< Yeremia 3 >

1 “Kama mtu akimpa talaka mkewe, naye akamwacha na akaolewa na mtu mwingine, je, huyo mume aweza kumrudia tena? Je, hiyo nchi haitanajisika kabisa? Lakini umeishi kama kahaba na wapenzi wengi: je, sasa utanirudia tena?” asema Bwana.
Wanaema, 'Mwanamume akimfukuza mke wake, naye akaondoka kwake na kuwa mke wa mwanamume mwingine. Je, anaweza kumrudia tena? Je huyo si najisi kabisa?' Huyo mwanamke ndiyo hii nchi! Mmetenda kama kama Kahaba aliye na wapenzi wengi, na sasa mnapenda kurudi kwangu tena? - asema BWANA wa majeshi.
2 “Inua macho utazame miinuko iliyo kame na uone. Je, pana mahali ambapo hawajalala nawe? Uliketi kando ya barabara ukiwasubiri wapenzi, ukakaa kama yeye ahamahamaye jangwani. Umeinajisi nchi kwa ukahaba wako na uovu wako.
Inua macho yako uvitazame vielele tasa! Je kuna mahali ambapo hukufanya ukahaba? Pembeni mwa barabara ulikaa ukisubiri wapenzi wako, kama vile Mwarabu jangwani. Uneiharibu nchi kwa ukahaba na uovu wako.
3 Kwa hiyo mvua imezuiliwa, nazo mvua za vuli hazikunyesha. Hata hivyo, una uso usio na haya kama wa kahaba; unakataa kutahayari kwa aibu.
Kwa hiyo chemichemi za mvua zilizuiliwa na mvua za vuli hazikunyesha. Lakini uso wako una kiburi, kama uso wa mwanamke kahaba. Unakataa kuona aibu.
4 Je, wewe hujaniita hivi punde tu: ‘Baba yangu, rafiki yangu tangu ujana wangu,
Na sasa hutaniita mimi: 'Baba yangu, hata marafiki zangu wa tangu ujanani! Je, atakuwa na hasira dhidi yangu milele?
5 je, utakasirika siku zote? Je, ghadhabu yako itaendelea milele?’ Hivi ndivyo unavyozungumza, lakini unafanya maovu yote uwezayo.”
Je, utaendelea kuwa na hasira zako?' Tazama! Umesema kuwa utatenda maovu, na kweli umetenda hivyo. kwa hiyo endelea kufanya hivyo!”
6 Wakati wa utawala wa Mfalme Yosia, Bwana aliniambia, “Umeona kile Israeli asiye mwaminifu amekifanya? Amepanda juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti uliotanda na amefanya uzinzi huko.
Kisha BWANA akanena nami katika siku za mfalme Yosia, “Je, unaona jinsi Israeli alivyoniasi? Yeye anaenda kwenye kila kilima na katika kila mti wenye majani mabichi, na kule anafanya kama mwanamke kahaba.
7 Mimi nilifikiri kuwa baada ya kuyafanya yote haya angelinirudia, lakini hakurudi, naye dada yake Yuda mdanganyifu aliona hili.
Nikisema, 'Baada ya kuwa amefanya mambo haya yote, atanirudia,' lakini hakurudi. Kisha dada yake Yuda ambaye ni mwasi pia aliona alichokifanya.
8 Nilimpa Israeli asiye mwaminifu hati yake ya talaka, na kumfukuza kwa ajili ya uzinzi wake wote. Hata hivyo nikaona kuwa Yuda dada yake mdanganyifu hakuogopa. Yeye pia alitoka na kufanya uzinzi.
Kwa hiyo nami nikaona kuwa kwa sababu amefanya uzinzi huu wote. Huyo Israeli aliyeasi! Nilimfukuza na kumpatia talaka ya ndoa. Lakini dada yake Yuda mwenye hiana hakuwa na hofu, na yeye akaenda kuafanya kama mwanamke kahaba!
9 Kwa sababu uasherati wa Israeli haukuwa kitu kwake, Yuda aliinajisi nchi kwa kuzini na mawe na miti.
Hukusikitika kuwa ameinajisi nchi, kwa hiyo wakatengeneza sanamu za mti na za jiwe.
10 Pamoja na hayo yote, Yuda dada yake mdanganyifu hakunirudia kwa moyo wake wote, bali kwa kujifanya tu,” asema Bwana.
Kisha baada ya haya yote, wala Yuda dada yake muasi hakurudi kwangu na moyo wake wote, bali alikuja na uongo! -asema BWANA wa majeshi,”
11 Bwana akaniambia, “Israeli asiye mwaminifu ana haki kuliko Yuda mdanganyifu.
Kisha BWANA akanena na mimi, “Israeli muasi amekuwa mwenye haki zaidi kuliko Yuda muasi!
12 Nenda, ukatangaze ujumbe huu kuelekea kaskazini: “‘Rudi, Israeli usiye mwaminifu,’ asema Bwana, ‘sitakutazama tena kwa uso uliokunjamana, kwa kuwa mimi ni mwenye huruma,’ asema Bwana, ‘Sitashika hasira yangu milele.
Nenda ukaseme maneno haya huko kaskazini. Uwaambie, 'Rudi wewe Israeli uliyeasi! - asema BWANA - sitakuwa na hasira dhidi yako. Kwa kuwa mimi ni mwaminifu - asema BWANA - sitakuwa na hasira milele.
13 Ungama dhambi zako tu: kwamba umemwasi Bwana Mungu wako, umetapanya wema wako kwa miungu ya kigeni chini ya kila mti unaotanda, nawe hukunitii mimi,’” asema Bwana.
