katika mwaka wa nne wa utawala wake.
Hili ndilo neno Yeremia nabii alilomwamru Seraya mwana wa Neria mwana wa Makseya alipokwenda na Sedekia mfalme wa Yuda huko Babeli katika mwaka wa nne wa kutawala kwake. Basi Seraya alikuwa afsa mwandamizi.
60 Yeremia alikuwa ameandika ndani ya kitabu kuhusu maafa yote yatakayoipata Babeli, yaani yote yaliyokuwa yameandikwa kuhusu Babeli.
Maana Yeremia alikuwa ameandika katika gombo kuhusu madhara yote yeliyokuwa yakienda kutendeka juu ya Babeli - maneno haya yote yaliyokuwa yameandikwa juu ya Babeli
61 Yeremia akamwambia Seraya, “Utakapofika Babeli, hakikisha kwamba umesoma maneno haya yote kwa sauti kubwa.
Yeremia akamwambia Seraya, “Unapokwenda Babeli, hakikisha unayasoma maneno haya yote.
62 Kisha sema, ‘Ee Bwana, umesema utaangamiza mahali hapa ili mtu wala mnyama asiishi ndani yake, napo patakuwa ukiwa milele.’
Nawe utasema, 'Yahwe, wewe! - wewe mwenyewe umesema kwamba utapaharibu mahali hapa. Hapatakuwa na wa kukaa, kwamba ni watu au wanyama. Patakuwa nchi isiyofaa daima.'
63 Utakapomaliza kusoma hiki kitabu, kifungie jiwe kisha ukitupe ndani ya Mto Frati.
Kisha mtakapomaliza kusoma gombo hili, funga jiwe kubwa juu yake na ulitupe katikati ya Frati.
64 Kisha sema, ‘Hivi ndivyo Babeli utakavyozama na usiinuke tena, kwa sababu ya maafa nitakayoleta juu yake. Nao watu wake wataanguka.’” Maneno ya Yeremia yanaishia hapa.
Sema, 'Babeli utazama kama hivi. Hautainuka kwa sababu ya mabaya ninayoyapeleka juu yake, nao wataanguka.” Maneno ya Yeremia yanaishia hapa.