< Yeremia 4 >
1 “Ikiwa utataka kurudi, ee Israeli, nirudie mimi,” asema Bwana. “Ikiwa utaondoa sanamu zako za kuchukiza mbele ya macho yangu na usiendelee kutangatanga,
“Kama utarudi, Israeli- asema BWANA - ikawa kwangu kwamba umerudi. Kama utaondoa hayo mambo yachukizayo mbele yangu na ukaacha kunikimbia mimi tena,
2 ikiwa kwa kweli, kwa haki na kwa unyofu utaapa, ‘Kwa hakika kama vile Bwana aishivyo,’ ndipo mataifa yatakapobarikiwa naye na katika yeye watajitukuza.”
na ukaapa hivi, 'kama BWANA aishivyo katika kweli, na haki, na katika hukumu.' mataifa yataniomba baraka, na yatanisifu mimi.
3 Hili ndilo asemalo Bwana kwa watu wa Yuda na kwa Yerusalemu: “Vunjeni mabonge kwenye mashamba yenu, wala msipande katikati ya miiba.
Kwa kuwa BWANA asema hivi kwa kila mmoja katika Yuda na Yerusalemu; 'Limeni shamba zenu na msipande katika miiba.
4 Jitahirini katika Bwana, tahirini mioyo yenu, enyi wanaume wa Yuda na watu wa Yerusalemu, la sivyo ghadhabu yangu itatoka kwa nguvu na kuwaka kama moto kwa sababu ya uovu mliotenda, ikiwaka pasipo wa kuizima.
Mtahiriwe kwa BWANA na kuondoa govi za mioyo yenu, ninyi wanaume wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu, vinginevyo hasira yangu itawaka kama moto na kuteketeteza, na hakutakuwa na mtu wa kuizima. Hii itatokea kwa sababu ya uovu wa matendo yenu.
5 “Tangaza katika Yuda na upige mbiu katika Yerusalemu na kusema: ‘Piga tarumbeta katika nchi yote!’ Piga kelele na kusema: ‘Kusanyikeni pamoja! Tukimbilie katika miji yenye maboma!’
Waambie Yuda na Yerusalemu isikie. Waambie, “pigeni baragumu katika nchi.” Tangazeni, “Kusanyeni pamoja. Twendeni kwenye miji ya Maboma.”
6 Onyesheni ishara ili kwenda Sayuni! Kimbilieni usalama pasipo kuchelewa! Kwa kuwa ninaleta maafa kutoka kaskazini, maangamizi ya kutisha.”
Inueni ishara za bendera na zielekezeni Sayuni, na kimbilieni usalama! Msibaki, kwa kuwa ninaleta majanga kutokea kaskazini na anguko kubwa.
7 Simba ametoka nje ya pango lake, mharabu wa mataifa amejipanga. Ametoka mahali pake ili aangamize nchi yenu. Miji yenu itakuwa magofu pasipo mtu wa kuishi humo.
Simba anakuja kutokea kwenye kichaka chake na yeye atakayeyaharaibu mataifa ameanza kuja. Anaondoka kwenye eneo lake ili aache hofu katika nchi yenu, kuibadili miji yenu kuwa uharibifu, ambapo hakuna hata mmoja atakayeishi. Kwa sababu hii vaeni magunia, lieni na kuomboleza.
8 Hivyo vaeni nguo za magunia, ombolezeni na kulia kwa huzuni, kwa kuwa hasira kali ya Bwana haijaondolewa kwetu.
Kwa kuwa nguvu ya hasira ya BWANA haijaondoka kwetu.
9 “Katika siku ile,” asema Bwana “mfalme na maafisa watakata tamaa, makuhani watafadhaika, na manabii watashangazwa mno.”
Ndipo itakapotokea katika siku hiyo - asema BWANA - mioyo ya mfalme na wakuu itakufa. Makuhani watasitaajabu na manabii watashangaa.'”
10 Ndipo niliposema, “Aa, Bwana Mwenyezi, umewadanganyaje kabisa watu hawa na Yerusalemu kwa kusema, ‘Mtakuwa na amani,’ wakati upanga uko kwenye koo zetu!”