Kiri uovu wako, kwa kuwa umefanya dhambi dhidi ya BWANA, Mungu wako; umemshirikisha njia zako mgeni chini ya kila mti wenye majani mabichi! wala hukuisikiliza sauti yangu! - asema BWANA.
14 “Rudini, enyi watu msio waaminifu, kwa kuwa mimi ni mume wenu,” asema Bwana. “Nitawachagua ninyi, mmoja kutoka kwenye mji, na wawili kutoka kwenye ukoo, nami nitawaleta Sayuni.
Rudini, enyi watu waasi! - asema BWANA - kwa kuwa mimi nimekuoa wewe! Nitakurudisha wewe mmoja katika mji, wawili katika ukoo mmoja, na nitawarudisha Sayuni!
15 Kisha nitawapeni wachungaji wanipendezao moyo wangu, ambao watawaongoza kwa maarifa na ufahamu.
Nitawapa wachungaji niwapendao, na watawachunga kwa maarifa na ufahamu.
16 Katika siku hizo, idadi yenu itakapokuwa imeongezeka sana katika nchi, watu hawatasema tena, ‘Sanduku la Agano la Bwana,’” asema Bwana. “Halitaingia tena kwenye mawazo yao wala kukumbukwa, hawatalihitaji wala halitatengenezwa jingine.
Ndipo itakapotokea kuwa utaongezeka na kuzaa matunda katika nchi hiyo siku hizo-asema BWANA. Hawataweza kusema kuwa, “Sanduku la agano la BWANA! Jambo hili hawatalikumbuka tena katika mioyo yao, kwa kuwa hawataliwaza tena wala kulijali tena. Usemi huu hawatausema tena.'
17 Wakati huo, wataita Yerusalemu kuwa Kiti cha Enzi cha Bwana, nayo mataifa yote watakusanyika Yerusalemu kuliheshimu jina la Bwana. Hawatafuata tena ukaidi wa mioyo yao miovu.
Katiak wakati huo watasema juu ya Yerusalemu, 'Hii ndiyo enzi ya BWANA,' na mataifa mengine yote yatakusanyika Yerusalemu katika jna la BWANA. Hawataishi katika taabu ya uovu wa mioyo yao.
18 Katika siku hizo, nyumba ya Yuda itaungana na nyumba ya Israeli, wao kwa pamoja watakuja kutoka nchi ya kaskazini hadi nchi niliyowapa baba zenu kama urithi.
Katika siku hizo, nyumba ya Yuda itaishi na nyumba ya Israeli. Watarudi pamoja kutoka katika nchi ya kaskazini katika nchi niliyowapa mababu wao kuwa urithi.
19 “Mimi mwenyewe nilisema, “‘Tazama jinsi nitakavyowatunza kwa furaha kama wana na kuwapa nchi nzuri, urithi ulio mzuri kuliko wa taifa jingine lolote.’ Nilidhani mngeniita ‘Baba,’ na msingegeuka, mkaacha kunifuata.
Lakini mimi, Nilisema, 'Jinsi nipendavyo kukuheshimu kama mwanangu na kukupa nchi ipendezayo, kuwa urithi mzuri kuliko ulio katika taifa lolote!' Nami nikasema, ''mtaniita baba yangu''.'Nami nitasema kwamba hamtageuka na kuacha kunifuata.
20 Lakini kama mwanamke asiye mwaminifu kwa mumewe, vivyo hivyo mmekosa uaminifu kwangu pia, ee nyumba ya Israeli,” asema Bwana.
Lakini kama mwanamke aliyemwasi mume wake, mmenisaliti, enyi nyumba ya Israeli - asema BWANA.”
21 Kilio kinasikika juu ya miinuko iliyo kame, kulia na kuomboleza kwa watu wa Israeli, kwa sababu wamepotoka katika njia zao na wamemsahau Bwana Mungu wao.
Sauti ilisikika juu ya nyanda, kilio na kusihi kwa watu wa Israeli! kwa kuwa wamezibadili njia; wamemsahau BWANA, Mungu wao.
22 “Rudini, enyi watu msio waaminifu, nami nitawaponya ukengeufu wenu.” “Naam, tutakuja kwako, kwa maana wewe ni Bwana Mungu wetu.
“Rudini enyi watu mlioasi! Nami nitawaponya na uasi wenu!” “Tazama! tutakuja kwako, kwa kuwa wewe ni BWANA, Mungu wetu!
23 Hakika zile ghasia za kuabudu sanamu kwenye vilima na milimani ni udanganyifu; hakika katika Bwana, Mungu wetu, uko wokovu wa Israeli.
Uongo hutoka kwenye vilima, kutoka kwenye milima mingi. Kwa hakika wokovu wa Israeli unapatikana kwa BWANA, Mungu wetu.
24 Tangu ujana wetu miungu ya aibu imeyala matunda ya kazi za baba zetu: makundi yao ya kondoo na ngʼombe, wana wao na binti zao.
Lakini miungu ya aibu imeramba kazi ambayo mababu zetu waliifanya - makundi yao ya kondoo na ng'ombe, wana wao na binti zao!
25 Sisi na tulale chini katika aibu yetu, na fedheha yetu itufunike. Tumetenda dhambi dhidi ya Bwana Mungu wetu, sisi na mababa zetu; tangu ujana wetu hadi leo hatukumtii Bwana Mungu wetu.”
Na tulale chini kwa aibu. Aibu yetu na itufunike, kwa kuwa tumefanya dhambi dhidi ya BWANA, Mungu wetu! Sisi wenyewe na mababu zetu, kutoka wakati wa ujana wetu hadi leo, hatujaisikiliza sauti ya BWANA, Mungu wetu!”

< Yeremia 3 >