< Yeremia 29 >

1 Haya ndiyo maneno ya ile barua ambayo nabii Yeremia aliituma kutoka Yerusalemu kwenda kwa wazee waliobaki miongoni mwa wale waliohamishwa, na kwa makuhani, manabii na watu wengine wote ambao Nebukadneza alikuwa amewachukua kwenda uhamishoni Babeli kutoka Yerusalemu.
Haya ni maneno katika waraka ambao Yeremia nabii alituma kutoka Yerusalemu kwa wazee waliosalia miongoni mwa mateka na makuhuni, manabii, na watu wote ambao Nebukadreza aliwapeleka utumwani kutoka Yerusalemu hadi Babeli.
2 (Hii ilikuwa ni baada ya Mfalme Yekonia na malkia mamaye, maafisa wa mahakama, viongozi wa Yuda na wa Yerusalemu, mafundi na wahunzi kwenda uhamishoni kutoka Yerusalemu.)
Hii ilikuwa baada ya Yekonia mfalme, mama yake mfalme, na watumishi wakuu, viongozi wa Yuda na Yerusalemu, na wahunzi walikuwa wamepelekwa mbali na Yerusalemu.
3 Barua ilikabidhiwa kwa Elasa mwana wa Shafani, na kwa Gemaria mwana wa Hilkia, ambao Sedekia mfalme wa Yuda aliwatuma kwa Mfalme Nebukadneza huko Babeli. Barua yenyewe ilisema:
Aliutuma waraka huu kwa mkono wa Elasa mwana wa Shafani, Gemaria, mwana wa Hilkia, ambaye Sedekia, mfalme wa Yuda, alikuwa amemtuma kwa Nebukadreza mfalme wa Babeli
4 Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, awaambialo wale wote niliowapeleka kutoka Yerusalemu kwenda uhamishoni Babeli:
Waraka ulisema, Yahwe wa majeshi, Mungu wa Israeli, anasema hivi kwa mateka ambao niliwasababisha kuwa mateka kutoka Yerusalemu hadi Babeli,
5 “Jengeni nyumba na mstarehe, pandeni bustani na mle mazao yake.
'Jengeni nyumba na muishi ndani yake. Pandeni bustani na mle matunda yake.
6 Oeni wake na mzae wana na binti, waozeni wana wenu wake, nanyi watoeni binti zenu waolewe, ili nao pia wazae wana na binti. Ongezekeni idadi yenu huko, wala msipungue.
Chukueni wake na mzae wana na mabinti. Kisha Kisha chukueni wake kwa ajili ya wana wenu, na wapatieni waume binti zenu. Wazae wana na mabinti na waongezeke ili msiwe wachache sana.
7 Pia tafuteni amani na mafanikio ya mji ambamo nimewapeleka uhamishoni. Mwombeni Bwana kwa ajili ya mji huo, kwa sababu ukistawi, ninyi pia mtastawi.”
Itafuteni amani ya mji ambako nimewafanya kuwa watumwa, na mkauombee kwangu kwa niaba yake kwa kuwa kutakuwa na amani kwenu kama mji uko katika amani.'
8 Naam, hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: “Msikubali manabii na wabashiri walioko miongoni mwenu wawadanganye. Msisikilize ndoto ambazo mmewatia moyo kuota.
Kwa maana Yahwe wa majeshi, Mungu wa Israeli, anasema hivi, 'Msiwaache manabii ambao wako katikati yenu na wabashiri wenu kuwadanganya, na msizisikilize ndoto ambazo ninyi wenyewe mnaota.
9 Wanawatabiria ninyi uongo kwa jina langu. Sikuwatuma,” asema Bwana.
Kwa maana wanatabiri uongo kwenu katika jina langu. Mimi sikuwatuma—hili ni tangazo la Yahwe.'
10 Hili ndilo asemalo Bwana: “Miaka sabini itakapotimia kwa ajili ya Babeli, nitakuja kwenu na kutimiza ahadi yangu ya rehema ya kuwarudisha mahali hapa.
Kwa maana Yahwe anasema hivi, 'Babeli atakapokuwa amewatawala kwa muda wa mika sabini, nitawasaidia ninyi na kulitimiza neno langu jema kwa ajili yenu ili kuwarudisha ninyi katika sehemu hii.
11 Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema Bwana, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo.
Kwa maana mimi mwenyewe naijua mipangao niliyonayo kwa ajili yenu—hili ni tangazo la Yahwe—mipango kwa ajili ya amani na siyo kwa ajili ya mabaya, ili kuwapa ninyi tumaini na siku zenu za mwisho.