Kwa hiyo nikasema, “Ahaa! BWANA. Kwa hakika umewadanganya watu hawa na Yerusalemu kwa kuwaambia, 'Kutakuwa na amani kwenu.'Wakati upanga unawaangukia dhidi ya maisha yao.”
11 Wakati huo watu hawa na Yerusalemu wataambiwa, “Upepo wa moto kutoka miinuko iliyo kame katika jangwa unavuma kuelekea watu wangu, lakini sio kupepeta au kutakasa,
Wakati huo itasemwa juu ya mji huu na Yerusalemu kuwa, “Upepo uwakao kutoka katika nyanda za jangwani utachukua njia yake kuelekea kwa binti ya watu wangu. Hautapepetwa wala kuwatakasa.
12 upepo wenye nguvu sana kuliko wa kupepeta na kutakasa utakuja kwa amri yangu. Sasa natangaza hukumu zangu dhidi yao.”
Upepo ulio na nguvu sana utakaokuja kwa amri yangu, na sasa nitapitisha hukumu dhidi yao.
13 Tazama! Anakuja kama mawingu, magari yake yanakuja kama upepo wa kisulisuli, farasi wake wana mbio kuliko tai. Ole wetu! Tunaangamia!
Tazama anavamia kama wingu, na magari yake ni kama dhoruba. Farasi wake wana mbio kuliko tai. Ole wetu kwa kuwa tutaharibiwa!
14 Ee Yerusalemu, usafishe uovu kutoka moyoni mwako na uokolewe. Utaendelea kuficha mawazo mapotovu mpaka lini?
Itakaseni mioyo yenu kutoka uovu wenu, Yerusalemu, ili kwamba muokolewe. Mawazo yako mabaya yatafikiri juu ya kutenda dhambi mpaka lini?
15 Sauti inatangaza kutoka Dani, ikipiga mbiu ya maafa kutoka vilima vya Efraimu.
Kwa kuwa kuna sauti iletayo habari kutoka Dani, na janga lijalo linasikika kutoka vilele vya milima ya Efraimu.
16 “Waambie mataifa jambo hili, piga mbiu hii dhidi ya Yerusalemu: ‘Jeshi la kuzingira linakuja kutoka nchi ya mbali, likipiga kelele ya vita dhidi ya miji ya Yuda.
Yafanyeni mataifa kulifikiria hili: Tazama, na uwatangazie Yerusalemu kuwa wale watekaji wanakuja kutoka katika nchi ya mbali ili kupiga kelel za vita juu ya miji ya Yuda.
17 Wamemzunguka kama watu walindao shamba, kwa sababu amefanya uasi dhidi yangu,’” asema Bwana.
Watakuwa kama walinzi wa shamba liliolimwa dhidi yake pande zote, kwa kuwa amekuwa mpinzani wangu - asema BWANA -
18 “Mwenendo wako na matendo yako mwenyewe yameleta haya juu yako. Hii ndiyo adhabu yako. Tazama jinsi ilivyo chungu! Tazama jinsi inavyochoma moyo!”
tabia na matendo yako yamesababisha haya yatokee kwako. Hii itakuwa adhabu yako. Jinsi itakavyokuwa vibaya kwako! itakupiga moyo wako.
19 Ee mtima wangu, mtima wangu! Ninagaagaa kwa maumivu. Ee maumivu makuu ya moyo wangu! Moyo wangu umefadhaika ndani yangu, siwezi kunyamaza. Kwa sababu nimesikia sauti ya tarumbeta, nimesikia kelele ya vita.
Moyo wangu! Moyo wangu! Niko katika maumivu ya moyo. Moyo wangu umefadhaika ndani yangu. Siwezi kunyamaza kwa kuwa nasikia sauti za pembe, sauti za vita.
20 Maafa baada ya maafa, nchi yote imekuwa magofu. Kwa ghafula mahema yangu yameangamizwa, makazi yangu kwa muda mfupi.
Anguko baada ya anguko limetangazwa, kwa nchi yote imeharibika mara. Wanaharibu masikani yangu na hema yangu ghafula.
