< Yeremia 25 >
1 Neno likamjia Yeremia kuhusu watu wote wa Yuda, katika mwaka wa nne wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, ambao ulikuwa mwaka wa kwanza wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babeli.
Hili ndilo neno ambalo lilimjia Yeremia juu ya watu wote wa Yuda. Ikawa mwaka wa nne wa Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda. Huo ndio mwaka wa kwanza wa Nebukadreza, mfalme wa Babeli.
2 Hivyo nabii Yeremia akawaambia watu wote wa Yuda na wale wote waishio Yerusalemu:
Yeremia nabii aliwahubiria watu wote wa Yuda na wenyeji wote wa Yerusalemu.
3 Kwa miaka ishirini na mitatu, kuanzia mwaka wa kumi na tatu wa utawala wa Yosia mwana wa Amoni mfalme wa Yuda, hadi siku hii ya leo, neno la Bwana limekuwa likinijia, nami nimesema nanyi mara kwa mara, lakini hamkusikiliza.
Akasema, “Kwa miaka ishirini na mitatu, tangu mwaka wa kumi na tatu wa Yosia mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda mpaka leo, maneno ya Bwana yamekuja kwangu. Nimewahubiria ninyi. Nilikuwa na nia ya kutangaza, lakini hamkunisikiliza.
4 Ingawa Bwana amewatuma watumishi wake wote hao manabii kwenu mara kwa mara, hamkusikiliza wala hamkujali.
Bwana akawapeleka watumishi wake wote manabii kwako. Walikuwa na nia ya kwenda, lakini hukusikiliza wala kutega masikio.
5 Walisema, “Geukeni sasa, kila mmoja wenu kutoka njia yake mbaya na matendo yake maovu, ndipo mtaweza kukaa katika nchi ambayo Bwana aliwapa ninyi na baba zenu milele.
Manabaii hawa walisema, 'Kila mtu auache uovu wake na udhalimu wa matendo yake na kurudi kwenye nchi ambayo Yahwe aliitoa wakati wa zamanai kwa ajili ya babu zenu na ninyi, kama zawadi ya kudumu.
6 Msiifuate miungu mingine ili kuitumikia na kuiabudu. Msinikasirishe kwa vitu ambavyo mmevitengeneza kwa mikono yenu.”
Kwa hiyo msiifuate miungu mingine ili kuiabudu au kuiinamia chini, na msimkasirishe kwa kazi ya mikono yenu ili kwamba awaumize.
7 “Lakini ninyi hamkunisikiliza mimi, tena mkanikasirisha kwa vitu mlivyovitengeneza kwa mikono yenu, nanyi mmejiletea madhara juu yenu wenyewe,” asema Bwana.
Lakini hamkunisikiliza-hili ndilo tamko la Bwana-kwa hiyo umenikasirisha kwa kazi ya mikono yako ili kujidhuru nafsi zemu.
8 Kwa hiyo Bwana Mwenye Nguvu Zote asema hivi: “Kwa sababu hamkuyasikiliza maneno yangu,
Basi, Bwana wa majeshi asema hivi, 'Kwa kuwa hukusikiliza maneno yangu,
9 nitayaita mataifa yote ya kaskazini na mtumishi wangu Nebukadneza mfalme wa Babeli,” asema Bwana. “Nitawaleta waishambulie nchi hii na wakazi wake wote, na dhidi ya mataifa yote yanayowazunguka. Nitawaangamiza kabisa na kuwafanya kitu cha kuchukiwa na kudharauliwa, na kuwa magofu daima.
tazama, nitaagiza amri ya kukusanya watu wote wa kaskazini- asema Bwana- na Nebukadreza, mtumishi wangu, mfalme wa Babeli, na kuwaleta juu ya nchi hii na wenyeji wake, na juu ya mataifa yote yaliyo karibu nawe. Kwa maana nitawaangamiza. Nitawageuza kuwa na hofu, kuwa kitu cha kuzomewa na ukiwa wa daima.
10 Nitawaondolea sauti ya shangwe na furaha, sauti ya bibi na bwana arusi, sauti ya mawe ya kusagia, na mwanga wa taa.
Sauti ya furaha na sherehe-sauti ya bwana arusi na bibi arusi, sauti ya mawe ya kusagia na mwanga wa taa-nitafanya mambo yote haya kutoweka kutoka kwa mataifa haya.
11 Nchi hii yote itakuwa ukiwa na isiyofaa kitu, nayo mataifa haya yatamtumikia mfalme wa Babeli kwa miaka sabini.”
Ndipo nchi hii yote itakuwa ukiwa na hofu, na mataifa haya watamtumikia mfalme wa Babeli kwa miaka sabini.
12 “Lakini miaka sabini itakapotimia, nitamwadhibu mfalme wa Babeli na taifa lake na nchi ya Wakaldayo kwa ajili ya hatia yao,” asema Bwana. “Nitaifanya kuwa ukiwa milele.