12 Kisha mtaniita, na mtakuja na kuniomba, nami nitawasikiliza.
Kisha mtaniita, na kwenda na kuniomba mimi, na nitawasikiliza.
13 Mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.
Kwa maana mtanitafuta na kunipata, kwa kuwa mtanitafuta kwa moyo wenu wote.
14 Nitaonekana kwenu,” asema Bwana, “nami nitawarudisha watu wenu waliotekwa. Nitawakusanya kutoka mataifa yote na mahali pote nilipokuwa nimewafukuzia, nami nitawarudisha mahali ambapo nilikuwa nimewatoa walipochukuliwa uhamishoni,” asema Bwana.
Kisha nitapatikana kwenu—hili ni tangazo la Yahwe—na nitawarudisha watu wenu waliofungwa; nitawakusanya kutoka mataifa yote na sehehemu zote ambako nimewatawanya—hili ni tangazo la Yahwe—kwa maana nitawarudisha kutoka sehemu ambako niliwasababisha kuwa mateka.
15 Mnaweza mkasema, “Bwana ameinua manabii kwa ajili yetu huku Babeli,”
Tangu mliposema kwamba Yahwe ameinua manabii kwa ajili yetu katika Babeli,
16 lakini hili ndilo asemalo Bwana kuhusu mfalme aketiaye kiti cha enzi cha Daudi, na watu wa kwenu wote wanaobaki katika mji huu, ndugu zenu ambao hawakwenda pamoja nanyi uhamishoni.
Yahwe anasema hivi kwa mfalme aliyeketi katika kiti cha enzi cha Daudi na watu wote wakaao katika mji huo, ndugu zenu ambao hawakwenda pamoja nanyi utumwani—
17 Naam, hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Nitatuma upanga, njaa na tauni dhidi yao, nami nitawafanya kuwa kama tini dhaifu zile ambazo ni mbovu sana zisizofaa kuliwa.
Yahwe wa majeshi anasema hivi, ''Ona, niko karibu kutuma upanga, njaa, na ugonjwa juu yao. Kwa maana nitawafanya kuwa kama tini mbovu ambazo ni mbaya sana hazifai kuliwa.
18 Nitawafukuza kwa upanga, kwa njaa na kwa tauni, nami nitawafanya kitu cha kuchukiza sana kwa falme zote za dunia, na kuwa kitu cha laana na cha kuogofya, cha dharau na kukemewa, miongoni mwa mataifa yote nitakakowafukuzia.
Kisha nitawafuata kwa upanga, njaa, na tauni na kuwafanya kuwa kitu cha kushangaza kwa falme zote juu ya dunia—kitu cha kuogofya, kitu cha kulaaniwa na kuzomewa, na kitu cha aibu miongoni mwa mataifa yote ambako nilimtawanya.
19 Kwa kuwa hawakuyasikiliza maneno yangu,” asema Bwana, “maneno ambayo niliwatumia tena na tena kupitia watumishi wangu manabii. Wala ninyi watu wa uhamisho hamkusikiliza pia,” asema Bwana.
Hii ni kwa sababu hawakulisikiliza neno langu—hili ni tangazo la Yahwe—ambalo nililituma kwao kupitia watumishi wangu manabii. Niliwatuma tena na tena, lakini hamkusikiliza—hili ni tangazo la Yahwe. '
20 Kwa hiyo, sikieni neno la Bwana, enyi nyote mlio uhamishoni, niliowapeleka Babeli kutoka Yerusalemu.
Kwa hiyo ninyi wenyewe sikilizeni neno la Yahwe, ninyi mateka wote ambao amewatuma kutoka Yerusalemu hadi Babeli,
21 Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo kuhusu Ahabu mwana wa Kolaya, na Sedekia mwana wa Maaseya, wanaowatabiria uongo kwa jina langu: “Nitawatia mikononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli, naye atawaua mbele ya macho yenu hasa.
'Yahwe wa majeshi, Mungu wa Israeli, anasema hivi kuhusu Ahabu mwana wa Kolaya na Sedekia mwana wa Maaseya, watabirio uongo kwenu katika jina langu: Ona, niko karibu kuwaweka katika mkono wa Nebukadreza mfalme wa Babeli. Atawaua mbele ya macho yenu.
22 Kwa ajili yao, watu wote wa uhamisho kutoka Yuda walioko Babeli watatumia laana hii: ‘Bwana na akutendee kama Sedekia na Ahabu, ambao mfalme wa Babeli aliwachoma kwa moto.’