21 Hata lini nitaendelea kuona bendera ya vita na kusikia sauti za tarumbeta?
Vita hivi vitaendelea mpaka lini? Ni mpaka lini nitasikiliza sauti za pembe?
22 “Watu wangu ni wapumbavu, hawanijui mimi. Ni watoto wasio na akili, hawana ufahamu. Ni hodari kutenda mabaya, hawajui kutenda yaliyo mema.”
Kwa kuwa upumbavu wa watu wangu - hawanijui mimi. Ni watu wajinga wasio na ufahamu. Wanaufahamu wa mambo maovu, tena hawajui kutenda mema.
23 Niliitazama dunia, nayo haikuwa na umbo tena ni tupu; niliziangalia mbingu, mianga ilikuwa imetoweka.
Niliiona nchi, na kuiona! ilikuwa ukiwa na utupu. Kwa kuwa hapakuwa na taa za mbinguni.
24 Niliitazama milima, nayo ilikuwa ikitetemeka, vilima vyote vilikuwa vikiyumbayumba.
Nilitazama katka miliima. Tazama, ilikuwa inatetemeka, na vilima vyote vilikuwa vinatikisika.
25 Nilitazama, wala watu hawakuwepo; kila ndege wa angani alikuwa ameruka zake.
Nilitazama. Tazama, hapakuwa na mtu, na ndege wote wa angani walikuwa wamekimbia.
26 Nilitazama, hata nchi iliyokuwa imestawi vizuri imekuwa jangwa, miji yake yote ilikuwa magofu mbele za Bwana, mbele ya hasira yake kali.
Nikaangalia. Tazama, mashamba yalikuwa jangwa na miji imeangushwa mbele za BWANA, mbele ya hasira yake.”
27 Hivi ndivyo Bwana asemavyo: “Nchi yote itaharibiwa, ingawa sitaiangamiza kabisa.
Hiki ndicho BWANA asemacho, “Nchi yote itakuwa uharibifu, lakini sitawaharibu wote kabisa.
28 Kwa hiyo dunia itaomboleza na mbingu zilizo juu zitakuwa giza, kwa sababu nimesema nami sitarudi nyuma, nimeamua na wala sitageuka.”
Kwa sababu hii nchi itaomboleza, na mbingu juu zitatiwa giza. Kwa kuwa nimesema haya na kuyakusudia; sitarudi nyuma; Sitaacha kuyatekeleza.
29 Kwa sauti ya wapanda farasi na wapiga upinde kila mji unakimbia. Baadhi wanakimbilia vichakani, baadhi wanapanda juu ya miamba. Miji yote imeachwa, hakuna aishiye ndani yake.
Kila mji utakimbia kutoka katka kelele za wapandafarasi na wenye pinde; Watakimbilia msituni, Kila mji utapanda hadi mahali pa miamba. Miji itatelekezwa, kwa kuwa hakutakuwa na mtu wa kuishi katika miji hiyo.
30 Unafanya nini, ewe uliyeharibiwa? Kwa nini unajivika vazi jekundu na kuvaa vito vya dhahabu? Kwa nini unapaka macho yako rangi? Unajipamba bure. Wapenzi wako wanakudharau, wanautafuta uhai wako.
Sasa umeharibiwa, utafanya nini? Japokuwa unavaa mavazi mekundu, unajipamba na mapambo ya dhahabu, na kuyafanya macho yako yaonekane makubwa na kupakwa wanja, wale wanaume waliokutamani sasa wanakukataa. Badala yake wanajaribu kukuua.
31 Nasikia kilio kama cha mwanamke katika utungu wa kuzaa, kilio cha uchungu kama cha anayemzaa mtoto wake wa kwanza: kilio cha Binti Sayuni akitweta ili aweze kupumua, akiinua mikono yake, akisema, “Ole wangu! Ninazimia; maisha yangu yamekabidhiwa kwa wauaji.”
Kwa hiyo nasikia sauti ya maumivu, yenye utungu kama ya mwanamke azaaye mtoto wake wa kwanza, sauti ya binti wa Sayuni. Atwetaye kupata pumzi. Ananyosha mikono yake na kusema, 'Ole wangu mimi! ninazimia kwa sababu ya wauaji hawa.'”