Kisha miaka sabini itakapokamilika, nitamuadhibu mfalme wa Babeli na taifa hilo, nchi ya Wakaldayo-hili ndilo tamko la Bwana-kwa uovu wao na kuifanya kuwa ukiwa milele.
13 Nitaleta juu ya nchi hiyo mambo yote niliyosema dhidi yake, yote yaliyoandikwa katika kitabu hiki, na kutolewa unabii na Yeremia dhidi ya mataifa yote.
Nami nitaleta juu ya nchi hiyo maneno yote niliyosema, na kila kitu kilichoandikwa katika kitabu hiki ambacho Yeremia ametabiri juu ya mataifa yote.
14 Wao wenyewe watakuwa watumwa wa mataifa mengi na wafalme wakuu. Nitawalipizia sawasawa na matendo yao na kazi ya mikono yao.”
Kwa maana pia mataifa mengi na wafalme wakuu watapata watumwa kutoka mataifa haya. Nitawalipa kwa matendo yao na kazi za mikono yao.'”
15 Hili ndilo Bwana, Mungu wa Israeli, aliloniambia: “Chukua kutoka mkononi mwangu kikombe hiki kilichojaa divai ya ghadhabu yangu, na kuyanywesha mataifa yote ambayo ninakutuma kwao.
Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, “Chukua kikombe hiki cha divai ya ghadhabu kutoka mkononi mwangu, ukawanyweshe mataifa yote niliyokutuma.
16 Watakapoinywa, watapepesuka na kukasirika sana kwa sababu ya upanga nitakaoupeleka katikati yao.”
Kwa maana watakunywa na kisha watalewa na kufanya wazimu mbele ya upanga ambao nitaupeleka kati yao.”
17 Hivyo nikakichukua kikombe kutoka mkononi mwa Bwana, na kuyafanya mataifa yote aliyonituma kwao kukinywa:
Basi, nikakichukua kikombe mkononi mwa Bwana, nikawanywesha mataifa yote ambayo Bwana alinituma:
18 Yaani Yerusalemu na miji ya Yuda, wafalme wake na maafisa wake, kuwafanya magofu na kuwa kitu cha kuchukiza, cha dhihaka na laana, kama walivyo leo;
Yerusalemu, miji ya Yuda, na wafalme wake, na wakuu wake, na kuwafanya kuwa ukiwa na kitu cha kutisha, na kuwa kitu cha kuzomewa na laana, kama ilivyo hata leo.
19 pia Farao mfalme wa Misri, watumishi wake, maafisa wake na watu wake wote,
Mataifa mengine pia walipaswa kunywa: Farao mfalme wa Misri na watumishi wake; maafisa wake na watu wake wote;
20 pia wageni wote walioko huko; wafalme wote wa nchi ya Usi; wafalme wote wa Wafilisti (wale wa Ashkeloni, Gaza, Ekroni na watu walioachwa huko Ashdodi);
watu wote wa urithi wa mchanganyiko na wafalme wote wa nchi ya Uzi; na wafalme wote wa nchi ya Wafilisti, na Ashkeloni, na Gaza, na Ekroni, na mabaki ya Ashdodi;
21 Edomu, Moabu na Amoni;
Edomu na Moabu na wana wa Amoni.
22 wafalme wote wa Tiro na Sidoni; wafalme wa nchi za pwani ngʼambo ya bahari;
Wafalme wa Tiro na Sidoni, wafalme wa pwani ng'ambo ya pili ya bahari,
23 Dedani, Tema, Buzi na wote walio maeneo ya mbali;
Dedani, Tema, na Busi pamoja na wale wanyoao nywele zao upande wa pili wa vichwa vyao, pia walipaswa kukinywa.
24 wafalme wote wa Arabuni na wafalme wote wa watu wageni wanaoishi katika jangwa;
Watu hawa pia walitakiwa kukinywa; wafalme wote wa Uarabuni na wafalme wote wa watu wa asili mchanganyiko wanaoishi nyikani;
25 wafalme wote wa Zimri, Elamu na Umedi;
wafalme wote wa Zimri, wafalme wote wa Elamu, na wafalme wote wa Wamedi;
26 na wafalme wote wa pande za kaskazini, wa karibu na wa mbali, mmoja baada ya mwingine; yaani falme zote juu ya uso wa dunia. Baada ya hao wote, mfalme wa Sheshaki atakunywa pia.
wafalme wote wa kaskazini, wale wa karibu na wale wa mbali—kila mmoja na ndugu zake na falme zote za ulimwengu ambazo ziko chini ya uso wa dunia. Hatimaye mfalme wa Babeli atakunywa baada yao wote.
27 “Kisha uwaambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: Kunyweni, mlewe na mtapike; angukeni, wala msiinuke tena kwa sababu ya upanga nitakaotuma miongoni mwenu.’