Kisha laana itatamkwa na wafungwa wote wa Yuda katika Babeli kuhusu watu hawa. Laana itasema: Yahwe awafanye kuwa kama Sedekia na Ahabu, ambao mfalme wa Babeli aliwaoka kwenye moto.
23 Kwa kuwa wamefanya mambo maovu kabisa katika Israeli, wamezini na wake za majirani zao, tena kwa Jina langu wamesema uongo, mambo ambayo sikuwaambia kuyafanya. Nami nayajua haya, na ni shahidi wa jambo hilo,” asema Bwana.
Hili litatokea kwa sababu ya mambo ya aibu waliyofanya katika Israeli walipofanya uzinzi na wake za majarani zao na kutangaza maneno ya uongo katika jina langu, mambo ambayo sikuwaamuru wayaseme. Kwa maana mimi ndiye nijuaye; mimi ni shahidi—hili ni tangazo la Yahwe.”'
24 Mwambie Shemaya Mnehelami,
Kuhusu Shemaya Mnehelami, sema hivi:
25 “Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: Ulituma barua kwa jina lako mwenyewe kwa watu wote wa Yerusalemu, kwa Sefania mwana wa kuhani Maaseya na kwa makuhani wengine wote. Ulimwambia Sefania,
'Yahwe wa majeshi, Mungu wa Israeli, anasema hivi: Kwa sababu ulituma barua kwa jina lako kwa watu wote katika Yerusalemu, kwa Sefania mwana wa Maaseya kuhani, na kwa makuhani wote, na ulisema,
26 ‘Bwana amekuweka wewe uwe kuhani badala ya Yehoyada ili uwe msimamizi wa nyumba ya Bwana. Unapaswa kufunga kwa mikatale na mnyororo wa shingoni mwendawazimu yeyote anayejifanya nabii.
“Yahwe aliwafanya ninyi kuwa makuhani badala ya Yehoyada kuhani, ili muwe wasimamizi wa nyumba ya Yahwe. Ninyi ni viongozi wa watu wote wajitiao wazimu na kujifanya wenyewe manabii. Mtawaweka katika mkatale na minyororo.
27 Kwa nini basi hukumkemea Yeremia Mwanathothi, aliyejifanya kama nabii miongoni mwenu?
Kwa hiyo sasa, kwa nini hamkumkemea Yeremia wa Anathothi, ambaye hujifanya mwenyewe nabii juu yenu?
28 Ametutumia ujumbe huu huku Babeli: Mtakuwako huko muda mrefu. Kwa hiyo jengeni nyumba mkakae; pandeni mashamba na mle mazao yake.’”
Kwa maana ametutumia sisi katika Babeli, 'Itakuwa muda mrefu. Jengeni nyumba na muishi ndani yake, na pandeni busitani na mule matunda yake.””
29 Kuhani Sefania, hata hivyo, akamsomea nabii Yeremia ile barua.
Sefania kuhani akaisoma barua hii mbele ya Yeremia nabii.
30 Ndipo neno la Bwana likamjia Yeremia kusema:
Kisha neno la Yahwe likaja kwa Yeremia, likisema,
31 “Tuma ujumbe huu kwa watu wote walio uhamishoni: ‘Hili ndilo Bwana asemalo kuhusu Shemaya Mnehelami: Kwa sababu Shemaya amewatabiria ninyi, hata ingawa sikumtuma, naye amewafanya kuamini uongo,
“tuma neno kwa mateka wote na sema, 'Yahwe anasema hivi kuhusu Shemaya Mnehelami: Kwa sababu Shemaya amewatabiria ninyi wakati mimi sikumtuma, na amewaongoza kuamini uongo,
32 hili ndilo Bwana asemalo: Hakika nitamwadhibu Shemaya Mnehelami pamoja na uzao wake. Hapatakuwa na yeyote atakayebaki miongoni mwa watu hawa, wala hataona mema nitakayowatendea watu wangu, asema Bwana, kwa sababu ametangaza uasi dhidi yangu.’”
kwa hiyo Yahwe anasema hivi: Angalia, niko karibu kumwadhibu Shemaya Mnehelami na uzao wake. Hapatakuwa na mtu wa kukaa miongoni mwa watu hawa kwa ajili yake. Hataona mema nitakayofanya kwa ajili ya watu wangu—hili ni tangazo la Yahwe—kwa maana ametangaza uasi dhidi ya Yahwe.””

< Yeremia 29 >