< Yeremia 34 >

1 Wakati Nebukadneza mfalme wa Babeli na jeshi lake lote, pamoja na falme zote na mataifa katika himaya aliyotawala walipokuwa wakipigana dhidi ya Yerusalemu pamoja na miji yote inayoizunguka, neno hili lilimjia Yeremia kutoka kwa Bwana:
Neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Yahwe, wakati Nebukadreza mfalme wa Babeli, majeshi yake yote, pamoja na falme zote za dunia, maeneo yote yaliyo chini ya mamlaka yake, na watu wake wote walikuwa wanapigana vita dhidi ya Yerusalemu na miji yake yote, kusema:
2 “Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli, kusema: Nenda kwa Sedekia mfalme wa Yuda umwambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Ninakaribia kuutia mji huu mikononi mwa mfalme wa Babeli, naye atauteketeza kwa moto.
'Yahwe, Mungu wa Israeli, anasema hivi: Nenda na uzungumze kwa Sedekia mfalme wa Yuda na useme kwake, 'Yahwe asema hivi: Angalia, niko karibu kuutia mji huu mkononi mwa mfalme wa Babeli. Atauchoma moto.
3 Hutaweza kuepuka mkono wake, bali hakika utatekwa na kukabidhiwa kwake. Utamwona mfalme wa Babeli kwa macho yako mwenyewe, naye atazungumza nawe ana kwa ana. Nawe utakwenda Babeli.
Hautapona kutoka mkono wake, kwa maana kwa hakika utakamatwa na kutiwa mkononi mwake. Macho yako yatayaangalia macho ya mfalme wa Babeli; atazungumza kwako moja kwa moja ukiwa unaenda Babeli.'
4 “‘Lakini sikia ahadi ya Bwana, ee Sedekia mfalme wa Yuda. Hili ndilo asemalo Bwana kukuhusu: Hutakufa kwa upanga,
Sedekia mfalme wa Yuda, sikiliza neno la Yahwe! Yahwe anasema hivi kuhusu wewe, 'Hautakufa kwa upanga.
5 utakufa kwa amani. Kama vile watu walivyowasha moto wa maziko kwa heshima ya baba zako, wafalme waliokutangulia, ndivyo watu watakavyowasha moto kwa heshima yako na kuomboleza, wakisema: “Ole, Ee Bwana!” Mimi mwenyewe ninaweka ahadi hii, asema Bwana.’”
Utakufa katika amani. Kama kwenye mafukizo ya babu zako, wafalme waliokuwepo kabla yako, watauchoma mwili wako. Watasema, 'Ole, bwana!” Watakuomboleza. Sasa nimesema—hili ni tangazo la Yahwe.”
6 Ndipo nabii Yeremia akamwambia Sedekia mfalme wa Yuda mambo haya yote huko Yerusalemu,
Kwa hiyo Yeremia nabii akatangaza kwa Sedekia mfalme wa Yuda maneno haya yote katika Yerusalemu.
7 wakati jeshi la mfalme wa Babeli lilipokuwa likipigana dhidi ya Yerusalemu na miji mingine ya Yuda ambayo bado ilikuwa imara, yaani Lakishi na Azeka. Hii ilikuwa miji pekee yenye ngome iliyobaki katika Yuda.
Jeshi la mfalme wa Babeli likafanya dhidi ya Yerusalemu na miji yote ya Yuda iliyobaki: Lakishi, na Azeka. Miji hii ya yuda ilisalia kama miji yenye maboma.
8 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Bwana, baada ya Mfalme Sedekia kufanya agano na watu wote huko Yerusalemu ili kutangaza uhuru kwa watumwa.
Neno lilomjia Yeremia kutoka kwa Yahwe baada ya mfalme Sedekia kufanya agano na watu wote katika Yurusalemu, ili kuwatanagazia uhuru
9 Kila mmoja alipaswa kuwaacha huru watumwa wake wa Kiebrania, wanawake na wanaume. Hakuna yeyote aliyeruhusiwa kumshikilia Myahudi mwenzake kama mtumwa.
ya kwamba kila mtu lazima amwachie huru mtumwa wake wa Kiebrania, wote wa kiume na wa kike, kwa hiyo mtu alipaswa kutomtumikisha Myahudi, ambaye alikuwa ndugu yake.
10 Kwa hiyo maafisa wote na watu walioingia katika agano hili wakakubali kwamba watawaacha huru watumwa wao wa kiume na wa kike, na hawatawashikilia tena kama watumwa. Wakakubali na wakawaacha huru.
Kwa hiyo watu wote na viongozi wakaingia katika agano kwamba kila mtu amwachie huru mtumwa wake wa kiume na waikke ili asiwe mtumwa tena. Walitii na kuwaweka huru.
11 Lakini baadaye wakabadili mawazo yao, na kuwarudisha wale watumwa waliokuwa wamewaacha huru, wakawafanya tena watumwa.
Lakini baada ya hapo walibadili akili zao. Wakawarudisha watumwa ambao walikuwa wamewaachia huru. Wakawalazimisha kuwa wataumwa tena.