Bwana akaniambia, “Basi, uwaambie, 'Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi kunywa na kulewa, kisha tapika, uanguke, wala usisimame mbele ya upanga nitakaoutuma kati yenu.'
28 Lakini kama wakikataa kupokea kikombe kutoka mikononi mwako na kunywa, waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: Ni lazima mnywe!
Kisha itatokea kwamba ikiwa wanakataa kuchukua kikombe mkononi mwako ili kunywa, utawaambia, 'Bwana wa majeshi asema hii lazima mnywe.
29 Tazama, nimeanza kuleta maafa juu ya mji ulio na Jina langu, na je, kweli ninyi mtaepuka kuadhibiwa? Hamwezi kuepuka kuadhibiwa, kwa maana nitaleta vita juu ya wote waishio duniani, asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.’
Kwa maana, tazama, nitaleta janga juu ya mji ulioitwa kwa jina langu, je ninyi mtaachiliwa msiadhibiwe? Hutakuwa huru, kwa maana nitaita upanga juu ya wenyeji wote wa nchi! - ndilo tamko la Bwana wa majeshi.'
30 “Basi sasa toa unabii kwa maneno haya yote dhidi yao, uwaambie: “‘Bwana atanguruma kutoka juu; atatoa sauti ya ngurumo kutoka makao yake matakatifu na kunguruma kwa nguvu sana dhidi ya nchi yake. Atapiga kelele kama wao wakanyagao zabibu, atapiga kelele dhidi ya wote waishio duniani.
Basi wewe mwenyewe, Yeremia, tabiri kwao maneno haya yote. Uwaambie, 'Bwana atanguruma kutoka juu, naye atapaza sauti yake toka makao yake matakatifu, na radi kutoka mahali pake patakatifu; naye atapiga kelele kama wale wakanyagao zabibu dhidi ya wote wanaoishi duniani.
31 Ghasia zitasikika hadi miisho ya dunia, kwa maana Bwana ataleta mashtaka dhidi ya mataifa; ataleta hukumu juu ya wanadamu wote na kuwaua waovu wote,’” asema Bwana.
Kelele huja mpaka mwisho wa nchi, kwa sababu mgogoro kutoka kwa Bwana utaleta mashtaka dhidi ya mataifa. Ataleta haki kwa wote wenye mwili. Yeye atawatia waovu katika upanga-hili ndi'o tamko la Bwana.'
32 Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo: “Tazama! Maafa yanaenea kutoka taifa moja hadi jingine; tufani kubwa inainuka kutoka miisho ya dunia.”
Bwana wa majeshi asema hivi, 'Tazameni, taabu itatokea toka kwa taifa hadi taifa, na dhoruba kubwa itatokea toka pande za mwisho za dunia.
33 Wakati huo, hao waliouawa na Bwana watatapakaa kila mahali, kuanzia mwisho mmoja wa dunia hadi mwisho mwingine. Hawataombolezewa wala kukusanywa au kuzikwa, lakini watakuwa kama mavi yaliyoenea juu ya ardhi.
Kisha wale waliouawa na Bwana watakuja kutoka upande mmoja wa dunia hadi mwingine; hawataomboleza, kukusanyika, au kuzikwa. Watakuwa kama samadi chini.
34 Lieni na kuomboleza, enyi wachungaji, mgaagae mavumbini, ninyi viongozi wa kundi. Kwa maana wakati wenu wa kuchinjwa umewadia; mtaanguka na kuvunjavunjwa kama vyombo vizuri vya udongo.
Pigeni Yowe, wachungaji, na pigeni kelele ya kuomba msaada! Gaagaa katika ardhi, enyi mlio hodari katika kundi. Kwa kuwa siku yako ya kuuawa na kutawanywa imekuja. Utaanguka kama kondoo waliochaguliwa.
35 Wachungaji hawatakuwa na mahali pa kukimbilia, viongozi wa kundi hawatapata mahali pa kutorokea.
Wachungaji hawatakuwa na pa kukimbilia. Hakuna kutoroka kwa watu walio hodari katika kundi.
36 Sikia kilio cha wachungaji, maombolezo ya viongozi wa kundi, kwa maana Bwana anayaharibu malisho yao.
Kuna mlio wa wasiwasi wa wachungaji na milio ya kulalama kwa watu walio hodari katika kundi, kwa kuwa Yahweh anayaharibu malisho yao.
37 Makao yao ya amani yataharibiwa kwa sababu ya hasira kali ya Bwana.
Kwa hiyo, malisho ya amani yataharibiwa kwa sababu ya hasira ya Bwana.
38 Kama simba ataacha pango lake, nchi yao itakuwa ukiwa kwa sababu ya upanga wa mdhalimu, na kwa sababu ya hasira kali ya Bwana Mungu.
Kama simba, ameacha shimo lake, kwa kuwa ardhi yao itakuwa kitu cha kushangaza kwa sababu ya hasira ya muonevu, kwa sababu ya ghadhabu yake kali'”