< Yeremia 24 >
1 Baada ya Yekonia mwana wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, pamoja na maafisa, mafundi stadi na wahunzi wa Yuda, kuchukuliwa kutoka Yerusalemu kwenda Babeli na Nebukadneza mfalme wa Babeli kwenda uhamishoni huko Babeli, Bwana akanionyesha vikapu viwili vya tini vilivyowekwa mbele ya Hekalu la Bwana.
2 Kikapu kimoja kilikuwa na tini nzuri sana, kama zile za mavuno ya kwanza. Kikapu cha pili kilikuwa na tini dhaifu sana, mbovu mno zisizofaa kuliwa.
3 Kisha Bwana akaniuliza, “Je, Yeremia, unaona nini?” Nikamjibu, “Ninaona tini zile zilizo nzuri ni nzuri sana, lakini zilizo dhaifu ni mbovu mno zisizofaa kuliwa.”
4 Kisha neno la Bwana likanijia:
5 “Hili ndilo Bwana, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Kama zilivyo hizi tini nzuri, ndivyo ninavyowaona kuwa bora watu wa uhamisho kutoka Yuda, niliowaondoa kutoka mahali hapa kwenda katika nchi ya Wakaldayo.
6 Macho yangu yatakuwa juu yao kwa ajili ya kuwapatia mema, nami nitawarudisha tena katika nchi hii. Nitawajenga wala sitawabomoa, nitawapanda wala sitawangʼoa,
7 nitawapa moyo wa kunifahamu mimi, kwamba mimi ndimi Bwana. Watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao, kwa maana watanirudia kwa moyo wao wote.
8 “‘Lakini kama zilivyo zile tini dhaifu, ambazo ni mbovu mno zisizofaa kuliwa,’ asema Bwana, ‘ndivyo nitakavyomtendea Sedekia mfalme wa Yuda, maafisa wake na mabaki wengine kutoka Yerusalemu, wawe wamebaki katika nchi hii, au wanaishi Misri.
9 Nitawafanya kuwa chukizo kabisa na kitu cha kulaumiwa katika mataifa yote ya dunia, watakuwa aibu na kitu cha kudharauliwa, chombo cha dhihaka na kulaaniwa, popote nitakapowafukuzia.
10 Nitautuma upanga, njaa na tauni dhidi yao hadi wawe wameangamia kutoka nchi niliyowapa wao na baba zao.’”