12 Ndipo neno la Bwana likamjia Yeremia kusema:
Kwa hiyo neno la Yahwe likaja kwa Yeremia, likisema,
13 “Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: Nilifanya agano na baba zenu nilipowatoa Misri, kutoka nchi ya utumwa. Nilisema,
“Yahwe, Mungu wa Israeli, anasema hivi, 'Mimi mwenyewe nilifanya agano na babu zenu katika siku ambayo niliwatoa nje ya nchi ya Misiri, nje ya nyumba ya utumwa. Hapo ndipo niliposema,
14 ‘Kila mwaka wa saba, kila mmoja wenu ni lazima amwache huru mtumwa ambaye ni Mwebrania mwenzenu aliyejiuza kwenu. Baada ya kukutumikia kwa miaka sita, ni lazima umwache huru aende zake.’ Hata hivyo baba zenu hawakunisikiliza wala kunijali.
Katika mwisho wa mwaka wa saba, kila mtu lazima amwachie ndugu yake, Mwebrania mwenzake aliyejiuza mwenyewe kwako ili kukutumikia kwa miaka sita. Mwagize aende kwa uhuru.” Lakini babu zenu hawakunisikiliza wala kutega masikio yao kwangu.
15 Hivi karibuni tu mlitubu na kufanya yaliyo sawa machoni pangu: Kila mmoja wenu aliwatangazia uhuru Waebrania wake. Hata mlifanya agano mbele zangu ndani ya nyumba iitwayo kwa Jina langu.
Sasa ninyi wenyewe mlitubu na kuanza yaliyomema katika macho yangu. Mlitangaza uhuru, kila mtu kwa jirani yake, na mlifanya agano mbele zangu kwenye nyumba iitwayo kwa jina langu.
16 Lakini sasa mmegeuka na kulinajisi jina langu. Kila mmoja wenu amemrudisha mtumwa wa kiume na wa kike ambao mlikuwa mmewaacha huru waende zao walikotaka. Mmewalazimisha kuwa watumwa wenu tena.
Lakini tena mmegeuka na kulichafua jina langu; mmemsababisha kila mtu kumleta tena mtumwa wake wa kiume na wa kike, wale mliowachie kwenda walikotaka. Mmewalazimisha kuwa watumwa tena.'
17 “Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana: Hamkunitii mimi. Hamkutangaza uhuru kwa ndugu zenu. Hivyo sasa, ninawatangazia ninyi ‘uhuru,’ asema Bwana: ‘uhuru’ ili kuanguka kwa upanga, tauni na njaa. Nitawafanya mwe chukizo kwa falme zote za dunia.
Kwa hiyo Yahwe asema hivi, 'Ninyi wenyewe hamkunisikiliza. Mlipaswa kuwa mmetangaza uhuru, kila mmoja wenu, kwa ndugu zenu na Waisraeli wenzenu. Kwa hiyo angalia! Niko karibu kutangaza uhuru kwenu—hili ni tangazo la Yahwe—uhuru wa upanga, tauni, na njaa, kwa maana naenda kuwafanya kitu cha ajabu katika macho aya kila ufalme juu ya dunia.
18 Watu waliovunja agano langu, na ambao hawakutunza masharti ya agano walilofanya mbele zangu, nitawafanya kama ndama waliyemkata vipande viwili, kisha wakatembea kati ya vile vipande vya huyo ndama.
Kisha nitashughulika na watu waliolivuja agano langu, ambao hawakuyashika maneno ya agano ambalo walilithibitisha mbele zangu walipomkata ng'ombe dume katika vipande viwili na kutembea katika vipande vyake,
19 Viongozi wa Yuda na Yerusalemu, maafisa wa mahakama, makuhani na watu wote wa nchi waliopita kati ya vile vipande vya ndama,
na kisha viongozi wa Yuda na Yerusalemu, matowashi na makuhani, na watu wote wa nchi wakatembea katika vipande vya yule ng'ombe dume.
20 nitawatia mikononi mwa adui zao wanaotafuta uhai wao. Maiti zao zitakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi.
Nitawatia katika mikono ya adui zao na katika mikono ya hao wanaoutafuta uhai wao. Miili yao itakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama juu ya dunia.
21 “Nitamtia Sedekia mfalme wa Yuda na maafisa wake mikononi mwa adui zao wanaotafuta uhai wao, kwa jeshi la mfalme wa Babeli, lililokuwa limeondoka kwenu.
Kwa hiyo nitawatia Sedekia mfalme wa Yuda na viongozi wake kwenye mikono ya adui zao na kwenye miko ya wale wanaoutafuta uhai wao na katika mikono ya majeshi ya mfalme wa Babeli ambayo yameinuka dhidi yenu.
22 Nitatoa amri, asema Bwana, nami nitawarudisha tena katika mji huu. Watapigana dhidi yake, wautwae na kuuteketeza kwa moto. Nami nitaiangamiza miji ya Yuda hivyo pasiwe na yeyote atakayeweza kuishi humo.”
Angalia, niko karibu kutoa amari—hili ni tangazo la Yahwe—na nitawaleta tena kwenye mji huu ili wapigane dhidi yake, na kuunguza kwa moto. Kwa maana nitaigeuza miji ya Yuda kuwa sehemu za ukiwa ambamo hapatakuwa na wakaaji.”

< Yeremia 34 >